Saturday, March 24, 2012

Mkulima wa Msoga, Msoma Vitabu

Jana nimekutana tena na Gilbert Mahenge, mkulima wa Msoga, Bagamoyo, ambaye tumeshakuwa marafiki. Nilishaandika habari zake hapa, nikimnadi kuwa ni msomaji makini wa vitabu.

Alikuja tukakutana Dar es Salaam, katika hoteli ya Deluxe, Sinza. Lengo kubwa la kukutana lilikuwa kuongelea shughuli za kampuni yangu ya Africonexion, tukazama katika kutafakari changamoto zinazotokana na utandawazi wa leo, na fursa zake.

Mahenge alishasoma kitabu changu cha CHANGAMOTO, kama nilivyoelezea kabla. Anapenda kuyanukuu niliyoandika. Basi, hiyo jana, nilimletea vitabu vyangu vingine viwili avione, yaani Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, Matengo Folktales, na Notes on Achebe's Things Fall Apart. Ili kuzuia malalamiko na maulizo miongoni mwa wasomaji wa blogu hii, niseme tu kuwa vitabu hivi vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 na 0717 413 073.

Tulipokuwa tunaongelea masuala ya changamoto za malengo na maendeleo ya mtu binafsi, nilitaja suala la mtu kuwa ngangari katika kufuatilia malengo, bila kukata tamaa. Hapo Mahenge akakumbushia mvumbuzi aliyehangaika kuunda balbu ya umeme, akashindwa mara elfu. Nami nikamtaja mvumbuzi huyo, kuwa ni Thomas Eddison. Tukaongelea zaidi habari za mvumbuzi huyo, ambaye alikuwa mtundu sana katika shule ya msingi, akijaribu hiki na kile na kuvunja vitu, hadi mwalimu akamfukuza shule. Hakumaliza shule ya msingi, lakini alikuja kuwa mvumbuzi wa vitu vingi sana katika uwanja wa tekinolojia, mvumbuzi maarufu labda kuliko wanadamu wote.

Mwaka jana, wakati niko Marekani, tuliongea kwa simu na Mahenge. Aliniambia kuwa ana hamu ya kusoma kitabu cha Parched Earth cha Elieshi Lema. Kwa bahati nzuri, nilikuwa nimeacha nakala hapa Dar, na nikafanya mpango akaja kukichukua. Hiyo jana, tayari aliniambia aliyosoma katika kitabu hicho.

Sasa basi, unapokutana na mkulima ambaye yuko katika upeo wa kuongelea masuala mengi namna hiyo, ni faraja tupu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...