Friday, May 20, 2022

USHIRIKI WANGU KATIKA MATAMASHA

 

Mimi kama mwandishi, ninashiriki matamasha ya vitabu na tamaduni, kama inavyoonekana pichani. Hii ni fursa kwangu ya kufahamiana na watu, kuwajulisha kuhusu shughuli zangu kama mwalimi na mwandishi, na pia kusikia mawazo na mitazamo yao. Ni fursa pia ya watu kujipatia vitabu vyangu.

Ushiriki wangu kwenye shughuli hizi una manufaa kwangu na kwa jamii. Hayo huelezwa katika vyombo vya habari, na mfano ni huu hapa.

Mimi mwenyewe nimetamka mara kwa mara kuwa nayaona matamasha haya kama darasa, ambamo nafundisha na kujifunza.


Monday, May 16, 2022

VITABU VYANGU, NAFSI YANGU

Vitabu vyangu si vitu vilivyo nje yangu. Ni sehemu ya nafsi yangu, kama kilivyo kichwa changu au ulivyo moyo wangu. Haiwezekani kuvitenganisha na mimi mwenyewe.

Ninaandika vitabu si tu ili watu waifahamu mada, bali pia ili wanifahamu. Kwa hiyo, sielei angani kwa nadharia na hoja zisizofikika kirahisi. Ninaongelea mambo yanayomgusa binadamu. Vitabu hivi ni sauti yangu na pumzi yangu.

Nitakapokuwa siko diniani, vitabu hivi vitaendelea kuongea na walimwengu, vikiwasilisha sauti yangu. Kwa njia ya kazi zao, waandishi tangu kale wametamani na wamefanikiwa kuishi hata baada ya kufariki.

Gilgamesh, shujaa wa kale wa Mesopotamia, alitamani hivyo, akataka kuandika jina lake, lisitoweke. Akina Shakespeare na Shaaban Robert bado tunao, kadhalika akina Tolstoy, Muyaka, Achebe na wengine kwa maelfu.

Wednesday, May 11, 2022

Mpiga Debe Mpya

Nimeanzisha programu ya mazungumzo mtandaoni Zoom ninayoyaita "Cross Cultural Conversations." Nilianza tarehe 16 Aprili, na ninafanya kila Jumamosi, saa kumi na mbili jioni hadi saa moja na nusu kwa saa za Afrika Mashariki.

Siku mojawapo, baada ya mhadhara wangu juu ya "Money in African and American Culture," mhudhuriaji aitwaye Kelly aliweka picha ya vitabu vyangu kwenye ukurasa wake wa Facebook, pamoja na ujumbe huu:

Beautiful afternoon to sit in Miss Samantha's yard! I'm reading work from Joseph Mbele, suggested by my friend Anita. Joseph is leading a recurring Zoom call on Saturday mornings (10 to 11:30) with intriguing conversations, focusing on different topics. My inbox is always open, I'd be happy to share the next Eventbrite link.

Imetokea hivyo, kwamba tangu nianze programu hii, wahudhuriaji wamekuwa wapiga debe wangu wakuu. Wanawaambia wengine na kuwashawishi wahudhurie. Matangazo ya mada ninaweka Facebook siku chache kabla ya mhadhara. Yeyote anakaribishwa kujisajili kwa kutumia linki inayoambatishwa kwenye tangazo.

Monday, April 25, 2022

Mdau Wangu Makini Katutembelea

Leo hapa Chuoni St. Olaf alifika mama mmoja kutoka Togo ambaye anaishi kwenye mji wa mbali kiasi kutoka hapa nilipo. Alimleta binti yake kwenye programu fulani ya wanafunzi. 

Mama huyu ni mdau wangu hodari, kwa maana kwamba ni msomaji wa tangu zamani wa vitabu vyangu na maandishi mengine, na ni mfuatiliaji wa shughuli zangu za kuelimisha jamii. 

Kwenye haya matamasha, huwa sikosi kuwaona waAfrika  wa nchi kama vile Somalia,  Kenya, Ethiopia, Uganda, Sudani, Congo, Nigeria, Togo, Liberia au Ghana. Ninafurahi kuwa wadau kutoka nchi zote hizo wamenunua na wamevutiwa na kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.



Friday, March 18, 2022

Nimekutana na Mdau Wangu Mwingine

Leo nilienda Mall of America kukutana na Tanya, mjumbe wa bodi ya shule za Osseo District. Tulifahamiana miezi kadhaa iliyopita, siku nipotoa mhadhara kwa Rotary Club of Brooklyn Park. Alikuwa mmoja wa wahudhuriaji, na nilimfahamu siku hiyo kama mjumbe wa bodi ya shule za Osseo District.

Nilikuwa nimemwomba tukutane, kwa sababu nilikuwa na mambo ya kumwuliza. Moja ni kuhusu uwezekano wa kujenga uhusiano baina ya shule za Osseo District na shule ya Bukoba, Tanzania, ambayo uongozi wake uliniomba niwatafutie uwezekano huo hapa Marekani.. 

Jambo jingine nililotaka kuongea naye ni muendelezo wa yale machache tuliyogusia siku ya mhadhara wangu, ambao yanahusu kuzuia au kutatua migogoro inyotokea shuleni. Tulikuwa tumakubaliana kwamba tofauti za tamaduni zinachangia tatizo hilo.

Jambo la tatu ni kuwa nilitaka kumpa nakala ya Chickens in the Bus: Embracing Cultural differences. Nilishampa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences baada kukutana mara ya kwanza. Ilikuwa ni furaha leo kusaini hiki kitabu na kumkabidhi. Huyu namhesabu kama mdau wangu muhimu.

Tumeongea mengi yanayohusu shule, kuhusu migogoro mashuleni itokanayo na tofauti au changamoto za tofauti za tamaduni na kadhalika. Tumegundua kuwa kwa ujumla tuna mitazamo inayofanana. Tumekubaliana kushirikiana kwa dhati siku zijazo katika kutafuta njia za kutatua changamoto zilizopo.
 

Saturday, March 12, 2022

 WADAU WA UTALII KWENYE MHADHARA WANGU ARUSHA

Tarehe 8 Januari, 2022, nilitoa mhadhara Arusha, mada ikiwa "challenges of cultural differences," yaani changamoto za tofauti za tamaduni. Hii ni mada ambayo naiongelea na kuiandikia sana. Mwandaaji wa mhadhara alikuwa mama Ama, mMarekani Mweusi. Walihudhuria watu wa mataifa mbali mbali, lakini zaidi kutoka Marekani na Tanzania. Tuilkaa kwa takriban saa tatu.
Baadhi ya waTanzania waliohudhuria ni vijana wa kampuni ya utalii iitwayo Rift Valley Cultural Tourism, ambayo makao yake ni Karatu. Kupitia kwa mkurugenzi wa kampuni, wote walikuwa wamepata nakala za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences," na walikuwa wamekisoma. 

Waliposikia kuwa ninatoa mhadhara, waliamua kuhudhuria. Tulifurahi kukutana. Baada ya mhadhara, tulipiga hii picha inayoonekana hapa juu; baadhi yao wameshika kitabu changu. Wadau wa utalii ni wanufaika wa moja kwa moja wa kitabu hiki. Hii ilidhihirika mwaka 2007 wakati mkurugenzi wa J.M. Tours aliponunua nakala kadhaa akawapa madreva waongoza watalii wake wasome. 

Walikifurahia kwa msingi kwamba kiliwawezesha katika kushughulika na watalii. Niliandika kuhusu hilo kwenye makala yangu, "My Arusha Readers."
Ninawapongeza Rift Valley Cultural Tourism kwa kutambua fursa na kuitumia. Niko tayari kuwa nao bega kwa bega katika masuala ya utalii na utamaduni, kubadilishana uzoefu na kuelimishana. 

Mbali ya vitabu vyangu, ambavyo vinapatikana mtandaoni, nawakaribisha kwenye chaneli yangu ya YouTube.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...