Friday, July 31, 2015

Tamasha la Afrifest ni Kesho, Agosti 1

Kesho ndio siku ya tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, Minnesota. Ni fursa ya watu kukutana, kujifinza kuhusu mambo mbali mbali ya historia, siasa na tamaduni za wa-Afrika na wanadiaspora wenye asili ya Afrika. Ni fursa ya kuuenzi mchango wa watu weusi katika dunia.

Afrifest inafuata nyayo za viongozi maarufu waliofanya juhudi katika kujenga mshikamano miongoni mwa watu wenye asili ya Afrika, mshikamno ulioendana na ajenda za kujitambua na kupigania uhuru na ukombozi.

Watu hao maarufu ni kama Henry Sylvester-Williams,  Marcus Garvey, George Padmore, W.E.B. DuBois,  Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta, Nnamdi Azikiwe, Julius Nyerere, Kenneth Kaunda na Walter Rodney.

Katika sanaa, tunawakumbuka watunzi na waandishi maarufu kama Antar bin Shaddad (Saudi Arabia), Alexander  Pushkin (Urusi), Claude McKay (Jamaica na U.S.A), Peter Abrahams (Afrika Kusini na Jamaica) na Leopold Sedar Sengor (Senegal). Tunawakumbuka wanamuziki kama Bob Marley (Jamaica) na Miriam Makeba (Afrika Kusini). Wanamitindo wa mavazi  nao huonesha ubunifu wa watu weusi.

Mbali na michezo ya watoto, kutakuwepo na mambo mengine kemkem, siku nzima, ya kuelimisha na kuburudisha. Bora kuja kujionea, kuliko kusimuliwa. Tamasha litafanyika kesho, tarehe 1 Agosti, Northview Junior High School, Brooklyn Park, Minnesota, kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tatu usiku.

Thursday, July 30, 2015

Nimepata Vitabu vya Warsha: Jamii na Taaluma

Leo nimepata vitabu vya warsha itakayofanyika hapa chuoni St. Olaf tarehe 17-20, mwezi Agosti, kuhusu jamii na taaluma. Warsha itawahusisha maprofesa wachache, kuongelea masuala kama nafasi ya mwanataaluma katika jamii, itikadi katika taaluma, na uhuru wa taaluma.

Washiriki wa warsha tunapata vitabu vya bure, ambavyo tutavijadili katika warsha. Tutaanza na viwili. Kimoja ni Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities, kilichotungwa na Martha C. Nussbaum. Cha pili ni Versions of Academic Freedom, kilichoandikwa na Stanley Fish. Kwetu tuliomo katika masomo ya nadharia ya fasihi, maandishi ya Stanley Fish katika uwanja huo ni maarufu sana.

Baada ya vitabu hivyo, tutajadili Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education, kitabu cha George Yancey, na Professors and Their Politics, ambacho kimehaririwa na Neil Gross na Solon Simmon. Hiki cha pili ni mkusanyo wa insha za wataalam mbali mbali.

Warsha itakuwa nzito, sawa na masomo ya kiwango cha juu kabisa. Tutakuwa tunasoma kurasa nyingi kila siku kwa maandalizi ya mjadala wa masaa mawili kila siku. Ni fursa ya kujinoa katika fikra na mitazamo juu ya masuala muhimu ya taaluma, ufundishaji, na nafasi na mchango wetu katika jamii. Ni fursa pia ya sisi wenyewe kubadilishana mawazo na kufahamiana. Cha zaidi ni kuwa ninapenda vitabu vya kufikirisha na kuelimisha, na kuvipata vya bure si jambo dogo.

Tuesday, July 28, 2015

Kitabu Umechapisha, Kazi ni Kukiuza

Pamoja na kuandika vitabu, ninajitahidi kujielimisha kuhusu masuala yanayohusiana na uchapishaji, utangazaji, na uuzaji wa vitabu. Kwa bahati nzuri, kuna vitabu vingi na vingine vinaendelea kuchapishwa, na pia makala nyingi kuhusu masuala hayo.

Napenda kuongelea suala la kukiuza kitabu. Niliwahi kuongelea suala hili katika blogu hii. Nimeliongelea pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ni suali linalonigusa na kunifikirisha daima, nami napenda kuwashirikisha waandishi wengine katika kulitafakari.

Usemi kwamba chema chajiuza, kibaya chajitembeza unaweza kuwa na mantiki nzuri kuhusiana na vitabu. Wateja wakiridhishwa au kufurahishwa na kitabu, hawakosi kuwaambia wengine. Aina hii ya utangazaji, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "word of mouth," ni muhimu sana.

Mimi mwenyewe nimeshuhudia hivyo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Tangu nilipokichapisha kitabu hiki, mwaka 2005, wasomaji wamekuwa wakiwaambia wengine. Kwa lugha ya mitaani, wanakipigia debe.

Waandishi wengi hawajui kuwa baada ya kuchapisha kitabu, wana jukumu la kukitangaza na kukiuza. Wengi wanamtegemea mchapishaji afanye kazi hiyo. Hakuna shaka kwamba mchapishaji hujitahidi kukitangaza kitabu. Anawajibika kufanya hivyo, kwani anatafuta fedha za kugharamia uchapishaji, kuwalipa wafanyakazi wake, na kujipatia faida.

Lakini, waandishi tunapaswa kuona mbali zaidi. Kwanza, tusijiziuke. Mchapishaji hawezi kufanya kila kitu, hata kama angependa. Gharama za kukitangaza kitabu ni kipingamizi kwa mchapishaji, hasa yule ambaye si tajiri.

Pili, dunia inabadilika muda wote, nasi tunawajibika kujifunza mambo mapya muda wote. Leo hii kuna tekinolojia zinazomwezesha mwandishi kujichapishia kitabu chake. Katika mazingira haya, mwandishi anawajibika kubeba jukumu la kutangaza na kuuza kitabu. Si busara kutegemea "word of mouth" pekee.

Haikuwa rahisi kwangu kuanza kuvitangaza vitabu vyangu. Kutokana na malezi, mila na desturi, nilijiuliza italeta picha gani katika jamii iwapo ningekuwa natangaza na kuuza vitabu vyangu. Nilielezea wasi wasi huo katika blogu hii, na jinsi nilivyojikomboa.

Leo sioni tatizo kutangaza vitabu vyangu. Nimejifunza na ninaendelea kujifunza umuhimu na mbinu za kufanya hivyo, kwa kusoma vitabu na makala mbali mbali. Ndio maana mara kwa mara naandika katika blogu hii kuhusu matamasha ya vitabu ninayoshiriki. Kusoma kumenileta katika upeo huu mpya. Elimu ni mkombozi.

Saturday, July 25, 2015

Rais Obama na Dada Yake Auma Obama

Ujio wa Rais Obama nchini Kenya juzi umezua mambo mengi, ikiwemo furaha isiyo kifani miongoni mwa watu wa Kenya, Afrika Mashariki, na kwingineko. Kitendo cha Rais Obama kukutana na ndugu zake katika chakula cha jioni ni jambo la kukumbukwa. Kwa namna ya pekee, wengi tuliguswa na namna Rais Obama na dada yake Auma Obama walivyokutana.

Nilivyomwona dada huyu, nilikumbuka kuwa niliwahi kumtaja katika blogu hii baada ya kununua kitabu chake, And Then Life Happens: A Memoir. Niliingia mtandaoni nikaona mahojiano aliyofanyiwa na mtangazaji wa CNN. Halafu nilikitafuta kitabu chake katika maktaba yangu nikakipitia, kwa kuwa nilikuwa sijakisoma, bali nilikuwa nimekipitia juu juu tu.

Hakuna ubishi kwamba Auma Obama ni mama mwenye fikra za kusisimua na uwezo mkubwa wa kujieleza. Hilo linajitokeza wazi katika mahojiano yake. Masimulizi ya maisha yake, yaliyomo katika kitabu chake, yana mambo yanayoweza kuwahamasisha watoto wetu, hasa wasichana, wawe wanajiamini na kuwa watafuta elimu na maendeleo, wakijua kuwa wao wana uwezo sawa na mtu mwingine yeyote.

Kitu kingine kilichonivutia juu ya Auma Obama ni kwamba anakimudu sana ki-Jerumani, lugha ambayo alianza kujifunza alipokuwa Kenya na baadaye alipokuwa masomoni Ujerumani, ambako aliishi na kufanya kazi kwa miaka mingi. Kitabu chake alikiandika kwa lugha hiyo. Ninukuu maelezo yake kuhusu jambo hilo:

This book was originally written in German. Some may wonder why, when English is actually a language I grew up with, next to my native tongue, Luo. But the fact that I studied and worked in Germany made it seem natural to tell my story in the language in which I had spent my formative adult years. The writing came more easily to me, and in many ways my main audience was a German one.

Natafsiri kwa ki-Swahili kama ifuatavyo:

Kitabu hiki kiliandikwa awali kwa ki-Jerumani. Baadhi ya watu huenda watashangaa kwa nini, wakati ki-Ingereza ni lugha niliyokua nayo, sambamba na lugha mama yangu ya ki-Jaluo. Lakini ukweli kwamba nilisoma na kufanya kazi Ujerumani ilisababisha iwe rahisi kwangu kujieleza katika lugha ambayo ilinilea miaka ya kukua kwangu katika utu uzima. Uandishi huo ulikuja kirahisi kwangu, na kwa vyovyote, hadhira yangu kuu ilikuwa ni ya wa-Jerumani.

Kwa kuhitimisha, ninapenda kusema jinsi ninavyoguswa na ukweli kwamba mtu na dada yake, yaani Rais Obama na Auma Obama, wote wana vipaji vinavyofanana. Mbali ya kuwa ni waandishi, wote wanajituma katika kutumikia jamii. Katika mahojiano yake, Auma Obama anaongelea shughuli za taasisi yake iitwayo Sauti Kuu ambayo inashughulika na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Wednesday, July 22, 2015

Mdau Kanikumbuka

Katika ujumbe wangu wa leo, naendelea na jadi yangu ya kuandika habari za wadau wangu, yaani wasomaji wa vitabu vyangu au wale wanaofaidika na ushauri ninaowapa, hasa kuhusu tamaduni na utandawazi katika dunia ya leo. Napenda kujiwekea kumbukumbu hizi.

Mwanzoni mwa wiki hii, tarehe 19, nilipata ombi la urafiki katika Facebook. Nilivyoona jina la mhusika, Sandy, nilihisi kuwa si jina geni. Nilipoangali picha yake, nilikumbuka kuwa ni mama aliyewahi kunitembelea hapa Chuoni St. Olaf akiwa na rafiki yake, Desemba 2011. Niliandika habari za ujio wao katika blogu hii. Bila kuchelewa, nilikubali mwaliko wa urafiki.

Jana nimepata ujumbe wa mama huyu katika Facebook. Wakati tulipoonana, huyu mama na mwenzake walinunua vitabu vyangu, na aliniambia kuwa nakala ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences alikuwa anamnunulia rafiki yake ambaye alikuwa anapanga safari ya kwenda Afrika.

Kwa bahati mbaya tulipoteana kwa miezi mingi. Hatukuwa na mawasiliano. Baada ya kuungana tena katika Facebook, jana huyu mama ameniandikia ujumbe mfupi: My friend loved your book about the African culture. She had a wonderful experience.

Nimefurahi. Ni jambo la kushukuru kukumbukwa na mdau namna hii. Inaonyesha kuwa tulivyokutana mara ya kwanza tulikutana kwa uzuri na kumbukumbu zikabaki. Nashukuru pia kusikia kuwa rafiki ya huyu mama amekifurahia kitabu changu na safari yake ya Afrika.

Taarifa za aina hii kutoka kwa wadau wangu nazipata muda wote. Zinanipa raha maishani na hamasa ya kuendelea kufanya ninayofanya kama mwandishi na mtoa ushauri. Kuridhika na kufurahi kwa wadau ni tunu kubwa kwangu kuliko malipo ya fedha. Ninamshukuru Mungu kwa yote. Ninamwomba aendelee kunipa uzima siku hadi siku, na akili timamu, niweze kuendelea na majukumu.

Monday, July 20, 2015

Kinachotokea Ukidondosha Pochi Yako Dubai

What happens if you drop your Wallet in Dubai ??Hats Off (y)

Posted by RJ Rijin on Thursday, January 15, 2015

Friday, July 17, 2015

Tumesoma "The Dilemma of a Ghost" na "Anowa"

Leo Ijumaa tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula wa kiangazi. Tumesoma tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost na Anowa, ambazo ni miongoni mwa tamthilia maarufu za Afrika. Hata hivi, kama ilivyo kawaida yangu, nimewatahadharisha wanafunzi kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi ya fasihi ni dhana potofu. Haiwezekani kumaliza, kwa maana ya kuielewa kikamilifu hadi kikomo, hata tukiisoma tena na tena

Ninapenda kufundisha The Dilemma of a Ghost sio tu kwa kuwa ni kazi nzuri kisanaa, bali pia kwa namna inavyoyaanika masuala ya maisha. Mfano muhimu ni suala la mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Msingi wa mahusiano hayo katika tamthilia hii ni ndoa baina ya kijana aitwaye Ato, kutoka Ghana, na Eulalie, mwanamke m-Marekani Mweusi.

Hao wawili wanakutana na kuoana wakiwa Marekani, ambako Ato alikuja kusoma. Eulalie, kama walivyo wa-Marekani Weusi wengi, anafurahi sana kwamba atakwenda Afrika, ambako ni asili ya watu wake. Ana imani kuwa atapokelewa kama mtoto wa nyumbani na atakuwa na maisha ya raha. Ato anachangia matumaini hayo kwa kumwelezea Eulalie mambo mazuri ya Afrika, pamoja na kutia chumvi.

Hali inakuwa tofauti baada ya wawili hao kufika nyumbani kwa Ato. Eulalie anakumbana na madharau kutoka kwa ndugu za Ato kwa kuwa ni kizalia cha watumwa. Tofauti za tamaduni zinachangia matatizo baina yake na ndugu hao.  Hali inaendelea kuwa mbaya na kumkosesha raha Eulalie hadi hatimaye mama mkwe wake anapoamua kurekebisha hali na kuufanya ukoo umkubali.

The Dilemma of a Ghost imesheheni matumizi ya fani ya fasihi simulizi, kama vile nyimbo na hadithi za mapokeo. Dhamira ya kijana kujifanyia uamuzi wake wa kuoa bila kuwashirikisha wanafamilia ni dhamira inayojitokeza katika hadithi nyingi za mapokeo za Afrika. Katika riwaya yake, The Palm Wine Drinkard,  Amos Tutuola aliweka hadithi ya "The Complete Gentleman" yenye muundo huo.

Matumizi ya fani ya fasihi simulizi yanajitokeza zaidi katika tamthilia ya Anowa. Humo tunashuhudia mambo yanayompata Anowa, msichana mzuri kuliko wote ambaye alikuwa anawakataa vijana wote waliokuwa wanamchumbia. Hatimaye anajichagulia mwenyewe kijana ambaye wazazi wake hawaridhiki naye. Yeye na mume wake wanahama nyumbani na kwenda mbali ambako wanajitafutia maisha. Hata hivi mwisho wao si mzuri.

Muundo wa hadithi ni ule unaofahamika katika hadithi za ki-Afrika na zinginezo ulimwenguni. Majivuno na ukaidi kwa wazee, wahenga, au miungu, hayana mwisho mwema. Wagriki wa kale walikuwa na dhana ya "hubris," kuielezea tabia hii. Waandishi kadhaa wa Afrika wametunga hadithi zenye dhamira hiyo. Mifano ni riwaya ya Things Fall Apart ya Chinua Achebe na riwaya ya Chaka ya Thomas Mofolo.

Kumalizia wiki hii ya kwanza, na ili kuwapa wanafunzi fursa ya kutafakari masuala muhimu, nimewapa jukumu la kuandika insha fupi moja kufuatana na maelekezo haya:

1) Discuss a female character in The Dilemma of a Ghost or Anowa.

2) Write about children in The Dilemma of a Ghost and Anowa.

3) Discuss the relationship between one couple--a man and a woman--in The Dilemma of a Ghost or Anowa.

Wednesday, July 15, 2015

Tamasha la Afrifest: Agosti 1

Tamasha la Afrifest linakaribia. Litafanyika Agosti 1 mjini Brooklyn Park, Minnesota. Tamasha hili, ambalo hufanyika kila mwaka wakati kama huu, ni fursa kwa watu wenye asili ya Afrika kuonyesha mchango wao kihistoria katika nyanja mbali mbali.

Kunakuwa na maonesho ya mchango wa watu wenye asili ya Afrika katika historia ya binadamu, kuanzia chimbuko lake Afrika hadi kuenea katika nchi za mbali, kama vile Mashariki ya Kati, Asia, Ulaya, Marekani ya Kaskazini, ya Kati, na ya Kusini.

Ni fursa ya kujikumbusha historia ya himaya za kale barani Afrika, utumwa, ukoloni, mapambano dhidi ya ukoloni, juhudi za kuwaunganisha watu wenye asili ya Afrika ulimwenguni ("Pan-Africanism"). Afrifest hukumbushia itikadi na harakati zingine zaidi ya "Pan Africanism," kama vile "Negritude" na "Rastafarianism." Tangu kuanzishwa kwa Afrifest, jukumu la kutoa elimu hii limekuwa juu yangu, na niliandaa kijitabu kiitwacho Africans in the World, ambacho hupatikana kwenye tamasha.

Afrifest ni fursa ya kuonyesha utamaduni wa watu wenye asili ya Afrika unavyojidhihirisha katika vyakula, mavazi, fasihi, muziki na kadhalika. Ni fursa ya watu wa nchi na mataifa mbali mbali kukutana na kufahamiana. Huwavutia watu wa kila namna, kama vile wale ambao wamesafiria Afrika au wanawazia kwenda, au wale wenye mahusiano na wa-Afrika wa huku ughaibuni yaani wanadiaspora. Huwavutia hata wale ambao hawana uhusiano na Afrika, kwa mfano wale ambao wanapenda tu kujua kuhusu Afrika.

Ninapenda kushiriki matamasha ya Afrifest kama mtafiti na mwalimu wa tamaduni na fasihi, zikiwemo fasihi za wa-Afrika na wengine wenye asili ya Afrika. Zaidi ya hayo, ninaelezea shughuli zangu kama mshauri katika programu za vyuo vya Marekani za kupeleka wanafunzi Afrika.

Katika Afrifest, sawa na matamasha mengine, nawakilisha vitabu vyangu na kukutana na wadau mbali mbali. Ni fursa ya kuongelea mambo ya uandishi, na hasa uzoefu wangu wa kuandika juu ya wa-Afrika na wa-Marekani.

Si rahisi kuelezea kila kitu kinachofanyika katika Afrifest. Mambo ambayo sijayagusia ni pamoja na maonesho ya taasisi zinazotoa huduma za kijamii. Kuna michezo ya watoto, na kwa mwaka huu, tumeanzisha program ya ziada: nitakuwa na wasaa wa kuwaelimisha na kuwaburudisha watoto na hata vijana na watu wazima kwa hadithi za jadi kama za wa-Matengo.

Tuesday, July 14, 2015

Nawashangaa CCM

Ninawashangaa wanaCCM wanaolalamikia mchakato wa chama chao wa kumpata mgombea urais. Mwaka 2010 CHADEMA walilalamika sana kwamba wamefanyiwa rafu na CCM. Hakuna yeyote katika CCM aliyewasikiliza CHADEMA, wala kuwaonea huruma. CCM wote waliibeza CHADEMA, kwamba ingojee uchaguzi ujao.

Sasa leo wanalalamika kuwa wamefanyiwa rafu huko huko CCM. Sio kwamba hao wanachukia rafu. Wanalalamika kwa sababu rafu wamefanyiwa wao. Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa naona kuwa hawana sababu ya kulalamika, kwani wanavuna walichopanda. Labda watajifunza umuhimu wa kutetea haki wakati wote na kwa yeyote.

Sunday, July 12, 2015

Kesho Naanza Tena Kufundisha

Hiki ni kipindi cha kiangazi, ambacho kwa ki-Ingereza huitwa "summer." Katika chuo chetu cha St.Olaf, walimu hatuwajibiki kufundisha kipindi hiki, ambacho hudumu karibu miezi minne. Ila kama mwalimu anapenda, anaweza kufundisha. Kozi za kipindi hiki cha kiangazi hudumu wiki yapata tano, lakini kozi inafanana kwa uzito wake sawa na kozi za muhula wa kawaida.

Kwa miaka niliyofundisha hapa, mara kwa mara nimefundisha kozi wakati wa kiangazi. Uzuri wake mojawapo ni kuwa wanafunzi huwa wachache, na kwetu tunaofundisha fasihi, ni wakati mzuri wa kujaribisha vitabu vipya. Kozi ambayo nitafundisha kipindi hiki ni fasihi ya Afrika (African Literature).  Nitatumia vitabu kutoka sehemu mbali mbali za Afrika.

Kitabu kimojawapo ni Minaret, ambayo ni riwaya ya Leila Aboulela wa Sudan. Nilifundisha riwaya hii muhula uliopita, na iliwavutia wanafunzi na mimi pia. Ingawa ni hadithi ya kubuniwa inatupa picha nzuri ya maisha ya watu wa Khartoum, ambao ni wa-Islam wa tabaka la juu, si walalahoi. Wanafunzi wangu walishukuru kusoma riwaya hii kwa vile iliwapa fursa ya kuielewa angalau misingi ya u-Islam. Kutokana na jinsi tulivyopendezwa na riwaya hii, niliamua kuifundisha tena, na ninapangia kufundisha riwaya zingine za Leila Aboulela siku za usoni, panapo majaliwa.

Kitabu kingine ni The Thing Around Your Neck, ambacho ni mkusanyo wa hadithi za Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria. Huyu ni mwandishi ambaye ametukuka miaka ya karibuni na anasifika sana. Nimefundisha kazi zake kadhaa: Purple Hibiscus, Half of a Yellow Sun, na Americanah. Ni mwandishi mwenye kipaji sana, ingawa ni mdogo kwa umri.

Nitafundisha pia tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost and Anowa. Aidoo ni mwandishi mkongwe, ambaye alianza kujipatia umaarufu kimataifa miaka ya sitini na kitu kwa tamthilia na hadithi fupi, na hatimaye riwaya. Nimefundisha baadhi ya kazi zake. Nimefundisha The Dilemma of a Ghost mara kadhaa.

Kitabu kingine nitakachofundisha ni The Tuner of Silences, ambayo ni riwaya ya Mia Couto wa Msumbiji. Sijawahi kusoma chochote alichoandika mwandishi huyu, lakini ninajua kuwa ni maarufu. Kwa hivyo, niliona nijiongezee ufahamu wangu sambamba na kufundisha kazi ya fasihi kutoka katika lugha ambayo si ya ki-Ingereza. Riwaya hii imetafsiriwa kutoka k-Reno. Ingawa katika idara yetu ya ki-ingereza hapa chuoni St. Olaf tunapendelea kufundisha kazi zilizoandikwa kwa ki-ingereza, tunaona si vibaya mara moja moja kufundisha kazi zilizotafsiriwa kwa Ki-Ingereza.

Nitafundisha pia tamthilia ya Athol Fugard iitwayo Valley Song. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa Afrika Kusini, ambaye tamthilia zake kadhaa nimewahi kufundisha. Mifano ni Master Harold and the Boys, A Lesson From Aloes, na Sorrows and Rejoicings. Nimefundisha Sorrows and Rejoicings mara kadhaa, na kila mara nazidi kuguswa upya.

Kitabu cha sita ni The Beautiful Things That Heaven Bears, ambayo ni riwaya ya Dinaw Mengestu, mwandishi chipukizi wa Ethiopia. Sijawahi kusoma kazi yoyote ya mwandishi huyu, ila najua kuwa tayari ameshajijengea sifa. Nimeanza kusoma hii riwaya yake na ninaiona ni yenye mvuto mkubwa kwa jinsi inavyoelezea maisha ya vijana wa ki-Afrika hapa Marekani. Hii ni dhamira moja muhimu katika riwaya ya Americanah ya Chimamanda Ngozi Adichie, ambaye nimemtaja hapo juu.Tuesday, July 7, 2015

Ukiwa na Siri Iweke Kitabuni

Wengi wetu tumesikia kwamba ukiwa na siri iweke kitabuni; mw-Afrika hataiona. Kwetu wa-Tanzania, hali ni hiyo hiyo. Mwaka hadi mwaka, tumekuwa tukisikia jinsi utamaduni wa kusoma vitabu unavyokosekana Tanzania. Si jambo la kujivunia.

Nimekuwa nikiandika mara kwa mara hali ninayoiona hapa Marekani, katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba. Wa-Marekani kama inavyoonekana katika picha nilizoweka hapa, wana tabia tofauti.

Picha ya katikati niliipiga katika tamasha la vitabu Minneapolis. Ya chini niliipiga katika tamasha la vitabu Mankato. Picha ya juu kabisa sikumbuki niliipata wapi. Zote zinaonyesha jinsi watu wanavyosaka vitabu na kuchungulia yaliyomo. Sijui kama kuna siri iliyofichwa kitabuni ambayo hawataigundua.

Ninaweza kuleta mfano moja mdogo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambamo nimeweka taarifa kuhusu wa-Marekani na wa-Afrika. Tangu kichapishwe, mwaka 2005, maelfu ya wa-Marekani wamekisoma. Wanazijua siri zilizomo.

Mama mmoja m-Tanzania aliyeanzisha na anaendesha taasisi fulani alikuja hapa Marekani kuonana na washirika wake. Kwenye jimbo la Colorado aliulizwa kama amesoma kitabu hiki. Alikiri kuwa hakuwa amekisoma. Baada ya kurudi Tanzania, aliwasiliana nami akanielezea tukio hili. Tulifanya mpango, nikampelekea nakala.

Hiyo si hali ya kujivunia. Wenzetu wa-Marekani wanazoeshwa kuvipenda vitabu tangu utotoni. Wanakulia katika utamaduni huo. Kutokana na kulelewa katika utamaduni huo, hata wazee wananunua na kusoma vitabu, kama vilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Sunday, July 5, 2015

Majadiliano na Profesa Joseph Mbele

MAJADILIANO HAYA YAFENYIKA KATI YA MANDELA PALLANGYO. NA PROFESA JOSEPH MBELE WA CHUO KIKUU CHA OLAF CHA MAREKANI.
PROFESA JOSEPH MBELE

Safari yako ya uandishi ilianza muda mrefu. Je ni kipi kinakutia moyo na kuzidi kufanya kazi hii ngumu?
PROF: JOSEPH MBELE
Mimi ni mwalimu na ninauona uandishi kama sehemu ya ufundishaji au aina ya ufundishaji. Ndio maana uandishi wangu unaelekea zaidi katika mambo yanayoelimisha. Kazi pekee niliyoitamani hata kabla sijaanza shule ilikuwa ni ualimu. Kwa hivyo, ninapenda kuandika kama ninavyopenda kufundisha darasani.

Uliwahi kukutana na maneno mabaya kama kukatishwa tamaa au kukashifiwa wakati ulipokuwa unaanza fani?
PROF: JOSEPH MBELE
Sikuwahi kukutana na maneno ya aina hiyo tangu mwanzo. Uandishi wangu umekuwa zaidi wa kitaaluma, ambao unatokana na utafiti. Hakuna wakati ambapo uandishi wangu huo umeleta maneno mabaya au ya kukatisha tamaa. Lakini kwa kuwa ninaandika pia magazetini na mitandaoni kuhusu masuala ya kawaida ya maisha, wakati mwingine nakutana na maneno mabaya. Hapa ninamaanisha maneno yasiyozingatia hoja, bali yananilenga mimi. Ninawaona wanaofanya hivyo kuwa ni wajinga, wasiojiamini, kwani hata hawajitambulishi. Ninawaheshimu watu wanaopinga hoja kwa hoja. Wanatajirisha mijadala na wanatupanua mawazo.

Umeandika vitabu vingi. Licha ya kuwa ni Profesa mwenye kazi nyingi. Je unawezaje kutenga muda wa kuandika na kutekeleza majukumu mengine kwa ufasaha? Na je vitabu vyako vinapatikanaje?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema, uandishi wangu kwa ujumla ni mwendelezo tu wa ufundishaji. Uandishi unanisaidia kufafanua mambo akilini mwangu. Ninapoandika kuhusu masuala ya kawaida ya jamii, najiona ninaburudisha akili yangu. Mara kwa mara naandika kwa mizaha, na hiyo inaburudisha. Baada ya burudani hiyo, akili inakuwa tayari kufanya kazi ngumu. Uandishi wa masuala ya kawaida, pamoja na usomaji wa vitabu, ni burudani ya kutosha.
Vitabu vyangu vinapatikana mtandaoni, http://www.lulu.com/spotlight/mbele na Amazon.com. Vinapatikana kama vitabu halisi, lakini vingine pia kama vitabu pepe. Ninapenda vipatikane Tanzania pia. Kwa sasa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana kwenye kituo cha utalii cha Burunge, mkoani Manyara: imborutours@gmail.com
kitabu 1

Fani hii ya uandishi, unadhani vijana tumeivamia? Au basi unaridhishwa na kiwango cha uandishi wa vijana hasa tunaochipukia?
PROF: JOSEPH MBELE
Ninadhani yeyote mwenye hamu ya kuandika awe huru kufanya hivyo. Kinachotakiwa ni uvumilivu, kwani haiwezekani kuwa mwandishi bora haraka bila uzoefu. Pia, ni lazima vijana na waandishi kwa ujumla wawe wasomaji makini. Kutegemea na aina ya uandishi ambayo kijana anataka kuandika, awasome waandishi wa mataifa mbali mbali waliotukuka katika aina ile ya uandishi.

Watu wengi wanadhani kazi ya uandishi inalipa na kutajirisha haraka-haraka. Wakati mwaandishi uambulia mrahaba wa asilimia kumi (10%) katika mauzo ya kazi yake ama asilipwe kabisa.
PROF: JOSEPH MBELE
Mwandishi aandike pale anapoona ana jambo la kusema. Msukumo utoke ndani mwake, na akisha andika ajisikie ametua mzigo. Asihamakie mambo ya nje, kama vile pesa. Mategemeo ya pesa hayaleti uandishi bora. Fundisho hili tumepewa na waandishi maarufu, kama vile Ernest Hemingway wa Marekani na Mario Vargas Llosa wa Peru. Jambo la msingi ni mwandishi kuiridhisha nafsi yake, na kuikubali kazi yake, kwamba imewasilisha kwa uaminifu na ukweli yale aliyokuwa nayo moyoni. Akiridhika kabisa, hiyo ni tunu bora kuliko pesa. Fedha ni matokeo. Vile vile, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha ya kuwawezesha kumudu maisha kutokana na uandishi. Waandishi chipukizi watambue hilo, na wale ambao hawana nia ya dhati ya kuwa waandishi wakumbuke hilo, wasije wakajisumbua na ndoto za bure.
Ninavyofahamu, mrahaba wa 10% au zaidi kidogo ni wa kawaida duniani kote, isipokuwa kwa waandishi maarufu.

Je wewe unadhani ni sahihi mtu kuandika kitabu mwaka ama zaidi na kulipwa ujira wa kipuuzi namna hii?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema, msukumo wa mwandishi uwe kusema yaliyomo moyoni mwake, kwa uaminifu na ukweli kadiri inavyowezekana. Kutokana na hilo, waandishi makini hutumia muda mwingi kurekebisha maandishi yao. Ukisoma habari za waandishi maarufu, kama Hemingway, utashangaa jinsi walivyokuwa wanarekebisha maandishi yao mara nyingi sana, na pengine kuishia kutoridhika na kuyaweka kando. Haraka haraka haina baraka. Kitabu kinaweza kuhitaji miaka mingi kukifikisha katika hali ya kumridhisha mwandishi makini. Mimi mwenyewe nilitumia miaka yapata 23 kukiandaa kitabu cha Matengo Folktales.
kitabu 2

Wachapishaji wengi duniani walikuwa kama miungu watu. Na hata basi hao watunzi waliokuwa na vipaji vikubwa kama akina Shaaban Robert, bado awakuwa na sauti mbele yao. Walikiwa ni watu wa kunyenyekewa sana na hata watu kujipendekeza. Ili tu kazi zao zichapishwe.
Lakini sasa naona kiburi hiki kinaanza kufyekwa-fyekwa na utandawazi. Mimi ninaomba utufafanulie ni namna gani waandishi wanaoteseka miaka na miaka wanaweza kufanya kusudi kuchapisha kazi zao kwa kutumia mtandao
PROF: JOSEPH MBELE
Ni kweli, wachapishaji wamekuwa kama miungu watu. Hata Shaaban Robert alilalamika kuhusu wachapishaji. Ni kweli kuwa siku hizi kuna tekinolojia za uchapishaji mtandaoni ambazo zinamwezesha mwandishi yeyote kuchapisha kitabu chake. Kinachotakiwa ni kwa mwandishi kujibidisha kusoma kuhusu tekinolojia hizi na akiamua, azitumie. Kuna aina tofauti za uchapishaji wa mtandaoni, na ni juu ya mwandishi kuamua anaipenda zaidi ipi.

Je kuna madhara gani yanaweza kujitokeza katika mfumo wa kujichapishia katika hiyo mitandao?
PROF: JOSEPH MBELE
Sidhani kama kuna madhara. Badala yake, naona uchapishaji wa mtandaoni umeleta demokrasia zaidi katika uwanja wa uchapishaji, tofauti na jadi tuliyozoea ya wachapishaji kuhodhi mamlaka.
Kuna watu ambao wanalalamika kuwa uhuru huu umesababisha machapisho ya viwango duni kuchapishwa kiholela. Hilo ni suala tata. Tukiangalia kwa upande wa wasomaji ambao tunaweza kuwaita wateja, nafikiri tunapaswa kutambua kuwa wao ndio waamuzi. Ninaamini kuwa wataweza kupambanua kati ya kilicho bora na kilicho duni.

Mtu anapochapisha katika mtandao labda. Labda mwingine anataka tu achapishe haraka-haraka ili aonekane na kupata pesa, bila hata kazi yake kuhaririwa uoni ni tatizo pia?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema hapa juu, ninawategemea wateja. Kama mwandishi atachapisha kitabu duni, anaweza kuwadanganya wanunuaji wa mwanzo, lakini wateja huambiana kuhusu kitu walichonunua. Kama ni kibovu, kitakosa wanunuaji. Isipokuwa, labda niongezee kuwa mtazamo wangu huu umejengeka katika imani kwamba wateja ni watu wenye akili, kwani kama akili yao ni duni, hoja yangu itadhoofika.

Kuingia kwa teknolojia kwa kasi. Je unahisi ipo siku haya makampuni ya kuchapisha yatageuka na kuwa maghala?
PROF: JOSEPH MBELE
Suala hili linajadiliwa sana katika ulimwengu wa leo. Jambo moja linalojitokeza ni kwamba makampuni kama yale ya Marekani yameshaanza kujihami kwa kuingia katika matumizi ya hizi tekinolojia mpya za uchapishaji, sambamba na uchapishaji wa jadi. Hakuna anayejua kama uchapishaji wa jadi utakufa kabisa. Nikitoa mfano wa kuwepo kwa vitabu pepe, jambo moja ambalo ni wazi ni kuwa watu wengi wanataka kushika kitabu mkononi kama zamani, pamoja na kwamba siku hizi kuna vitabu pepe.

Licha ya mfumo wa kujichapishia mtandaoni kwa mrahisi kidogo. Uoni kama ni ishara ya kukubali na kukaribisha ukoloni mpya kwa mikono miwili? Au kusema shikamoo ukoloni?
PROF: JOSEPH MBELE
Tekinolojia ya kujichapishia mtandaoni, kama nilivyosema, imeboresha demokrasia katika uchapishaji. Kwa msingi huo, hata waandishi ambao hawakuwa na fursa ya kujieleza kwa walimwengu sasa wanayo fursa. Ukoloni wa fikra ambao ulisambazwa sana na vitabu, vitabu vilivyochapishwa kwa mtindo wa kibabe kama tulivyosema hapa juu, unaweza kupigwa vita na wanyonge kwa kutumia tekinolojia hii ya uchapishaji mtandaoni.

Kuna watu wanaondika. Na wapo wengi wanaojifunza kuandika na wanapenda! Lakini wanakatishwa tamaa kutokana na mifumo iliyopo kama kupuuzwa na kuachwa.
Naomba uwape neno na kuwatia nguvu.
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema hapa juu, mtu mwenye nia ya dhati ya kuandika hawezi kuyumbishwa. Anafuata msukumo wa moyoni mwake hadi mwisho. Anayekatishwa tamaa ni yule ambaye hakuwa thabiti katika nia na msukumo wa ndani. Mimi mwenyewe, naandika vitabu kwa sababu siridhiki na vile ninavyovisoma. Ninaandika vitabu ambavyo ningependa viwepo bali havipo, vitabu ambavyo ningependa kuvisoma, bali sivioni. Kwa hivi, kwa kiasi kikubwa ninajiandikia mwenyewe. Siyumbishwi na yeyote.
Ustahimilivu ni muhimu katika uandishi. Waandishi maarufu wa kimataifa wanaongelea jambo hilo. Wanakumbana na vipingamizi, lakini hawakati tamaa. Kipingamizi kimoja ni kuwa kuna nyakati ambapo mwandishi anashindwa kuandika. Akili haifanyi kazi. Mwandishi wa kweli hakati tamaa. Anajua kuna wakati utakuja ambapo ataweza kuendelea kuandika.
Vile vile wako waandishi ambao kazi zao zilikataliwa mara nyingi na wachapishaji. Hawakukata tamaa. Baada ya kuchapishwa, kazi hizo hizo zilizokataliwa zilikuja kuwa maarufu. Mwandishi mwenye msukumo wa
kutoka ndani, ana kiu ya kuandika. Akisha andika anakuwa na faraja au furaha. Hawezi kuacha kuandika, wala hawezi kukatishwa tamaa.

Picha zote kwa hisani ya http://www.josephmbele.blogspot.com
CHANZO: Mandelapallangyo.com

Friday, July 3, 2015

Mungu (Allah) Hana Ubaguzi

Blogu yangu hii ni uwanja huru kwa fikra na mijadala, ikiwemo mijadala kuhusu dini. Leo, kwa kifupi na lugha rahisi, napenda kuibua suala la dini na ubaguzi.

Laiti sisi tunaosema tuna dini tungetambua kuwa Mungu hana ubaguzi. Mungu, ambaye kulingana na tofauti za lugha, huitwa kwa majina mbali mbali, anathibitisha jinsi anavyowapenda wanadamu, wa dini zote, na wasio na dini.

Mungu anateremsha baraka zake bila ubaguzi. Anawapa uzazi watu wenye dini, sawa na wasio na dini. Wa-Islam wanazaa, wa-Kristu wanazaa, wa-Hindu wanazaa, na wa dini zingine kadhalika. Wasio na dini wanazaa.

Mungu anateremsha mvua kuotesha mbegu katika mashamba ya wa-Islamu, ya wa-Hindu, ya wa-Kristu, na ya wengine, hata wasio na dini. Kuku wa mu-Islam anataga mayai na kuangua vifaranga, sawa na kuku wa m-Kristu, sawa na kuku wa asiye na dini. Mungu hana ubaguzi katika kuteremsha neema zake.

Sasa basi, kwa nini wanadamu wengi wanaosema wana dini ni wabaguzi? Kwa nini wanatumia kigezo cha dini kujifanya wao ni bora kuliko wengine? Wanapobaguana namna hii, wanafuata njia ya Mungu au ya shetani?

Thursday, July 2, 2015

Leo ni Kumbukumbu ya Kifo cha Hemingway

Leo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwandishi Ernest Hemingway. Alikufa tarehe 2 Julai, mwaka 1961, nyumbani mwake Ketchum, Idaho. Alikufa katika nyumba nayoonekana pichani ambayo ilipigwa na Jimmy Gildea wakati wa safari zake za kuandaa filamu ya Papa's Shadow.

Maelezo ya namna Hemingway alivyokufa yanapingana kidogo. Kila mtu anakiri kuwa alikufa kwa risasi ya bunduki. Karibu kila mtu anasema kuwa Hemingway alijiua kwa kujipiga risasi, akiwa peke yake ghorofa ya juu.

Lakini mke wake, Mary Welsh Hemingway, ambaye wakati wa tukio alikuwa katika nyumba hiyo kwa chini, alitoa tamko kuwa ilikuwa ni ajali:

Mr. Hemingway accidentally killed himself while cleaning a gun this morning at 7:30 A.M. No time has been set for the funeral services, which will be private.

Kila ninapowazia kifo cha Hemingway, nakumbuka jinsi alivyokuwa na mikosi ya ajali katika maisha yake. Ninavyowazia kuwa alijiua, nakumbuka misiba kadhaa ya watu kujiua katika ukoo wa Hemingway. Ninawazia pia kuwa mimi nimeishi miaka mingi kumzidi Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 akafa mwaka 1962.

Ninajiuliza nimefanya nini katika miaka yangu yote hii, nikijifananisha na Hemingway, ambaye alikuwa mwandishi maarufu aliyeongoza njia kwa aina yake ya uandishi, akapata tuzo ya Nobel mwaka 1954.

Hemingway aliongelea kifo, tena na tena, katika maandishi yake. Kauli yake moja inayojulikana zaidi ni hii:

Every man's life ends the same way. It is only the details of how he lived and how he died that distinguish one man from another.


Wednesday, July 1, 2015

Vitabu Nilivyojipatia Wiki Hii

Kama ilivyo kawaida yangu, napenda kuongelea vitabu nimeongeza katika maktaba yangu. Wiki hii, ambayo bado haijaisha, nimejipatia vitabu vinne. Cha kwanza ni Jake Riley: Irreparably Damaged, kilichotungwa na Rebecca Fjelland Davis. Nilikinunua tarehe 28 mwezi huu, katika tamasha la vitabu, Deep Valley Book Festival, mjini Mankato kutoka kwa mwandishi, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Kufuatana na maelezo, hii ni hadithi ya kubuniwa.

Katika tamasha hilo, nilinunua pia kitabu kiitwacho No Behind, kilichotungwa na Louise Parker Kelly. Tuliongea kidogo, na mwandishi, akaniambia kuwa ni mwalimu na kuwa kitabu chake ni hadithi ya kubuniwa, kuhusu maisha na harakati za mtoto wa shule eneo la Washington D.C.

Kitabu kingine ambacho nilikipata jana ni Noontide Toll. Ni mkusanyo wa hadithi fupi za Romesh Gunesekera, mwandishi mahiri sana wa Sri Lanka. Sikumbuki kama nilikinunua kitabu hiki. Huenda wachapishaji wameniletea kwa kuwa nimewahi kuagiza vitabu vingine vya Gunesekera kwa kufundishia. Gunesekera ni mmoja wa waandishi wanaonivutia sana kwa uwezo wao wa kutumia ki-Ingereza.

Kitabu kingine, Lucy: the Beginnings of Humankind, nilikinunua jana katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf. Waandishi wake ni Donald Johanson na Maitland Edey. Nilivutiwa na jina la Lucy kwenye uso wa kitabu, nikahisi kuwa kitabu kinamhusu binadamu wa kwanza, ambaye masalia yake yalivumbuliwa Ethiopia. Nilipokisogelea, niliona kuwa ni hivyo.

Kutokana na maelezo kwenye jalada la mbele, kitabu hiki kinasimulia namna uvumbuzi huu ulivyotokea na maelezo kuhusu binadamu huyu wa kwanza. Kwa mujibu wa uchambuzi katika gazeti la The New York Times Book Review, dhamira ya kitabu hiki ni "One of the most compelling scientific investigations ever undertaken." Ni wazi kuwa kitabu hiki ni hazina isiyo kifani.