Wednesday, April 15, 2015

Soma Misahafu Upate Akili, Halafu Changanya na Zako

Kati ya vitabu vinavyochangamsha na kutajirisha sana akili ni misahafu ya dini mbali mbali. Hayo ni maoni yangu, yanayotokana na uzoefu wangu. Ninayo misahafu ya dini kadhaa. Ninayo Qur'an, kwa miaka zaidi ya thelathini. Kabla ya kuipata Qur'an, nilikuwa na Biblia.

Qur'an niliipata kwenye mwaka 1984 nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Kati ya marafiki zangu walikuwepo wa-Islam, na mmoja wao kutoka Sudan, alinitafutia Qur'an ilivyotafsiriwa kwa ki-Ingereza na Abdullah Yusuf Ali. Uzuri wa tafsiri hii ni kuwa ina maelezo mazuri ya vipengele mbali mbali.


Bhagavad Gita, msahafu maarufu wa u-Hindu, nilijipatia miaka ya hivi karibuni, sambamba na vitabu vingine vya dini hii.

Kwa nini mimi, ambaye ni m-Kristu (m-Katoliki) niwe na misahafu ya dini zingine? Kwa nini ninasoma, angalau kidogo kidogo, misahafu ya dini mbali mbali? Nina sababu zangu, na Mungu anajua, na ndiye atakayenihukumu.

Kwanza, ninatambua wajibu wa kuwaheshimu wanadamu wote. Mimi kama m-Kristu, nakumbuka Yesu alitupa changamoto kubwa pale alipotuasa kumpenda Mungu na kuwapenda watu wote, hata maadui zetu. Nina wajibu wa kuwafahamu wanadamu bila mipaka.

Mimi ni mwalimu wa fasihi za kimataifa. Ninaposoma na kufundisha fasihi za mataifa mbali mbali, ninapata fursa ya kuwafahamu wanadamu wa tamaduni mbali mbali. Kuzifahamu imani za dini zao ni hivyo hivyo. Ni muhimu kusoma misahafu ya dini mbali mbali, kama namna ya kuchangia maelewano.

Fasihi aghalabu zimefungamana na imani za dini. Bila kuyaelewa angalau mambo ya msingi ya u-Islam, kwa mfano, utafundishaje riwaya kama Twilight in Delhi, ya Ahmed Ali wa India na Pakistan; Minaret, ya Leila Aboulela wa Sudan; au The Fall of the Imam, ya Nawal el Saadawi wa Misri? Bila kuelewa angalau misingi ya u-Hindu, utafundishaje riwaya kama Untouchable, ya Mulk Raj Anand wa India? Bila kuielewa misingi ya u-Kristu, utafundishaje utungo wa Paradise Lost wa John Milton? Jawabu ni wazi: sherti nisome hiyo misahafu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...