Laiti ningekuwa kama Hemingway , mwandishi maarufu sana duniani. Ningeandika kuhusu nchi yangu na watu wake kwa umakini, ubunifu, na ukweli wa kumgusa kila msomaji. Ningeandika kuhusu maziwa, mito, milima na mabonde. Ningeandika kuhusu fukwe, nyanda na visiwa. Ningeandika kuhusu miji na vijiji, mitaa na vitongoji. Nimetamka hayo , na nimeanza kufanya mazoezi . Lakini bado njia ni ndefu mbele yangu. Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyeangalia mazingira, matukio, na tabia za wanadamu kwa macho na akili yote, aliyejawa nidhamu ya kutumia lugha, akiangalia kila neno, tena na tena, akibadili na kusahihisha tena na tena, akitafuta namna ya kuandika sentensi sahihi yenye ukweli mtupu. Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyetufundisha kuwa kazi ya mwandishi ni kujitoa mhanga ili nafsi yake yote ibakie katika kitabu tu, asibakishe hata chembe nje ya kitabu. Kila kitabu kiwe ni mauti ya mwandishi, vinginevyo kitabu hiki ni mzaha na udanganyifu. Je, nitayaweza hayo? Hemingway aliandika kuhus