Saturday, October 31, 2009

KWANZA JAMII limetua Mwanza


Gazeti la KWANZA JAMII linapatikana Mwanza, kwa mujibu wa picha hizi zilizotoka katika blogu ya Mjengwa tarehe 29 Oktoba, 2009 na 30 Oktoba, 2009. Nami napenda kufuatilia maendeleo ya gazeti hili.

Wednesday, October 28, 2009

KWANZA JAMII Mikumi

Picha hii imechapishwa tarehe 28 Oktoba, 2009, katika blogu ya Mjengwa. Maggid Mjengwa amepiga picha hii Mikumi. Mimi kama mwandishi katika gazeti la KWANZA JAMII nafurahi kuona gazeti hili, ambalo bado changa, linavyojikongoja na kuendelea kuenea nchini, hadi kwenye miji midogo na vijijini. Siku chache zilizopita tulipata habari za KWANZA JAMII kufika kijijini Roya. Bofya hapa. Kama wahenga walivyosema, pole pole ya kobe humfikisha mbali.

Friday, October 16, 2009

Warsha Dar es Salaam: Utamaduni na Utandawazi


Tarehe 5 Septemba, mwaka huu, niliendesha warsha Dar es Salaam, kuhusu Utamaduni na Utandawazi. Warsha hii iliandaliwa na Tanzania Discount Club. Siku chache kabla, tarehe 29 Agosti, niliendesha warsha nyingine Tanga, kuhusu Utamaduni, Utandawazi na Maendeleo. Warsha hii, ambayo ilihudhuriwa na watu wa mataifa mbali mbali, nimeiongelea kidogo hapa na hapa.

Warsha hii ya Dar es Salaam ilinipa fursa ya kukutana na waTanzania kutoka sekta binafsi, taasisi mbali mbali na Ubalozi wa Marekani.
Warsha ilidumu kuanzia saa nne na nusu asubuhi hadi saa 11 jioni. Sehemu ya kwanza ilihusu masuala ya jumla: dhana ya utamaduni, kama nilivyoielezea katika kitabu changu Africans and Americans, na dhana ya utandawazi. Kwa mtazamo wangu, utandawazi ni jambo ambalo lilianza zamani kabisa, pale binadamu wa mwanzo walivyosambaa duniani wakitokea Afrika Mashariki. Hapo ndipo utandawazi ulipoanzia, na baada ya hapo, kumekuwa na aina na awamu mbali mbali za utandawazi, hadi kufikia zama zetu hizi, ambazo zimeshuhudia utandawazi wa ubepari ambao uliongelewa vizuri na Karl Marx na Frederick Engels katika Communist Manifesto. Leo hii, tekinolojia, na hasa tekinolojia ya mawasiliano, inawezesha aina nyingine za utandawazi, ambazo hata akina Karl Marx hawakuziwazia, kwani hazikuwepo. Utandawazi unajitokeza katika uchumi, siasa, utamaduni, na mambo mengine mengi.
Baada ya maelezo haya ya jumla niliingia kwenye suala la nafasi ya utamaduni katika utandawazi, nikielezea jinsi kuwepo kwa tamaduni mbali mbali duniani kunavyoathiri au kuathirirwa na utandawazi. Nilitoa mifano ya athari hizi. Kutokana na utafiti na uzoefu wangu, niliongelea kwa undani masuala yanayojitokeza katika mahusiano baina ya Wamarekani na Waafrika, kama nilivyoeleza katika kitabu changu.
Washiriki wote walifurahiwa na warsha hii na walitaka warsha za aina hii zifanyike siku za usoni, katika vyuo na taasisi mbali mbali.
Kwa upande wangu, nilifurahi kupata fursa ya kuongea na waTanzania wenzangu na kuwaeleza yale ambayo nimekuwa nawaeleza waMarekani kwa miaka kadhaa. Imenipa motisha ya kuendelea kufanya warsha za aina hii.
Jambo mmoja nililosisitiza ni kuwa ni muhimu warsha kama hii iwe ni sehemu ya elimu endelevu, ni muhimu tuendelee kuwasiliana. Baadhi ya washiriki walijipatia nakala za kitabu changu. Siku zijazo itawezekana kufanya warsha juu ya yaliyomo na yatokanayo na kitabu hiki, kama ambavyo inafanyika huku Marekani. Kitabu kinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0717 413 073 au 0754 888 647

Kadiri dunia inavyoendelea na utandawazi, ni muhimu tujizatiti kwa kuelewa yanayotokea na kujiweka sawa ili kukabiliana na kuitumia hali inayojitokeza. Kwa wale ambao wamelala, utandawazi unaweza kuwa tishio na kipingamizi, lakini kwa walio makini utandawazi unaweza kuwa fursa ya kufanya mambo ya maana.

Wednesday, October 14, 2009

Mwalimu Angerudi Leo Angejisikiaje?

Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Oktoba 13-19, 2009

Profesa Joseph L. Mbele

Imetimia miaka kumi tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alipofariki London, Oktoba 14, 1999. Ni jambo jema kutumia muda huu kumkumbuka kwa namna ya pekee, kwa mchango wake kwa Tanganyika (na baadaye Tanzania), Afrika na dunia kwa ujumla. Ni vizuri pia kutumia muda huu kutafakari mwenendo wa nchi yetu, tukilinganisha na makusudio aliyokuwa nayo Mwalimu wakati wa uhai wake.

Mchango wa Mwalimu katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika unatambulika. Akishirikiana na viongozi wengine wa sehemu mbali mbali za nchi, wa dini na rangi mbali mbali, na wananchi kwa ujumla, Mwalimu Nyerere aliongoza Tanganyika kufikia Uhuru, Desemba 9, 1961.

Hapo alitoa hotuba ambayo maneno yake ni vigumu kusahaulika, kwa jinsi yalivyoelezea kwa ufasaha hisia na matumaini ya Taifa letu changa. Mwalimu alisema, “Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau.”

Hotuba hii ilikuwa ni kielelezo kizuri cha malengo aliyokuwa nayo Mwalimu kwa nchi yetu. Ilisisimua nchi nzima na kuleta changamoto kwa wananchi katika ari ya kulijenga Taifa lao. Katika hotuba na maandishi yake mbali mbali, miaka yote ya maisha yake, Mwalimu Nyerere alifafanua masuala na wajibu mbali mbali wa wananchi, viongozi, na Taifa kwa ujumla. Aliweka sera ya kujenga uchumi wa kijamaa, ambamo njia kuu za uchumi zinamilikiwa na umma, kupitia serikali yao, kwa manufaa ya umma. Alielezea wajibu wa kila mtu kufanya kazi, na kupata kipato kutokana na mchango wake. Aliongelea kutokomeza unyonyaji, iwe ni wa mtu dhidi ya mwingine, au tabaka la jamii dhidi ya tabaka jingine.

Kuhusu elimu alifundisha kuwa elimu ni haki ya kila binadamu, itolewe kwa watu wote, bure. Mwalimu alifafanua wajibu wa wasomi kuwa ni kuutumikia umma. Elimu ilitakiwa iwe inayochochea udadisi wa kifikra, na kujitegemea. Alisisitiza kuwa elimu haina mwisho. Alijenga utaratibu wa elimu ya watu wazima na kisomo chenye manufaa, ili watu waweze kujiendelea katika fani mbali mbali, iwe ni ukulima, uvuvi, useremala, na kadhalika. Pamoja na kuona elimu kuwa ni namna ya kupambana na adui ujinga, elimu ilihesabiwa kuwa njia ya kuondokana na utumwa wa kimawazo na ukoloni mambo leo.

Mwalimu alijali suala la huduma za afya na matibabu, akiyachukulia mambo hayo kuwa ni haki ya kila mtu. Ingekuwa uwezo wa nchi kuwa mdogo, huduma zingepelekwa kila mahali. Na katika kuwazia hilo, akaona kuwa vijiji vya ujamaa ndio mfumo muafaka wa kuwezesha huduma kama elimu, afya, na burudani kuwafikia wananchi.

Kisiasa, Mwalimu Nyerere alisimama kidete kutetea wanyonge na kujenga misingi ya demokrasia ya wakulima na wafanyakazi. Muda mfupi tu baada ya Uhuru, Mwalimu aliandaa na kutangaza Azimio la Arusha na miongozo mbali mbali ya kujenga usawa katika nchi yetu.

Mwalimu Nyerere alishughulikia utamaduni pia, akihamasisha watu kuuthamini utamaduni wao, maadili, lugha, na sanaa. Mwalimu aliipa kipaumbele lugha ya kiSwahili akaifanya lugha ya Taifa. Aliitumia katika hotuba na maandishi yake, kuanzia insha hadi mashairi. Alitafsiri tamthilia za Shakespeare: “The Merchant of Venice” na “Julius Caesar” kwa kiSwahili, akathibitisha utajiri wa lugha ya kiSwahili na pia kuwafungulia waTanzania milango waone utajiri uliomo katika falsafa na uandishi wa bingwa huyu ambaye alisifiwa pia sana na Shaaban Robert.

Mwalimu alitambua kuwa nchi yetu msingi wake mkuu ni wakulima. Kwa hivi alijibidisha kujenga sera ya kuleta maendeleo vijijini. Kufuata na hali halisi ya nchi yetu, aliona kuwa njia muafaka ni viijiji vya ujamaa. Sera hii ilikuwa na lengo la kuleta maendeleo vijijini katika usawa na kujitegemea. Ni sera aliyoifafanua mara kwa mara, kuanzia pale alipotangaza Azimio la Arusha.

Taifa letu lilihitaji kuwa na sera kuhusu uhusiano wetu na nchi zingine na nafasi yetu duniani. Mwalimu alisisitiza kuwa nchi yetu ni huru na haifungamani na upande wowote. Tuko tayari kuwa marafiki na nchi yoyote kwa misingi ya kuheshimiana. Hatumruhusu rafiki yetu kutuchagulia maadui zetu.

Kwa vile watu wengi Afrika na duniani walikuwa bado wanapigania uhuru na ukombozi, nchi yetu ilikuwa na msimamo wa kuunga mkono harakati za ukombozi duniani kote. Tulikuwa bega kwa bega na wenzetu katika nchi za kusini mwa Afrika, Palestina, Sahara Magharibi. Tuliunga mkono harakati za Wamarekani weusi, na kadhalika.

Maisha yake yote, Mwalimu alizingatia mwelekeo huo. Hakuwahi kuchepuka kutoka kwenye imani yake juu ya Ujamaa. Wako ambao wanadai kuwa aliwahi kusema kuwa Ujamaa umeshindwa. Madai hayo hayana ukweli. Hakuna ushahidi ambao umetolewa kwamba Mwalimu aliwahi kusema kuwa Ujamaa umeshindwa. Ni uzushi tu ambao wengi wameusikia na wanaurudia kama vile ungekuwa ukweli.

Leo hii Tanzania haifuati mwelekeo wa Mwalimu. Wazo la kujenga uchumi unaojitegemea limetupwa kando. Badala ya kuendeleza malengo ya Azimio la Arusha, kuyaweka katika hali ya kuendana na mazingira ya leo, chama tawala cha CCM kilileta Azimio la Zanzibar, ambalo Mwalimu Nyerere alilishutumu. Azimio la Zanzibar lililegeza masharti ya uongozi yaliyowekwa miaka iliyotangulia.
Leo tunaongelea kukua kwa uchumi, lakini si mgawanyo wa mali katika jamii. Nchi yetu ina matabaka, na tofauti kati ya matajiri na maskili inazidi kuwa kubwa. Hii ni hali ya hatari kwa siku za usoni.

Kwa sera zake, kama zilivyotamkwa katika Azimio la Zanzibar, CCM ilifungua milango ambayo hatimaye imeuwezesha ufisadi kuota mizizi na kustawi katika nchi yetu. CCM haishughuliki katika kudumisha urithi wa Mwalimu Nyerere. Inaonekana wazi kuwa CCM ingependa fikra za Mwalimu Nyerere zisahaulike, kutokana na ukweli kuwa CCM imeachana na fikra hizo, na pia kwa miaka mingi kabla hajafariki, Mwalimu Nyerere alikuwa anaishutumu na kuikosoa CCM.

Mara kwa mara zinapatikana taarifa za namna watu sehemu mbali mbali za dunia wanavyomwenzi Mwalimu Nyerere. Lakini tukifananisha na Tanzania tunaona kuwa nabiii huheshimiwa, isipokuwa nchini kwake. Hata hivi, tunayo fursa ya kujirekebisha, na dalili za kuleta matumaini zipo. Kwa mfano katika maadhimisho ya kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka huu, Taasisi ya Mwalimu Nyerere itatoa vitabu kadhaa vya maandishi ya Mwalimu, yakiwemo maandishi ambayo hayajawahi kuchapishwa. Habari hii inaleta matumaini.

Napenda kumalizia kuwa niliyoandika hapa ni dondoo tu. Kila kipengele kinastahili makala ya pekee, hata kitabu. Lakini nina suali: je, leo hii Watanzania tunaweza kudiriki kusema kuwa tuwashe mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuleta matumaini, upendo na heshima kwa wenzetu ulimwenguni? Ni nani duniani anayetuangalia leo akatamani kuwa kama tulivyo? Mwalimu Nyerere angerudi nchini leo, angejisikiaje?

Sunday, October 11, 2009

Tamasha la Vitabu, Minneapolis, 2009

Jana, tarehe 10 Oktoba, nilishiriki tamasha la vitabu mjini Minneapolis. Tamasha hili hufanyika kila mwaka mara moja. Nimeshahudhuria mara kadhaa miaka iliyopita, lakini hali ni mpya kila mwaka. Kwa mfano, waandishi maarufu wanaoalikwa kama wageni rasmi huwa tofauti kila mwaka. Pia, pamoja na kuwa baadhi ya waandishi na wachapishaji na wauza vitabu huja mwaka hadi mwaka, wako pia wengi ambayo ni wapya. Hapo juu mbele kabisa ni mezani pangu. Baadhi ya vitabu vyangu vinaonekana.
Watu wanawahi, na milango ukumbi wa maonesho inapofunguliwa, saa nne asubuhi, ukumbi unafurika watu. Siku nzima hali ni hiyo hiyo; kuna msongamano wa watu wakiwa wanaangalia na kununua vitabu, wakiongea na waandishi na wachapishaji, na kadhalika.

Waandishi wa kila aina wanakuwepo, wake kwa waume, wazee kwa vijana. Siku hizi wengi wanachapisha vitabu vyao kwa kutumia fursa zitokanazo na maendeleo ya tekinolojia, bila kupitia kwa wachapishaji kama ilivyokuwa zamani. Kila mtu anaweza kutumia tekinolojia hiyo ya kujichapishia mwenyewe, ambayo inapatikana sehemu mbali mbali mtandaoni, ili mradi awe na kompyuta iliyounganishwa mtandaoni.

Wamarekani wanafurika kwenye tamasha la vitabu sawa sawa na sisi waTanzania tunavyofurika sokoni kununua vyakula. Pamoja na hali ya uchumi kuwa ya matatizo nyakati hizi, watu wananunua sana vitabu. Sijui ni lini waTanzania wataanza kupata mwamko wa kuviona vitabu kuwa ni muhimu kiasi hicho. Niliwahi kutoa kauli hiyo kwenye mahojiano na mwanablogu maarufu Muhiddin Issa Michuzi tarehe 4 Septemba, 2009.
Wamarekani wanaliona tamasha la vitabu--au duka la vitabu--kama sehemu muhimu ya kujiongezea elimu na kupanua mawazo. Mazungumzo na waandishi, wachapishaji na wauza vitabu yanaendelea siku nzima. Watu wanakuja kutoka miji ya karibu na mbali pia. Wanakuja kuangalia vitabu, kuvinunua, kuongea na waandishi na wachapishaji, kujenga mitandao ya ushirikiano katika shughuli za uchapishaji na uuzaji wa vitabu na kadhalika.



Katika tamasha la jana, nilipangiwa meza namba 19, kama inavyoonekana hapa juu. "Africonexion" ni kampuni yangu, ambayo niliisajili hapa Minnesota. Inshughulika na warsha, uandishi na uchapishaji wa vitabu, elimu kuhusu utalii, mahusiano baina tamaduni mbali mbali, na kadhalika. Siku za usoni nitaiingiza kampuni hii Tanzania.
Kama inavyoonekana hapa juu, tamasha hili ni kazi kubwa kwa waandishi, kukaa na kuongea na watu siku nzima. Ingawa inachosha, ni shughuli muhimu kwa namna mbali mbali.
Hapo juu niko na Bukola Oriola, dada Mnigeria ambaye mwaka huu nilimsaidia kuchapisha kitabu chake kwa kutumia tekinolojia niliyoelezea hapo juu kwa kupitia kampuni ya Lulu. Anaendelea kuandika.

Hapo juu niko na Profesa Mahmoud El Kati, Mmarekani mweusi, ambaye ni mtu maarufu katika miji jirani ya Minneapolis na St. Paul, akiwa ni mwalimu, mtafiti, mwandishi na mwanaharakati. Nimefahamiana naye kwa miaka kadhaa.

Thursday, October 8, 2009

Uraia wa nchi Mbili

Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Oktoba 6-12, 2009

Profesa Joseph L. Mbele

Tarehe 4 Septemba, 2009, nilipata fursa ya kukutana na ndugu Muhiddin Issa Michuzi, mwanablogu maarufu Tanzania. Pamoja na maongezi kuhusu masuala mbali mbali, alinifanyia mahojiano mafupi kwa ajili ya kuweka kwenye blogu yake. Suali moja aliloniuliza ni kuhusu msimamo wangu juu ya suala la uraia wa nchi mbili. Nilijibu kifupi, kutokana na uchache wa muda. Lakini suali hili limekuwa mawazoni mwangu kwa miaka kadhaa, tangu lilipoanza kuongelewa na waTanzania.

Nilimweleza Ndugu Michuzi kuwa binafsi sitaki uraia wa nchi nyingine. Nilililelewa katika misingi ya kujitambua kuwa mimi ni mTanzania tu. Isipokuwa, nilisema kuwa watoto wa siku zijazo, watakuwa waishi katika dunia tofauti na yetu, na itakuwa dunia ambayo itakuwa imefungamana sana na kuwa kama kjiji. Hata mipaka ya nchi huenda haitakuwepo, wala nchi hazitakuwepo. Kwa hivi suala la uraia nalo litakuwa na sura tofatuti.

Tukiacha suala la hisia binafsi, ni vema kuangalia upana wa suala la uraia wa nchi mbili. Jambo moja na msingi ni kuwa sheria na taratibu za nchi mbali mbali kuhusu uraia zinatofautiana. Hali kadhalika, sheria na taratibu kuhusu uraia wa nchi mbili zinatofautiana kutoka nchi hadi nchi. Ziko nchi zenye sheria ngumu kuliko ilivyo katika nchi zingine. Ziko nchi ambazo sheria zake ni nyepesi.

Marekani ni nchi moja yenye sheria ngumu kuhusu uraia wa nchi mbili. Watu wengi wanachukua uraia wa Marekani. Na nadhani waTanzania wengi nao wanataka kuchukua uraia wa Marekani. Lakini ukweli ni kuwa wanaochukua uraia wa Marekani wanakula kiapo ambacho ni kizito sana. Katika kiapo hiki, wanaukana kabisa utii na uaminifu kwa kiongozi au dola ya nchi walikotoka. Ndio kusema, Mtanzania anayechukua uraia wa Marekani, anaapa hatambui amri ya kiongozi wa Tanzania juu yake. Anaapa kuwa atabeba silaha kuitetea Marekani kwa mujibu wa sheria. Kiapo hiki kinanitisha, kwa jinsi Marekani ilivyo na historia ya kushambulia nchi zingine, hasa nchi maskini.

Katika mijadala kuhusu uraia wa nchi mbili, suala linajadiliwa kwa namna ya kuelezea faida tu. Sisikii maelezo kuhusu wajibu na majukumu yanayotokana uraia wa nchi mbili. Ukweli ni kuwa hakuna nchi inayotoa uraia kama njugu, bila masharti na bila kumtwisha mhusika majukumu. Marekani inamtegemea mtu anayechukua uraia wa nchi ile kuapa kuwa atashika silaha kuitetea Marekani kwa mujibu wa sheria. Huo ni mfano mmoja wa majukumu yanayoambatana na uraia wa nchi mbili.

Kama nilivyosema, nchi nyingine hazina masharti kama haya ya Marekani. Kuna nchi ambazo hazina kiapo kama hiki cha Marekani. Nikisikia Mtanzania amechukua uraia wa nchi hizo, sioni kipingamizi chochote.

Kitu kimoja ambacho naamini waTanzania wengi hawajui ni kuwa Marekani yenyewe haipendelei raia wake wachukue uraia wa nchi zingine. Inatambua kuwa uraia wa nchi mbili unaweza kuleta matatizo. Vile vile Marekani inawatahadharisha raia wake kuwa kuchukua uraia wa nchi nyingine kunaweza kuhatarisha uraia wao wa Marekani. Hii inaweza kuwa ni ajabu kwa wale wanaoamini kuwa Marekani ndio nchi yenye uhuru kuliko nchi zingine duniani.

Hata hivi, kuna aina ya uraia wa nchi mbili ambao Marekani inautambua bila kipingamizi. Mtoto anayezaliwa Marekani na ambaye wazazi wake si raia wa Marekani anahesabiwa kuwa raia wa Marekani na pia raia wa nchi ya wazazi wake. Huu uraia wa nchi mbili hauna mgogoro katika taratibu na sheria za Marekani. Kadhalika, sheria za Marekani zinamtambua mtoto wa waMarekani anayezaliwa nchi nyingine kuwa ni raia wa Marekani, pamoja na kuwa anaweza pia kuwa raia wa nchi ile alimozaliwa. Huu ni uraia wa nchi mbili ambao Marekani inautambua bila tatizo.

Kwa upande wa Tanzania, tunao pia watoto wanaozaliwa nchi za nje lakini wazazai wao ni waTanzania. Naona ni sahihi kuwatambua watoto hao kuwa raia wa nchi mbili. Vile vile, kuna mtoto ambaye mzazi wake mmoja ni Mtanzania na mzazi mwingine si mTanzania. Mtoto huyu naona anastahili kuhesabiwa kuwa raia wa nchi mbili.

Sababu moja wanayotoa Watanzania wanopigania uraia wa nchi mbili ni kuwa uraia wan chi mbili utawafungulia milango ya uwekezaji nchini Tanzania au itawaletea urahisi wa uwekezaji. Sina hakika kama hoja hii ina uzito, kwani watu wengi ambao si raia wa Tanzania wanawekeza Tanzania bila matatizo. Je, ni kweli kwamba uraia wa nchi mbili ndio utawafungulia njia waTanzania kuwekeza nchini? Ni kweli kuwa wanapokuwa hawana uraia wa nchi mbili wanakutana na vipingamizi katika uwekezaji nchini? Naona suala hili linahitaji ufafanuzi.

Katika mahojiano na Ndugu Michuzi, nilisema kuwa kwa jinsi dunia inavyokwenda, chini ya utawandazi, labda nchi zitatoweka, na itabaki dunia tu. Vizazi vijavyo, vinavyolelewa katika mazingira tofauti na yale niliyokulia mimi vitakuwa na hisia na msimamo tofauti na wangu kuhusu uraia. Katika dunia ya leo inayozidi kukumbwa na utandawazi, juhudi za nchi mbali mbali kuungana kiuchumi, kisiasa, na kadhalika, yawezekana mipaka ya nchi itatoweka. Suala la uraia litachukua sura mpya. Labda hapatakuwa na sababu ya uraia wa nchi yoyote, wala uraia wa nchi mbili. Labda watu watakuwa raia wa Afrika Mashariki, basi, au raia wa Afrika basi, badala ya kuwa raia wa Tanzania, Cameroon, au Sudan, kama ilivyo sasa. Malumbano ya uraia wa nchi mbili sherti yazingatie huu uyakinifu.

Sunday, October 4, 2009

Diwani--"KWANZA JAMII Limefika Roya!"

(Taarifa hii imechapishwa katika blogu ya Mjengwa tarehe 4 Oktoba, 2009. Nikiwa ni mwandishi mmojawapo wa KWANZA JAMII, nafurahi jinsi gazeti hili linavyojitahidi kuingia vijijini. Hata kijijini kwangu, Wilaya ya Mbinga, linafahamika)

Mchana huu Diwani wa Kata ya Roya Bw. Emmanuel Kigodi amempigia simu mwandishi wa KWANZA JAMII Victor Makinda kumjulisha kuwa nakala nne za KWANZA JAMII zimemfikia. Gazeti hilo limebeba habari kubwa ukurasa wa mbele yenye kuhusiana na ujambazi uliotokea kwenye kata hiyo hivi karibuni. Kwa mujibu wa Diwani Kigodi, gazeti hilo la KWANZA JAMII sasa limekuwa gumzo kijijini Roya na linazunguka kwa wanakijiji wenye hamu ya kusoma habari zake!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...