Thursday, September 12, 2013

Wa-Tanzania Tusiwachokoze Wanya-Rwanda

WaTanzania tunapaswa kuwa waangalifu sana tunapoongea na Wanya-Rwanda au tunapowaongelea. Hao ni watu ambao wamepitia majanga ambayo waTanzania hatuwezi hata kufikiria.

Wengi wao wameshuhudia ndugu, jamaa, marafiki wakiuawa kikatili. Wengi wameshuhudia familia yao yote ikichinjwa kwa mapanga. Wengi waliachwa wakiwa wakiwa tangu utotoni. Majanga yaliyowapata, sisi waTanzania hatujawahi kushuhudia katika maisha yetu, na hata tukijaribu kufikiria, tutakuwa tunaelea hewani tu. Undani wake na ukweli wake hatutaweza kuuelewa.

Wa-Tanzania tunashangaa kwa nini wanya-Rwanda wamepandisha jazba sana kutokana na ushauri wa Rais Kikwete kwamba wafanye mazungumzo na wapinzani wao walioko Kongo. Hatuelewi kwa nini ushauri uliotolewa kwa nia njema, kwa vigezo vyetu, umewatibua kiasi hicho. Wa-Tanzania wengi wameamua wanya-Rwanda wamevuka mpaka katika msimamo wao.

Ninaamini wa-Tanzania tunakosea katika kudhani hivyo. Angalia Israel. Mauaji ya kimbari yaliyowapata wa-Yahudi miaka ya elfu moja mia tisa arobaini na kitu hawajasahau hata chembe. Na mtu asithubutu kuwagusa kwa hilo; atatonosha vidonda na kuamsha jazba kali kuliko maelezo.

Hapa Marekani, kwa mfano, kila mtu, kila kiongozi wa serikali, anaogopa kulipuuzia au kulifanyia mzaha tukio la mauaji yale ya kimbari. Hakuna anayethubutu kuwashauri wa-Yahudi wafanye mazungumzo na yeyote ambaye ni mhusika au mtetezi wa mauaji yale. Hakuna mtu anayeweza kushinda urais hapa Marekani kama hathibitishi wazi wazi kuwa atasimama sambamba na Israel kama rafiki.

Wa-Yahudi waliunda kitengo cha utafiti cha Simon Wiesenthal, ambacho kazi yake kubwa ni kuwasaka na kuwanasa wote waliohusika na mauaji yale. Kitengo hiki kimefanya kazi sana na kinaogopwa kwa umakini wake katika kuwasaka na kuwanasa watuhumiwa popote duniani. Hisia za wa-Yahudi kuhusu mauaji ya kimbari yaliyowapata, ni kama vile yalitokea mwaka uliopita.

Ingawa wanya-Rwanda hawajaunda kituo kama hiki cha Simon Wiesenthal, sina shaka kwamba hisia zao ni sawa na zile za wa-Yahudi. Ni kitulizo cha aina fulani kwamba mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari imesaidia na inaendelea kusaidia kufanikisha jukumu la kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wahusika au watuhumiwa wa mauaji ya kimbari.

Nimeona nitumie mfano huu wa wa-Yahudi, ili kufafanua ushauri wangu kwamba wa-Tanzania tuwe waangalifu sana tunapoongea na wanya-Rwanda.  Kitu tunachokiona sisi ni kidogo, kwao ni janga la kutisha kuzidi jinamizi lolote. Tahadhari hii inapaswa izingatiwe hasa na vyombo vyetu vya habari.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...