Sunday, June 24, 2018

Maongezi ya Kina Leo na Msomaji Wangu

Leo nimekuwa na maongezi ya kina na msomaji wangu, mchungaji ambaye nilishamtaja katika blogu hii. Tulikutana mjini Hastings, Minnesota, tukaongeaa kwa saa mbili na robo. Tulikuwa tumeahidiana kwamba nikasaini nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho mchungaji alikuwa anampelekea mtu fulani wa karibu.

Tuliongea sana kuhusu shughuli zetu za kuelimisha na kuhamasisha jamii ya watu weusi juu ya masuala ya kujitambua. Mchungaji ameendelea kunifahamisha kuwa kitabu changu kinamsaidia kujitambua kama mtu mwenye asili ya Afrika, ingawa ana pia asili ya ki-Cherokee na ki-Faransa. Anataka kitabu hiki kitumike kuwaelimisha vijana wa-Marekani Weusi, waweze kujitambua na kujivunia walivyo na silika za u-Afrika, ili wasiwe wanabezwa na wazungu.

Nami naelewa vizuri tatizo lilivyo kwa hao vijana. Wanashinikizwa kubadili mwenendo, lugha, na mambo yao mengine, ili wafuate ya wazungu. Mashuleni wanashinikizwa, kudhibitiwa, na kuadhibiwa kwa mienendo yao ambayo mamlaka zinaitafsiri kama utovu wa nidhamu.

Jukumu lililopo, ili pawe na suluhu, ni kwa walimu na viongozi wa shule kufanya juhudi ya kujielimisha kuhusu utamaduni wa wa-Marekani Weusi ambao misingi yake kwa kiasi fulani, au kwa kiasi kikubwa, ni u-Afrika. Wa-Afrika walivyoletwa utumwani huku Marekani, walikuja na tamaduni zao, ambazo zimerithishwa tangu kizazi hadi kizazi, ingawaje zimekuwa zikiathirika na mabadiliko na mazingira kutoka kizazi hadi kizazi.

Hata hivyo, baadhi ya misingi na vipengele vya u-Afrika vimeendelea kuwepo. Kwa mfano, wa-Afrika tuna namna yetu ya kuongea, kama nilivyoelezea katika kitabu changu, hasa kurasa 32-39 na 44-45. Na nimeelezea kitabuni kwamba ninapokutana na wa-Marekani Weusi, ninatambua vipengele hivi vya u-Afrika katika tabia na mienendo yao.

Ninashukuru kufahamiana na mchungaji huyu ambaye ana tafakari za kina kuhusu masuala na ana ukarimu moyoni mwake wa kunielezea anavyojisikia na anavyowazia kuhusu ujumbe wowote uliomo katika kitabu changu. 

Friday, June 22, 2018

Nimehudhuria Mhadhara Kuhusu Frantz Fanon

Jioni hii nilikuwa St. Paul kuhudhuria mhadhara juu ya Frantz Fanon uliotolewa na Dr. Moustapha Diop. Mhadhara uliandaliwa na Nu Skool, jumuia ya wa-Marekani Weusi ambayo nimewahi kuiongelea katika blogu hii.

Niliona ni lazima nikahudhurie mhadhara huu, ambao mada yake ilikuwa "Becoming Fanon: A Portrait of the Decolonized" kwa kuzingatia umuhimu wa fikra za Fanon katika harakati za ukombozi sehemu mbali mbali za dunia, hasa ukombozi wa fikra.

Nilikutana  na fikra za Fanon kwa mara ya kwanza nilipokuwa mwanafunzi chuo kikuu cha Dar es Salaam, katika idara ya Literature, miaka ya 1973-76. Aliyetufundisha ni mwalimu Grant Kamenju, na vitabu vya Fanon alivyotumia ni The Wretched of the Earth na Black Skin White Masks. Katika kufundisha fasihi ya Afrika, ninaona umuhimu wa kurejea katika fikra za Fanon mara kwa mara. Sielewi utakosaje kurejea kwenye fikra za Fanon.

Katika mhadhara wake, Dr. Diop alielezea kifupi maisha ya Fanon, akajikita zaidi katika kufafanua jinsi baina ya mwaka 1956 hadi 1961 Fanon alivyobadilika na kuwa Fanon tunayemjua kama mwanamapinduzi. Fanon alikuja kuwa mwanaharakati hadi akafukuzwa nchini Algeria. Alikwenda Tunisia, ndipo alipoendesha harakati, ikiwemo kuwapiga msasa wapiganaji wazalendo wa Algeria kabla hawajaingia nchini mwao kupambana na jeshi la wakoloni.

Jambo jingine ambalo nimejifunza katika mhadhara huu ni kuwa The Wretched of the Earth hakukiandika, kutokana na hali ya afya yake, bali alimwelezea mke wake kwa mdomo, naye akaandika. Ilichukua miezi kadhaa. Dr. Diop alitoa muhtasari wa mambo muhimu aliyotufundisha Fanon na akawataja watu walioendeleza fikra  za Fanon Afrika na Marekani, wakiwemo Kwame Nkrumah na Steve Biko.

Tuesday, June 19, 2018

Vitabu Vinapobebana

Nadhani kila msomaji wa vitabu anatambua manufaa na raha ya kusoma vitabu vya aina mbali mbali. Hivi ninavyoandika, ninakaribia kumaliza kusoma Riding the Waves of Culture: Understanding Diversity in Global Business, kitabu ambacho nilikitaja siku kadhaa katika blogu hii.

Nimekifurahia sana kitabu hiki, kwa jinsi kinavyoongelea masuala ya tofauti za tamaduni, mada ambayo ninashughulika nayo sana. Kinanifanya nielewe undani wa yale niliyoandika katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Kwa mfano, sura ya kitabu hiki iitwayo "How We Manage Time," imenipa msamiati wa kuelezea yale niliyoelezea katika sura iitwayo "Time Flies But Not in Africa." Nimeelewa kwamba msimamo wetu wa-Afrika ni "synchronic" au "polychronic" na msimamo wa wa-Marekani ni "sequential." Tofauti zetu ambazo nimezielezea katika kitabu changu zimejengeka katika mitazamo hiyo miwili.

Nitoe mfano. Kama ninavyoeleza katika kitabu changu, sisi tunaonekana hatuna nidhamu ya kuchunga muda, katika mazingira yetu, wakati wa-Marekani wanachunga sana muda, katika mazingira yao. Hizi ni tofauti tu, wala si ishara kwamba utamaduni moja ni bora kuliko mwingine. Kila utamaduni una mantiki yake.

Dhana zilizomo katika Riding the Waves of Culture zimenipa mianya ya kufafanua yale niliyoandika katika kitabu changu. Tofauti kubwa kati ya vitabu hivi viiili ni kuwa Riding the Waves of Culture kimeandikwa kitaaluma na ni kikubwa, wakati Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimeandikwa kiwe rahisi kusomwa na yeyote na ni kifupi sana.

Thursday, June 14, 2018

Mwalimu Mwingine Aongelea Kitabu Changu

Ni jadi yangu kuwatambua wasomaji wanaosema neno kuhusu vitabu vyangu. Ni namna ya kuwashukuru kwa kutumia muda wao kukisoma kitabu na kutumia tena muda kuandika maoni yao. Ninatambua kwamba wanafanya hivyo kwa hiari, na wangeweza kutumia muda wao kwa namna nyingine. Ninawashukuru.

Wiki hii amejitokeza mwalimu Khalid Kitito, ambaye amekitumia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika ufundishaji wake hapa Marekani, akaandka maoni kwenye mtandao wa PublicReputation:

Africans and Americans written by Joseph Mbele is an excellent book to read about cultural differences between Americans and Africans. He examined the deep culture and not surface culture. It brings out clearly the understanding as to why Americans and Africans have different perspective of time, relationships, work, family, love, respect among others. I used it to teach in my Culture and Identity Class and found it useful. The book provided a forum for insightful discussions and at the end of the course students were able to view other cultures as different and not weird. It is also easy to read and understand, thus suitable for general readers.

Napenda kugusia tathmini yake kuwa ninaibua "deep culture." Wanataaluma wa tamaduni wanasisitiza suala hili la "deep culture." Tunapokutana na utamaduni wowote, tunaona mambo mengi, lakini ili kuyaelewa yale tunayoyaona, tunatakiwa kuelewa msingi wake. Hii ndio "deep culture." Inachukua muda sana kuuelewa utamaduni kwa maana hiyo. Ndivyo ilivyokuwa kwangu, katika kutafakari utamaduni wa wa-Marekani. Ilinichukua miaka karibu ishirini ya kuishi na wa-Marekani kabla sijathubutu kuandika kitabu changu. Kwa upande mwingine, kwa kuwa mimi ni mtafiti na mwalimu wa fasihi na "folklore" na ni mw-Afrika, haikuwa shida kwangu kuelezea "deep culture" kwa upande wa wa-Afrika.

Pamoja na kumshukuru mwalimu Kitito, kwa kuandika maoni yake, ninatoa mwaliko kwa yeyote mwingine aliyesoma au kutumia kitabu changu chochote kuandika maoni yake katika ukurasa huu wa PublicReputation.

Friday, June 8, 2018

Tunasoma "Homegoing," Riwaya ya Yaa Gyasi


Tarehe 4 Juni, nilianza kufundisha kozi ya kiangazi hapa chuoni St. Olaf juu ya fasihi ya Afrika (African Litterature). Nimefundisha kozi hiyo mara kadhaa miaka iliyopita. Baada ya mimi kutoa utangulizi siku mbili za mwanzo, tulianza kusoma riwaya ya Yaa Gyasi iitwayo Homegoing.

Yaa Gyasi alizaliwa Ghana akakulia hapa Marekani. Nilikutana naye katika tamasha la Hemingway mjini Moscow, katika jimbo la Idaho akiwa ni mgeni rasmi wa tamasha kufuatia riwaya yake kushinda tuzo ya PEN/Hemingway kwa mwaka 2017.

Homegoing, inaturudisha nyuma karne tatu zilizopita, kwenye nchi ambayo leo ni Ghana. Tunaona jamii inavyoishi mila na desturi zake na mahusiano ya watu, lakini tunaona pia shughuli ya biashara ya utumwa. Tunaona jinsi watu walivyokuwa wakitekwa kufanywa watumwa na wengi kupelekwa pwani kwenye kasri ya Cape Coast kuhifdhiwa humo katika mazingira ya ovyo kupindukia, wakisubiri kuvushwa bahari kwenda Marekani.

Homegoing inafaa kusomwa sambamba na tamthilia ya The Dilemma of a Ghost, ya Ama Ata Aidoo, ambayo iliigizwa mara ya kwanza mwaka 1964, ikachapishwa mwaka 1965. Tungo hizi zinafaa kulinganishwa hasa kwa kuwa zinahusika na dhamira ya watu kuchukuliwa kutoka Afrika Magharibi kwenda utumwani Marekani. Vile vile zote zinatumia vipengele vya sanaa ya fasihi simulizi. Wanafunzi wangu nami bado tunaisoma riwaya hii, na tutajua mengi zaidi kadiri tunavyoendelea kusoma.

Sunday, June 3, 2018

Vitendea Kazi vya Kampuni Yangu

Mwaka 2002, nilianzisha na kusajili kampuni ambayo niliita Africonexion, kama nilivyoandika katika blogu hii. Nilisajili kama kampuni binafsi, usajili ambao hapa Marekani hujulikana kama "sole proprietorship." Niliamua kuanzisha na kusajili kampuni hii ya kutoaelimu na ushauri wa masuala ya utamaduni kwa kuwa tayari nilikuwa na uzoefu wa shughuli hizo, nikihudumia vyuo, makanisa, mashirika, jumuia na watu binafsi.

Shughuli zangu hizi zimekuwa na mafanikio makubwa, kwa maana kwamba nimewasaidia watu kuelewa na kuepukana na mambo ambayo yanaweza kusababisha migogoro na kutoelewana. Wale ambao tayari walishakumbana na migogoro na kutoelewana nimewasaidia kufahamu kwa nini walijikuta katika migogoro na kutoelewana. Lakini mimi mwenyewe nimefanikiwa pia kujifunza mengi katika shughuli zote hizo.

Napenda kuelezea siri moja kubwa ya mafanikio haya. Siri hiyo ni kujielimisha kwa kutumia vitabu. Vitabu ndio vitendea kazi vyangu. Sichoki kununua na kusoma vitabu. Kulingana na shughuli za kampuni yangu, ninanunua na ninasoma vitabu kuhusu masuala kama utandawazi, utamaduni, na saikolojia. Jana, kwa mfano, bila kutegemea, nilikiona kitabu kiitwacho Riding the Waves of Culture, katika duka la Half Price Books, mjini Apple Valley. Nilipokiona tu, nilitambua kuwa kitakuwa kitendea kazi muhimu.

Mbali na kutumia vitabu vya wengine, ninatumia pia kitabu nilichoandika mwenyewe, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kitabu hiki kilitokana na uzoefu nilioongelea hapa juu. Si mimi tu ambaye ninakichukulia kitabu hiki kama kitendea kazi muhimu. Mifano ni profesa na mwandishi maarufu Becky Fjelland Brooks, ambaye aliakiongelea kitabu katika blogu yake. Mzee Patrick Hemingway, ambaye aliwahi kuishi Tanzania miaka yapata ishirini na tano, aliwahi kuniambia kuwa kitabu hiki ni "a tool of survival" yaani kimbilio la usalama.

Hili suala la kuviona vitabu kama vitendea kazi ni muhimu. Hainiingii akilini mtu aanzishe biashara, kwa mfano, halafu asitafute na kusoma vitabu au maandishi mengine juu ya uendeshaji wa biashara. Atafanikishaje malengo yake kama hafahamu vitu kama saikolojia ya binadamu, ambao ndio wateja wake? Atafanikiwaje kama hafahamu namna ya kuwasiliana na watu? Kama wateja wake ni wa tamaduni tofauti na utamaduni wake, ni muhimu mno afahamu tofauti hizo.

Nilivutiwa na msimamo wa Mama Barbro Finskas Mushendwa, mmiliki wa kampuni ya utalii ya J.M Tours, yenye makao yake Arusha, Tanzania. Baada ya kusoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, aliamua kununua nakala kadhaa kwa ajili ya wafanyakazi wake, ambao walikuwa ni madreva wa watalii. Aliona haraka kuwa kitabu hiki kinafaa kama kitendea kazi na madreva wake walinithibitishia hivyo, kama nilivyoripoti katika blogu ya ki-Ingereza.

Mmiliki wa kampuni yoyote anajua ulazima wa vitendea kazi kama vile magari na kompyuta, sawa na mkulima navyojua ulazima wa jembe na shoka. Lakini sijui ni wamiliki wa makampuni na wafanya biashara wangapi wa Tanzania wenye mtazamo kama wa Mama Mushendwa, wa kutambua kuwa vitabu ni vitendea kazi. Ninaona wanaanzisha kampuni au biashara na kuziendesha kimazoea,  au kwa kutegemea kudra ya Mungu au hata waganga wa kienyeji. Daima ninaona matangazo ya waganga wa kienyeji wakinadi dawa za mafanikio kibiashara.

Ninapoongelea mada hii ya vitabu kama vitendea kazi, ninakumbuka juhudi aliyofanya Mwalimu Nyerere katika kutekeleza kile alichoita elimu yenye manufaa. Aliwahimiza watu kujisomea ili kuboresha shughuli walizokuwa wanafanya. Chini ya uongozi wake, vilichapishwa na kusambazwa vitabu kuhusu kilimo, uvuvi, useremala, na kadhalika. Ninakumbuka kwamba kijijini kwangu, vitabu hivyo vilihifadhiwa katika nyumba ya baba yangu.

Pamoja na mimi kutumia vitabu vya wengine kama vitendea kazi, ninashukuru kwamba nami ni mwandishi. Ninapangia kuendelea kuandika ili kuchangia ufanisi katika shughuli zangu na za wengine.