Wednesday, August 28, 2013

Zawadi Baada ya Mhadhara Finland

Bado nina mengi ya kusema kuhusu safari  yangu ya wiki iliyopita nchini Finland, kwenye mkutano. Nina kumbukumbu nyingi, na kama nilivyowahi kusema zamani, blogu yangu ni mahali ninapojiwekea mambo yangu binafsi.

Kama nilivyotamka, nilialikwa kutoa mhadhara maalum, ambao hapa Marekani huitwa "keynote address." Mada yangu ilikuwa "The Epic as a Discourse on National Identity."

Baada ya kutoa mhadhara, mtoa mhadhara alikuwa anakabidhiwa ua. Ua hilo ni shukrani ya waandaaji wa mkutano.










Hapa kushoto anaonekana Profesa Pekka Hakamies, mwenyekiti wa kamati ya maandilizi, ambaye aliniletea mwaliko.

Tulioalikwa kutoa hiyo mihadhara maalum tulikuwa watano, kila mtu akatoa mhadhara wake kwa wakati tofauti. Mhadhara wa aina hiyo hutolewa mbele ya washiriki wote wa mkutano, na unategemewa kuweka msingi au changamoto za kujadiliwa na washiriki katika vikao mbali mbali ambamo mada mbali mbali hutolewa.

Katika kuhudhuria hivyo vikao vya baadaye, nilifurahi kuwasikia washiriki mara kadhaa wakinukuu yale niliyoyosema. Katika taaluma, haya ni mafanikio. Wazo hili linaweza kuwa gumu kwa wa-Tanzania wengi kulielewa, kwani wanadhani mafanikio ni pesa. Kama huna pesa, wa-Tanzania hao wanakushangaa ukiwaambia umefanikiwa.
 
Jambo linalofurahisha pia ni kuwa unapokuwa umealikwa kama nilivyoalikwa, halafu ukachangia mkutano kwa ufanisi, unakuwa umewahakikishia waandaaji kuwa hawakukosea kukualika, na unakuwa umewaridhisha washiriki kwa kuwapa mawazo na fikra mpya.

Ni fursa pia ya kukitangaza chuo chako. Nilipokuwa mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976 hadi 1990, shughuli zangu hizi zilikuwa zinakitangaza chuo kile. Lakini kuanzia mwaka 1991, nilivyoondoka kabisa kutokana na mizengwe ya pale, nimeridhika kabisa kuwa mwajiriwa wa Chuo cha St. Olaf na kukitangaza.

Tofauti na fikra au hisia za wa-Tanzania wengi, sijabadili uraia, na sitabadili, wala sijawahi hata kuwazia kwa namna yoyote kuchukua uraia wa Marekani. Badala yake, nimejitafutia njia kadhaa muhimu za kuitumikia nchi yangu kwa kutumia fursa za hapa ughaibuni.

Sunday, August 25, 2013

Ziara Yangu Finland Imefanikiwa Sana

Tarehe 19 hadi 24 nilikuwa kwenye Chuo Kikuu cha Turku, Finland, kwenye mkutano wa kitaaluma. Nilialikwa nikatoe mmoja ya mihadhara maalum, "keynote address." Mhadhara wangu ulikuwa "The Epic as a Discourse on National Identity." Utafiti, ufundishaji na uandishi wangu kuanzia kwenye mwaka 1977 umekuwa zaidi kuhusu masimulizi kama yale ya Iliad, Odyssey, Dede Korkut, Sundiata, Liongo Fumo, Kilenzi, Beowulf, Gassire, Ibonia, na Kalevala. Anayeonekana pichani kulia, ni Profesa Pekka Hakamies, mwenyekiti wa jopo la maandalizi, aliyenialika. Washiriki walikuja kutoka pande mbali mbali za dunia.






Hapa kushoto niko mbele ya kanisa moja, mjini Turku. Sikupata muda wa kuingia ndani, bali nilikuwa napita hapo nje kila nikiwa njiani baina ya hoteli nilyofikia na sehemu ya mkutano, mwendo wa dakika kama 15 kwa mguu.
















Jioni ya tarehe 23 nilialikwa Helsinki, kwa chakula cha jioni. Hapo nilikutana na wa-Tanzania kadhaa waliokuja kujumuika nami. Ukarimu wao sitausahau.












Friday, August 16, 2013

Nangojea Kukaguliwa "Eapoti"

Wadau, wiki ijayo ninasafiri kwenda Finland, kwenye mkutano, nikitokea uwanja wa ndege wa Minneapolis. Sasa kuna haka kasuala ka waBongo kukaguliwa sana kwenye hivyo viwanja vya ndege. Nasubiri zamu yangu.

Hii mijitu iliyotufikisha hapa imetuhujumu sana waBongo. Nasikia mingine ni mijitu mikubwa serikalini, na mingine eti ni mifanyabiashara. Biashara gani hii kama si uroho wa fisi, ujambazi, na uuaji?

Hii mijitu imechangia kuathirika kwa afya na maisha ya wengi nchini, na kinachoudhi ni kuwa inaachwa iendelee kutanua na kufanya hujuma hizo. Haya ni baadhi ya matunda ya kuwa na CCM madarakani. Nchi hii iko mikononi mwa CCM. Nawapongeza wana-CCM na vikofia vyao, na magwanda yao ya kijani, kwa kutufikisha hapa tulipo.

Miaka yote iliyopita, nilikuwa najivunia kuwa m-Tanzania, kutokana na kazi kubwa aliyofanya Mwalimu Nyerere. Ilikuwa ni heshima kuwaambia watu popote duniani kuwa mimi ni m-Tanzania. Miaka hii ya leo najisikia aibu kuwa m-Tanzania.

Sunday, August 11, 2013

Afrifest 2013 Ilifana Minnesota

Jana, mjini Brooklyn Park hapa Minnesota, yalifanyika maonesho ya Afrifest. Afrifest ni tamasha linalofanyika mara moja kwa mwaka, likiwajumuisha watu wenye Asili ya Afrika na wengine wowote wale, kwa lengo la kufahamiana, kujielimisha, na kujipatia burdani mbali mbali. Watu wa kila aina walishiriki, wazee, vijana, na watoto.

Hapa kushoto tunawaona watoto wakiwa na mpiga ngoma maarufu hapa Minnesota. Aliwaonyesha namna ya kupiga ngoma, na pia aliwaelezea maana na matumizi ya ngoma katika tamaduni za Afrika.










Watu walikuwa wameambiwa kuwa tamasha lilipangiwa kuanza saa sita mchana. Kuanzia hapo watu walikuwa wanafika, kwa wakati wao.

























Vijana kutoka benki ya Wells Fargo walifanya kazi nzuri ya kujitolea, kuwahudumia waliohudhuria. Walikuwa wamevalia tisheti nyekundu.













Hapa ni banda ambapo watu walikuwa wanajipatia chakule. Wahusika wanajua sana kuandaa vyakula, kama vile wali na kuku.











Siku nzima, kulikuwa na muziki kutoka sehemu mbali mbali za Afrika. Vibao vya akina Diamond na Mr. Nice kutoka Tanzania vilisikika.














Hapa naonekana kwenye meza yangu nikiwa na vitabu vyangu. Nimekaa na mdau wangu wa siku nyingi, Ndugu Nyangweso.

Mimi kama mwalimu, mchango wangu mkubwa katika siku ya Afrifest ni kuelimisha umma kuhusu historia na masuala mbali mbali ya watu wenye asili ya Afrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika, hadi himaya mbali mbali zilizojitokeza Afrika, biashara ya utumwa ndani na nje ya Afrika, ukoloni, harakati za uhuru, changamoto za leo na fursa za siku za usoni.




Yapata saa 10 na nusu alasiri, kama taarifa zilivyokuwa zimeelezea, Mheshimiwa Al Franken, seneta kutoka Minnesota, alijitokeza kwenye tamasha. Kulitokea msisimko mkubwa, kwani kila mtu alitaka kumsalimia na kuongea naye. Picha nyingi zilipigwa, ambazo ni kumbukumbu nzuri.

Friday, August 9, 2013

Afrifest 2013, Minnesota

Kesho, Agosti 10, ndio ile siku ya tamasha la Afrifest hapa Minnesota. Ni tamasha linalofanyika mara moja kwa mwaka, kwa lengo la kuwakutanisha watu wenye asili ya Afrika na wengine pia. Afrifest ni fursa ya kufahamiana, kuelimishana, na kuburudika na maonesho mbali mbali ya michezo na tamaduni.

Kwa taarifa zaidi kuhusu tamasha la kesho, angalia tangazo nililobandika hapa. Pia soma nilivyoandika katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Kama una watoto, na unakaa maeneo haya ya Twin Cities, jiulize watoto hao wana fursa zipi za kupanua mawazo ili wawe raia wa dunia ya utandawazi wa leo. Unawaandaa vipi waweza kuwa na uzoefu wa kufanya kazi na kushirikiana na watu wa mataifa na tamaduni mbali mbali.

Ni wazi kuna vitu vikubwa ambavyo mzazi unaweza kufanya kwa lengo hilo. Lakini vile vile, kuna vitu kama haya matamasha ambayo yanachangia. Mimi kama mtafiti, mwalimu na mwandishi nahudhuria Afrifest kila mwaka. Napata fursa ya kufahamiana na watu, kukutana na wale ambao tunafahamiana, kuongelea shughuli zangu, na kuonesha vitabu na machapisho yangu mengine.

Kati ya vivutio vikubwa vya kesho ni kuwa Seneta Al Franken wa Minnesota atatembelea Afrifest yapata saa 10:30 alasiri hadi saa 11:00. Hiyo ni fursa ya nadra ya kuonana na mtu wa hadhi kama yake katika serikali ya Marekani.

Sunday, August 4, 2013

Mapendekezo ya Mwigulu Nchemba Kuhusu Ajira kwa Vijana

Jana, kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mwigulu Nchemba ametoa mapendekezo kuhusu ajira, ambayo anasema atayawasilisha Bungeni kama hoja binafsi:

Habari vijana wenzangu, Nategemea kupeleka HOJA BINAFSI BUNGE LA 26 AUGUST 2013 KUHUSU AJIRA KWA VIJANA.

HINTS,
1) Kuitaka Serikali iitishe sensa ya wahitimu wote wa fani zote na ifanye uchambuzi wa ikama ya utumishi katika wizara, idara, mikoa, halmashauri- serikali za mitaa, na mashirika yake ya Umma. Lengo ni kujua idadi ya wahitimu wasio na kazi na nafasi zilizowazi. Utafiti wangu ni kwamba KWA UPANDE WA SERIKALI;

(A) KILA OFISI ya serikali INASHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE ipasavyo KWA AJILI YA UPUNGUFU WA WATUMISHI, HAKUNA OFISI IMETIMIA WATUMISHI
(B) KUNA WATU WENGI SANA WANAKAIMU NAFASI MPK WENGENE WANAKAIMU NAFASI ZILIZOKUWA ZINAKAIMIWA yaani KAIMU KAIMU AFISA UTUMISHI NK NA NAFASI YAKE HIVYO HIZI NI tatu nafasi kwa mtu mmoja
(C) KUNA WATU wanapewa ajira za mikataba na WANAONGEZEWA MIKATABA KWA KIGEZO KUWA HAKUNA MTU ANAYEWEZA KUZIBA NAFASI HIYO au hakuna mwenye uzoefu.

KWA UPANDE WA PILI SASA WA WAHITIMU;

(1) KILA MTAA KUNA KIJANA AU VIJANA WAHITIMU WANA MIAKA 2 HADI 5 HAWANA KAZI WANAZUNGUKA NA BAHASHA MPAKA SOLI ZA VIATU ZINAKWENDA UPANDE
(2) KILA MTAA VIJANA WAPO WAKIOMBA KAZI WANAAMBIWA HAWANA UZOEFU wa 2 or 3 yrs, Au anayetakiwa awe na 4yrs experience hata katika ngazi za ofisa wa ngazi za kuanzia ilihali hakuna chuo kinafundisha uzoefu
(3) Vijana wapo na diploma hawajulikani walipo kwa Serikali na wamekaa miaka 2 hadi 5 na diploma zao wanasubiri kazi. kipindi ambacho angewezeshwa kwenda shule angeshavuka diploma na degree angekuwa hata na master.

Kufuatia hali hii
(i) vijana wanaitwa bomu ili hali VIJANA NI NGUVU KAZI YA TAIFA
(ii) Vijana wana stress, wamekata tamaa hawaoni future na wengine wanahasira sana
(iii) Vijana wahitimu wanatunzwa na wazee ambao hawakwenda shule hivyo kuwa mzigo kwa wazazi.

Lengo ni kuitaka serikali ikishajua idadi ya wahitimu na ikama yake cos ofisi ziko wazi mlioko ofisini mkisema ukweli msiogope mabosi wenu mtakiri hili

(1) Serikali ifanye re allocation ya vijana kwenye nafasi za kazi kufuatana na ujuzi wao,
(2) Serikali ianze kufanya attachment kwa vijana wapate uzoefu maofisini na hata kuwalipa half a saraly of a full employed officer ili kuondokana na tatizo la kukosa uzoefu kwa kijana aombapo kazi.
(3) Vijana wawe tayari kujitolea kulipwa hata half a saraly ili wapate uzoefu
(4) Uwezo wa kazi na marks za kwenye vyeti ni vitu viwili tofauti, serikali ikiwa attach ofisini vijana itajua uwezo wao itaacha kuongezea wastaafu mikataba kwa vigezo kuwa hakuna mwenye uwezo wa kuziba nafasi hiyo
(5) Serikali ibane matumizi yake ili itenge fedha ya kuendeleza wahitimu. Mtu mwenye diploma kusubiri kazi miaka 5 ni kipindi angeweza kuwa na degree na masters yake.
Baadhi sehemu za kukata matumizi ya serikali bila kuathiri kazi za serikali ni kwenye magari na mafuta ya magari. Unakuta bosi anakaa bunju halafu dreva gongolamboto halafu ofisi posta, au bosi kiluvya dreva mbagala ofisi posta kila siku trip hizo, pia training nje ya nchi kwa mtu mwenye 59yrs nakutumia milions and milions zisitishwe ili tuandae generetion ya kupokea majukumu.
Pia serikali ikishajua waliopo pia iandae projection ya tunakoelekea in three to five yrs hali itakuwaje na serikali inampango gani. Cos maisha bora yanaletwa na KAZI.
SERIKALI IKISHAJUA IWEKE BAJETI AMA YA GUARANTEE AU YA KUFUFUA VIWANDA VYOTE VILIVYO LABOUR INTENSIVE ili kuchukua vijana wahitimu na wa mtaani. SENSA HII SIO GHARAMA NI KUWATANGAZIA TU WAHITIMU WAKAJIANDIKISHE KTK OFC ILIOKARIBU AU KUPELEKA CV kwa DC the cv zinachambuliwa.

This is a rough idear. You can add or improve.

VIjanaaaaaaaa, itikieni NGUVU KAZI YA TAIFA

********************************************************************
Nami nimemjibu katika ukurasa huo huo wa Facebook kama ifuatavyo
:


Kwanza kabisa, andika ki-Swahili ipasavyo, sio kuchanganya na maneno ya ki-Ingereza, kama ufanyavyo. Tunapaswa kuonyesha kuwa tunaiheshimu lugha yetu. Kiswahili kinajitosheleza, sawa na lugha zingine. Lugha ni kioo cha nafsi na upekee wa jamii au taifa. Kuiheshimu lugha ni dalili ya kujiheshimu.

Hasa kwa mtu anayehesabiwa kuwa ni kiongozi, sherti kuonyesha mfano katika hili. Kama kiongozi unashindwa kuonyesha heshima kwa lugha yetu, unashindwa kuonyesha heshima wa utambulisho huu wa Taifa letu, ni kiongozi gani, na unawafundisha nini watoto wetu?

Ujumbe wako kuhusu ajira unapwaya sana. Hujaweka suala hili katika mkabala wowote, wala hujalifanyia utangulizi unaoonyesha kuwa unaelewa historia na upana wa suala hili. Hata dhana yenyewe ya ajira unayotumia ni finyu. Papo hapo unadai kuwa umefanya utafiti. Ni ajabu.

Hujazingatia tulikotoka, kwa Mwalimu Nyerere, ambaye aliongelea masuala haya ya ajira. Aliongelea masuala ya elimu kwa vijana, akisisitiza kuwa tuwape elimu ya kujitegemea. Inaonekana hujasoma lolote kuhusu mawazo ya Mwalimu Nyerere juu ya suala hili la elimu ya kujitegemea.

Ungefanya utafiti kuhusu kinchoendelea duniani, angalau ungegundua kuwa katika dunia ya leo, watu huongelea umuhimu wa kutoa elimu kwa vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri, kujitengenezea ajira.

Hilo hujataja, na haionekani unalifahamu. Wewe unaongelea ajira serikalini. Dhana hiyo, ingawa ilikuwa na mantiki kubwa miaka ya zamani, inapitwa na wakati. Na wewe kama kiongozi, ulipaswa utambue hilo, ili uweze kutoa ushauri mwafaka kwa hao vijana.

Unajiita kijana, lakini mawazo yako ni yale yaliyokuwa yanakubalika karne iliyopita, sio mawazo ya karne ya 21. Katika karne ya 21 kuwajengea vijana dhana kuwa waelekeze nguvu katika kutafuta ajira serikalini ni upotoshaji. Hii dhana kwamba Tanzania inahitaji viongozi vijana ni upuuzi, kama vijana wenyewe ni akina Mwigulu Nchemba. Hawafai kuongoza, kwa sababu hawajui dunia ikoje na inakwenda wapi.

Ingekuwa Mwigulu Nchemba unajua dunia ya leo ikoje na inakwenda wapi, kuhusu hili suala la ajira, ungefahamu kuwa sekta inayokuwa kwa kasi kuliko zote hapa duniani ni utalii. Hujataja jambo hilo, ambalo liko wazi miongoni mwa wote wanaofuatilia maendeleo ya uchumi na ajira katika karne hii.

Sekta ya utalii ndio inayokua kwa kasi kuliko zote, na ndio inayoleta matumaini ya kutoa ajira nyingi kuliko hiyo serikali ambayo ndio msingi wa mapendekezo yako.

Kama mtu unataka kutoa mchango katika suala la ajira kwa vijana, ni muhimu sana kuwafungua macho kuhusu sekta hii ya utalii, na jinsi ya wao kujiandaana kujipanga kunufaika na sekta hii.

Sisemi kuwa suala la ajira serikalini lisahauliwe. Lakini ninachosema ni kuwa tuwe na upeo mpana, upeo wa kuelewa hali halisi ya dunia ya leo. Tuwe pia watu ambao tumesoma yale aliyosema Mwalimu Nyerere kuhusu elimu ya kujitegemea.

Mwigulu ukiwa ni katibu mwenezi, nilitegemea unaeneza mawazo thabiti ya kuliendeleza Taifa. Lakini naona unaeneza mawazo rejareja, baadhi yakiwa yamepitwa na wakati. Mtu kama wewe hufai kuwa kiongozi. Wala usije ukadhani mimi ni CHADEMA. Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nawashuhudia CCM mnavyojikanyaga.

Ninapenda kusema neno moja zaidi kuhusu Nyerere. CCM mmemsaliti Mwalimu Nyerere. Yeyote anayesoma "Azimio la Arusha" na maandishi mengine ataliona hilo. CCM ni chama kinachohujumu mapinduzi aliyoyawazia Mwalimu Nyerere.

Ungemsoma Mwalimu Nyerere, ungefahamu kuwa alikuwa anakazana sana kuleta mapinduzi vijinini, ili kuwe na fursa za kiuchumi na ajira, na hivi kupunguza ndoto ya vijana kuhamia mijini. Wewe andiko lako lote kuhusu ajira unawaelekeza vijana waende katika ajira za serikali. Ni kuwavutia waende mijini. Hujasema lolote kuhusu kuboresha maisha ya vijijini, uchumi wa vijijini, na ajira huko huko vijijini.

Kwa kumalizia, ningependa kujua iwapo Mwigulu Nchemba unasoma vitabu vyovyote. Ningependa kujua kama una vitabu nyumbani kwako. Ningependa kujua iwapo tangu mwaka huu uanze hadi leo, umesoma vitabu vingapi.

Saturday, August 3, 2013

Tundu Lissu: Pigeni Kelele Kuokoa Watanzania

Lissu: Pigeni kelele kuokoa Watanzania
Penulis : mtandao-net on Saturday, August 3, 2013 | 10:09 PM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeutaka umoja wa vijana wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IYDU) kupiga kelele kote duniani ili kuwanusuru Watanzania wanaouawa hovyo kwa sababu za tofauti za siasa hapa nchini.

Akizungumza na uongozi wa umoja huo (IYDU) jijini Dar es Salaam wiki hii, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni Tundu Lissu alisema ni wakati wa vijana kuwaokoa wenzao wa Tanzania ambao kujiunga kwao na siasa kumesababisha wachukiwe na watawala.

“Watu wanauawa hadharani na hakuna hatua zinazochukuliwa…nendeni katika nchi zenu katika mabunge yenu mkapige kelele katika haya yanayotokea Tanzania; inaweza kusaidia na mkawa mmewasaidia Watanzania,” alisema Lissu. Tundu Lissu alisema viongozi wengi wamekamatwa na kufunguliwa kesi nyingi mahakamani, na hivyo kuifanya CHADEMA kuwa katika wakati mgumu kuliko mwingine wowote katika uendeshaji wa siasa za vyama vingi hapa nchini.

Chama hicho kimedai kuwa hali ya kisiasa hususan kwao na baadhi ya wapinzani nchini ni ngumu, kutokana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na serikali kwa kutumia vyombo vya dola.

Lissu alisema viongozi wa upinzani wamefunguliwa kesi za ugaidi kwa lengo la kuwafanya watumie muda mwingi katika kesi hizo, badala ya kuishughulikia serikali pale inaposhindwa kutimiza wajibu wake.

Mbali na kesi hizo, kumekuwa na matukio ya kikatili ya kuteka, kutesa na hata mauaji dhidi ya watu wanaoshabikia upinzani na wale wanaoikosoa serikali katika mambo ya msingi na yenye maslahi ya nchi.

Lissu amesema wabunge wa CHADEMA licha ya uchache wao, wakiwemo baadhi wa vyama vingine vya upinzani, wamejitahidi kupambana bila woga bungeni kutetea wananchi lakini wamekuwa wakizidiwa na wingi wa wenzao wa CCM, ambao wamekuwa wakipitisha maamuzi mengi ya hovyo na yasiyo na manufaa kwa nchi.

Mapema akiwaaga vijana hao, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, amewataka vijana kutokata tamaa kutokana na mambo yanayotokea nchini.

Mbowe alisema CHADEMA haitarudi nyuma katika harakati za kutwaa madaraka ya dola hata kama watawala waliopo madarakani hawapendelei nafasi zao kuwaponyoka.

“Tunafahamu katika siasa kuna magumu mengi lakini niwahakikishieni kuwa ninyi mna nafasi kubwa ya kuleta mageuzi sehemu yoyote kama mtakuwa na dhamira na kuvishinda vitisho mbali mbali dhidi yenu,” alisema Mbowe.

Katika ziara yao hapa nchini vijana hao wa IYDU walitembelea ofisi mbali mbali ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje na ubalozi wa nchi za Ulaya nchini (EU).

Mkurugenzi wa masuala ya Mashariki ya Mbali, Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Simba Yahya, alikiri kuwa watumishi wa umma wanashindwa kutofautisha utendaji wa serikali na chama kilichoko madarakani.

“Itachukua muda kwa wafanyakazi kutenganisha hali hii….. kiuhalisi wanatakiwa wawe watendaji kwani wapinzani wa leo wa serikali ndio wanaweza kuwa mabosi wao wa kesho,” alisema Yahya.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...