Sunday, June 29, 2014

Maelezo Mafupi Kuhusu Kitabu Changu cha "Africans and Americans"Wiki kadhaa zilizopita, katika blogu hii, walijitokeza watu kwa jina la "anonymous" wakisema hili au lile kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kitu cha kushangaza ni kuwa hapakuwa na dalili yoyote kuwa watu hao walikuwa wamekisoma. Jambo hili halikubaliki popote, nami niliwashutumu hao akina "anonymous."

Kitu kingine cha kushangaza ni kuwa wote wametokomea gizani; hawajasikika tena. Ingekuwa ni watu makini, walioelimika, wangeonyesha kile kinachoitwa "intellectual curiosity." Wangeweza kukitafuta kitabu hiki wakakisoma, halafu wakaja na uchambuzi wao uliojikita katika kuelewa wanaongelea nini.

Utaratibu ni kuwa mtu unasoma kitabu na kisha unakijadili. Tena ni bora ukinukuu vifungu kutoka katika kitabu hicho, ili kuthibitisha kauli zako. Huu ndio utaratibu unaotegemewa na kukubalika. Hakuna hata "anonymous" moja aliyenukuu neno lolote kutoka katika kitabu changu. Kama kitabu hujakisoma, ni bora ukae kimya, uwasikilize waliosoma.

Kuna wanablogu kadhaa ambao wamekisoma kitabu hiki na wamekiongeleqa kwa msingi huo. Mifano ni Jeff Msangi, Simon Kitururu, Yasinta Ngonyani, Dada Subi, Bwaya, na Sophie Becker. Hao wote, baada ya kukisoma kitabu changu hiki, wamekiongelea mtandaoni.

Haingekuwa lazima akina "anonymous" wanunue kitabu changu, kwani kinapatikana katika maktaba kadhaa. Lakini napata picha kuwa watu hao hawajaelimika, kwani hawakuonyesha hiyo "intellectual curiosity" kuhusu suala hilo ambalo walikuwa wanalitolea kauli. Kwa mtazamo wangu, ishara muhimu ya kuelimika ni kuwa na hii "intellectual curiosity" maisha yote.

Utaratibu ni kuwa mtu unasoma kitabu na kisha unakijadili. Mimi kama mwandishi nimewahi kuelezea mazingira yaliyonifanya nikaandika kitabu hiki, na sababu za kuandika. Nilielezea malengo yangu. Katika video ambayo nimeiweka hapa, nimeongelea kwa kifupi sana, mazingira yaliyonifanya niandike kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na namna wasomaji wanavyokiona. Sikuelezea kila kitu, bali ni muhtasari tu. Tena, nilikuwa sijajiandaa, bali yalikuwa ni mazungumzo ya papo kwa papo.

Ni muhimu, tunapokiongelea kitabu, pamoja na mengine yote, kuangalia malengo ya mwandishi, ambayo huwa yametajwa katika kitabu chenyewe. Tathmini ya kitabu inapaswa kuangalia pia iwapo mwandishi amefanikiwa kutimiza malengo yake au la. Tunapokuwa tumekisoma kitabu, tunakuwa na uwezo na haki ya kuelezea chochote kilichomo, kiwe ni kizuri au dosari.

Kama una ufahamu wa kutosha, ukaelezea dosari za kitabu, unakuwa umemsaidia mwandishi. Mimi mwenyewe ni mhakiki, na nimechapisha tahakiki za vitabu kadhaa, nikielezea ubora na dosari zake. Na hilo ndilo nililotegemea, na ndilo ninalotegemea, kutoka kwa yeyote anayeongelea vitabu vyangu. Ni suala la kuelimishana.

Friday, June 27, 2014

Ninaendelea Kupona

Picha hizi nimejipiga mwenyewe dakika chache zilizopita, mchana huu. Ninajaribu kujizoeza mtindo huu wa kujipiga picha. Lakini vile vile, nimeona niziweke hapa, ili kuwathibitishia ndugu, marafiki na wengine wanaonikumbuka, kwamba hali ya afya yangu inaendelea kuimarika. Wasiwe na wasiwasi sana juu yangu. Yaonekana Mungu ameamua niendelee kuwepo duniani na kutekeleza majukumu kwa jamii.

Nawashukuru wote kwa kuniombea, nami, kama nilivyowahi kutamka, nategemea kuingia tena darasani kufundisha wiki ya kwanza ya Septemba, utakapoanza muhula mpya.

Hiki kikofia nilichovaa alininunulia binti yangu Zawadi. Ninakipenda sana, hasa kwa vile tuko katika kipindi cha jua hapa Marekani.

Sunday, June 22, 2014

Ziara Fupi Mjini Northfield, Minnesota

Jana alasiri, binti yangu wa kwanza, Deta, alinipeleka hapo katikati ya mji, eneo la posta. Nilitaka kwenda kuangalia mafuriko ya mto Cannon, ambayo niliyaelezea jana katika blogu hii. Hapa naleta picha kadhaa alizopiga. Sikujua kama amewahi kupiga picha.

 
Nilifurahi nilipoziona picha alizopiga, ingawa yeye si mzoefu. Ninaonekana katika hizi picha zote. Katika picha mbili, mto wa Cannon, ambao umefurika, unaonekana pia.
Nimezileta picha hizi ili kuwathibitishia ndugu na marafiki kuwa hali ya afya yangu inaendelea kuwa njema, ingawa imechukua miezi mingi sasa. Ninategemea kuanza kufundisha tena wakati muhula mpya wa shule utakapoanza, wiki ya kwanza ya mwezi Septemba, Insha'Allah.


Hapa kushoto naonekana nimeketi sehemu ya "park" hapa mjini. Nimeshika mkongojo ambao umenisaidia kutembea kwa miezi kadhaa, ila sasa naweza kutembea bila kuutumia.Nimetoka mbali; namshukuru Mungu.

Saturday, June 21, 2014

Mafuriko Marekani

Wa-Tanzania tumezoea kusoma habari za mafuriko yanayotokea Dar es Salaam wakati wa mvua. Tumezoea kutoa lawama kwa wahusika wanaopaswa kushughulikia miundombinu na pia tunatoa lawama kwa watu wanaoishi mabondeni, kwani tunasikia ripoti kadha wa kadha kuwa wanagoma kuhama. Kumbe, adha ya mafuriko na maafa mengine ya aina hiyo hutokea sehemu mbali mbali za dunia, kama tunavyosikia katika vyombo vya habari. Hapa Marekani, kwa mfano, mafuriko hutokea mara kwa mara, sababu ya mvua kubwa, au wakati barafu na theluji zinapoyeyuka kufuatia kumalizika kipindi cha baridi kali. Mito hujaa, madaraja hufurikwa, nyumba za watu na sehemu za biashara huathirika.

 Wiki hii, katika jimbo hili la Minnesota na sehemu za jirani, kuna mafuriko makubwa kutokana na mvua kubwa. Uongozi wa jimbo unahangaika kujiandaa kutathmini hasara inayotokea, na kuna taarifa kuwa uongozi huo umepeleka habari kwa Rais Obama, ili atangaze hali ya dharura. Tangazo la aina hii huiwezesha serikali kutoa pesa za kufidia hasara. Serikali ina fungu maalum la fedha kukabiliana na dharura kama hizo Nimepiga picha hizi katika mji mdogo wa Northfield, ambapo ninaishi. Kuna mto unaopita mjini humo, ambao unaitwa Cannon River. Unaweza kuona jinsi ulivyofurika, hali ambayo hutokea mara moja moja, wakati wa mvua kubwa au kuyeyuka kwa barafu na theluji. Mito mingine ya sehemu hii ya Marekani imefurika pia. Taarifa zilizopo ni kuwa mto Mississippi, ambao hauko mbali na hapa, unaendelea kufurika, ingawa tayari umeshafurika.

Nimeleta habari hii, ili kukumbushia kuwa maafa hutokea sehemu mbali mbali za dunia, hata katika nchi zenye miundombinu imara na bora kama Marekani. Mbali ya mafuriko, hapa Marekani kuna vimbunga viitwavyo "tornado" ambavyo uharibifu wake hausemeki. "Tornado" ikitua kwenye mji, inavunja majumba na hata kurusha magari hewani na kuyabwaga sehemu tofauti, pengine mbali na pale yalipokuwepo. Sehemu zingine za dunia zinakumbwa na kimbung, sehemu zingine zinakumbwa na tetemeko la nchi na kusababisha uharibifu mkubwa. Hivi karibuni, kwa mfano, tumeshuhudia jinsi sehemu ya mlima ilivyoporomoka kule Afghanistan na kupoteza maisha ya watu wengi na mali zao. Kilichopoo, pamoja na kuchukua tahadhari, kama vile kujenga katika maeneo yanayoonekana yana usalama, tukae tukiomba Mungu atuepushie mbali majanga hayo.

Thursday, June 19, 2014

Tamthilia ya Shakespeare Imenijia Katika Ndoto

Usiku wa kuamkia leo, niliota ndoto fupi, na katika ndoto hii nilijikuta nakumbuka maneno ya Morocco, mhusika katika tamthilia ya Shakespeare, "The Merchant of Venice." Maneno yenyewe ni haya:

As much as he deserves! Pause there, Morocco,
And weigh thy value with an even hand,
If thou be'st rated by thy estimation,
Thou dost deserve enough; and yet enough
May not extend so far as the lady....

Nimefurahi kuwa nimeikumbuka ndoto hii, na maneno haya ya Morocco, wakati akijaribu bahati yake ya kumpata mrembo Portia.

Nilipokuwa kijana, kati ya waandishi niliowapenda sana ni Shakespeare. Marafiki zangu na mimi tulipenda sana hotuba za wahusika wa tamthilia za Shakespeare, tukafurahia kuzikariri, tukistaajabu umahiri wa Shakespeare katika kutumia lugha na kuelezea masuala mbali mbali.

Shaaban Robert alimwenzi sana Shakespeare. Alisema kuwa akili ya Shakespeare ilikuwa kama bahari, ambayo mawimbi yake yaligusa kila pwani ya dunia.

Labda wakati umefika wa kusoma tena tamthilia za Shakespeare.

Thursday, June 12, 2014

Tuyatunze Mazingira

Kitu kimoja kinachofurahisha hapa ninapoishi na kufanya kazi, ni jinsi mazingira yanavyotunzwa.
Kila siku naenda nje na kunyoosha miguu, ili kusaidia uponaji wangu.
Nina mazoea ya kuketi na kuangalia mimes mbali mbali, maua, na nyasi zilivyokatwa vizuri au zilivyoondoshwa ili kuipisha miti ya maua.. Ni mazingira yanayopendeza sana.Ndege wa aina aina wanafuata sehemu hizo, nami nimezoea kuwaangalia. Wanapendeza.


Vinyama vidogo vidogo naviona vikicheza.

Hewa ni safi. Inaburudisha nafsi. Mazingira yamependezeshwa pia kwa maua.


Hapa nimeweka picha kadhaa nilizopiga hatua chache kutoka maskani yangu.

Hakuna takataka kama vile plastiki, matairi yaliyochakaa, makopo, na uchafu mwingine ambao umesagaa sehemu nyingi za nchi kama Tanzania.

Baada ya kuyazoea mazingira haya safi, nakerwa  kuangalia hali kama ile ya Dar es Salaam. Inakuwa vigumu kuamini kama mji ule wanaishi watu.

Milima ya takataka imezagaa mitaani.  Mitaro yenye maji machafu sana inapita humo mitaani. Hakuna anayeshtuka kuona ukatili huu wa kutisha dhidi ya mazingira. Waliosoma na wasiosoma na hao tunaowajta viongozi, wote hawana elimu. Wanaendeleza ukatili huu dhidi ya mazingira, pamoja na kwamba hali hiyo ni chimbuko la magonjwa.

Wednesday, June 4, 2014

Kazi na Dawa, Longido


Hapa niko katika baa mojak kwenye mji mdogo wa Longido. Ilikuwa ni mwezi Januari, 2013, wakati nilipokuwa Tanzania nikiendesha kozi ya "Hemingway in East Africa." Naonekana nikisoma kitabu kimoja cha Hemingway, True at First Light.

Nadhani tulikuwa na kipindi baadaye mchana ule, nami nilikuwa katika maandalizi.


Kutokana na kazi nzito, na pia joto, ilinibidi kujipatia kitu kidogo cha kuburudisha koo na akili. Hapa naonekana nimeshika kachupa ka bia na glasi.

Watanzania wengi tumejiaminisha kuwa katika hali ya uchovu na joto, bia ndio wakati wake. Tunasema "kazi na dawa." Sijui kama ni ukweli au tumejiwekea hiyo dhana kwa maslahi yetu tu, au ni uzembe. Labda soda ingetosha, au maji. Sijui.

Tuesday, June 3, 2014

Wanafunzi Wangu Kwenye Lango la Ngorongoro

Katika mizunguko na wanafunzi wangu kaskazini mwa Tanzania, mwezi Januari 2013, tulifika pia kwenye hifadhi za Taifa.

Picha hii hapa kushoto nilipiga kwenye lango la kuingilia Ngorongoro. Tulikuwa tumeshaangalia ndani,  na sasa tulikuwa tunarudi tena kwenye magari, kuendelea na safari ya kuingia katika hifadhi.

Walikuwepo wanafunzi 29, wote kutoka chuo cha St. Olaf, Minnesota, ambapo nafundisha. Niliwaleta Tanzania kujifunza kuhusu mwandishi Ernest Hemingway: safari zake na kuishi kwake Afrika Mashariki, tukiwa tunasoma maandishi yake kuhusu sehemu hizo, hasa Green Hills of Africa na True at First Light, na pia hadithi fupi, barua, na makala katika majarida.

Hemingway alisafiri na kuishi Afrika Mashariki miaka ya 1933-34 na 1953-54.

Wanafunzi waliifurahia sana safari hii na walijifunza mengi, ambayo kwa ujumla huwa hayafundishwi katika vyuo. Nimefanya utafiti wa miaka karibu kumi, na ndio msingi wa kutunga kozi hii iitwayo "Hemingway in East Africa." Nimeandika mara kadhaa katika blogu zangu kuhusu kozi hii.