Saturday, December 27, 2008

Kijitabu Changu Kipya















Miaka miwili iliyopita niliombwa kushiriki katika maonyesho ya utamaduni wa Mwafrika, soma hapa, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mjini Minneapolis katika jimbo la Minnesota, Marekani. Maonyesho hayo yalipangwa kujumlisha mambo mengi: historia ya Mwafrika duniani na harakati alizopitia, mafanikio na mchango wake, na hali yake ya sasa na baadaye.

Wasanii, wabunifu wa mavazi, wanamuziki, na wengine walialikwa kutoa mchango wao. Mimi nilialikwa kuandaa vielelezo vya mambo muhimu katika historia ya Mwafrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika hadi kusambaa kwa Waafrika sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Marekani, Ulaya, na Asia.

Nilifanya utafiti nikaandika habari hizo kwa mtindo wa insha fupi kumi. Kila insha niliiweka kwenye bango kubwa na kila bango liliambatana na picha kadhaa. Siku ya tamasha, niliyabandika mabango hayo kwenye kuta za ukumbi niliopangiwa. Watu walifika humo na kusoma kwa wakati wao, wakiangalia pia zile picha.

Mama mmoja aliyehudhuria na kuangalia maonyesho yangu alipendekeza kuwa nitoe kitabu, ili watu waweze kuendelea kusoma majumbani. Nilifuata ushauri wa huyu mama, na kitabu nilikitoa, chenye habari na picha zile zile zilizomo kwenye mabango.

Kitabu ni kidogo, maana nilikuwa na mabango kumi tu, lakini kinaibua masuala mengi. Kwa mfano, nawakumbusha wasomaji kwamba Afrika ndipo binadamu walipotokea. Pamoja na kuongelea masuala kama utumwa, ukoloni, harakati za kupigania uhuru, na majukumu yanayotukabili leo na siku za usoni, nawakumbusha wasomaji kuhusu mchango wa Waafrika katika nyanja mbali mbali, mchango ambao haujulikani vizuri au umesahaulika kabisa hata miongoni mwa Waafrika wenyewe.

Kuhusu upatikanaji wa kijitabu hiki, tuma barua pepe info@africonexion.com.

4 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Asante sana Profesa. Ni kweli twahitaji kuwaelimisha wengi juu ya mengi yaliyo na yanavyotokea Afrika. Kuna mengi wasiyoyajua na pia hata yale mengi wayajuayo hawayajui kwa usahihi. Hili lasikitisha mno. Kwa hiyo naamini kwa wale wenye kukisoma wataelewa na kuendelea kuelewesha uma.
Asante na Kila la kheri katika uelimishaji na ukomboaji wa fikra za wengi katika mwaka ujao wa 2009.

www.changamotoyetu.blogspot.com/2008/12/happy-new-year-bloggers.html

Mbele said...

Shukrani. Kama unavyojua, huku ughaibuni watoto wa kiAfrika wana tatizo la kupata elimu kuhusu Afrika. Wazazi nao kwa ujumla wanahangaika na kazi na hawana muda wa kuwaelimisha hao watoto. Vile vile, wenyeji wa huku ughaibuni pamoja na watoto wao, hawaelewi sana kuhusu Afrika na mchango wa Waafrika duniani. Ndio maana mimi, kama mwalimu, niliona niandike kijitabu hiki, kipunguze tatizo hili.

Khalfan Abdallah Salim said...

Ahsante kwa maandishi yako. Nimejaribu kutuma barua pepe kuomba kopi ya kijitabu hicho, lakini imeshindikana, barua yangu imerejeshwa. Naomba unitumie kwa:donkasam@yahoo.com

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim,

Shukrani kwa ujumbe wako. Samahani kwa usumbufu. Nilichelewa kulipia anwani hii kwa vile nilikuwa mgonjwa kwa muda mrefu. Inabidi niifufue, ndipo iweze kutumika.

Ninayo nyingine, ambayo ni africonexion@gmail.com.

Kijitabu hiki hakipatikani mtandaoni. Itabidi uniletee anwani ya posta.

Narudia samahani, na asante.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...