Saturday, October 15, 2011

Tamasha la Vitabu, Minneapolis

Leo, mjini Minneapolis lilifanyika tamasha la vitabu, ambalo hufanyika kila mwaka, mwezi Oktoba. Tamasha hili huandaliwa na jarida la Rain Taxi.










Ingawa kila mwaka, kwa miaka kadhaa sasa, nimeshiriki tamasha hili, kwa maana ya kupeleka vitabu vyangu, mwaka huu nilighilibika kidogo. Nilidhani nimefanya mpango wa kulipia meza, halafu nikaenda Tanzania. Niliporudi kutoka Tanzania, nikagundua kuwa hapakuwa na meza iliyobaki. Mwakani, Insh'Allah, nitakuwa makini zaidi.






Kutokana na kughafirika huko, vitabu vyangu havikuwepo mwaka huu. Hata hivi, nilifunga safari, maili 45, kwenda kuangalia tamasha hili.










Pamoja hali ya uchumi wa Marekani kuwa mbaya miaka hii, na watu wengi kukosa ajira au kuishi katika wasi wasi mkubwa kuhusu hali yao ya uchumi kwa siku za usoni, inashangaza jinsi tamasha la vitabu linavyowavutia. Wanafahamu umuhimu wa vitabu kiasi kwamba wako tayari kusamehe mengi mengine ili hela walizo nazo waje kuzitumia hapa.





Nilifurahi kumwona huyu mama hapa kushoto, Shatona Kilgore-Groves, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Ni mwandishi na mhamasishaji wa elimu katika jamii, hasa wa-Marekani Weusi. Mwaka huu niliandika mapitio ya kitabu chake cha kwanza. Soma hapa.







Niliangalia jinsi watu walivyokuwa wanavichambua na kuvinunua vitabu, na mtu huwezi kudhani kuwa hali ya uchumi wa nchi hii ni mbaya kama ilivyo. Unaona wazi kuwa hii ni jamii iliyoelimika. Kuelimika, kwa mtazamo wangu, ni kuwa na kiu au ari ya kutafuta elimu kwa maisha yako yote.







Siku nzima, tangu asubuhi, watu wanafurika kwenye tamasha hili, na wanaonekana wakiwa makini sana katika kuviangalia vitabu, kuongea na waandishi na wachapishaji. Wanakuwepo pia wahariri.









Wazazi wengi huja na watoto wao. Ni wazi kuwa malezi ya aina hii yanawafanya watoto hao wakue katika mkondo huo huo wa kuthamini vitabu maisha yao yote. Hata kwetu Tanzania, watoto wanapenda vitabu. Tunawaangusha sisi watu wazima, kama nilivyoelezea hapa.







Nilivutiwa na meza ambapo palikuwa panauzwa vitabu vilivyotumika. Sio kwamba ni vitabu vichakavu. Nilitumia muda kwenye meza hii, nikajionea uwingi wa vitabu vya fani mbali mbali, kwa bei nafuu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...