Sunday, April 29, 2012

Vazi la Taifa

Jioni moja, mwezi uliopita, nikiwa natembea kwenye mtaa moja eneo la Sinza, Dar es Salaam, nilikutana na m-Maasai. Aliniuliza iwapo nimekutana na wa-Maasai wawili kwenye njia hiyo niliyotokea. Nilimwambia kuwa sijakutana nao. Tutafakari suali la huyu m-Maasai. Ni wazi alijua kuwa m-Maasai anafahamika popote alipo. Mavazi yake yanamtambulisha. Ndio maana aliniuliza alivyoniuliza. Huwezi ukamwuliza mtu Dar es Salaam iwapo amekutana na wa-Nyakyusa wawili, au wa-Chagga wawili, au wa-Matengo wawili. Hawatambuliki kama anavyotambulika m-Maasai. Picha niliyoweka hapa, ambayo inawatambulisha hao watu wawili, niliipiga Morogoro, eneo la stendi kuu ya dala dala. Nawajibika kusema kuwa kuhusu suala hili la vazi la Taifa, wa-Tanzania tumepotea njia, kama walivyopotea wengine wengi kuanzia enzi za ukoloni. Kuna jambo ambalo tunaweza kujifunza kutoka kwa wa-Maasai. Katika kutafakari suala hili, turejee kwenye kauli ya Frantz Fanon, mwanafalsafa na mtaalam wa masuala ya jamii, hasa zile zilizoathirika na ukoloni, ambaye tulikuwa tunamsoma sana enzi za ujana wetu, lakini sijui kama wa-Tanzania wa leo wanamsoma. Anasema hivi: The way people clothe themselves, together with the traditions of dress and finery that custom implies, constitutes the most distinctive form of a society's uniqueness, that is to say the one that is the most immediately perceptible.... It is by their apparel that types of society first become known, whether through written accounts and photographic records or motion pictures. Thus, there are civilizations without neckties, civilizations with loin-cloths, and others without hats. The fact of belonging to a given cultural group is usually revealed by clothing traditions....(Frantz Fanon, A Dying Colonialism, trans. Haakon Chevalier, New York: Grove Weidenfeld, 1965, uk.35).

Friday, April 27, 2012

Nyumbani u-Matengo

Kuna usemi wa ki-Ingereza kwamba uende Mashariki au Magharibi, lakini nyumbani ndio bora zaidi. Tatizo ni kufafanua dhana ya nyumbani. Nikiwa Dar es Salaam, nasema nyumbani ni Songea. Nikiwa Songea nasema nyumbani ni Mbinga. Nikiwa Mbinga nasema nyumbani ni Litembo. Nikiwa huku ughaibuni, naiona Tanzania yote kama nyumbani. Utawasikia wa-Afrika waishio ughaibuni wakisema Afrika ni nyumbani. Dhana ya nyumbani ni tata. Leo napenda kuleta taswira za nyumbani u-Matengo.
Hapa juu ni eneo baina ya Kindimba na Litembo. Zao la ngano linaonekana likiwa tayari kuvunwa.

Hapa kushoto ni sehemu moja karibu na Litembo, kwenye njia itokayo Ngwambo.
Hapa kushoto ni kijijini kwangu Lituru mwendo wa dakika kumi hivi kutoka kwenye nyumba yetu, ukielekea upande wa kushoto. Kule ng'ambo unaonekama mlima maarufu wa Kengema au Likengema, ambao unatazamana na nyumba yetu, kwa ng'ambo.
Hapa kushoto ni misheni Litembo, penye shule na hospitali. Nilizaliwa hapo nikasoma shule ya msingi hapo. Enzi zile, shule ya msingi iliishia darasa la nne. Mlima Kengema unaonekana kule ng'ambo, mrefu kuliko yote. Kwa taarifa zaidi kuhusu Litembo, soma hapa.

Wednesday, April 25, 2012

Yenu Bar, Ubungo

Pale Ubungo, eneo la stendi ya dala dala, upande wa pili wa barabara ya Morogoro kuna baa kadhaa. Nilipokuwa nasoma Chuo Kikuu Dar, kuanzia mwaka 1973, tulikuwa tunatinga eneo hilo kukata kiu. Bia zilikuwepo, na chibuku pia, kama sikosei. Baa moja iliyojulikana sana ni Yenu Bar, ya mzee mmoja Mchagga, maafuru kama Mzee Manywele. Mwanzoni mwa mwezi wa nne, mwaka huu, nilipokuwa nateremka kutoka eneo la Kimara, niliona sherti nipige picha ya Yenu Bar. ili wengine walioifahamu zamani wapate kujikumbusha enzi zile. Enzi zile, wanafunzi wa Chuo Kikuu tulikuwa makini sana katika masomo. Kwa hivi, ni baada ya kazi nzito ndio tulikuwa tunavinjari maeneo kama Yenu Bar, sio vingine.

Darasa Babati, Kuhusu Hemingway


Hapa juu ni picha niliyopiga Babati, mwaka 2007 au 2008.
Nilikuwa hapo Babati na wanafunzi kutoka chuo cha Colorado, ambao walikuja Tanzania kwenye kozi niliyotunga kuhusu mwandishi Hemingway. Katika picha naonekana nikiendesha darasa.
Hapa juu, chini ya dirisha, anaonekana profesa William Davis wa chuo cha Colorado, ambaye alitanguzana na wanafunzi, akanisaidia kufundisha kozi hiyo. Alikuwa hajawahi kuja Afrika, na kwa hivyo alitaka kupata uzoefu.

Sunday, April 22, 2012

Pesa za Majini

Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali,  kama vile Sumbawanga, Nigeria, na Malawi.

Kwa mujibu wa matangazo hayo waganga hao hutibu maradhi mbali mbali na hutatua matatizo mengine, kama vile nguvu za kiume, kufaulu masomo na kumvuta aliye mbali.  Hayo mengine mimi sina utaalam nayo, ila nimevutiwa na hili wazo la kufaulu masomo kwa kutumia dawa. Mimi kama mwalimu, naona ni jambo la ajabu kabisa.

Mwaka huu nimeona pia matangazo ya waganga yanayotaja pesa za majini. Yaani ukitaka hizo pesa, unaweza kuzipata. Makubwa haya.


Thursday, April 19, 2012

Nimesafiri Salama; Namshukuru Mungu

Nimesafiri salama kutoka Dar es Salaam hadi, nikawasili hapa Minnesota usiku wa tarehe 16 Aprili. Hapa kushoto ni picha niliyopiga ya bawa la ndege ya Swiss Air niliyosafiria. Niliipiga juu ya bahari ya Atlantic.

Namshukuru Mungu kwa kunifikisha salama, nikizingatia kuwa hata kuja kwangu kufundisha hapa haikuwa mpango wangu. Kwa kweli, wahusika walipoanza kuniulizia kama nitakuwa tayari kuja kufundisha hapa, nilisita, sikukubali. Nilikuwa tayari nafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baada ya kuishi Marekani miaka ya 1980-86 nikiwa nasomea shahada za juu. Yaliyotokea baada ya hapo, hadi nikakubali kuja kufundisha, ni hadithi ndefu. Nitakapoisimulia, walimwengu watakubaliana nami kuwa ilikuwa ni mpango wa Mungu. Kwa hivi, namshukuru kwa kunifikisha tena salama, niendelee na majukumu aliyonipangia.

Wednesday, April 18, 2012

Nimerejea Marekani: Chakula Hakipendezi

Baada ya kukaa Bongo wiki sita, nimerejea Marekani usiku wa kuamkia jana. Niilala nikaamka, na siku yote ya jana nimekosa raha. Nilijaribu kula kuku, nikaishiwa hamu. Kuku wa hapa hawana ladha kama wale wa kienyeji wa Bongo. Utadhani unatafuna vipande vya plastiki.

Nimejaribu kula ndizi. Ni hivyo hivyo. Hazifui dafu mbele ya ndizi nilizokula Morogoro, Sinza, na Ubungo. Nikajaribu chungwa. Ni vile vile. Nataenda dukani, na nitayaona maembe na mananasi. Najua kuwa hayafui dafu mbele ya yale ya Bongo. Sitayafurahia kama ninavyoyafurahia yale ya Bongo.

Tuesday, April 10, 2012

Humphrey, Mdau Mpya

Safari hii katika kukaa kwangu hapa Tanzania, nimepata fursa ya kukutana na wasomaji wengi wa maandishi yangu, wakiwemo wadau ambao taarifa zao nishaziandika hapa na hapa.

Nimebahatika pia kufahamiana na kuongea mara nyingi na mdau mpya, Humphrey, msomaji makini wa vitabu na makala. Hapa kushoto anaonekana ameshika vitabu vyangu. Katika maongezi, yeye ni mwepesi kugusia au kukumbushia maandishi mbali mbali. Wengi nchini mwetu hawasomi vitabu, na engine husoma kwa ajili ya mitihani. Wadau kama Humphrey husoma kutokana na ari ya kujielimisha.

Humphrey aliposikia kuwa nimeandika vitabu, aliviagiza hima kutoka kwa mjasiriamali anayeviuza hapa Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 na 0717 413 073. Amekuwa akiwaambia rafiki zake kuhusu vitabu hivyo, hasa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho anasema amekisoma na kukirudia mara kadhaa. Baada ya kukipitia, baadhi ya hao marafiki zake wameamua kujipatia nakala. Namshukuru Humphrey kwa kusaidia kusambaza fikra zangu, kwani hili ni lengo langu kama mwalimu katika jamii.

Niliwahi kuandika kuhusu duka la Asili, lililoko mbele ya hoteli ya Lion, Sinza, ambalo mmiliki wake ni Humphrey. Humo dukani kuna dawa na vyakula asili, lakini utavikuta pia vitabu vya taaluma mbali mbali ambavyo Humphrey anavisoma. Hapo nimeviona hata vitabu ambavyo sikuwahi kuvisikia, kama vile kitabu cha Jikomboe cha Dr. Godfrey Swai, ambacho ni cha taaluma ya afya, kwa lugha ya ki-Swahili.

Nimepata fursa kadhaa za kujumuika na Humphrey na marafiki zake saa za jioni hapo nje ya duka lake. Maongezi yamekuwa ya maana sana, kuhusu masuala ya uchumi, siasa, utandawazi, na hata utafiti katika lugha na desturi za makabila mbali mbali. Ukiwa hapo unajikuta umechangamsha akili. Naweza kusema kuwa yeyote anayethamini elimu na mandeleo, watu wa aina hiyo ndio wa kuandamana nao. Simu ya Humphrey ni 0713 545 410

Monday, April 9, 2012

Foleni Ubungo

Tatizo moja kubwa la mji wa Dar es Salaam ni msongamano wa magari na vyombo vingine vya usafiri mabarabarani. Picha hizi nilipiga leo eneo la Ubungo, nikiwa nateremka kwa mguu kukaribia kituo cha daladala.

Kuna sababu kadhaa zinazoleta msongamano huu, kama vile barabara kuwa ndogo. Hata hivyo, sababu nyingine, ambayo haisemwi, ni tabia ya kila mwenye gari kutaka kutumia gari lake, hata kama watu wawili wanakaa mtaa moja na wanafanya kazi sehemu moja kule mjini.

Wenzetu Marekani wana utamaduni wanaouita "car-pooling," yaani watu mnasafiri pamoja katika gari la mmoja wenu, hata kama wote mna magari, Tanzania mambo ni tofauti. Wote wanaendesha magari yao, hata kama wanatoka mtaa mmoja na wanakwenda sehemu hiyo hiyo ya kazi kule mjini. Halafu, mwenye gari anaona ni lazima apande gari hata kama anakwenda sehemu ya karibu, ambapo angeweza kwenda kwa mguu.

Magari binafsi yanawazuzua wa-Tanzania. Je, kuna anayekumbuka kuwa kutembea kuna manufaa kwa afya? Kuna anayekumbuka kwamba utitiri wa magari katika barabara za mahali kama Dar es salaam unachafua sana hewa? Kwa hoja hii ya uchafu wa hewa, siamini kama Dar es Salaam ni mahali salama kama ilivyo vijijini.

Sunday, April 8, 2012

Mahindi na Nyanya, Morogoro

Picha hii nilipiga juzi kwenye kituo cha mabasi cha Msamvu, Morogoro. Ningeweza kuandika insha kuhusu picha hii, nikielezea inavyonikumbusha maisha ya utoto wangu kijijini, utajiri wa nchi yetu, na matatizo ya wale wanaoshabikia vyakula vya kutoka nje ya nchi, vinavyouzwa katika hayo yanayoitwa maduka ya kisasa, matatizo ya fikra ambayo nimeyalezea katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Saturday, April 7, 2012

Nimetua Morogoro

Juzi nilishinda Morogoro. Nilitaka kuyafaidi tena mazingira na hali ya hewa ya mji huu marufu, ambao niliutembelea pia mwaka juzi, nikaandika habari zake hapa










Ukisafiri kwa basi kwenda Morogoro, hakuna shaka kuwa utapita mahali paitwapo Msamvu. Hapa ni kituo kikuu cha mabasi, na pia sehemu ya biashara za aina aina.

Tuesday, April 3, 2012

Duka Asili, Sinza

Hapa ni eneo la Sinza, Dar es Salaam, mbele ya hoteli ya Lion, ambayo ni hapo upande wa kulia. Pana duka liitwalo Asili. Linauza dawa za asili, kama vile Amana, dawa ya kutibum malaria; MamaPlus, dawa ya tumbo la uzazi; Asili-T, dawa ya kuongeza kinga dhidi ya magonjwa mwilini; BabaPlus, dawa ya nguvu za kiume. Vile vile duka hili linauza vyakula dawa kama vile rosella, mlonge (moringa), unga wa ubuyu na mafuta ya ubuyu.




Mmiliki wake, Humphrey Yona Kimaro, ni msomi, mpenda mazungumzo kuhusu mambo mbali` mbali ya maendeleo na jamii. Hapa dukani pake nimekutana na marafiki wake kadhaa, ambao nao ni makini katika mambo hayo. Humphrey anavyo baadhi ya vitabu vyangu. Kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimeshakuwa changamoto ya mijadala kwenye vikao jioni baada ya kazi. Kwa taarifa zaidi na mawasiliano, tembelea tovuti ya Asilia au piga simu 0767 445 410.

Monday, April 2, 2012

Nimetembelea Baruti, Dar es Salaam

Jana nilitembelea eneo la Baruti, Dar es Salaam. Hapa kushoto nimeweka picha ya msikiti niliouna pale, karibu na kituo cha dala dala, nami hupenda kupiga picha za nyumba za ibada. Ni sehemu muhimu kwetu waumini wa dini.







Nilienda Baruti kufuatilia ulizo la mwanablogu Rachel, alyeandika kwenye blogu hii, akitaka kujua kama Bahama Mama bado iko, nami nikampa ahadi kuwa ningeenda kuangalia. Nilikuta pamefungwa. Kwa nje hali ilionyesha kuwa ukarabati unaendelea, kama nilivyokuwa nimedokezwa. Niliishia kupiga pich ya kibao kinachoonekana hapa kushoto.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...