Monday, November 16, 2009

Ziara Katika Shule ya Sayansi ya Mazingira

Kwa miaka yapata kumi, nimekuwa nikialikwa kila mwaka kwenda kwenye shule ya sayansi ya mazingira mjini Apple Valley, Minnesota, kutoa mhadhara kwenye somo la falsafa za jadi na mazingira.Mimi kama mtafiti wa masomo yahusuyo masimulizi na falsafa za jadi na utamaduni kwa ujumla, nimetumia fursa hii kuwaeleza wanafunzi namna binadamu, tangu mwanzo wake hapa duniani, alivyoweza kuyatafakari, kuyatathmini na kuyaelezea mazingira. Tangu enzi za mwanzo binadamu aliunda lugha kama chombo mahsusi cha kumwezesha kufanya yote hayo. Uundaji wa lugha halikuwa jambo rahisi, tangu kuvipa majina viumbe na vitu vyote vilivyomzunguka hadi kusema na kuelewana na binadamu wengine.

Kila mwaka, mwalimu Todd Carlson, ambaye amekuwa akinialika, anawaelezea wanafunzi kuhusu utafiti wangu juu ya fasihi simulizi na falsafa za jadi, na anawasomesha kitabu changu cha Matengo Folktales. Hadithi, nyimbo na semi ni baadhi ya mikondo aliyotumia binadamu kuyaelezea mazingira yake na kukidhi duku duku ya akili yake kuhusu yote yaliyomzunguka. Historia ya binadamu imeenda sambamba na upanuaji na utajirishaji wa urithi huo. Hakuna kitu wala kiumbe ambacho binadamu hakukipa angalau jina. Jina ni simulizi ambalo linapambanua kitu au kiumbe kimoja na kingine. Kutoka kwenye kiwango cha majina, binadamu ametunga hadithi, nyimbo, na semi kuhusu misitu, wanyama, ndege, maporomoko ya maji, tufani, ukame, na kadhalika. Hadithi, nyimbo, na semi hizo zimeelezea pia mahusiano ya binadamu na yote hayo. Kuna pia maombezi na matambiko, na njia zingine za kumsaidia binadamu kukabiliana na mazingira na hali mbali mbali za maisha.Mwalimu Carlson anaonekana katika picha hapo juu upande wa kulia kabisa, akiwa ameweka mkono kiunoni. Wanafunzi wa shule hii wanajifunza mambo ya msingi yanayohusu mazingira na namna ya kuyahifadhi. Wanapata fursa ya kutembelea nchi za nje pia, kujifunza.
Katika kutembelea kwangu shule hii nimeona jinsi wanafunzi walivyo makini na wenye duku duku ya kujua mambo. Ni wanafunzi hodari kabisa. Kila ziara imekuwa ya kuridhisha sana. Taarifa na picha hizi zinatokana na ziara yangu ya tarehe 10 Novemba, 2009.

3 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Sawa. Nami nikipata muda pengine siku moja nitaweza kuandika kitabu juu ya visa asili vya Kisukuma. Najua kwamba katika utafiti wako ulifika mpaka nyumbani Ntuzu kule Gabu ambako shujaa wetu Sita aliwapiga chenga Wamasai kwa kuwageuza ng'ombe na kuwa mawe. Bado kuna Ng'wanamalundi na mengineyo mengi tu. Mambo haya yanapotea kwa kasi sana na bila kuyaweka katika maandishi basi tutayapoteza. Muda ukifika nitaomba msaada wako.

Mbele said...

Ni kweli, nimeshafika Gabu mara kadhaa kwenye utafiti wa masimulizi ya Wasukuma na vipengele vingine vya utamaduni wao. Hapo Gabu nilishasikiliza masimulizi ya Sitta Nindwa, na Wamasai. Kwenye makaburi ya Sitta na mkewe nimefika. Kwenye miamba nimepanda na kuona mambo kadha wa kadha yanayohusiana na habari zao.

Nimefanya hivyo sehemu mbali mbali za Usukumani, nikitafuta habari za watu wengine maarufu, kama vile Ng'wanamalundi na Gindu Nkima na Ibambangulu. Ibambangulu alikuwa na uwezo wa kujitanua akawa mkubwa hadi kujaza chumba. Lakini aliuawa kwa kudonolewa na kuku.

Ni hazina ya elimu ambayo tunapaswa kuifundisha mashuleni, na tunapaswa kuifanyia mkakati iwekwe katika utalii, na wanavijiji wawe ndio waongozaji wa mradi huu wa kuwaelimisha watalii.

Katika maandishi yangu, ninajaribu kuwahamasisha waTanzania watambue umuhimu wa utafiti wa aina hii katika kuboresha utalii, na vile vile ninawahamasisha watambue umuhimu wa vitabu, kwa lengo hilo hilo la kuboresha utalii. Kwa mfano, nimewahi kuandika kwamba tungekuwa tunasoma vitabu kama vya Shaaban Robert na kufanya utafiti kuhusu maisha yake, tungeweza kuingiza elimu hii katika kuifanya miji alimoishi iwe sehemu za utalii, kama vile Pangani, Mpwapwa, na Longido.

Lakini waTanzania kwa ujumla ni wavivu kupindukia. Wameshaua kitu kinachoitwa elimu. Kilichobaki sasa ni ubabaishaji, sherehe, ulabu, na mashindano ya urembo yanayotumia vigezo vya ughaibuni. Nchi yetu iko gizani na inazidi kutokomea humo gizani. Kwa mwendo tunaokwenda, Taifa la kesho litakuwa kichekesho duniani.

Lakini sisi ambao tunaotambua janga hili tukishirikiana tunaweza kusaidia kuokoa jahazi. Naafiki wazo lako la kusaidiana katika suala hili.

Naleta hapa picha nilizopiga kule Gabu na sehemu zingine. Ukibofya kwenye picha zilizopo upande wa kushoto, zinajitokeza zikiwa kubwa zaidi. Bofya hapa

Unknown said...

Nijambo Jema Wekeni Kwenye Vitabu Watanzani Wengi Wapate History

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...