Wednesday, August 31, 2011

Wadau Wawili Wamenitembelea

Leo hapa Sinza nimepata bahati ya kutembelewa na wadau wawili wa maandishi yangu.

Kwanza alifika ndugu Renatus Mgusii kutoka Segerea. Huyu tumefahamiana mtandaoni na ni msomaji wa maandishi yangu, kuanzia blogu hadi vitabu. Tuliongea mengi kuhusu masuala ya elimu, tofauti za tamaduni na athari zake katika dunia ya leo na mengine kadha wa kadha. Nimefurahi kukutana na mdau huyu, msomaji makini na mwenye uchungu na elimu.



Mdau wa pili alifika majira ya jioni. Huyu ni Gilbert Mahenge wa Msoga. Huyu niliwahi kuandika habari zake katika blogu hii, kwamba alikuwa mdau wa kwanza hapa Tanzania kununua na kusoma kitabu changu cha CHANGAMOTO. Niliguswa kumwona amefika na nakala yake. Tumeongea mengi kuhusu siasa, maendeleo na elimu. Alipiga simu Msoga nikapata fursa ya kumsalimia mkuu wa kijiji.

Tuesday, August 30, 2011

Safari ya Bagamoyo

Mizunguko yetu nchini Tanzania imemalizika. Safari yetu ya mwisho tulienda Bagamoyo, tarehe 27 Agosti. Tulitembelea Caravan Serai, ambayo ni makumbusho ya historia. Nilitaka wanafunzi wangu wapate fununu kidogo ya umaarufu wa Bagamoyo katika historia.







Historia hii imejumlisha mambo mengi, ikiwemo biashara ya watumwa na pembe za ndovu, mji huu kuwa makao makuu ya serikali ya kikoloni ya wa-Jerumani, mapigano ya Bushiri dhidi ya wa-Jerumani. Kwa upande wangu kama mwanafasihi, naukumbuka mji wa Bagamoyo kwa vile hapo aliishi Mgeni bin Faqihi, mtunzi wa "Utenzi wa Rasi 'lGhuli," ambao ni hazina kubwa katika urithi wa utamaduni wetu, ingawa wengi hawaujui. Labda iko siku jamii yetu itaamka.

Tulizunguka mitaani, hadi ufukweni, tukafaidi upepo mwanana na mandhari ya kuvutia. Kwa hayo na mengine mengi, Bagamoyo ni mji maarufu kwa utalii.

Saturday, August 20, 2011

Matema Beach

Leo nimeshinda Matema Beach, kandoni mwa Ziwa Nyasa. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika mahali hapa. Niliweka kipaumbele kufika hapa katika safari ya kuzunguka na wanafunzi kutoka Marekani ambao nimewaleta Tanzania.




Matema Beach panapendeza sana. Ingawa ni kijiji kidogo, kuna hoteli kadhaa hapa. Moja ni Lutheran Center ambayo inaonekana pichani kushoto.





Hapa ni baadhi ya nyumba za kulala wageni hapo Lutheran Center.


Hapa kushoto ni kibanda kimojawapo cha kulala wageni hapo Lutheran Center.











Hoteli nyingine ni Matema Beach Resort. Hapo kushoto kuna picha za baadhi ya nyumba za kulala wageni.








Ninapokuwa maeneo kama haya ya Matema Beach, najikuta nikitafakari hili na lile. Wakati huu ufukwe wa Matema Beach ni huru kwa wananchi kutembea, kuogelea, na kupumzika.

Lakini nahisi kuwa siku itakuja ambapo wenye pesa watajichukulia sehemu hizi na kujenga uwigo hadi ziwani. Baada ya kuwekewa uzio, wananchi hawataweza kupita tena maeneo hayo. Hali hii nimeiona sehemu mbali mbali Tanzania, kama vile Ukerewe. Huu ni ubovu wa sera za serikali ya Tanzania ambao unanikera.

Friday, August 19, 2011

Mitaani Mbeya

Nimepata fursa ya kupita mitaa ya Mbeya. Ni mji uliojengeka kwenye miinuko na mabonde kiasi kwamba sio rahisi kujua ukubwa wake.


Nimepita maeneo ya u-Hindini, Mwanjelwa, Mama John na Uyole. Majina ya maeneo mengine nimesahau. Ila nilienda hadi shule ya Ivumwe.

Nategemea kutembelea Mbeya tena mwakani.

Mbeya: Dobi Miwani Ameamia Sokoine

Leo asubuhi niliamka hapa Mbeya, nikaanza kupita mitaani kwa mguu. Nilipofika eneo la u-Hindini, niliona tangazo: Dobi Miwani Ameamia Sokoine. Nami nimeona niwaletee wadau, kuwaepushia usumbufu.

Napenda blogu yangu iwe bega kwa bega na wajasiriamali wadogo wadogo, katika harakati zao za kujitafutia chochote, kama nilivyogusia hapa.







Thursday, August 18, 2011

Niko Mbeya

Jana jioni nimeingia mjini Mbeya, nikitokea Njombe. Niko na wanafunzi kutoka Marekani, ambao hatimaye nitawapeleka Chuo Kikuu Dar es Salaam ambako watasoma kwa muhula mmoja.

Kwa vile ilikuwa ni usiku, sikuweza kuuona mji vizuri. Leo asubuhi nimeanza kutembelea maeneo ya mji, kama vile Mwanjelwa. Nategemea kupata fursa ya kuuona mji huu na pia sehemu zingine za mkoa wa Mbeya.

Wednesday, August 17, 2011

Leo Ninatimiza Miaka 60

Leo natimiza miaka sitini tangu kuzaliwa. Huu si umri mdogo, nami namshukuru Muumba kwa kunipa fursa ya kuwepo ulimwenguni kiasi hiki. Ninavyokumbuka maisha yangu, ninatamani kama ningekuwa nimefanya mengi na makubwa zaidi kuliko niliyofanya kwa manufaa ya wanadamu. Ninatamani kama ningekuwa nimejiepusha na mabaya, nikawa mtu bora wa kupigiwa mfano. Lakini haiwezekani tena kuirudisha miaka iliyopita. Bora niangalie mbele, nijaribu kufanya bidii zaidi, ingawa sijui nimebakiza miaka mingapi hapa duniani.

Friday, August 12, 2011

Kalenga Kwenye Makumbusho

Jana, pamoja na wanafunzi wangu, tulitembelea makumbusho ya Mkwawa, yaliyopo Kalenga, karibu na Iringa. Tulipata maelezo mengi ya historia ya wa-Hehe. Tulipata fursa ya kuangalia vitu mbali bali vilivyomo katika makumbusho hayo, kama vile silaha za jadi, zana za kilimo, vyombo vya nyumbani, picha, na maandishi. Kitu cha kukumbukwa zaidi ni fuvu la Chifu Mkwawa.

Hapo ni mahala muhimu kwa kwenda kujifunza historia sio tu ya wa-Hehe bali ya Tanzania. Kwa mfano, katika makumbusho haya kuna kuna zana za mawe za kale zilizopatikana Isimila.

Idara inayohusika na hifadhi ya makumbusho hayo inafanya kazi nzuri katika mazingira magumu. Hata hivi, hakuna sababu yoyote kwa nini Tanzania isiweke kipaumbele katika kuipa idara hii kila msaada unaohitajika. Umma wa wa-Tanzania unapaswa pia kuamka ili utambue umuhimu wa makumbusho kama haya. Haipendezi, kwa mfano, kuona watu wanajichukulia viwanja na kujenga nyumba katika maeneo ambayo ni ya kihistoria. Wa-Tanzania tujiulize: je, iwapo ukuta mkuu wa China ungekuwa katika nchi yetu, tungekuwa tumeutunza kama wanavyofanya wa-China? Naogopa kuwa kutokana na elimu duni, watu wangeng'oa mawe ya ukuta huo na kujengea nyumba.
Ikitunzwa vizuri na kutangazwa ipasavyo, hifadhi kama hii ya Kalenga ni hazina yenye mchango mkubwa katika elimu sio tu ya wa-Tanzania bali walimwengu kwa ujumla. Ni kivutio ambacho kinaweza kuchangia sana katika uchumi wa eneo hili.

Wednesday, August 10, 2011

Msosi Iringa

Leo nimeshinda Iringa, pamoja na wanafunzi wangu. Safari yetu ni ya masomo, kama nilivyoelezea hapa. Sehemu moja tuliyotembelea ni Chuo Kikuu Kishiriki Iringa tukaonana na kiongozi mmojawapo wa chuo, Mchungaji Dr. Richard Lubawa, mtunzi wa kitabu cha Shoulder to Shoulder.

Pichani naonekana na mwanafunzi Ryan Campbell tukiwa tunaudhibiti ugali na maini katika hoteli ya Wilolesi Hilltop, karibu na Kihesa. Ryan hakuushangaa ugali, kwani alishapambana nao Zambia alipokuwa na miaka 17.
(Picha imepigwa na Bailey Putney)

Tuesday, August 9, 2011

Nimeingia Iringa Jioni Hii

Jioni hii nimeingia mjini Iringa, nikitokea Dar es Salaam. Nimekuja na wanafunzi katika programu ya LCCT ambayo huleta wanafunzi kutoka vyuo vinne vya Marekani kuja kusoma chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa muhula moja, na pia huwawezesha wanataaluma na maafisa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenda kwenye vyuo hivyo kwa utafiti au kujiongezea uzoefu kwa miezi minne.

Tumesafiri na wadau wa programu ya Bega kwa Bega, ambao wanaishi Minnesota. Hii ni programu inayowashirikisha wa-Marekani na watu wa Iringa katika mipango mbali mbali ya maendeleo, kama vile elimu, afya, na maji safi. Ingawa mimi sikuwafahamu wadau tuliosafiri nao leo, wote wananifahamu. Wameniambia kuwa mwaandaaji na kiongozi wa safari yao, ambaye anaonekana pichani, wa pili kutoka kulia, aliwahimiza kusoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ni faraja kwa mwandishi yeyote kujua kuwa watu wanasoma maandishi yake.

Tumefikia Iringa Lutheran Centre, na tutakuwa hapa wiki moja. Wadau wa hapa tunaweza kuonana katika siku hizo. Namba zangu za simu ni 0754 888 647 na 0717 413 073

Picha zinazoonekana hapa tumepiga tukiwa katika hoteli mmoja Mikumi, tuliposimama ili kupata chakula cha mchana.

Sunday, August 7, 2011

Mdau Kanitembelea



Leo nimepata bahati ya kutembelewa na mdau Emmanuel Sulle ambaye yuko masomoni Chuo Kikuu cha Maryland, College Park. Imetokea kuwa sote tuko Dar es Salaam kwa wakati huu.

Aliniletea ujumbe kuwa anayapenda maandishi yangu akataka kuniona, kwani hatujapata kuonana. Alikodi teksi akanifuata. Yeye ni mtafiti makini mwenye nia thabiti ya kuchangia taaluma kwa maandishi. Tumeongea mengi, kuhusu utafiti na uandishi, pia umuhimu wa kuwahamasisha vijana kujiendeleza kielimu.






Friday, August 5, 2011

Mitaani Mbamba Bay

Agosti tarehe 2 nilisafiri kutoka kijijini kwangu Lituru nikapitia Mbinga, na kufika Mbamba Bay, mwambao wa Ziwa Nyasa kwa matembezi.

Mbamba Bay, ingawa mji mdogo sana, unavutia kwa utulivu wake na mazingira, ukiwa ufukweni mwa Ziwa linalomeremeta kwa maji yake maangavu, kama nilivyowahi kuandika hapa.

Nilikuwa na bahati kwamba tarehe 3 Agosti ilikuwa siku ya jua na hali ya hewa ya kuvutia sana. Nami nilitumia fursa hii vilivyo. Niliteremkia ufukweni kufurahia upepo mwanana na mandhari murua ya Ziwa.


Kukaa nje ya nchi yako kunakupa mtazamo tofauti wa masuala ya nchi yako. Kwa mfano, hapa Tanzania, watoto wetu wana uhuru sana wa kucheza na kuzunguka mitaani, tofauti na Marekani, ambako watoto huangaliwa sana muda wote na wazazi au walezi wao, kwani si salama kuwaacha watoto bila uangalizi. Wa-Marekani wanaokuja huku kwetu wanashangaa wanapowaona watoto wakijizungukia wenyewe mitaani, raha mstarehe. Nimeongelea tofauti hizo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Joto la Mbambay ni kishawishi kikubwa cha kutafuta sehemu ya kujipatia kinywaji baridi. Nami nilisogea baa hii iitwayo Bush House, nikatuliza kiu.



Hali ya Mbamba Bay ni ya utulivu usio kifani. Ni mahali pazuri kwa mapumziko. Kadiri siku zinavyopita, nina imani kuwa Mbamba Bay patakuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa nje na ndani ya nchi. Nami niliamua kufika Mbamba Bay ili kupiga picha nichangie katika kuitangaza sehemu hii ya Tanzania.










Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...