Vitabu vya Kukumbukwa Nilivyosoma Mwaka 2014
Leo, siku ya mwisho ya mwaka 2014, napenda kujikumbusha vitabu nilivyosoma mwaka huu ambavyo nitavikumbuka kwa namna ya pekee. Sitavitaja vitabu tulivyovisoma darasani. Kwanza, napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushuhudia mwaka 2014 ukiisha, huku zikiwa zimebaki saa nne tu hadi kuanza kwa mwaka 2015. Ingawa huu umekuwa mwaka mgumu kwangu kuliko miaka yote ya maisha yangu kwa sababu ya kuugua, nashukuru nimefikia hapa nilipo, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, huduma za madaktari, wauguzi na familia yangu, na maombi ya ndugu na marafiki. Kutokana na hali yangu hiyo, sikuweza kusoma kama ilivyo mazoea yangu. Hata hivi, kila nilipojisikia nafuu, nilishika kitabu na kusoma, hata nilipokuwa nimelazwa hospitalini. Vitabu ni moja ya vitulizo vyangu, na madaktari na wauguzi walitambua jambo hilo. Nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Abbott Northwestern, mjini Minneapolis, nilikwenda na kitabu cha mashairi ya Robert Frost kiitwacho Robert Frost: Selected Poems , ambacho binti yangu