Showing posts with label Shakespeare. Show all posts
Showing posts with label Shakespeare. Show all posts

Thursday, September 27, 2018

Nimenunua Tena Tungo Zote za Shakespeare

Tarehe 24 Septemba, nimenunua tena kitabu cha tungo zote za William Shakespeare.  Nilikinunua katika duka la Half Price Books mjini Apple Valley nilipotoka Burnsville kuangalia kitabu changu kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Ingawa tayari nina vitabu vinne vyenye tungo zote za Shakespeare, sikuona tatizo kununua hiki pia. Kuwa na nakala mbali mbali za kitabu cha tungo za Shakespeare kuna mantiki nzuri kwa sababu tungo hizo zimehaririwa kwa namna mbali mbali. Hii imekuwa ni sehemu ya historia ya uchapishaji wa tungo za Shakespeare.

Mara kwa mara neno linaloonekana kwenye nakala fulani si lile linaloonekana kwenye nakala nyingine au limeandikwa kwa namna tofauti na lilivyo katika nakala nyingine. Hali hiyo ni ile inayoonekana katika miswada ya tungo za zamani, sehemu mbali mbali ulimwenguni, ikiwemo za huku kwetu, kama zile za Liongo Fumo.

Tofauti hazikwepeki, kwa sababu uandishi katika enzi za Shakespeare ulikuwa tofauti na wa leo. Leo kitabu kikichapishwa, tunategemea ni nakala sahihi ya mswada ulivyoridhiwa na mwandishi. Wakati wa Shakespeare, hapakuwa na utaratibu huo. Watu walikuwa wananakili andiko walivyoweza, na tofauti mbali mbali zilijidhihirisha kutoka kwa mnukuzi hadi mwingine.

Kadhalika waigizaji wa tamthilia majukwaani walikuwa wanatamka, pengine bila kujitambua, maneno yaliyofanana sauti, ingawa maneno ya mwandishi yalikuwa tofauti. Hiyo nayo ni sababu ya waandishi kuandika maneno tofauti.

Kwa hali hiyo, ni busara kuwa na nakala tofauti za kitabu hiki cha tungo zote za Shakespeare. Hata mtu ukiwa na kitabu cha tamthilia mojawapo tu, ni busara kuwa na nakala zilizohaririwa na wahariri tofauti wa kitabu hicho.

Faida nyingine ni kwamba baadhi ya nakala hizi zina maelezo ya wahariri juu ya mambo mbali mbali, yakiwemo maana za maneno na semi. Maelezo haya ni msaada mkubwa kwetu, kwani ki-Ingereza cha wakati wa Shakespeare kina tofauti nyingi na kiIngereza cha leo.

Sunday, July 9, 2017

Wole Soyinka na Madikteta wa Afrika

Wole Soyinka ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika. Ameandika tamthilia, riwaya, mashairi, insha, na wasifu wake. Pia ametafsiri riwaya ya ki-Yoruba ya D.O. Fagunwa. Tafsiri hiyo inaitwa Forest of a Thousand Daemons: A Hunter's Saga.

Pamoja na umahiri wake katika kubuni visa na katika kuimudu lugha ya ki-Ingereza, Soyinka anachota sana mbinu na vipengele vingine vya sanaa na masimulizi ya jadi, hasa ya wa-Yoruba, lakini pia ya mataifa mengine, akienda mbali hadi u-Griki ya kale. Umahiri wake kama mwandishi umetambuliwa kwa namna mbali mbali, ikiwemo tuzo ya Nobel katika fasihi, ambayo alitunukiwa mwaka 1986.

Katika kazi zake, anashughulikia masuala ya aina mbali mbali, kama vile siasa, itikadi, ukoloni, ukoloni mambo leo, utamaduni, na fasihi ya Afrika na kwingineko. Udikteta ni mada ambayo Soyinka ameishughulikia tangu zamani, sio tu katika maandishi na mahojiano, bali pia kama mwanaharakati. Tamthilia ya Kongi's Harvest ni mfano mzuri. Tamthilia hii tuliisoma nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1973-76.

Wiki hii nimesoma A Play of Giants. Ni tamthilia ambayo inazama zaidi katika mada ya madikteta wa Afrika. Nilifahamu jambo hilo tangu zamani, kama nilivyoelezea siku chache zilizopita katika blogu hii. Soyinka anawaumbua madikteta hao. Anatumia kejeli kuelezea fikra na matendo yao, ulevi wa madaraka, uduni wa akili zao, na ukandamizaji wa haki za binadamu. Uduni wa akili zao unadhihirika kwa namna wanavyoongelea mambo yasiyo na maana, na kama wanaongelea mambo ya maana, hoja zao ni za ovyo kupindukia.

Madikteta hao wanaongelea jinsi wanavyoweza kudumu madarakani. Wanabadilishana mawazo na uzoefu wao. Wazo moja ni kutawala kwa mkono wa chuma na kuwafanya raia waishi kwa hofu. Hofu inaweza kujengwa mioyoni mwa raia kwa kutumia ushirikina na kuwafanya waamini kuwa mtawala anaona kila kinachoendelea nchini, Kwa njia hiyo, raia wanaogopa hata kuwazia kupinga utawala, kwani wanaamini kuwa mtawala atajua.

Udikteta ni mada ambayo imeanishwa katika kazi za fasihi tangu zamani sana. Tunaisoma katika The Epic of Gilgamesh, kwa mfano, na katika baadhi ya tamthilia za Shakespeare. Katika kusoma A Play of Giants, nimewazia sana riwaya ya Ngugi wa Thiong'o, Wizard of the Crow, ambamo dikteta anaumbuliwa pamoja na mfumo wa utawala wake kwa njia ya kejeli, sawa na anavyofanya Soyinka.

Ingawa kuna matumizi ya kejeli, A Play of Giants si tamthilia ya kufurahisha, bali inatibua akili na kunifanya nijiulize binadamu tunawezaje kuishi katika himaya ya udikteta. Kejeli ya mwandishi inanifanya mimi msomaji nicheke, lakini si kicheko cha furaha, bali dhihaka juu ya madikteta na aibu juu yetu wanadamu.

Tuesday, December 27, 2016

Nimejutia Kusoma "Hamlet" Wakati wa Sikukuu

Siku kadhaa zilizopita, nilianza kusoma Hamlet, tamthilia ya Shakespeare, kama nilivyoandika katika blog ya ki-Ingereza. Tamthilia hii haikuwa ngeni kwangu. Ni moja ya tungo za Shakespeare ambazo nimezifahamu au kuzisoma tangu ujana wangu.

Lakini kuna jambo ambalo sikulizingatia nilipoamua kusoma Hamlet wakati huu, ambao ni wa sikukuu ya Krismasi. Ulikuwa si wakati muafaka wa kusoma Hamlet, hadithi yenye matukio ya kusikitisha. Mkondo mkuu wa hadithi hii ni jinsi baba ya Hamlet alivyouawa na ndugu yake, mfalme Claudius, ambaye miezi miwili tu kufuatia msiba huo alimwoa mama yake Hamlet. Mambo haya yanampa Hamlet msongo mkubwa wa mawazo.

Mzimu wa marehemu baba yake unamtokea Hamlet na kumweleza ufedhuli uliofanyika na kisha kumwelekeza alipize kisasi. Hamlet anatafakari afanye nini. Hasira na huzuni zake anazieleza kwa hisia na ufasaha tena na tena, kwa mfano katika tamko hili:

Ham. O that this too too solid flesh would melt
Thaw and resolve itself into dew!
Or that the Everlasting had not fixed
His canon 'gainst self-slaughter! O God! God!
How weary, stale, flat, and unprofitable
Seem to me all the uses of this world!
Fie on't! ah, fie! 'Tis an unweeded garden
That grows to seed; things rank and gross in nature
Possess it merely. That it should come to this!
But two months dead--nay, not so much, not two!
So excellent a king, that was to this
Hyperion to a satyr; so loving to my mother
That he might not beteem the winds of heaven
Visit her face too roughly. Heaven and earth!
Must I remember? Why, she would hang on him
As if increase of appetite had grown
But what it fed on; and yet, within a month--
Let me not think on't! Frailty, thy name is woman!
....
              Act I. Sc. II

Tafakari yake inamfanya hata ajiulize kama aendelee kuishi na kupambana na masaibu ya maisha kwa mategemeo ya kuyamaliza, au atoe uhai wake, kama tunavyomsikia katika tamko hili maarufu sana:

Ham. To be, or not to be, that is the question:
Whether 'tis nobler in the mind to suffer
The slings and arrows of outrageous fortune
Or to take arms against a sea of troubles,
And by opposing end them. To die--to sleep--
No more; and by a sleep to say we end
The heartache, and the thousand natural shocks
That flesh is heir to. 'Tis a consummation
Devoutly to be wished. To die--to sleep.
To sleep--perchance to dream: ay, there's the rub!
For in that sleep of death what dreams may come
When we have shuffled off this mortal coil,
Must give us pause....
                                              Act. III. Sc. I

Ili kuzipata vizuri hisia za Hamlet, tushuhudie jinsi Laurence Olivier alivyoliigiza tamko hili la pili, katika filamu ya mwaka 1948, ambayo niliiangalia kwa mara ya kwanza mwaka 1971, nilipokuwa Mkwawa High School, Tanzania:

Monday, November 14, 2016

Ninajikumbusha "Hamlet"

Wiki hii, pamoja na majukumu ya kawaida ya kufundisha, nimeamua kujikumbusha enzi za ujana wangu kwa kusoma Hamlet, tamthilia mojawapo maarufu kabisa ya Shakespeare. Kila ninapokumbuka tamthilia hii, ninakumbuka nilivyoangalia filamu yake yapata mwaka 1971, Mkwawa High School, Iringa.  Sir Laurence Olivier aliigiza nafasi ya Hamlet, kama nilivyogusia katika blogu hii.

Miaka ile ya ujana, tulifahamu ki-Ingereza vizuri hadi kusoma maandishi ya Shakespeare na kuyafurahia. Shakespeare ni kipimo kizuri cha ufahamu wa ki-Ingereza. Umahiri wake katika kutumia maneno na kutunga sentensi unadhihirika katika tungo zake zote. Ninanukuu hapa hotuba ya Claudius, mfalme wa Denmark, kwa Hamlet, ambayo ni kielelezo cha umahiri huo:

Tis sweet and commendable in your nature, Hamlet,
To give these mourning duties to your father;
But you must know, your father lost a father;
That father lost, lost his, and the survivor bound
In filial obligation for some term
To do obsequious sorrow. But to persever
In obstinate condolement is a course
Of impious stubborness. 'Tis unmanly grief;
It shows a will most incorrect to heaven,
A heart unfortified, a mind impatient,
An understanding simple and unschooled;
For what we know must be, and is as common
As any the most vulgar thing to sense,
Why should we in our peevish opposition
Take it to heart? Fie! 'tis a fault to heaven,
A fault against the dead, a fault to nature,
To reason most absurd, whose common theme
Is death of fathers, and who still hath cried,
From the first corse till he that died today,
"This must be so." We pray you throw to earth
This unprevailing woe, and think of us
As of a father; for let the world take note
You are the most immediate to our throne,
And with no less nobility of love
Than that which dearest father bears his son
Do I impart toward you. For your intent
In going back to school in Wittenberg,
It is most retrograde to our desire;
And we beseech you, bend you to remain
Here in the cheer and comfort of our eye,
Our chiefest courtier, cousin, and our son.


Saturday, April 18, 2015

Misahafu na Balaa Linaloitwa Dini

Si kila kinachoitwa dini ni dini. Katika historia, kumekuwepo na uovu mwingi ambao umefanyika kwa jina la dini. Hadi leo, uovu wa aina hiyo unaendelea kufanyika. Siku nyingine, panapo majaliwa, nitaleta na kuongelea mifano, kwa uwazi na haki.

Misahafu imetumika na inaendelea kutumika kuhalalisha uovu. Kwa kiasi fulani hii ni kwa sababu mtu anaweza kuzipata nukuu kutoka katika msahafu ambazo zinapingana au zina utata. Lakini vile vile ni suala la tafsiri. Wataalam wa lugha wanatueleza kuwa matumizi ya lugha yanatoa mwanya wa tafsiri mbali mbali.  

Kwa msingi huo, watu waovu wanaweza kutafsiri nukuu za msahafu kwa namna ya kuhalalisha uovu. Katika tamthilia ya Shakespeare, The Merchant of Venice, Antonio anasema, "The devil can cite Scripture for his own purpose." Shetani anaweza kunukuu msahafu kwa faida yake mwenyewe. Historia imethibitisha ukweli huo tena na tena.
 

Tatizo jingine ni imani miongoni mwa waumini wa dini kwamba kila kilichomo katika misahafu sherti kikubaliwe na kufuatwa kilivyo, bila mabadiliko. Imani hii ni chanzo cha matatizo makubwa.

Mtu ukiusoma msahafu wowote bila upendeleo wala ushabiki, utaona kuwa msahafu ulitokea katika mazingira maalum ya kihistoria, kijamii, na kitamaduni. Kuna mambo katika misahafu ambayo yalikusudiwa kwa jamii za zamani, na hayatuhusu sisi watu wa leo.

Kwa msingi huu, ni muhimu tujijengee utamaduni wa kuichambua misahafu ili tuone ni yepi yanatufaa na yepi yaliwafaa watu wa zamani lakini hayatufai sisi watu wa leo.


Mungu ametujalia akili. Tuzitumie. Mungu ametuweka katika dunia tofauti na ile ya watu wa zamani. Tuna ufahamu  na akili tofauti na watu wa zamani, katika masuala kama haki za binadamu.

Utandawazi wa leo na tekinolojia imetupa ufahamu tofauti wa ulimwengu na watu wake, ufahamu wa mahusiano tunayoyahitaji katika dunia ya leo ambayo siku hadi siku inageuka kuwa kijiji.

Je, katika mazingira hayo, ni sahihi kuishikilia misahafu neno kwa neno, kikasuku, badala ya kupambanua yale yanayotuhusu na yale yaliyowahusu watu wa zamani? Je, ukasuku huu, unaosababisha au kuhalalisha balaa juu ya balaa, na maovu ya kila aina, ndio dini?

Kwa kumalizia ujumbe wangu, napenda kusisitiza mtazamo wangu kuwa mijadala ya dini ni muhimu, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

 

Monday, December 8, 2014

Vitabu Nilivyonunua Juzi

Juzi, Jumamosi,  nilienda Minneapolis, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation, ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la Half Price Books, ambalo nimeliongelea mara kadhaa katika blogu hii.

Ingawa ilikuwa jioni sana,  watu walikuwa wengi humo dukani: watu wazima, vijana, na watoto. Nami nilijichanganya nao, nikaangalia angalia sehemu zenye vitabu vya fasihi. Nilinunua vitabu vinne, ambavyo nitavielezea leo.

Lakini kabla ya kuelezea vitabu hivi, napenda kujikumbusha kitu kimoja kilichonigusa, wakati nimesimama katika foleni ya kulipia vitabu. Mbele yangu walikuwepo baba na mama na watoto wadogo wawili wasichana. Walikuwa wameshaweka vitabu vyao kwenye kaunta ya kulipia, huku wakiwaelezea wale watoto jinsi watakavyowasomea vitabu. Kati ya vile vitabu kwenye kaunta, niliviona viwili vikubwa vikubwa vya Harry Potter. Muda wote wale watoto walikuwa na furaha na msisimko. Kwa mara nyingine tena, nilishuhudia jinsi wenzetu wanavyowalea watoto wao katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.

Kitabu kimojawapo nilichonunua ni Much Ado About Nothing, ambayo ni tamthilia ya Shakespeare iliyohaririwa na Barbara A. Mowat na Paul Werstine. Wasomaaji wa Shakespeare wanajua kuwa tamthilia zake zimehaririwa na wahariri mbali mbali katika hii miaka 500 tangu kufariki kwake.

Tamthilia za Shakespeare, ambazo ni 37, hupatikana pia zikiwa zimekusanywa katika kitabu kimoja kikubwa sana. Ingawa ninazo nakala za kitabu hiki--nakala mbili hapa Marekani na nyingine Tanzania--huwa napenda, mara moja moja kununua hivi vitabu vya tamthilia moja moja, kwa vile ni rahisi kubeba katika mkoba na kwenda navyo popote.

Kitabu kingine nilichonunua ni The Pickwick Papers, kilichotungwa na Charles Dickens. Wengi wetu tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu tunamkumbuka Dickens na riwaya zake, kama vile Oliver Twist na A Tale of Two Cities. Binafsi, nilimpenda sana Dickens, na nilisoma vitabu vyake kadhaa. Nimewahi kumwongelea Dickens katika blogu hii.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Hemingway on Hunting. Nimenunua toleo lililochapishwa na The Lyons Press, mwaka 2001. Kitabu hiki ni mkusanyo wa maandishi ya Ernest Hemingway yanayohusu uwindaji. Mhariri wake ni Sean Hemingway, mjukuu wa mwandishi mwenyewe. Pia kuna utangulizi mfupi ulioandikwa na Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Sean amekusanya maandishi kutoka katika vitabu  kama vile Green Hills of Africa, For Whom the Bell Tolls, Across the River and into the Trees, na pia makala na barua mbali mbali alizochapisha Ernest Hemingway katika magazeti.

Ingawa mengi ya maandishi hayo ninayo, niliona ni vema kuwa na kitabu hiki ambacho kinahusu hili suala la uwindaji. Ningependa kusema pia kuna kitabu cha aina hiyo hiyo, ambacho ni mkusanyo wa maandishi ya Hemingway kuhusu uvuvi, na kingine kuhusu uandishi. Hemingway, katika falsafa na nadharia zake, aliongelea uhusiano baina ya  uandishi na uwindaji.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Minaret, riwaya iliyotungwa na Leila Aboulela, ambaye alikulia Khartoum na anaishi Dubai na Aberdeen. Ni mwandishi maarufu, ambaye ameshajitwalia tuzo kadhaa kwa uandishi wake. Ingawa nimesikia habari zake kwa miaka kadhaa, sikuwahi kusoma kitabu chake hata kimoja. Leila Aboulela anajulikana kwa umahiri wake kisanaa, pia kwa jinsi anayowaelezea suala la wanawake katika u-Islam kwa mtazamo tofauti na ilivyozoeleka. Nina dukuduku ya kusoma Minaret, kwa kuanzia, na nitapenda pia kusoma riwaya zake zingine.

Monday, January 9, 2012

Mabepari wa Venisi: Tafsiri ya Julius Nyerere

Wiki kadhaa zilizopita, mawazo yangu yalitekwa sana na kumbukumbu za tafsiri za tamthilia za Shakespeare zilizofanywa na Julius Nyerere. Nilipata hamu ya kuziangalia na kuzisoma. Kwa kuanzia, niliagiza nakala ya Mabepari wa Venisi.

Kama nakumbuka sawa sawa, tulisoma The Merchant of Venice tulipokuwa kidatu cha nne. Tulikuwa tunafahamu ki-Ingereza kiasi cha kuweza kusoma na kuelewa maandishi hayo ya Shakespeare. Ni tofauti na leo, ambapo uvivu na uzembe vimesababisha ufahamu wa ki-Ingereza udidimie sana na hata kutoweka. Uvivu huo unajitokeza pia katika ufahamu wa ki-Swahili.

Nyerere aliichapisha tafsiri yake mwaka 1969, muda mfupi tu baada ya Azimio la Arusha. Kwa hivi, tafsiri yake ilikuwa na mvuto wa pekee miongoni mwetu, kwani tulikuwa tunavutiwa na nadharia za ujamaa. Hata neno mabepari lilikuwa likitumika sana, sambamba na maneno kama mabwanyenye. Ilikuwa rahisi kuelewa kwa nini Nyerere aliamua kuitafsiri tamthilia hii ya Shakespeare. Kwa kutumia tabia, fikra, na kauli za Shailoki, mfanyabiashara wa Venisi, Shakespeare alionyesha kwa umahiri mwenendo wa ubepari. Shailoki ni kielelezo bora cha dhana ya Nyerere kuwa ubepari ni unyama.

Mwanzoni mwa kitabu cha Mabepari wa Venisi kuna picha ya Shailoki, iliiyochorwa na Sefania Tunginie. Picha hii nayo inanikumbusha enzi za ujana wangu, nilivyokuwa naiangalia. Mimi mwenyewe nilikuwa mchoraji, na nilikuwa navutiwa na picha za wachoraji kama Sefania Tunginie, Sam Ntiro, na Elias Jengo.

Nimekumbuka hayo yote, na nimekitafuta kitabu cha Mabepari wa Venisi ili kujikumbusha umahiri wa Nyerere katika lugha ya ki-Ingereza na ki-Swahili. Kama kweli unakijua ki-Ingereza na ki-Swahili, huwezi ukasoma tafsiri ya Nyerere usikiri kuwa alikuwa na akili na ufahamu usio wa kawaida wa undani wa lugha hizo mbili. Hata hivi, kama wewe ni mtu makini sana, unaweza kubadili neno hapa au pale, katika tafsiri ya Nyerere. Angalia, kwa mfano, alivyotafsiri maneno ya Antonio, mwanzoni kabisa mwa tamthilia:



Ant. In sooth, I know not why I am so sad.
It wearies me; you say it wearies you;
But how I caught it, found it, or came by it,
What stuff 'tis made of, whereof it is born,
I am to learn;
And such a want-wit sadness make of me
That I have much ado to know myself.

Tafsiri ya Nyerere ni hii:

ANTONIO: Kusema kweli sijui kisa cha huzuni yangu;
Inanitabisha sana; wasema yakutabisha;
Bali nilivyoipata, au kuiambukizwa,
Au imejengekaje, imezawa jinsi gani,
Ningali sijafahamu,
Na huzuni yanifanya kuwa kama punguani,
Kunifanya nisiweze kujifahamu mwenyewe.

Kama nilivyosema, miaka ya ujana wetu, tuliweza kuelewa lugha ya Shakespeare, tena kwa undani. Leo sijui ni wa-Tanzania wangapi wanaoweza kumwelewa Shakespeare. Ngoja nilete kisehemu cha hotuba maarufu ya Portia, halafu ujaribu kutafsiri, uone unakifahamu ki-Ingereza na ki-Swahili kiasi gani:

Por. The quality of mercy is not strained,
It droppeth as the gentle rain from heaven
Upon the place beneath. It is twice blest--
It blesseth him that gives, and him that takes.
'Tis mightiest in the mightiest. It becomes
The throned monarch better than his crown.
His sceptre shows the force of temporal power,
The attribute to awe and majesty,
Wherein doth sit the dread and fear of kings;
But mercy is above this sceptred sway,
It is enthroned in the hearts of kings,
It is an attribute to God himself;
And earthly power doth then show likest God's
When mercy seasons justice.


Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...