Monday, June 15, 2015

Namshukuru Msomaji

Napenda kuweka kumbukumbu nyingine katika hii blogu yangu, kama ilivyo desturi. Wikiendi hii nimeona ujumbe kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ujumbe huu, ulioandikwa na Ruth Ann Baker kwenye mtandao wa Amazon, unasema:

Learned some things I don't think I could find elsewhere. There is Lots of info on relationships and social etiquette.

Nimenakili ujumbe kama ulivyoandikwa. Nimefurahi kusikia maoni ya mtu ambaye amekisoma kitabu. Namshukuru kwa kutumia muda wake adimu kuandika maoni yake, katika ukumbi ambapo watu duniani kote wanaweza kuusoma.

Ni faraja kwangu ninapoona kuwa mtu baada ya kutumia fedha zake kukinunua kitabu, na muda wake katika kukisoma, anaona hajapoteza fedha wala muda. Ningejisikia vibaya sana iwapo hali ingekuwa kinyume, kama msomaji angeona amepoteza fedha zake na muda wake.

Nimeona niandike hayo, kwani ni jadi yangu kufanya hivyo, kuwahakikishia wasomaji wa vitabu vyangu kwamba ninawaheshimu na ninawashukuru kwa maoni yao. Maoni yao ni tunu wanayonipa, bila mimi kuwalipa chochote. Ni motisha kwangu, niendelee kuandika. Malipo muafaka ninayoweza kuwalipa ni kuendelea kuandika na kujitahidi kuandika kwa ubora zaidi muda wote.

Nimefurahi pia kuona msomaji huyu amenunua toleo la Kindle la kitabu hicho. Nimewahi kuandika kuwa kitabu hiki kinapatikana kama kitabu pepe katika Kindle na pia lulu.com. Ninajifunza katika kufuatilia jinsi wasomaji wanavyokwenda na wakati katika tekinolojia ya uchapishaji wa vitabu.

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ni wajibu na uungwana wa aina yake kuwashukuru wachangiaji wako hata kama hukubalilani na mawazo yao. Endelea hivyo kaka.

Mbele said...

Ndugu Mhango, kama tunavyokubaliana, kushukuru ni uungwana na wajibu. Dunia ingekuwa bora kuliko ilivyo kama "shukrani" ingejengeka katika tabia ya kila mwanadamu, sambamba na "samahani."

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...