Monday, August 17, 2015

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kusherehekea siku hii. Kati ya hao marafiki, napenda kuwataja wawili wanaoonekana pichani hapa kushoto. Kulia anaonekana Larry Fowler, na kushoto anaonekana Bob Mitchell. Mwaka jana nilipokuwa nimelazwa hospitalini mjini Minneapolis, walifunga safari kuja kuniona. Zikipita wiki mbili tatu hatujaonana, hawakosi kunitafuta. Wanafurahi kupiga gumzo na michapo nami.

Waliniletea ujumbe siku zilizopita, wakisema kuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu wangependa kunipeleka mahali tukale chakula cha mchana. Siku zilivyopita, walikuwa wananikumbusha. Leo, nilipomaliza kufundisha, Larry alinifuata chuoni St. Olaf tukaenda kwenye hoteli ambapo tulipata chakula na kupiga michapo.

Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuishuhudia siku hii. Ni neema ambayo sistahili. Napaswa kutambua kwamba kila siku katika maisha yangu ni dhamana, niitumie kwa mambo mema. Nizingatie wajibu wa kuvitumia kikamilifu vipaji alivyonipa Mungu kwa manufaa ya wanadamu.

Wengi hawakupata bahati ya kufikia umri niliofikia, lakini wamefanya makubwa, yasiyo kifani. Kama ilivyo kawaida yangu, nawakumbuka hasa waandishi maarufu, kama William Shakespeare, Alexander Pushkin, Ernest Hemingway, na Shaaban Robert. Hawakuishi miaka mingi kama yangu. Kuwafikiria watu kama hao kunanifundisha unyenyekevu. Siwezi kujivunia chochote nilichoweza kufanya, bali ni kumshukuru Mungu na kuendelea kumtegemea.

Inavyoonekana, kila ninaposherehekea kumbumbuku ya siku ya kuzaliwa kwangu, fikra zangu za msingi kuhusu maisha yangu zinajirudia. Ninajikuta nikifananisha mchango wangu ulimwenguni na ule wa watu maarufu, na kukiri kuwa, ingawa ninajitahidi, mchango wangu bado ni hafifu. Nimekuwa nikiandika hivyo katika blogu hii. Hii ni changamoto kwangu, daima na siku zijazo.

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele nakukutakia siku njema ya kuzaliwa. Mungu azidi kukupa siha na uhai uishi kuiona mia na ushei, Aaamin. Nimependa uwazi wako wa kuweka wazi tarehe uliyozaliwa tofauti na wengi wanaoigiza mambo kiasi cha kuficha umri wao sijui ili iweje japo ni chaguo lao. Nakushauri uzidi kunywa chai kwa sana kwani ni mojawapo ya vinywaji safi kwa umri mrefu.

Happy Birthday Prof Mbele,
Happy Birthday to you
May you live happily
May you do what you want to do
May you remain healthy and active
May you always be impressive
Have a very spiffy Birthday brother Mbele

Mbele said...

Ndugu Mhango

Shukrani kwa ujumbe wako murua. Kwa kweli sioni shida kuelezea mambo yangu binafsi. Hata kitabu changu kiitwacho "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences" kina mambo yangu binafsi ambayo wachache wangethubutu kuyaanika hadharani, hasa wasomi wa kiwango cha juu, ambao hujiona bora kuliko wanadamu wengine. Mimi najiona mtu wa kawaida sana na hupenda kujichanganya na watu wa kawaida.

Ulivyotaja chai, umenikumbusha ziara yangu ya wiki moja China. Kila mahali wanakukaribisha kwa chai. Wote tunajua jinsi Wa-China wanavyozienzi dawa na matibabu yao ya jadi, na walinieleza manufaa ya chai.

Narudia shukrani, na nakutakia kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...