Wednesday, April 22, 2015

Filamu Inayoongelea Kozi Yangu Ya Hemingway

Leo, Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi waliofika Tanzania mwezi Januari 2013, kwenye kozi yangu ya Hemingway in East Africa ameniletea nakala ya awali ya Papa's Shadow, filamu ambayo ameitengeneza kutokana na kozi ile. Nimeiangalia leo hii na binti yangu Zawadi, na tumeifurahia.

Wakati nilipokuwa nawachagua wanafunzi wa kuwepo katika kozi hii, Jimmy aliomba awemo katika msafara wetu ili akarekodi kumbukumbu ("documentary"). Alikuja na vifaa vyake, akawa anarekodi matukio na sehemu mbali mbali tulizotembelea, kama vile Arusha mjini, hifadhi za Ngorongoro na Serengeti, Karatu, na Longido.

Baada ya kozi kwisha, wazazi wa Jimmy, kaka yake na dada yake walifika kumchukua Jimmy wakaenda kupanda Mlima Kilimanjaro. Filamu inaonyesha safari hiyo pia, sambamba na maneno maarufu ya Hemingway aliyoyaweka mwanzoni mwa hadithi yake maarufu, The Snows of Kilimanjaro:

Kilimanjaro is a snow-covered mountain 19,710 feet high, and is said to be the highest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngaje Ngai," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude.

Jimmy alikuwemo katika safari yangu ya Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway. mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Pichani hapo kushoto tunaonekana nyumbani kwa Mzee Hemingway katika mji wa Craig. Kuanzia kushoto ni Clay Cooper, Jimmy, Mzee Hemingway, na mimi. Clay alikuwa mmoja wa wanafunzi waliokuja kwenye kozi yangu Tanzania.

Pamoja na yote hayo, filamu inajumlisha pia sehemu alipozaliwa Ernest Hemingway, yaani Oak Park, na sehemu alipofia na kuzikwa, jimbo la Idaho. Filamu ina maelezo mengi ya Mzee Patrick Hemingway na mimi kumhusu Ernest Hemingway na maandishi na fikra zake. Jimmy aliwahi kunihoji kabla ya safari yetu ya Montana, na amejumlisha mengi niliyoyasema katika mahojiano yale.

Filamu hii ni kumbukumbu nzuri sana. Kwa namna ya pekee, inaitangaza Tanzania na Mlima Kilimanjaro, na inaitangaza kozi yangu, ambayo lengo lake lilikuwa kuuelimisha ulimwengu kuhusu jinsi Ernest Hemingway alivyoandika kwa umakini, ufahamu, na upendo mkubwa kuhusu watu wanyama, na mazingira kama alivyoshuhudia katika safari na kuishi kwake Afrika Mashariki miaka ya 1933-34 na 1953-54.

Kuna sehemu katika filamu ambapo Mzee Patrick Hemingway anakitaja kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho anakipenda, na tunamwona akisoma sehemu ya kitabu hicho, ukurasa 89, ambayo nimenukuu makala ya Ronald G. Ngala, iliyoandikwa kwa ki-Swahili. Mzee Patrick Hemingway anasoma nukuu hii pamoja na tafsiri yangu.

Ingawa tulimshuhudia Mzee Patrick Hemingway akisoma, mimi kama mwandishi wa kitabu hiki nimeguswa kuona tukio hili limo katika filamu. Baada ya kazi ngumu ya zaidi ya miaka miwili, filamu imekamilika, na inategemewa kupatikana siku za karibuni. Nitaleta taarifa.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...