Makala ya "Kwanza Jamii" Yachapishwa Marekani
Wiki kadhaa zilizopita, nilipata mwaliko kutoka kwa Ndugu Maggid Mjengwa, kuwa niandike makala katika gazeti lake jipya la Kwanza Jamii . Nilikubali, na niliandika makala ya kwanza yenye kichwa "Maendeleo ni Nini?." Makala hii ilichapishwa mwezi Aprili, 2009. Siku moja, katika maongezi na Mmarekani Mweusi mmoja katika mji wa Minneapolis, nilimwambia kuwa nimeanza kuandika makala za kiSwahili katika gazeti moja la nyumbani Tanzania. Kwa vile alikuwa na duku duku ya kujua zaidi kuhusu makala hizo, nilimweleza kuhusu makala yangu hiyo ya kwanza. Huyu Mmarekani tulikuwa tumefahamiana kwa wiki kadhaa, tukiwa katika shughuli za kuandaa tamasha la utamaduni wa kiAfrika, liitwalo Afrifest . Alivutiwa na mada na mtazamo wa makala, akasema ingefaa kuchapishwa katika gazeti la mtandaoni ambalo yeye na watu wengine walikuwa wanaliandaa. Alisema kuwa mawazo niliyoandika kuhusu maendeleo yatawafaa watu wa Marekani pia, kama vile waMarekani Weusi, ambao nao wamepitia msukosuko wa kutawali