Wednesday, March 10, 2010

Mteja Anapofurahi

Leo mama moja Mmarekani ameniandikia ujumbe kwenye ukurasa wangu wa Facebook. Anaelezea kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans, na jinsi kilivyomsaidia alipokuwa Afrika Mashariki:

I remember being glad I had read it. Observations from someone who has lived in both Minnesota and East Africa, and a scholar no less, were a lot more insightful than my Lonely Planet.

Ni faraja kwangu kupata maoni ya wasomaji. Ni furaha kuwasikia kuwa wameridhika. Niliandika kitabu kwa sababu niliona kuna tatizo duniani lililohitaji ufumbuzi, tatizo la maelewano baina ya watu wa tamaduni mbali mbali. Lengo langu halikuwa kujipatia pesa. Hii Lonely Planet anayoitaja ni kampuni maarufu inayochapisha vitabu kwa ajili ya wasafiri. Vitabu hivi vinaelezea taarifa za nchi mbali mbali. Basi, nimetabasamu kusoma kauli ya huyu mama, kuwa kitabu changu ni tishio kwa Lonely Planet. Wakae chonjo.

Ni kweli kuwa watu wananunua kitabu hiki. Na mimi nazingatia hilo. Lakini jambo la msingi zaidi kwangu ni kuwa mteja aridhike. Asione kuwa alipoteza hela zake au kitu alichonunua hakikumridhisha. Mteja anapofurahi kama huyu wa leo, nami nafurahi.

Mara kwa mara, huwa naalikwa kwenda kutoa mihadhara kuhusiana na kitabu hiki au maandishi yangu mengine. Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, wanaonialika wananiuliza gharama ya mihadhara yangu ni kiasi gani.

Ningekuwa mtu ninayeweka pesa mbele, ningesema hii ni fursa yangu ya kuwakomoa na kutajirika. Lakini mimi, pamoja na mahitaji mengi ya pesa ambayo sote tunayo, siwezi kufanya hivyo. Kwa nini nifanye jambo ambalo haliendani na dhamiri yangu? Sipendi makuu, na sikulelewa katika mkondo wa kujilimbikizia utajiri.

Ninaridhika na malipo ya wastani. Vile vile, hata kama taasisi au jumuia inayonialika haina pesa, mimi huwa naenda kuwapa mhadhara. Akili niliyo nayo nilipewa na Mungu, haikuwa haki yangu, wala siwezi kujivunia. Nina wajibu wa kuitumia kwa manufaa ya wanadamu, si kwa manufaa yangu binafsi. Ninaamini kuwa nikifanya ubinafsi, Mungu anaweza kuninyang'anya.

Furaha ya mteja ni malipo tosha kwa juhudi zangu, na ni njia ya kumtukuza Mungu aliyenipa uwezo.

9 comments:

Fadhy Mtanga said...

Prof. Mbele hakika wastahili pongezi kwa moyo huo. Hapa nyumbani wasomi wametokwa kabisa na moyo huo. Ili wapate pesa zaidi wameziasi hata taaluma zao na wanapigana vikumbo katika mtanange wa Oktoba 25.
Narudia kukupongeza.
Uandishi wako ni tunu kwa jamii yetu.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Wow!!! Kuna kipindi hapa tulijaribu kumwalika Ngugi wa Thiong'o kuja kutoa mhadhara. Gharama ilikuwa ni dola 35,000 na hata kuongea naye haikuwezekana. Tuliongea na ajenti wake tu. Mkutano ulikuwa juu ya Fasihi ya Kiafrika na mwelekeo pamoja na dhima yake katika zama hizi za utandawazi. Kwa sisi Waafrika tulishangazwa na jambo hili kwani pengine mtu ungeweza kudhani kwamba kwa kuwa huyu ni Mwafrika mwenzetu pengine angeweza hata kujitolea au kupunguza gharama kidogo. Ndiyo roho ya ubepari hii, inafukuza ubinadamu na ikishakuingia basi kila kitu kinageuka na kuwa biashara.

Mwaka fulani pia tukamwalika Profesa Herman Batibo kutoka chuo kikuu cha Botswana kuja kutoa mhadhara hapa. Naye kama wewe, japo ni maarufu sana, alikuwa tayari kuja kutoa mhadhara wake hata bure kama tusingekuwa na pesa za kumlipa. Tulivutiwa mno na moyo huu kwani ni watu wachache sana ambao wamejaliwa kuwa nao.

Asante Prof. kwa moyo huu na kama nilivyogusia katika post yangu niliyoiweka hapa:

http://matondo.blogspot.com/2010/02/siku-niliyokutana-na-ubinadamu-wa-kweli.html

ni matendo kama haya ambayo hasa yanaupambanua ubinadamu wetu; na yanaweza kubadilisha na kuacha athari chanya za kudumu kwa binadamu wenzetu tunaokutana nao!

Subi Nukta said...

Nadhani kitendo cha mimi kuweka kitabu hiki katika ukurasa wa mwanzo kabisa pale wavuti.com kinadhihirisha ni kwa kiasi gani nimeridhishwa na kuukubali wajihi wako katika ngazi si tu ya taaluma bali hata kimaisha. Unavyoishi maisha (approach to life) unanifunza mengi sana Prof pamoja na wengine wengi.
Nimejifunza mengi sana kutoka kwa wanye blogu mbalimbali Watanzania wanaoishi ndani na nje ya nchi na bado ninaendelea kujifunza.
Salam na heshima kwako Fadhy na Prof. Masangu.

Mbele said...

Ndugu Mtanga, shukrani kwa ujumbe wako. Tangu nilikozaliwa na kusoma shule ya msingi na hadi nasoma Chuo Kikuu Dar, kuanzia mwaka 1973 tulikuwa na walimu waliozingatia maadili ya kazi na kutuonyesha njia ipasayo.

Nina bahati pia kuwa nilisikia mwito wa Mungu, tangu nilipokuwa mtoto mdogo, wa kuwa mwalimu. Kazi ya ualimu sikuichagua, bali nilipewa na Mungu.

Sasa, ujuavyo, mtu akishaamini hivyo, sio rahisi kuyumbishwa na lolote. Siwezi kutumia wadhifa wangu wa ualimu kwa njia inayokiuka maadili yake, wala siwezi kukaa mahali nimevaa kofia ya ualimu, kumbe nafanya vitu vingine.

Matokeo ya msimamo huu ni kuwa nina raha na utulivu katika maisha yangu. Basi, ninapokuwa Tanzania, huwa naongea na vijana humo mitaani na vijijini, kuwapa ushauri kwa mujibu wa mtazamo wangu, wawe na malengo na juhudi, badala ya kuhangaika na mambo yanayopita.

Mbele said...

Dada Subi nakushukuru kwa ujumbe wako. Ninavyoangalia jinsi unavyouenzi mchango wangu. Ni heshima kubwa kwangu kuona unavyokitangaza kitabu kile. Imani kama yako juu yangu ni changamoto, kwani nawajibika kufanya juhudi zaidi.

Nami nakushukuru kwa jinsi unayotugawia ujuzi na uzoefu katika shughuli hizi za kublogu na mengine.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

unafanya hayo kwa kuwa tu unaogopa Mungu asikunyanganye akilizako??

kama ni hivyo jua tu atakunyanganya kwa kuwa utuazeeka na akili zichoke uwe zezeta au utakufa na akili hizo zitazikwa

kwa hiyo inabidi kufanya hilo kwa sababu nyingine na si kuofia Mungu aikunyanganye akili zake!!

yawezekana sio za mungu pia kwani yawezekana hakukuumba ili ujifunze uliyojifunza, ni fursa tu kufuatana na hitaji la mfumo wa kibepari ambao ni kinyume na Mungu

Mbele said...

Ndugu Kamala, shukrani kwa mchango wako. Ukweli ni kuwa sisi binadamu tuna mengi. Tunafanya mambo kwa misukumo au sababu mbali mbali, kama vile uzalendo, mapenzi kwa wanadamu wenzetu, ubinafsi, woga, kujitafutia umaarufu, kujipendekeza, au, kwa sisi tunaoamini Mungu, tunaweza kufanya mambo kwa kuogopa kwenda jehenamu, au kuwania kwenda mbinguni. Tunaweza kufanya wema au ukarimu kwa binadamu wenzetu kwa maslahi haya binafsi ya kujitengenezea njia ya kwenda mbinguni.

Lakini, naamini Mungu hadanganyiki. Atatumulika tu, kama hatuna upendo wa kweli kwa binadamu wengine bali tunawatumia kama ngazi ya kufikia mbinguni.

Tukirudi kwa upande wangu, nami nina yangu. Kwa hakika, ninaipenda kazi ya kufundisha na kuwaeleza wengine yale ninayoyajua. Huwa napata furaha ninapofanikiwa kumfungua akili binadamu mwengine na kisha kumwona amefurahi. Furaha yake inanigusa na kuiburudisha roho yangu, hata kama sipati pesa.

Kwa msingi huu, utaona kuwa kuna ubinafsi fulani, kwani napata furaha kutokana na kuwafurahisha wengine. Lakini nadhani huu ubinafsi ni wa manufaa kwa wote, na nadhani ni jambo jema kuliko pale tunapotafuta furaha yetu kwa kuwakomoa wengine au kuwatia matatani, kwa kuwatapeli na kadhalika.

Kwa vile mimi naamini Mungu, basi hili nililosema, kwamba naogopa uwezo wa Mungu wa kuninyang'anya akili nalo ni jambo linalosaidia kunisukuma katika shughuli zangu. Nimeongea ukweli na uwazi wangu, hata kama inaonekana ni hoja yenye walakini. Binadamu ndivyo tulivyo, ila wengine nadhani wanaogopa kujieleza kiukweli. Mimi siogopi kusema kuwa naogopa Mungu ataninyang'anya akili kama sitaitumia kwa manufaa ya wanadamu.

Ni kweli unavyosema, kwamba kuna kuzeeka na kufa. Lakini, kwa kuzingatia hilo, mimi naona wajibu wangu ni kufanya bidii kila siku kuitumia akili hii, iwe changamoto kwa wanadamu hata nitakapokuwa nimezeeka au nimetoka duniani.

Wanafunzi ninaowafundisha watabaki kama matunda ya akili yangu, na maandishi ninayoandika yatabaki. Leo hii watu bado tunawasikiliza akina Shakespeare au Shaaban Robert au Nyerere, ingawa walishafariki, lakini mawazo yao bado yemeenea duniani na yanafanya kazi. Basi na mimi nataka iwe hivyo. Wakati niko hai nafanya kila ninachoweza ili nitakapoondoka mawazo yangu yawe yanaendelea kuleta changamoto duniani.

Vile vile naafiki wazo lako kuwa huenda hatujui Mungu anataka nini, na labda tunajidanganya tunapodhani kuwa kwa kufanya kitu fulani tunafuata matakwa ya Mungu. Hiki ni kitendawili kwani sisi binadamu hatuwezi kuelewa kikamilifu matakwa ya Mungu, na pengina tunajidanganya tunapodhani tunatekeleza anayotaka Mungu.

Wanaogombana na kuuana katika hizi wanazoita vita za kidini nao wanaamini wanatekeleza matakwa ya Mungu. Hata Tanzania tunayo hii migogoro inayoitwa ya kidini. Ujinga wetu binadamu hauelezeki. Niliwahi kugusia suala hili. Bofya hapa.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

naona umejikita katika suala la Mungu zaidi, labda tunahitaji definition juu ya Mungu nini / nani?

kwa nini tufanye mambo kwa kumuogopa huyo Mungu na si vingibevyo.

japo baadhi ya sababu zako zinakubalika lakini juu ya Mungu na uoga kwake sielewi kwanini, na siju kwa nini hukutaja sababu hizo za msingi zaidi ukataja za Uoga wa akili zako na Mungu

Mbele said...

Mwalimu Matondo, huu mfumo wa Marekani ndio hivyo. Ukishakuwa na wakala, basi viwango lazima vitakuwepo, na ghafla utaona nami nimeshakuwa bidhaa adimu :-)

Kwa sasa najifanyia shughuli zote mwenyewe, ingawa nimesajili kikampuni kiitwacho Africonexion. Kama nitapanua hii kampuni na kuajiri watu na kuwa na ofisi, wakala, na kadhalika, bila shaka sitaweza kuendelea na haya mambo ya kutoa mihadhara kwa bei poa au bila malipo.

Halafu nadhani ni suala la ubepari, kwamba unavyozidi kuwa maarufu, na gharama yako kifedha inapanda. Kama Karl Marx alivyosema, pesa inakuwa ndio kigezo cha umaarufu na thamani ya binadamu, au thamani ya ujuzi wake. Inasikitisha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...