Wednesday, November 13, 2013

Kitabu Kinapendwa

Tangu nichapishe vitabu vyangu mtandaoni, ninaweza kufuatilia mauzo kila siku. Nimefungua duka mtandaoni, na nimetoa ushauri kwa waandishi wengine, hasa wa-Tanzania, kuhusu uzuri na ubora wa tekinolojia hii.

Ushauri wangu nimeutoa katika kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Lakini inaeleweka kuwa ukiwa na wazo ukaliweka kitabuni, usitegemee kama wa-Tanzania wataliona. Huu ni ukweli ambao umesemwa tena na tena. Nami sidhani kama nina la kuongeza. Papo hapo, falsafa yangu ni kuwa ukiwa na jambo la manufaa, waeleze wengine.

Kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ndicho chenye mauzo kuliko vingine vyote. Kila ninapoona kimenunuliwa, najiuliza ni nani huyu aliyenunua. Pengine inakuwa ni nakala moja, lakini pengine ni nakala za kutosheleza darasa. Nami sijui ni nani kaagiza. Hiki kitendawili kinanifanya niwe na dukuduku, na nafahamu kuwa sitapata jawabu.

Kuna wakati zinapita siku nyingi kidogo bila mtu kukinunua, lakini wakati mwingine hali hubadilika ghafla. Kwa mfano, Oktoba 31, niliona mtu kanunua nakala 51. Laiti ningemfahamu. Ningempelekea barua ya shukrani na pia nakala ya bure kama kifuta jasho. Lakini simjui. Ni kitendawili.

Namshukuru Mungu kwa jinsi alivyoniwezesha kuandika na kuwagusa walimwengu kiasi hicho. Yote ni uwezo wake.


Saturday, November 9, 2013

Nimenunua "Nomad," Kitabu cha Ayaan Hirsi Ali

Miaka kadhaa iliyopita, nilianza kusikia jina la Ayaan Hirsi Ali, mwandishi kutoka Somalia, ambaye alikuwa ameikimbia nchi yake na alikuwa anaishi Uholandi, ambako alifanikiwa hata kuwa mbunge. Ilionekana ni mwandishi mkorofi, kwa maana ya kwamba wengi walikerwa na kukasirishwa alivyokuwa anahoji utamaduni wa wa-Somali na u-Islam, hasa kuhusu masuala ya haki za wanawake.

Nilisoma kuhusu kitabu chake Infidel, ambacho kilisemekana kiliwakasirisha wa-Islam wengi. Nilikuwa na dukuduku ya kusoma maandishi yake, lakini, kutokana na majukumu mengi, sikufuatilia.

Hata hivi, nimezingatia ukweli kuwa, kuliko kutegemea ya kuambiwa, muhimu mtu kujisomea mwenyewe. Leo nimenunua kitabu cha Ayaan Hirsi Ali kiitwacho Nomad. Ingawa ninasoma vitu vingi kila siku, nitakipa kitabu hiki kipaumbele. Wakati huo huo, nitanunua vitabu vyake vingine. Insh'Allah, nitapata wasaa wa kuelezea nawazo yake.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...