Thursday, June 25, 2015

Habari ya Malipo ya Mhadhara Chuoni Winona

Jumanne wiki hii, nilikwenda Chuo Kikuu cha Winona kutoa mhadhara, kama nilivyoandika katika blogu hii. Katika safari kama hii, kuna mambo mengi, na haiwezekani kuyaongelea yote. Hata hivi, naona ni vizuri tu kuelezea angalau yale yenye umuhimu Fulani kwangu na labda kwa wengine. Napenda kuongelea suala la malipo ya mhadhara ule.

Wakati nilipoombwa kwenda kutoa mhadhara, mhusika aliniuliza malipo yangu ni kiasi gani. Huu ni utaratibu hapa Marekani, nami kama ilivyo kawaida yangu, nilimwambia kuwa siweki kipaumbele kwenye malipo, bali kutoa huduma itakiwayo. Kama wanaonialika wana uwezo wa kunilipa, kwangu ni sawa, kama wana uwezo kidogo, kwangu ni sawa, na kama hawana uwezo, kwangu ni sawa pia. Niko tayari kuitikia mwito kwa hali yoyote. Nilidhani suala lilikuwa limeishia hapo.

Siku kadhaa baadaye, mhusika alinielezea tena habari ya malipo, akataja kiasi ambacho angeweza kunilipa, kutokana na bajeti yake. Nilimjibu kuwa sina tatizo, nikamshukuru. Alipoleta mkataba, ambao ulitaja kiasi hicho cha malipo, niliusaini bila kusita, nikamrudishia.

Siku ilipofika, yaani hiyo tarehe 23 Juni, binti yangu Zawadi nami tulikwenda Chuoni Winona. Tulikaribishwa vizuri, tukaingia kwenye ukumbi wa mkutano wakati huo huo wanafunzi walipokuwa wanaingia. Baada ya kila mtu kuketi, mwenyeji wangu alisimama kunitambulisha. Alisema tunaye mgeni hapa, Dr. Mbele, profesa wa Chuo cha St. Olaf. Ni mtu ambaye nimemfahamu kwa miaka kadhaa, na nimemwomba aje atoe mhadhara.

Hadi hapo, sikuona kitu cha pekee, kwani huo ni utaratibu wa kawaida. Kilichokuwa cha pekee ni pale alipoanza kuelezea mazungumzo yetu juu ya malipo. Aliwaambia wanafunzi kuwa Dr. Mbele aliniambia kuwa hajali kama nina malipo kiasi gani ya kumpa, angekuja tu. Nasikitika kuwa kiasi nilichoweza kumwekea hakifanani na umaarufu wake. Niko njiani kutafuta hela kwa program nyingine, niweze kumwalika na kumlipa kiwango anachostahili.

Kwa kweli, sikutegemea angesema yote hayo, na nilimsikiliza kwa kumhurumia kwa jinsi alivyoonekana kujisikia vibaya kwamba ameshindwa kunitayarishia malipo ninayostahili. Nilifarijika alipomaliza maelezo yake na kunikaribisha nitoe mhadhara.

Baada ya mhadhara, mwenyeji wangu aliniongoza kwenda ofisini kwake, akanipa fomu ya malipo nisaini. Kisha akanipa cheki. Nilishangaa kuona cheki ilikuwa imezidi kile kiwango alichoniambia mwanzo. Nikaona kuwa alikuwa amejitahidi alivyoweza kuvuka kile kiwango tulichokubaliana. Na bado aliendelea kulalamika kuwa angeridhika kama angenilipa ninavyostahili.

Nimeona niongelee jambo hili, kwani ni kati ya mambo ambayo sitayasahau. Pia ni jambo lenye maana kwangu. Nimetamka tena na tena kuwa siweki pesa mbele, bali huduma. Hata hivi, ninafahamu jinsi wa-Marekani wanavyojali malipo. Wanazingatia umuhimu wa kumlipa mtu kile wanachoona ni haki yake.

Ningeweza kusema kuwa ninapaswa kuzingatia umuhimu wa kufuata utamaduni wa mahali nilipo. Lakini suala hili la malipo bado ni mtihani kwangu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Ninaamini kuwa kwa kuzingatia huduma kwa wanadamu, badala ya ubinafsi, sipotezi chochote. Badala yake, Mungu ananibariki. Ninaishi na raha moyoni. Ninafurahi kwamba binti yangu alishuhudia yote niliyoeleza hapo juu. Labda yatamsaidia maishani.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...