Tuesday, June 28, 2011

Naenda kwa wa-Nyakyusa

Hivi karibuni, nitakuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya masomo inayoendeshwa na vyuo kadhaa vya Marekani kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kabla ya kuwafikisha Chuo Kikuu Dar es Salaam ambapo watasoma kwa muhula mmoja, nitakuwa nao maeneo ya nyanda za juu, hasa Iringa. Lakini, katika kupanga safari hii, nimeamua kuwafikisha hadi Mbeya na Ziwa Nyasa, wakaone na kujifunza. Iringa naifahamu vizuri, ila Mbeya nilipita tu mara moja, miaka ya mwisho ya sabini na kitu.

Wakati nangojea kwenda Mbeya, nawazia utamaduni wa wa-Nyakyusa. Mimi kama mtafiti, nimesoma kiasi kuhusu masimulizi yao ya jadi. Ninakumbuka maandishi ya watafiti kama Monica Wilson. Nina kitabu kiitwacho The Oral Literature of the Banyakyusa, kilichoandikwa na Christon S. Mwakasaka. Nadhani nilikinunua Dar es Salaam, nikawa nakisoma mara moja moja.

Lakini wakati huu ninapongojea safari ya Mbeya, kitabu hiki kinanivutia kwa namna ya pekee. Kina hadithi za jadi, lakini vile vile nyimbo na tungo zingine zinazoelezea mambo ya hivi karibuni ya historia na siasa u-Nyakyusa na Tanzania kwa ujumla.

Natafuta maandishi mengine ya kuongezea ufahamu wangu. Kwa hilo naweza kusema nimeathiriwa na wa-Marekani. Wao, kabla ya kusafiri, wana hiyo tabia ya kusoma habari za sehemu waendako. Ni jadi nzuri. Kusafiri kunatupanua akili, lakini kusoma habari za tuendako kunautajirisha zaidi ufahamu wetu.

Saturday, June 25, 2011

Huwezi Kumaliza Masomo

Mwaka 1976, nilipata shahada ya B.A. katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nilipongezwa kwa kumaliza masomo. Mimi sikuishia hapo. Niliendelea na masomo, hapo hapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nikapata shahada ya M.A. mwaka 1978. Nilipongezwa kwa kumaliza masomo.

Miaka michache baadaye, nilienda Marekani, Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Nilisoma nikapata shahada nyingine ya M.A. mwaka 1982. Sikumaliza masomo. Niliendelea nikapata shahada ya Ph.D. mwaka 1986. Kwa mtazamo wa jamii yetu, nilimaliza masomo. Kwani baada ya shahada ya udaktari, kuna nini zaidi?

Mimi sikuona kama nimemaliza masomo. Niliona nimepata motisha tu ya kusoma na kujielimisha. Jambo la msingi nililojifunza ni kwamba elimu ni bahari pana isiyo na mwisho, na yale niliyosomea ni tone dogo sana. Ninaamini kuwa elimu ya kweli ni kutambua hilo, na kujitambua ulivyo mjinga, na utambuzi huo uwe ni chachu ya kukufanya ukazane kujielimisha maisha yako yote. Uuone ujinga kama adui anayekunyemelea na kukufukuza maisha yote. Kusaka elimu ndio mbio za kujinusuru.

Ndivyo ninavyofanya katika maisha yangu. Kwa kutambua mapungufu yangu, ninatafuta elimu muda wote, kwa utafiti, kununua vitabu, na kusoma kwa bidii.

Mwalimu Nyerere alituongoza kwenye njia hiyo. Alisisitiza kuwa elimu haina mwisho. Na huu ndio ukweli.

Na hapo sijaongelea elimu ambayo inapatikana nje ya shule. Sijaongelea elimu ya kijijini. Sijaongelea elimu inayopatikana kwa wavuvi, wafugaji, wawindaji, wacheza ngoma, wavuta mkokoteni, polisi, wachanganya zege, wabeba boksi, kondakta wa dala dala, na mama ntilie. Kila mmoja ana jambo la kunifundisha, na kila mmoja ana jambo la kukufundisha. Hayo nimeyagusia katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Wednesday, June 22, 2011

Kitabu Kimetua Mtandao wa Dartmouth Alumni

Kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimetua kwenye mtandao wa watu waliosoma katika Chuo cha Dartmouth. Waandaaji wa safari ya Tanzania wamekiteua kama kitabu muhimu kwa washiriki wa msafara huo. Angalia sehemu ya "Recommended Reading List."

Kati ya mambo yaliyonifanya niandike kitabu hiki ni kukidhi mahitaji ya wa-Marekani wanaoenda Afrika kwa sababu mbali mbali, kama vile masomo, utafiti, utalii na shughuli za kujitolea. Kilihitajika kitabu cha kuwaelewesha mambo ya msingi yanayotufautisha utamaduni wao na ule wa wa-Afrika.

Msimamo wangu ni kuwa pamoja na tofauti zilizopo miongoni mwa wa-Afrika wenyewe, na pamoja na tofauti zilizomo miongoni mwa wa-Marekani, kuna kitu tunachoweza kukiita utamaduni wa mw-Afrika, na kuna kitu tunachoweza kukiita utamaduni wa m-Marekani. Katika kuandika na kuongelea masuala hayo, najaribu kuthibitisha jambo hilo. Nafarijika kuwa juhudi hizi zinakubalika na watalaam na wadau kama hao wa Dartmouth Alumni.

Thursday, June 16, 2011

Shughuli ya Waandishi Imefana Minneapolis

Kama ilivyotangazwa kabla, waandishi wa-Marekani Weusi walijumuika katika duka la vitabu la Magers & Quinn Minneapolis. Nilijumuika nao, ingawa mimi si m-Marekani. Tunaonekana pichani kushoto. (Picha ni ya Magers & Quinn Booksellers)


Hii ilikuwa ni fursa ya waandishi kuonesha vitabu vyao na kuongea na wadau na wasomaji, ambao walihudhuria kwa wingi.
Shughuli hii ilitangazwa kama ya waandishi waMarekani weusi. Nilijionea mshikamano mkubwa baina yao na jumuia ya waMarekani weusi. Walifurika duka hili kubwa.Walikuja watu wazima, vijana, na watoto. Na wote walikuwa na shauku ya kujionea vitabu, kuvipitia na kuvinunua.


Waandishi tulikuwa na kazi kubwa ya kuongea na hao wadau na kujibu masuali yao. Lakini hayo ndio mategemeo ya kila mwandishi.
Huyu dada alisogea kwenye meza yangu, akajitambulisha kuwa mama yake ni m-Mtanzania. Ilikuwa ni ajabu. Wa-Tanzania tuliosoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, miaka thelathini na kitu iliyopita tulifahamiana na huyu mama yake. Tulifurahi kukumbushana historia hii.

Migongano ya Utamaduni wa wa-Marekani na Wa-Afrika

Nimealikwa na umoja wa watu wenye asili ya Afrika hapa Minnesota kuongoza mjadala, tarehe 18 Juni, keshokutwa, kuhusu matatizo yanayowakabili wa-Afrika hapa Marekani yatokanayo na tofauti za tamaduni. Umoja huo unawajumuisha wa-Afrika wanaoishi hapa Marekani, wa-Marekani Weusi, na watu wenye asili ya Afrika watokao Amerika ya Kusini, visiwa vya Caribbean, na kadhalika.

Taarifa kamili za mkutano ni hizi:

MAHALI PA KUKUTANIA:

Center for Families
3333 North 4th Street
Minneapolis, Minnesota

MUDA:

Juni 18, 2011. Saa 6-8 mchana.

Hakuna ki-Ingilio, na wote mnakaribishwa. Nangojea kwa hamu kwenda kuongoza mjadala huu muhimu kwa jamii.

Monday, June 13, 2011

Maonesho ya Utamaduni wa Afrika, Brooklyn Park

Tarehe 11 Juni, katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota, yalifanyika maonesho ya utamaduni wa Afrika, kama nilivyowahi kutangaza katika blogu hii. Kulikuwa na hotuba mbali mbali kuhusu masuala kama afya na mengine mengi.
Kulikuwa na ngoma za watu wa Kamerun ambao wanaonekana hapa kushoto. Tena mmoja wa wachezaji ni mwanasheria maarufu hapa Minnesota, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Alikuwa anayarudi magoma sawa na mtu wa kule kijijini.
Wadau wa aina aina walikuja kwenye maonesho hayo. Kwa upande wa Afrika Mashariki, walikuja wa-Kenya wengi na wa-Ganda, na kulikuwa na meza zao ambapo waliweka majina ya nchi zao. Hapakuwa na meza ya Tanzania, yenye bendera ya nchi kama ilivyokuwa kwa wenzetu. Mdau mmoja kutoka Ethiopia aliniuliza inakuwaje hakuna meza ya wa-Tanzania, wakati wengine wa Afrika Mashariki wana meza. Mimi natoka mji wa mbali, na nilikuwa nimejilipia maonesho hayo kama mtu binafsi sio kama mwakilishi wa Tanzania. Labda wa-Tanzania tusaidiane kutoa maelezo, maana nimeongelea sana kwenye blogu hii na zingine suala la wa-Tanzania kutoonekana kwenye shughuli za aina hii, zinazojumuisha mataifa mbali mbali. Tunakwenda kinyume na alivyotufundisha Mwalimu Nyerere.


Shirika moja dogo la wa-Marekani linaloshughulikia tatizo la kipindupindu Tanzania lilikuwa na meza ambapo taarifa mbali mbali zilikuwepo. Niliongea sana dada Katie JohnsTon ambaye ni mhusika. Yeye na mwenzake mmoja wanajiandaa kwa safari ya Tanzania.


Hapa kushoto kuna meza ya vitu kutoka Kamerun.

Akina mama kutoka Senegal na Togo walionesha vitu mbali mbali vya kwao, zikiwemo nguo, vikapu na vinyago.


Kulikuwepo pia na maonesho ya mitindo ya mavazi. Hapa kushoto anaonekana mwendeshaji wa shughuli hii, Dr. Woldu, aliyevaa nguo nyeupe, na msichana akipita na vazi mojawapo.

Fasihi simulizi na andishi ni sehemu muhimu ya utamaduni. Mimi kama mtafiti hurekodi urithi huo na kuuandikia makala na vitabu. Hapa kushoto anaonekana binti yangu akinisaidia kuonesha na kuelezea kazi zangu hizo. Nimemzoesha tangu alipokuwa mdogo zaidi, na anaweza kuniwakilisha hata kama nimesafiri.

Hapa kushoto niko na mwendeshaji mojawapo wa maonesho haya, Dr. Samuel Woldu kutoka Ethiopia. Mwenye shati la kitenge ni Bwana Albert Nyembwe kutoka Kongo Kinshasa. Ni mwanzilishi na mkurugenzi wa taasisi ya Cilongo. Pia ni shabiki na mpiga debe mkubwa wa maandishi yangu.Watoto wa umri mbali mbali, walikuwepo. Hawakuwa watazamaji tu, bali wengine walishiriki kwa vitendo, kama vile nyimbo.


Kwaya ya wa-Kenya iliimba nyimbo mbali mbali, tena kwa kiSwahili. Tukizingatia kuwa lugha ni msingi mkubwa wa utamaduni, hao wa-Kenya walituwakilisha vizuri sisi watu wa Afrika Mashariki.Kule nyuma kwenye kibanda cha Knight's Cafe akina mama walikuwa wanauza vyakula kutoka sehemu mbali mbali za Afrika. Hapo nilinunua na kuonja chakula kutoka Togo. Sio jambo gumu kuelewa jinsi utamaduni ulivyofungamana na chakula. Kwa kiasi kikubwa chakula ni utambulisho wa utamaduni.

Sunday, June 12, 2011

Anonymous Anasema Kitabu Hiki Hakina Jipya

Kwa wasomaji wa blogu yangu hii na ile ya ki-Ingereza, habari za kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences sio ngeni. Wengi wamekisoma kitabu hiki na wengine wamechangia maoni yao katika blogu hizi na zingine.

Juzi ametokea anonymous kwenye blogu hii akaandika hivi: "Nimekisoma hakina chochote kipya, ni kama vitabu vingine."

Mimi kama mtafiti na mwalimu huhamasisha elimu na kuelimishana. Nilimpa ukumbi anonymous atuelimishe zaidi na pia kututajia hivyo vitabu vingine. Habari kamili iko kwenye sehemu ya maoni hapa. Hadi sasa anonymous hajasema kitu tena. Bado nasubiri.

Saturday, June 11, 2011

Waandishi Tumekutana Leo

Leo nilienda Minneapolis kushiriki mkutano wa waandishi wa-Marekani Weusi, kama nilivyoandika hapa. Mkutano huu, uliofanyika katika Center for Families, ni sehemu ya maandalizi ya maonesho ya vitabu ya tarehe 16 mwezi huu, katika maktaba ya Magers and Quinn. Waandaaji wa shughuli zote hizi ni Jeffrey Groves na Shatona Kilgore-Groves, wanaoonekana hapa juu.

Mkutano wa leo ulikuwa ni wa kufahamiana. Kila mtu alipata fursa ya kutoa maelezo mafupi kuhusu maisha na shughuli zake za uandishi. Baadhi ni chipukizi, ambao wamechapisha kitabu kimoja tu, na baadhi ni wazoefu, waliochapisha vitabu kadhaa. Baadhi ya vitabu vinahusu maisha binafsi; vingine vinahusu mafunzo mbali mbali, hadithi za kubuni, mashairi, na falsafa. Wengine wameandika vitabu vya watoto. Nami nilipata fursa ya kuongelea vitabu nilivyoandika.
Watu waliongelea maisha yao na kwa nini wanaandika. Baadhi, kama hao akina mama wanoonekana kushoto, wamepitia maisha machungu yasiyoelezeka, yanayowafanya baadhi ya wanadamu wajiue. Kuandika ni namna ya kujiponya ili kuendelea na maisha
Baadhi ya waandishi nilikuwa nimefahamiana nao kabla, kama vile Mahmoud el Kati, Joyce Marrie, Gerard Montgomery, na Jeff na Shatona Groves, ambao kitabu chao, A Black Parent's Memoir, ninakiandikia mapitio. Lakini imekuwa bahati leo kufahamiana na waandishi wengi kwa mpigo.

Mkutano wa leo umeleta msisimko mkubwa miongoni mwa washiriki. Tumekubaliana kuwa kukutana kwa namna hii ni hatua nzuri na muhimu; inatakiwa iwe jadi ya kuendelezwa. Kutokana na mafanikio ya mkutano wa leo, sote tunayangojea kwa hamu maonesho ya Juni 16, ambayo watu wengi wanategemewa kuhudhuria.

Tuesday, June 7, 2011

Mwaliko Nyumbani kwa Wateja Wangu

Jana jioni nilikuwa nyumbani kwa familia inayoonekana katika hii picha. Ni familia ya Shannon Gibney, mwandishi chipukizi ambaye tayari ni maarufu.

Miaka michache iliyopita, Shannon Gibney alisoma kitabu changu cha Africans and Americans, akaandika mapitio katika Minnesota Spokesman Recorder, kama nilivyosema hapa.

Siku chache zilizopita alinialika nyumbani kwake kwa chakula cha jioni, tukapanga hiyo tarehe ya jana. Aliniambia kuwa mume wake, ambaye anatoka Liberia, na bado ni mgeni hapa Marekani, amekuwa akisoma kitabu changu.

Nilifurahi kukutana na familia hii. Kwa zaidi ya saa mbili nilizokuwa nao, maongezi yetu yalihusu masuala niliyoongelea katika kitabu, yaani tofauti za tamaduni za wa-Marekani na wa-Afrika. Wote wawili wanakifahamu vizuri sana kitabu hiki, na walikuwa wananikumbusha mengi, ingawa mimi ndiye mwandishi.

Huyu bwana aliezea mshangao wake kwa jinsi maelezo ya kitabu hiki yanavyofanana na hali ya Liberia, ingawa mimi mwandishi sijafika kule. Niliguswa na furaha yake kwamba niliyoandika yamemwelewesha mambo ya wa-Marekani ambayo yalikuwa yanamtatiza. Nami nashukuru kwa hilo.

Familia hii ilinikarimu vizuri sana, nami nimebaki nashangaa kwa jinsi uandishi wa kitabu unavyoweza kukujengea urafiki na watu kiasi hicho.

Friday, June 3, 2011

Maonesho Minnesota Mwezi Juni

Mwezi huu Juni nimealikuwa kushiriki katika maonesho sehemu mbili tofauti hapa Minnesota. Tarehe 11 nitakuwa Brooklyn Park, kushiriki maonesho ya African Health Action. Wahusika walinialika kwa msingi kuwa wameshaniona kwenye maonesho mengine hapa Minnesota.

Tarehe 16 Juni nimealikwa kushiriki maonesho ya waandishi wa-Marekani Weusi hapa Minnesota. Nilialikwa na mmiliki wa Black Parent Group, waandaaji washiriki wa onesho hilo, ambao wanafahamu kuhusu shughuli zangu, hasa kitabu cha Africans and Americans. Nimetangaza onesho hilo hapa.

Ingawa mimi si m-Marekani, huwa ni kawaida kwa hao wenzetu wa-Marekani Weusi kutujumlisha namna hiyo, kwa vile wanavyoangalia sana rangi ya mtu. Usishangae ukiona wa-Marekani Weusi wanapoandika orodha ya wa-Marekani Weusi maarufu, ukakuta majina ya watu kama Mzee Mandela.

Hao wa-Marekani weusi huwa wanafanya hivyo kwa nia njema na pia kutojua hisia zetu sisi wa-Swahili. Kwa upande wangu, nikizingatia hali halisi ya mahali ninapofundisha, ambacho ni chuo cha wazungu, ni nadra kupata fursa ya kuwa na wa-Marekani weusi. Kwa hivi, naona ni bora kushiriki mialiko yao na kujumuika nao vizuri, kuliko kuanza kuleta zogo ambalo hasara yake inaweza kuwa kubwa kuliko faida. Naamini ni busara kusema kuwa maongezi ya kujipambanua mimi ni nani yatakuja baadaye, baada ya kuzoeana.

Sehemu zote mbili nitakwenda kuonesha vitabu vyangu na kuongea na wadau kuhusu uandishi, uchapishaji, na masuala ya tamaduni katika ulimwengu wa utandawazi wa leo. Wadau mlioko Minnesota mnakaribishwa.

Thursday, June 2, 2011

Mfano wa Uandishi Bora wa ki-Ingereza

Kusoma kuna faida nyingi. Kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa lugha iliyotukuka ni neema. Nina bahati kuwa nafundisha somo la fasihi, na muda wote nawaongoza wanafunzi katika kutafakari na kujadili maandishi bora kabisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wiki chache zilizopita, tulisoma riwaya iitwayo Reef, iliyoandikwa na Romesh Gunesekera wa Sri Lanka na kusifiwa sana na wahakiki. Ingawa riwaya nzima imeandikwa kwa ki-Ingereza kilichopevuka na kinavutia sana, napenda kunukuu kipande kimoja ambacho kilinigusa kwa namna ya pekee. Mwandishi anaelezea safari ya gari katika kisiwa cha Sri Lanka. Ninaposoma uandishi kama huu, uliosheheni maneno na tamathali murua, hadi kuleta picha kamili na ya kugusa ya kile kinachoelezwa, huwa najiuliza kama kweli sisi wa-Tanzania tutaweza kufikia kiwango hiki. Ni changamoto kubwa na ni kipimo cha kujipima uwezo wetu:

We drove for hours; whistling over a ribbon of tarmac measuring the perpetual embrace of the shore and the sea, bounded by a fretwork of undulating coconut trees, pure unadorned forms framing the seascape into a kaleidoscope of bluish jewels. Above us a tracery of green and yellow leaves arrowed to a vanishing-point we could never reach. At times the road curved as though it were the edge of a wave itself rushing in and then retreating into the ocean. We skittered over these moving surfaces at a speed I had never experienced before. Through the back window I watched the road pour out from under us and settle into a silvery picture of serene timelessness. We overtook the occasional bus belching smoke or a lorry lisping with billowing hay; we blasted through bustling towns and torpid villages. We passed churches and temples, crosses and statues, grey shacks and lattice-work mansions.... (uk. 69)

Pamoja na mengine yote tuliyojadili darasani kwangu, niliwaelekeza wanafunzi kwenye kifungu hiki, kama mfano wa uandishi bora wa ki-Ingereza. Wanafunzi hao ni wa-Marekani, ambao lugha yao ni ki-Ingereza. Inakuwa ni changamoto ya aina yake kwao.