Saturday, April 29, 2017

Tamasha la Mataifa Limefana Rochester, Minnesota.

Leo tamasha la mataifa limefanyika mjini Rochester, Minnesota. Niliweka tangazo la tamasha hili katika blogu hii. Binti yangu Zawadi na mimi tulishiriki. Ni mwendo wa saa moja kutoka hapa Northfield ninapoishi.

Tulipanga vitabu vyangu na machapisho mengine mezani, tukatundika ukutani bendera ya Tanzania ambayo nilinunua siku zilizopita. Saa nne ilipotimia, ambayo ndiyo saa ya kufunguliwa tamasha, watu walianza kuja. Na hapo kwenye meza yetu tulianza kutembelewa na watu tangu dakika zile za mwanzo. Tuliongea nao, tukajibu masuali kuhusu vitabu hivyo na mambo mengine mengi, nao wakatueleza mambo mbali mbali.


Baada ya nusu saa hivi, ilianza shughuli ya kupeperusha bendera. Watu walielekezwa zilipowekwa bendera ili wachukue bendera ya nchi yao na kujiunga katika maandamano wakiwa wamebeba bendera. Nilikwenda nikaikuta bendera ya Tanzania, nikaibeba katika maandamano.

Tuliendelea kuongea na watu wa mataifa mbali mbali hapo kwenye meza yetu, tukapata pia fursa ya kuzunguka kwenye meza za wengine, na kupiga picha. Kwa namna ya pekee ninakumbuka tulivyozungumza na mama mmoja Mmarekani, kuhusu tofauti za tamaduni akatueleza yaliyomkuta Japani. Mila na desturi alizozizoea Marekani ziliwashangaza wenyeji. Nasi tulimweleza yanayotokea pale wa-Afrika wanapokuwa na wa-Marekani, kama nilivyoelezea katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Ninakumbuka pia nilivyoongea na mama anayeonekana pichani hapa kushoto amevaa hijab. Nilikumbuka kuwa nilimwona katika tamasha mwaka jana, ila hatukufahamiana. Jana tulipata hiyo fursa, mezani pake, ambapo aliweka machapisho ya ki-Islam, kama vile The Message of the Qur'an cha Muhammad Asad, Who Speaks for Islam cha John L. Esposito na Dalia Mogahed, na Wisdom for Life & The Afterlife: A Selection of Prophet Mohammad's Sayings, ambavyo vyote ninavyo.

Nilimwambia kuwa mimi ni mwalimu katika chuo cha St. Olaf; nimetunga kozi, "Muslim Women Writers." na sababu za kuitunga. Naye alinielezea kuhusu kipindi anachoendesha kiitwacho Faith Talk Show, tukakubaliana nije kuhojiwa katika kipindi hicho siku zijazo.

Baada ya kurejea kutoka kwenye tamasha, nimeangalia mtandaoni, nikaona taarifa za mama huyu kama vile hii hapa. Ninawazia kumwalika darasani kwangu nitakapofundisha tena kozi yangu.

Muda wote wa tamasha kulikuwa na vikundi vya burudani jukwaani na pia vyakula vya nchi mbali mbali. Ninaleta hapa baadhi ya picha za tamasha.





Thursday, April 27, 2017

Bendera ya Tanzania Kupepea Rochester, Minnesota

Kwa mara ya kwanza bendera ya Tanzania itapeperushwa katika tamasha la kimataifa mjini Rochester, Minnesota, tarehe 29 mwezi huu. Hili ni tamasha linaloandaliwa na Rochester International Association (RIA) kila mwaka. Nimewahi kuelezea kuhusu tamasha hili katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza.

Napenda kuelezea mchakato uliowezesha bendera ya Tanzania kupewa hadhi hiyo. Mwaka jana wa-Kenya wawili, Olivia Njogu na Kennedy Ombaye, ambao ni wanabodi wa RIA, waliniambia kuwa wangependa nijiunge nao. Niliguswa na wazo lao, nikaafiki. Waliwasilisha ujumbe kwa mwenyekiti wa bodi, Brian Faloon, nami nikawasiliana naye kumthibitishia utayari wangu wa kujiunga. Wazo lilipitishwa na bodi, nami nikajiunga.

Wiki chache zilizopita, bodi ilianza kujadili mipango ya tamasha la kimataifa kwa mwaka huu. Wakati suala la bendera lilipojadiliwa, mwanabodi Olivia Njogu aliniambia kuwa iwepo bendera ya Tanzania. Kwa kuwa sikuelewa utaratibu wa bendera ukoje, Olivia na wanabodi wengine walinihakikishia kuwa sitahitaji kuileta bendera, bali wataipata kwa muuzaji. Nilifahamu kuwa utaratibu wa tamasha ni kuwa linapoanza, panakuwa na maandamano ya watu wakiwa wamebeba bendera za nchi mbali mbali.

Mwaka jana niliposhiriki tamasha hili, nilikuwa na bendera ya Tanzania, ambayo nilikuwa nimeinunua mwaka juzi, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Lakini kwa kuwa nilikuwa bado mgeni katika tamasha hili, sikuwa nimefanya utaratibu wa kuijumlisha katika maandamano ya bendera. Niliitandaza kwenye meza yangu, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto.

Ninawashukuru tena wa-Kenya kwa urafiki na ukarimu ambao wamenionyesha tangu nilipokwenda nchini kwao kufanya utafiti, kuanzia mwaka 1989, hadi miaka yote niliyoishi huku Marekani. Jambo hili nimekuwa nikilitaja katika blogu hii.

Saturday, April 22, 2017

Yatokanayo na Ziara Ubalozi wa Tanzania Marekani

Wiki hii, tarehe 19, binti yangu Zawadi na mimi tulikwenda kwenye Ubalozi wa Tanzania mjini Washington DC kushughulikia pasposti mpya baada ya paspoti zetu kwisha muda wa matumizi yake. Nimeona niandike mambo yaliyoibuka mawazoni mwangu kutokana na ziara hiyo.

Kwanza tulijisikia vizuri kuingia katika jengo la Ubalozi, na kujisikia tumo katika ardhi ya Tanzania. Nilimweleza binti yangu jambo hilo, nikaongezea kwamba mtu wa taifa lolote akiingia humu kutafuta hifadhi na akapata, mamlaka ya nchi yake haiwezi kuingia na kumkamata. Itabidi wajaribu bahati yao kwa kufanya utaratibu wa kuiomba Tanzania ili wakabidhiwe huyu mtu wao. Tulitaja mfano wa Julian Assange wa WikiLeaks ambaye amejichimbia katika Ubalozi wa Ecuador, London.

Wazo jingine lililonijia tulipokuwa ndani ya Ubalozi ni jinsi wadhifa wa kuiwakilisha nchi ulivyo mkubwa na mzito nikilinganisha na uchache wa wawakilishi wetu katika Ubalozi. Ni wazi kuwa watu wachache tunaowapa wadhifa wa kuiwakilisha nchi yetu katika ofisi ya ubalozi hawawezi kufika kila mahali katika nchi kubwa kama hii ya Marekani. Kwa kuzingatia hilo, ni wazi kuwa sisi Wa-Tanzania wanadiaspora vote tunawajibika kuiwakilisha nchi yetu pale tulipo na tunapopata fursa ya kuwepo katika maeneo mengine.

Mimi ninakaa katika mji wa Northfield, jimbo la Minnesota, ambao ni mdogo sana lakini ni maarufu kwa kuwa na vyuo vikuu viwili: St. Olaf na Carleton. Katakana na wadhifa wangu kama mwalimu ninayeshughulika na watu kutoka sehemu zote za Marekani na sehemu mbali mbali duniani, nina fursa ya kufanya mengi pasipo kutegemea Ubalozi.

Ninashiriki matamasha, ninatoa mihadhara, na ninashiriki mikutano ya aina aina. Ninashiriki katika uendeshaji wa jumuia zinazowajumlisha watu wa mataifa mbali mbali hapa Minnesota, kama vile Afrifest Foundation. Wakati huu, baada ya kuteuliwa katika bodi ya Rochester International Association, nina wadhifa mwingine muhimu. Katika nafasi zote hizo, ninajiwakilisha mwenyewe lakini pia kama raia wa Tanzania.

Ingawa nilijua tangu zamani kuwa sisi wananchi tuna wajibu wa kuiwakilisha nchi yetu popote tulipo, ziara yangu Ubalozini imenipa hamasa zaidi katika mwelekeo huo. Nimesukumwa zaidi na ukweli kwamba wafanyakazi wa Ubalozini hawatoshi kabisa kwa majukumu yaliyopo ya kuiwakilisha na kuihudumia nchi huku ughaibuni.

Friday, April 14, 2017

Neno Kuhusu Matokeo ya Kuchapisha Kitabu

Mimi kama mwandishi wa vitabu ninafurahi ninapopata wasaa wa kuelezea uzoefu wangu na kutoa ushauri kwa waandishi wengine au wale wanaowazia kuwa waandishi. Mara kwa mara ninaandika kuhusu mambo hayo kwa kujiamulia mwenyewe, lakini mara kwa mara ninaandika kuwajibu wanaoniulizia. Baadhi ya mawasiliano hayo huwa ni ya binafsi, na mengine hufanyika katika blogu hii.

Leo nimeona niseme neno kuhusu matokeo ya kuchapisha kitabu. Ninaandika kufuatia uzoefu wangu wa hapa Marekani. Kuchapisha kitabu ni aina ya ukombozi kwa mwandishi kutakana na jambo lilolokuwa linakusonga mawazoni. Ni kama kutua mzigo. Baada ya kumaliza kuandika, unajisikia mwenye faraja, tayari kuanza au kuendelea na majukumu mengine. Ni aina ya ukombozi.

Kuna waandishi chipukizi wanaoamini kuwa kuandika kitabu kutawaletea umaarufu au fedha. Wazo hili ni bora kuliweka kando. Fedha si jambo la kulipa kipaumbele; kwa kiasi kikubwa ni kubahatisha. Kwanza, kuna vitabu vingi mno vinavyochapishwa kila mwaka. Kwa hapa Marekani tu, vitabu zaidi ya milioni huchapishwa kila mwaka, kwa mujibu wa taarifa zilizopo. Sio rahisi mwandishi anayeanza safari ya uandishi ajipambanue na kuwa maarufu. Kwa wastani, nakala za kitabu zinazouzwa kwa mwaka ni 250, na ukomo wa mauzo kwa miaka yote ya kuwepo kitabu ni pungufu ya nakala 3,000.

Kwa hapa Marekani, kuna jadi kwamba waandishi, wakishachapisha kitabu, hufanya safari za kutangaza kitabu hicho. Safari hizi hupangwa na kuratibiwa na wadau wa vitabu kama vile wachapishaji wa vitabu, wauzaji wa vitabu, waendeshaji wa majarida yanayojihusisha na vitabu, na vikundi vya wasomaji katika miji na maeneo mbali mbali. Wote hao wanashiriki katika kufanikisha ziara ya mwandishi. Wanatangaza kwa namna yoyote ile ziara hiyo, magazetini, katika redio, katika televisheni, au mitandao ya kijamii.

Popote anapofika mwandishi, watu hujitokeza kumsikiliza akiongelea kitabu chake. Wanapata fursa ya kumwuliza masuali. Nakala za kitabu zinakuwepo, na watu wanapata fursa ya kununua na kusainiwa. Wenye maduka ya vitabu hupenda kuandaa mikusanyiko hiyo. Mbali na kwamba wanampa mwandishi fursa ya kukutana na wasomaji, na kutangaza kitabu chake, ni fursa kwa hayo maduka ya vitabu kujitangaza. Ni jadi iliyozoeleka kwamba nyakati hizo, kunakuwa na punguzo la bei ya kitabu kinachotangazwa, na hiki kinakuwa ni kivutio cha ziada kwa wateja.

Lakini jambo la msingi ni kuwa watu wa Marekani wanathamini sana fursa ya kukutana na mwandishi. Mimi mwenyewe, ingawa bado si mwandishi aliyetunukiwa tuzo maarufu kama Pulitzer, ninashuhudia jinsi watu wanavyovutiwa na fursa ya kukutana nami, iwe ni kwenye matamasha au kwenye mihadhara ninayotoa.

Hizi fursa za waandishi za kwenda kuongelea vitabu vyao ndio njia moja kuu ya waandishi kujijenga katika jamii. Mwandishi kuonekana na kusikilizwa moja kwa moja na wasomaji na wadau wengine wa vitabu ni njia ya kujijenga mioyoni mwao. Kukutana na mwandishi namna hiyo kunaleta picha na hisia ya pekee pale msomaji anaposoma kitabu cha mwandishi huyo. Bila shaka wote ambao tumewahi kukutana na waandishi tunajisikia hivyo tunaposoma maandishi yao.

Nimegusia hapo juu kuwa kuna watu wanaowazia kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea umaarufu au fedha. Ni kweli, kutegemeana na kukubalika kwa kitabu katika jamii, mwandishi anaweza kupata umaarufu na fedha kiasi fulani. Lakini, kwa uzoefu wangu, ninapoalikwa kwenda kuongelea kitabu ndipo pana malipo makubwa, ukiachilia mbali kuwa vile vile nakala za vitabu zinauzwa hapo hapo. Vitabu ninavyoongelea hapa ni viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales. Kipo kingine ambacho nimekuwa nikiandika kwa miaka kadhaa, kuhusu athari za tofauti za tamaduni, ambacho nina hakika kuwa kitawagusa watu kwa namna ya pekee.

Ningependa mambo hayo niliyoelezea yafanyike Tanzania. Ninatamani uje wakati ambapo, mwandishi akishachapisha kitabu muhimu, kiwe ni cha fasihi au maarifa, awe na fursa ya kuzunguka nchini kuongelea kitabu chake. Ninatamani uje wakati ambapo wananchi watakuwa na utamaduni wa kuvipenda vitabu na kupenda kukutana ana kwa ana na waandishi na kuongea nao.

Wednesday, April 12, 2017

Blogu Yangu Imepanda Chati Ghafla

Tangu wiki mbili zilizopita, blogu yangu hii imepanda chati ghafla. Ninaongelea kigezo cha "pageviews," ambazo ninaziangalia kila nitakapo. Kwa miaka na miaka, "pageviews" za blogu hii kwa siku zilikuwa kama 130, sio zaidi sana na sio pungufu sana.

Lakini, kuanzia wiki mbili hivi zilizopita, "pageviews" zimeongezeka ghafla kwa kiwango kikubwa, na sasa ni yapata 900 au zaidi kila siku. Sielewi ni nini kimesababisha ongezeko hilo. Mkondo wa mada zangu haujabadilika. Kwa kiasi kikubwa ninashughulika na masuala ya elimu na utamaduni.

Nimeona kuwa ongezeko hilo la "pageviews," limetokea hapa Marekani. Kwa nchi zingine, kama vile Tanzania na Kenya, hali haijabadilika. Ni ajabu kiasi kwamba blogu ya ki-Swahili inasomwa zaidi Marekani kuliko Afrika Mashariki.

Mtu unaweza kujiuliza ni watu gani wanaosoma hii blogu ya ki-Swahili kwa wingi namna hii hapa Marekani. Ukweli ni kuwa kuna watu wengi hapa, hasa kutoka Kenya na Tanzania, wanaokifahamu ki-Swahili. Wako pia watu kutoka Burundi, Uganda, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vile vile, kuna wa-Marekani ambao wameishi Afrika Mashariki na wanakifahamu ki-Swahili. Pia kuna wa-Marekani wengi ambao wamejifunza au wanajifunza ki-Swahili katika vyuo vikuu mbali mbali hapa hapa Marekani. Ninahisi kuwa hao nao ni kati ya wasomaji wa blogu hii.

Ninavyowazia suala hili la ukuaji wa idadi ya "pageviews" katika blogu, ninawazia jinsi watu wanavyotumia blogu kwa matangazo, hasa ya biashara. Katika ulimwengu wa leo ambamo tekinolojia za mawasiliano zinaendelea kusambaa na kuimarika, wafanya biashara na wajasiriamali wanatumia fursa za mitandao kama vile blogu kutangaza shughuli zao.

Kwa upande wangu, sijajiingiza katika matumizi haya ya blogu, ukiachilia mbali matangazo ya vitabu vyangu na mihadhara ninayotoa au matamasha ninayoshiriki. Lakini, endapo nitabadili msimamo, bila shaka nitakaribisha matangazo ya waandishi, wachapishaji, na wauzaji wa vitabu, kwa sababu blogu yangu inajitambulisha kwa masuala ya aina hiyo.

Saturday, April 8, 2017

Mwaliko Chuo Kikuu cha Winona

Tangu mwaka uanze, nimetoa mihadhara au kufanyiwa mahojiano nje ya chuo ninapofundisha, mara nyingi kuliko kawaida. Nilitegemea kuwa kuanzia mwezi huu wa Aprili, hali ingebadilika. Lakini dalili hazionyeshi mabadiliko.

Tarehe 6, nilipata mwaliko kutoka kwa Alex Hines, mkuu wa idara ya Inclusion and Diversity katika Chuo Kikuu cha Winona, wa kwenda kutoa mhadhara:

We would like to extend an invitation for you to attend HOPE Academic & Leadership Academy during the week of June 26th through June 29th and conduct a two hour presentation from 7-9 p.m. on Embracing African and African American Culture.

Hii itakuwa ni mara ya tatu mimi kwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Winona. Mara ya kwanza, niliongelea masuala ya utamaduni kama nilivyoyaeleza katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mara ya pili, niliongelea mahusiano ya binadamu na uongozi, kwa kutumia kitabu cha Matengo Folktales, kama nilivyoandika katika blogu hii

Mwaliko huu wa sasa, kama ilivyoelezwa katika barua niliyonukuu hapa juu, msingi wake ni kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alex Hines, tangu tulipofahamiana, miaka mingi iliyopita, amekuwa ni mmoja wa wale wanaonitegemea katika programu zao. Ninafurahi kwa imani ya wadau juu yangu, nami ninahamasika kufanya makubwa zaidi kwa ajili yao.

Blogu hii ni mahali ninapohifadhi kumbukumbu zangu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Labda kuna siku nitapata wazo la kuandika kitabu kuhusu shughuli zangu. Ikitokea hivyo, kumbukumbu hizi zitanifaa.

Sunday, April 2, 2017

Mhadhara Chuo Kikuu cha Minnesota Juu ya Kitereza

Juzi tarehe 31, Dr. Charlotte (Shoonie) Hartwig na mimi tulitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Minnesota, juu ya mwandishi Aniceti Kitereza. Huyu ni mwandishi muhimu ambaye, hata hivyo, hafahamiki sana. Mama Shoonie amekuwa akiandika kitabu ambacho nami nimechangia, na mhadhara wetu ulihusu kitabu hiki ambacho tunategemea kukichapisha.

Kitereza alizaliwa mwaka 1896 katika kisiwa cha Ukerewe kilichomo katika Ziwa Victoria, upande wa Tanzania. Alisomea katika shule za wamisheni, na alipomaliza aliajiriwa kazi kadhaa. Alivyozidi kukua alipata dhamira ya kuhifadhi mila na desturi za zamani za wa-Kerewe, ili zisipotee. Kama sehemu ya juhudi hiyo aliandika riwaya katika lugha ya ki-Kerewe, ambao aliukamilisha mwanzoni mwa mwaka 1945. Andiko hili ni hazina ya mila na destruí za wa-Kerewe wa zamani, ila Kitereza aliandika kwa mtindo wa hadithi ya kubuni, ili wasomaji wasichoke kusoma.

Baada ya juhudi na mahangaiko ya miaka mingi ya kutafuta mchapishaji, na kufuatia ushauri wa marafiki zake wa-Marekani, Kitereza aliutafsiri mswada wake kwa ki-Swahili. Hata hivyo, aliendelea kungoja kwa miaka mingi hadi mwaka 1980 ambapo mswada ulichapishwa kama kitabu, Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buliwhali.

Mama Shoonie ni mtu pekee aliyesalia mwenye taarifa za ndani za Kitereza, kwani yeye na mumewe, Dr. Gerald Hartwig, walimfahamu vizuri Kitereza baada ya kuonana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1968 Ukerewe. Mbali ya kukutana naye mara kwa mara miaka ile ya mwanzo, waliendelea kuandikiana barua hadi miaka ya mwisho wa maisha yake. Kitereza alikuwa hodari wa kuandika barua; ananikumbusha waandishi kama Ernest Hemingway na Shaaban Robert.

Katika mhadhara wa juzi, Mama Shoonie alielezea maisha ya Kitereza na mambo aliyofanya kama mwandishi. Maelezo yake aliyaambatanisha na picha za Kitereza, mke wake, na familia nzima ya Hartwig. Watoto wa familia ya Hartwig walikuwa wadogo sana wakati huo. Mama Shoonie alielezea kuwa Kitereza alikuwa anajituma sana katika shughuli yake ya kuhifadhi mila na destruí za wahenga kwa kusukumwa na suali ambalo alilitunga mwenyewe, "Tunawajibika kuwafundisha nini watoto wetu?"

Ilipokuja zamu yangu, nilielezea kwa ufupi uandishi wa Kitereza kwa mujibu wa mtazamo wangu kama mwana fasihi. Nilisisitiza masuala kadhaa muhimu yanayojitokeza katika taaluma ya fasihi ya Afrika, hasa suala la uandishi katika lugha za ki-Afrika na suala la tafsiri. Niligusia jinsi riwaya ya Bwana Myombekere inavyoweza kutupa mtazamo mpya kuhusu historia ya riwaya ya ki-Afrika, na jinsi inavyoweza kuchambuliwa sambamba na kazi za waandishi kama Daniel O. Fagunwa na Amos Tutuola wa Nigeria, Gakaara wa Wanjau wa Kenya, na Shaaban Robert wa Tanzania. Huu utakuwa ni mtazamo wa fasihi linganishi.

Nimesoma tafsiri ya Kitereza ya riwaya yake. Ki-Swahili chake, ingawa kinatofautiana na ki-Swahili sanifu, kina ladha na mtiririko wa hadithi simulizi za lugha za ki-Bantu kama vile lugha yangu ya ki-Matengo. Kwa msingi huo, ninaipenda tafsiri ya Kitereza. Riwaya yake imetafsiriwa kwa ki-Faransa na ki-Jermani, lakini tafsiri hizo, kwa mujibu wa Profesa Gabriel Ruhumbika, zina walakini. Kauli ya Profesa Ruhumbika ina uzito sana, kwani lugha mama yake ni ki-Kerewe na pia yeye ni mashuhuri katika uwanja wa kutafsiri.

Profesa Ruhumbika mwenyewe ametafsiri kwa ki-Ingereza riwaya ya Kitereza kama ilivyoandikwa ki-Kikerewe, na tafsiri yake imechapishwa kama Mr. Myombekere and His Wife Bugonoka, Their Son Ntulanalwo and Daughter Buliwhali. Katika kuisoma tafsiri hii, nilivutiwa nayo, sawa na nilivyovutiwa na tafsiri ya ki-Swahili ya Kitereza mwenyewe. Ni tafsiri ambayo ninapendekeza isomwe na yeyote. Hivyo hivyo, ninakipendekeza kitabu cha Mama Shoonie kijacho. Ni kitabu chenye taarifa nyingi, zikiwemo barua na picha, ambazo ulimwengu haujaziona. 

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...