Sunday, January 31, 2010

Nimefika Chuoni Augustana

Jana nilifika chuoni Augustana, Illinois, kutoa mihadhara. Jana jioni niliongea na walimu wachache kuhusu masuala ya utamaduni na utandawazi katika dunia ya leo na umuhimu wa kuwaandaa wanafunzi wetu ipasavyo. Leo nimepata fursa ya kuongea na wanafunzi wapatao 40, ambao wanaenda Ghana na Senegal kwa masomo.Nimekuja hapa chuoni Augustana kusaidia kukuza mpango wa masomo kuhusu Afrika. Profesa John Tawiah Boateng, kutoka Ghana, aliyesimama nami hapa juu, kulia, ni mmoja wa wahusika wa mpango huu, chini ya mratibu wa masomo yahusuyo nchi za nje katika chuo cha Augustana, Dr. Kim Tunicliff. Hapa chini wanaonekana wote wawili, Dr. Tawiah Boateng akiwa katika kunitambulisha kwa waliohudhuria.
Dr Tunicliff tulifahamiana miaka iliyopita, alipokuwa makamu rais wa jumuia ya vyuo vinavyoshirikiana katika eneo la Marekani ya Kati, Associated Colleges of the Midwest (ACM). Nilikuwa mwanabodi katika bodi ya uongozi wa jumuia ya vyuo hivi, nikiwa mshauri wa mipango ihusuyo ushirikiano kati ya vyuo hivi na Zimbabwe na Tanzania. Ingawa yeye alishaondoka ACM, mimi bado ni mwanabodi. Ni wakati huo wa uongozi wa Dr. Tunicliff ndipo nilipohamasika kuandika kitabu cha Africans and Americans, ili kuchangia suala la kuwaandaa wanafunzi waendao Afrika. Hayo nimetaja katika utangulizi wa kitabu.. Katika kunitambulisha, Dr. Tawiah Boateng aliongelea mengi kuhusu shughuli zangu za utafiti na ufundishaji na pia shughuli za kuendeleza mipango ya kuwapeleka wanafunzi Afrika. Yeye, sawa na Dr. Tunicliff wanakipenda kitabu changu na wanakitumia katika matayarisho ya wanafunzi waendao Afrika. Nilitumia muda wa saa moja na nusu kuongelea masuala mbali mbali ya kuwatayarisha wanafunzi hao kwa safari yao ya Ghana na Senegal. Nilisema kuwa kuishi katika utamaduni tofauti na wetu ni changamoto inayotuelimisha kuhusu mapungufu yetu na pia kutupa fursa ya kuwaelimisha wengine. Mapungufu hayo ni pamoja na tabia ya kudhani kuwa tunavyofanya katika utamaduni wetu ni sahihi, na watu wa utamaduni tofauti wanahitaji kurekebishwa. Huo ni mtego unaotukabili sote. Katika kuandika kuhusu utamaduni wa wengine kazi kubwa ni ya kujisafisha roho ili tuweze kuandika kwa kutumia misingi ya kila utamaduni, badala ya kutumia misingi ya utamaduni wetu kama kigezo cha ubora. Baada ya mhadhara wangu na masuali, tulitawanyika, tukaenda kupata chakula cha jioni.

Kwa mwandishi yeyote ni faraja kuona maandishi yake yanasomwa kwa makini. Nami nilifurahi kuona kuwa wote waliohudhuria walikuwa wamesoma kitabu changu. Masuali waliyouliza yalionyesha kuwa wamefuatilia kwa makini yale niliyoandika. Baada ya yote, baadhi ya wanafunzi waliendelea kuongea nami, na niliombwa kuweka sahihi kwenye nakala za vitabu vyao, kisha tukapiga hii picha ya mwisho.

Monday, January 25, 2010

Kiapo cha Uraia wa Marekani

Mtu anapoomba uraia wa Marekani, anakula kiapo, wakati wa kupewa uraia huo, na katika kiapo hiki anatamka kuwa hatambui mamlaka ya kiongozi wa nchi anakotoka juu yake, wala hatambui mamlaka ya serikali ya nchi anakotoka juu yake. Anaukana kabisa utii na uaminifu kwa kiongozi, serikali au himaya ya nchi alikotoka. Kiapo ni hiki hapa:

I hereby declare, on oath, that I absolutely and entirely renounce and abjure all allegiance and fidelity to any foreign prince, potentate, state, or sovereignty of whom or which I have heretofore been a subject or citizen; that I will support and defend the Constitution and laws of the United States of America against all enemies, foreign and domestic; that I will bear true faith and allegiance to the same; that I will bear arms on behalf of the United States when required by the law; that I will perform noncombatant service in the Armed Forces of the United States when required by the law; that I will perform work of national importance under civilian direction when required by the law; and that I take this obligation freely without any mental reservation or purpose of evasion; so help me God.

Friday, January 15, 2010

Kitabu Kuhusu Mlima Kilimanjaro

Asubuhi ya leo, nikiwa nazunguka katika duka la vitabu hapa chuoni St. Olaf, niliona kitabu kipya kuhusu Mlima Kilimanjaro. Nilikichukua na kuanza kukisoma. Ni kitabu chenye maelezo yalioyoandikwa na Michael Moushabeck na picha zilizopigwa na Hiltrud Schulz.

Mwanzoni mwa kitabu, Moushabeck anasema kuwa wazo la kitabu hiki alilipata wakati anahudhuria tamasha la vitabu London. Pale alikutana na mwandishi ambaye alikuwa ana mswada wa kitabu kuhusu Kilimanjaro. Waliongea, na Moushabeck akaamua kusafiri kuja Tanzania.

Kitabu hiki ni rekodi ya safari hiyo, kwa maneno na picha. Moushabeck anasema kuwa alijiandaa kwa kusoma sana kuhusu Mlima Kilimanjaro na mambo mengine, kabla na wakati wa safari ya kuja Tanzania. Na katika kitabu hiki anatumegea mawili matatu aliyoyapata katika kusoma huko. Kwa mfano, amemnukuu Ernest Hemingway, yule mwandishi maarufu, alivyouelezea Mlima Kilimanjaro. Amewanukuu waandishi maarufu kama T.S. Eliot, Marianne Moore, na kadhalika. Kitabu hiki kinavutia, kwa maelezo yake mazuri na picha.

Kama ilivyo kawaida yangu, nilipokuwa nakisoma, nilishindwa kujizuia kuwazia uzembe wa wa-Tanzania. Jambo hili nimelilalamikia na nitaendelea kulilalamikia. Wa-Tanzania hawaonekani kwenye matamasha ya vitabu. Sasa je, akili wanayoipata wenzetu kwenye shughuli kama hizi wa-Tanzania wataipata? Wa-Tanzania hawana utamaduni wa kusoma vitabu. Je, wataweza kuitangaza nchi yao kwa ufanisi? Hazina kama Mlima Kilimanjaro imo nchini mwetu. Lakini wanaoitangaza na kufaidika zaidi na hazina hii ni wageni, wakati sisi tunashinda vijiweni tukiilalamikia serikali kwa kukosa sera.

Je, tunahitaji sera ili tununue kitabu na kukisoma? Tutajuaje dunia inavyokwenda? Ni wazi kuwa, katika mchakato wa maendeleo ya dunia, wa-Tanzania watakuwa wasindikizaji. Ni wazi kuwa wameamua hivyo, na wameridhika. Nimeelezea sana matatizo ya wa-Tanzania katika kitabu changu kipya, CHANGAMOTO.

Saturday, January 9, 2010

Arusha na Kansas City: Miji Rafiki

Kama ilivyo kwa miji mingi hapa Marekani na duniani kwa ujumla, mji wa Kansas una utaratibu wa kujenga urafiki na miji mingine duniani. Arusha ni mji moja ambao tayari una urafiki huo na mji wa Kansas, kama inavyoonekana kwenye tovuti hii.

Nilifahamu habari ya uhusiano huu baina ya mji wa Kansas na Arusha tangu miaka kadhaa iliyopita, kwa kusoma taarifa mtandaoni. Kuna taarifa nyingi, lakini iliyonivutia zaidi ni ile ya harakati za Pete O'Neal, mwenyeji wa mji wa Kansas, ambaye aliikimbia nchi yake akahamia Arusha. Shughuli zake hapo Arusha ni pamoja na kuwa kiungo baina ya wa-Marekani na wa-Tanzania, kama inavyoelezwa hapa. Habari za mwanaharakati huyu zinaelezwa vizuri katika filamu iitwayo A Panther in Africa.

Katika kufuatilia habari hizi, nilianza kupata wazo la kuwasiliana na watu wa mji wa Kansas wanaoshughulika na mpango huu wa urafiki baina yao na Arusha. Nilishatembelea mji wa Kansas, kwa utafiti kuhusu mwandishi Ernest Hemingway, lakini si kuwa kufuatilia uhusiano baina ya mji huu na Arusha.

Mwaka huu, nilialikwa Kansas. Fursa hii ilitokana na Dr. Mbaari Kinya, mwanasayansi Mkenya, ambaye tulionana kwenye mkutano katika Chuo cha Principia, Illinois, ambapo nilikuwa mtoa mada mwalikwa. Dr. Kinya anaendesha taasisi inayoshughulikia nishati, mazingira, tekinolojia na maendeleo ya wanawake. Taarifa zake hizi hapa. Nilipoelezwa kuwa Dr. Kinya anaishi mjini Kansas, nilimweleza kwamba nafuatilia masuala ya uhusiano baina ya mji wa Kansas na Arusha, naye alisema anafahamiana na mratibu wa mpango huu. Aliporejea Kansas, alimpa taarifa zangu Eslun Tucker, na huo ukawa mwanzo wa mawasiliano baina ya Eslun nami. Kwa bahati nzuri, Eslun ni rafiki ya baadhi ya wa-Kenya waishio Kansas. Nao waliniulizia iwapo ningeweza kuhudhuria kumbukumbu ya Jamhuri ya Kenya, tarehe 12 Desemba. Elsun Tucker ni mama mmoja mwenye mawazo mapana kuhusu ulimwengu. Tofauti na wengi wetu ambao ni wa-Afrika au wenye asili ya ki-Afrika na tumejikita upande wetu tu, yeye ana uzoefu wa watu weusi wa kuanzia Marekani, hadi Caribbean, Afrika Mashariki na Afrika Magharibi.
Nilienda Kansas terehe 12 Desemba, kukutana na wahusika wa mpango huu wa urafiki baina ya Kansas na Arusha na pia kushiriki sherehe za kuazimisha kumbukumbu ya Jamhuri ya Kenya.
Katika kikao chetu alihudhuria pia Harvey Marken. Huyu ni mwalimu na mshiriki katika mpango wa ushirikiano baina ya Kansas na Arusha. Harvey Marken alitembelea Tanzania mara moja, ziara ambayo ilimgusa akaamua kujishughulisha na maendeleo ya shule ya Shangarao.

Alikuwepo pia Deo Rutabana, mwenyekiti wa jumuia ya wa-Tanzania wa mjini Kansas. Yeye ni mdau wa shughuli za maendeleo Tanzania. Nilivutiwa na ajenda za timu hii ya Kansas na ari yao ya kujenga na kuboresha mahusiano baina ya watu wa Marekani na Tanzania na Afrika kwa ujumla
Kati ya shughuli wanazofanya ni kuwawezesha watu kutoka miji hiyo miwili kutembeleana. Safari hizi zinahusisha watu wazima, vijana na watoto wa shule pia. Lengo moja kubwa ni kukuza maelewano baina ya watu wa Tanzania na Marekani.
Watu walioanzisha wazo hili la kujenga uhusiano baina ya mji wa Kansas na Arusha huenda walikuwa na ajenda fulani maalum, kwa mujibu wa taratibu za mipango ya aina hii. Lakini ukweli ni kuwa mbegu iliyooteshwa imekua na kueneza matunda sehemu nyingi. Imezaa mipango mingi yenye wahusika wa sehemu mbali mbali, Marekani na Tanzania. Mtandao huu utaendelea kupanuka.
Lengo langu kubwa ni kutafakari namna mahusiano ya aina yoyote baina ya watu wa tamaduni mbali mbali yanavyoathiriwa na tofauti za tamaduni.
Ni wazi kuwa, katika suala kama hili la uhusiano baina ya Arusha na Kansas, masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa m-Tanzania na ule wa m-Marekani yatajitokeza. Ni lazima yashughulikiwe, sambamba na masuala mengine yote.
Katika mazungumzo ya aina hii tuliyofanya, mambo mengi yalijitokeza, mawazo na ushauri. Ni namna nzuri ya kuboresha mipango ilikwisha anza, na pia kuandaa mipango mingine.


Kamati ya Kansas inafahamu umuhimu wa kushughulikia suala la utamaduni. Kwa mfano, imeandaa kijitabu cha kufundishia ki-Swahili. Kuna wazo pia la kuandaa kijitabu kuhusu mapishi na vyakula. Zote hizi ni juhudi za kuuleta utamaduni wa ki-Tanzania katika mawazo na maisha ya watu wa Marekani. Ni muhimu vile vile wa-Tanzania nao tufanye juhudi kuwaelewa wa-Marekani, ili tunapokuwa pamoja tusiwe tunakutana kama wageni daima. Tunayo fursa ya kupunguza ugeni na kujenga maelewano ya karibu zaidi.