Friday, June 12, 2015

Siku ya Mhadhara Chuo Kikuu Winona Inakaribia

Siku hazikawii. Zimebaki siku kumi na moja tu kufikia siku ya mhadhara wangu Chuo Kikuu cha Winona, utakaotokana na utafiti wangu juu ya falsafa zilizomo katika masimulizi ya jadi kama inavyodhihirika katika kitabu changu cha Matengo Folktales. Niliandika taarifa ya awali ya mhadhara huu katika blogu hii.

Leo nimeamka nikiwa nauwazia mhadhara huu kwa dhati. Nimejikuta nikijikumbusha mambo muhimu. Ninataka kwenda kutoa mhadhara madhubuti, wa kusisimua na kuelimisha. Hili huwa ni lengo langu kila ninapokubali mwaliko kama huu wa kwenda kutoa mhadhara popote.

Ninatambua wajibu wangu wa kuitendea haki taaluma. Ni wajibu wangu kama mtafiti na mwalimu kuitendea haki taaluma. Ni wajibu wangu kuwa mfano wa kuigwa na vijana wanaotafuta elimu, kama hao vijana watakaonisikiliza Chuoni Winona.

Ninatambua wajibu wangu wa kuwathibitishia wanaonialika kwamba hawakukosea kwa kunialika. Ninataka wasikilizaji wangu wakiri kuwa uamuzi wa kunialika ulikuwa sahihi. Sitaki wanaonialika na wanaonisikiliza niwaache wakisema kuwa afadhali wangemwalika mtu mwingine. Sitaki. Nataka wote wakiri kuwa mimi ndiye niliyefaa kutoa mhadhara ule. Wakiri kuwa mimi ndiye niliyefaa kujibu au kujadili masuali yao.

Ninatambua wajibu wangu mbele ya Mungu. Uhai wangu siku hadi siku, akili timamu, na vipaji alivyonipa Mungu ni dhamana kwa faida ya wanadamu. Ninapovitumia vipaji hivi ipasavyo, ninatimiza wajibu wangu kwa Mungu. Ninamtukuza Mungu. Ni furaha kwangu kutambua kwamba kutumia vipaji kwa namna hii ni kumtukuza Mungu, sawa na kusali.

Hayo ndiyo mawazo ambayo yamekuwa yakizunguka akilini mwangu tangu asubuhi. Ni aina ya mawazo yanayonisukuma nyakati kama hizi, ninapojiandaa kutekeleza mialiko. Ninapokubali mwaliko, ninafanya hivyo kwa dhati. Nikiona sitaweza kwa vigezo nilivyofafanua hapa juu, huwa nakiri tangu mwanzo ili wahusika wamtafute mtu mwingine, hata kama kwa kufanya hivyo ninajikosesha malipo yanayoendana na mwaliko.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...