Thursday, July 23, 2020

Kitabu Muhimu kwa Wageni Marekani

Tarehe 11 mwezi huu, nilipata ujumbe kutoka kwa jamaa aishiye eneo la kati la jimbo hili la Minnesota. Anasema kuwa wana jumuia yao ambayo inawakaribisha na kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi kimaisha. 

Anasema kuwa wanatumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na wanakiona ni bora sana kwa malengo yao. Kauli kama hizi si ngeni kwangu. Nimezisikia tangu mwaka 2005 nilipochapisha kitabu. Sehemu ya ujumbe ni hii hapa:

I  have been involved with a local organization in St. Joe that works to help refugees and immigrants adjust to and succeed in central Minnesota. Our group is called Cultural Bridges. 

I have been sharing your book, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, with members of our group. Everyone who has read it has really enjoyed it and we see it as an excellent resource as we work to fulfill our mission as an organization.

Friday, July 17, 2020

Yatokanayo na Picha ya Msomaji Nami

Picha hii ilipigwa tarehe 27 Julai, 2019, Soma Book Cafe, Dar es Salaam. Wadau wa vitabu, yaani waandishi, wachapishaji, wauzaji, na wasomaji wa vitabu, tulikusanyika kuongelea masuala yanayotuunganisha.

Huyu ninayeonekana naye pichani ni Chiombola Joseph ambaye nilimfahamu siku hiyo. Nilikuwa nimetoa mhadhara kuhusu "Writing About Americans," naye akawa mmoja wa wale walionunua vitabu vyangu vilivyokuwa vikiuzwa na Soma Book Cafe. Napenda kusema neno juu ya hilo na mengine yatokanayo.

Uamuzi wa kununua kitabu si wa kawaida na si rahisi katika jamii yetu waTanzania. Huyu ndugu alinunua viwili. Sikumbuki wanauzaje, lakini lazima nusu laki au zaidi ilimtoka. Zingatia kuwa vitabu vyangu si udaku na haviko katika orodha ya vitabu vinavyofundshwa mashuleni na vyuoni nchini. Anayeamua kununua vitabu vyangu Tanzania ninamwona kama mtu wa pekee. Najiuliza, ni nini kinachomtuma kufanya hivyo? Bila shaka ni hamu tu ya kutaka kujua mambo. Mimi mwenyewe niko hivyo. Sichoki kununua na kusoma vitabu.

Kwa upande wangu kama mwandishi, na ili kuwajuza wasomaji wangu, napenda niseme kwamba kitu kimojawapo kilichonisukuma kuandika hivi vitabu viwili ni kule kutoridhika kwangu na vitabu vya wengine nilivyovisoma.

Nilikuwa ninafundisha "Oral Literature" (fasihi simulizi) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976. Mwaka hadi mwaka, sikuona kitabu cha nadharia kilichoniridhisha kwa kufundishia somo hilo.

Jawabu likawa kwamba kulalamika kuhusu hali hakutoshi. Ni lazima kutafuta suluhu. Nikaamua kuanza kuandaa kitabu ambacho kingeniridhisha. Baada ya miaka 23 nilichapisha kitabu cha "Matengo Folktales." Hadi sasa ninaridhika nacho, na waalimu wengine wanakitumia kufundishia, kama vile hapa Marekani na Uingereza.

Habari ni hiyo hiyo kuhusu kitabu cha "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Tangu kuja kwangu kufundisha hapa Marekani, mwaka 1991, nilihusika kama mshauri katika programu za ushirikiano baina ya vyuo vya Marekani na nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.

Nilikuwa mtoa ushauri katika masuala ya tofauti za tamaduni, ili kuwaandaa wanafunzi kabla hawajaenda Afrika, na pia baada ya wao kurejea tena Marekani, kujibu masuali yao kuhusu yale waliyoyashuhudia Afrika.

Niliona mapema kuwa hapakuwa na kitabu cha kuniridhisha kuhusu masuala hayo. Suluhisho likawa kuandaa kitabu changu, kazi iliyonichukua muda mrefu, hasa mwaka 2005 ambapo nilizama katika kazi hiyo tu kwa miezi yapata mitano. Ninaridhika na kitabu hiki, na maelfu hapa Marekani wamekisoma na wengi wanakisoma.

Hata hivi, ninaandika kitabu kingine juu ya mada hii ya tofauti za tamaduni, ili kufafanua zaidi mawilii matatu niliyoongelea au kugusia, na pia kuleta mapya.

Kwa hiyo, utaona kwamba kwa kiasi fulani, vitabu ninaandika kujiridhisha mimi mwenyewe, ingawa nina lengo la kuelimisha wengine pia. Ni kazi ngumu inayohitaji ustahimilivu mkubwa. Kama unawazia hela, utaona kuwa ni kazi isiyolipa. Ukitaka hela, achana na wazo la kitabu, uende Mererani ukatafute mawe ya tanzanite.

Mtu anayenunua kitabu changu namwona kama ameanzisha uhusiano fulani nami. Anaingia katika nafsi yangu na kujionea, angalau kwa kiasi fulani. Uhusiano huo ni wa kudumu, kwani si rahisi mtu kusahau kila alichosoma kitabuni, hasa pale anapokutana na jina la mwandishi au taarifa yoyote juu yake.

Thursday, July 16, 2020

Sasa Nimesoma "The Comedy of Errors" (Shakespeare)

Jana nilimaliza kusoma "The Comedy of Errors," tamthilia mojawapo ya Shakespeare, ambaye alliandika tamthilia 37, na labda zaidi kidogo. Katika ulimwengu wa fasihi, Shakespeare ni kinara. Wanafasihi wanaweza kuhoji kwa nini ninatumia neno fasihi kuziongelea tamthilia. Malumbano huenda yasiishe.

"The Comedy of Errors" ni tamthilia inayoelezea matatizo na mikanganyiko itokanayo na uwepo wa watu kadhaa katika jamii ambao wanafanana maumbile na sura kiasi kwamba ukikutana na mmoja, halafu baadaye ukakutane na mwingine, hutajua hata kidogo kuwa ni mwingine. Tamthilia hii inaonyesha migogoro, kutoelewana, na magomvi kwa sababu hiyo.

Kusoma maandishi ya Shakespeare kunahitaji mwendo wa taratibu. KiIngereza chake ni cha zamani, miaka mia tano iliyopita, na utamaduni ni vile vile. Ni chemsha bongo kwa sisi watu wa leo, sawa na kusoma tungo za zamani za kiSwahili kama vile "Al Inkishafi" au "Utenzi wa Rasi 'lGhuli." Kwa mtazamo wangu, chemsha bongo hii ina manufaa kwa afya ya akili, sawa na mazoezi ya mwili yalivyo na manufaa kwa afya zetu.

Shakespeare ni mwandishi wa waandishi. Alitambuliwa na anaendelea kutambuliwa hivyo na waandishi wakuu duniani. Shaaban Robert, mwandishi wetu maarufu kuliko wote, alisema kuwa akili ya Shakespeare ni kama bahari kubwa sana, ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe zote za dunia.

Saturday, July 4, 2020

Tunasoma Fasihi ya Afrika

Baada ya muhula wa masomo kwisha hapa chuoni St. Olaf, mwezi Mei, sasa ninafundisha kozi maalum ya fasihi ya Afrika. Kwa miaka, nimefundisha kozi hiyo. Ni fursa kwa watu kuufahamu mchango wa waAfrika katika kutafakari masuala ya maisha ya binadamu (kwa maana ya kifalsafa ya "the human experience" na "the human condition") kwa njia ya fasihi.

Ninapofundisha fasihi ya Afrika, ninaanza kwa kuielezea Afrika kama chimbuko la binadamu, tekinolojia, lugha, fasihi, falsafa, na yengine yite ambayo binadamu anahusika nayo.

Safari hii ninafundisha Changes: A Love Story, Maru, Season of Migration to the North, na Woman of the Ashes.

Nimesoma baadhi ya vitabu vya waandishi wote wanne na caribou vyote nilivyovisoma nilivbsoma katika kufundisha. Naweza kusema ninafahamu zaidi kazi za Ama Ata Aidoo na Mia Couto.

Hata hivyo, vitabu hivi ninavyofundisha sikuwahi kuvisoma. Kila mara ninapofundisha kozi hii, au nyingine yoyote ya fasihi, nina jadi hiyo ya kufundisha angalau baadhi ya vitabu ambavyo sijasoma kabla. Ninajua kuwa kuna waandishi wengi maarufu tangu karne zilizopita na wengine wanaendelea kujitokeza. Kwa hiyo, nami ninataka kujiongezea upeo muda wote.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...