Saturday, May 30, 2015

Ualimu ni Wito

Ualimu unahitaji moyo. Anayedhani ni mchezo, aiangalie na kuitafakari katuni hii.

Bahati mbaya jina la mchoraji sijalipata, ningemshukuru.

Friday, May 29, 2015

Toleo Jipya la "Green Hills of Africa" Linaandaliwa

Nilimpigia simu Mzee Patrick Hemingway tarehe 22 mwezi huu, tukaongea kwa saa moja na robo. Tuliongelea mambo mengi, kama nilivyogusia katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Mzee Patrick Hemingway ni mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway.

Mwandishi huyu ni wa pekee, sio tu kwa kuwa alishinda tuzo ya Nobel, bali pia kwa kuwa mtindo wake wa kuandika ulichangia kubadilisha uandishi wa ki-Ingereza wa karne iliyopita. Katika mfumo wa elimu wa Tanzania wa miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu, wanafunzi tulikuwa tunasoma angalau kitabu kimoja cha Ernest Hemingway, For Whom the Bell Tolls, sambamba na vitabu vingine maarufu vya waandishi mbali mbali.

Katika mazungumzo yetu, Mzee Patrick Hemingway aliniarifu kuwa toleo jipya la kitabu cha Green Hills of Africa litachapishwa miezi ya karibuni. Nilifurahi kusikia habari hii. Green Hills of Africa ni masimulizi ya Ernest Hemingway juu ya safari aliyofanya nchini Tanganyika, mwaka 1933-34. Nilisisimka Mzee Hemingway aliposema kuwa katika toleo hili kutakuwemo "diary" ya mama yake, Pauline, aliyoandika wakati wa safari hiyo.

Nilifahamu kuhusu kuwepo kwa hiyo "diary," na nilifahamu kuwa imehifadhiwa katika chuo kikuu cha Stanford. Kwa miaka kadhaa nilikuwa nikiwazia kwenda kuisoma. Kwa hivi, hii habari kwamba itachapishwa imenifurahisha kwa namna ambayo siwezi kuieleza.

Habari ya kuchapishwa toleo jipya la Green Hills of Africa ni muhimu sana. Tanzania ingeweza kuitumia hii kama fursa adimu ya kujitangaza kwa ajili ya utalii.  Lakini kutokana na kukosekana kwa utamadini wa kusoma vitabu, sitegemei jambo hilo litafanyika. Tofauti na zamani, Tanzania ya leo haimjui Hemingway.

Wenzetu katika nchi zingine wamechangamkia fursa za namna hii na wanafaidika. Mfano moja ni mji uitwao Pamplona, nchini Hispania. Mji ule tangu zamani una jadi yake ya mchezo wa "bull fighting" ambao unamshindanisha shujaa na fahali uwanjani. Ernest Hemingway alitembelea Pamplona mwaka 1923 akavutiwa na mchezo huo. Aliandika kitabu The Sun Also Rises, ambacho kilielezea "bull fighting" na kuufanya mji ule uwe maarufu sana, unaovutia maelfu ya watalii, ingawa haukuwa na umaarufu huo kabla. Sehemu zingine ambamo Hemingway aliishi au alipita na kuandika habari zake, kama vile Oak Park (Illinois), Michigan Kaskazini, Paris, Key West (Florida), Bimini, na Cuba, zinavuna faida kutokana na utalii. Nimewahi kuelezea hayo katika blogu hii.

Nina hakika kuwa mimi ni m-Tanzania wa kwanza kuifahamu habari ya toleo jipya la Green Hills of Africa, na nimeona niiweke hapa katika blogu yangu, nikijua kuwa kuna wa-Tanzania watakaoisoma. Laiti nchi yetu ingekuwa imeamka, ingeanza kujiandaa kuchuma faida za toleo jipya la kitabu hiki kwa kuitangaza Tanzania na sehemu zote alizopitia Hemingway nchini mwetu. Ingekuwa jamii yetu inathamini vitabu, ingeandaa matangazo na makaribisho ya toleo hili jipya. Hii ingekuwa pia fursa ya kuhamasisha utalii wa ndani. Lakini, sina imani yoyote kuwa haya yatafanyika. Ninaifahamu nchi yangu: ni kwenye miti ambako hakuna wajenzi.

Tuesday, May 26, 2015

Mwaliko Chuo Kikuu cha Winona

Nimepata mwaliko kutoka Chuo Kikuu cha Winona, Minnesota, kwenda kutoa mhadhara tarehe 23 Juni. Huu utakuwa ni mchango wangu katika semina ya mafunzo kwa wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali itakayofanyika Juni 17-27. Kama ilivyo kawaida yangu, nimeona niweke kumbukumbu hapa.

Mafunzo haya yatalenga kuwaandaa wanafunzi hao kwa masomo ya juu, waweze kuifahamu hali halisi ya maisha ya chuoni na taratibu za taaluma, waweze kujijengea hali ya kujitambua na uwezo wa uongozi.

Mratibu wa mafunzo, Alexander Hines, ambaye anafahamu kiasi shughuli zangu,  aliniambia tuangalie ni kipi kati ya vitabu vyangu viwili kitafaa zaidi kwa semina hii: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences au Matengo Folktales. Nilishauri kwamba hicho cha pili kingeendana vizuri zaidi na dhamira kuu ya semina.

Tumekubaliana. Tumekubaliana nikaelezee ni nini tunaweza kujifunza kutokana na tamaduni za jadi za Afrika katika masuala haya ya kujitambua, falsafa ya maisha, na uongozi katika dunia ya leo na kesho.

Kama ilivyo kawaida yangu, huwa napokea mialiko ya kutoa mchango wa mawazo kufuatana na mahitaji ya wale wanaonialika. Itabidi nitafakari na kuandaa mawazo yatakayotoa mchango unaohitajika katika semina. Wazo la kutumia kitabu cha Matengo Folktales kama msingi ni wazo muafaka, kwani masimulizi haya ya jadi yanathibitisha jinsi wahenga wetu walivyoyatafakari masuala muhimu ya maisha, mahusiano, na mengine yanatuhusu leo na yataendelea kuwa muhimu daima.
 

Sunday, May 24, 2015

Angalizo kwa Wenye Vyama: Tanzania ni Yetu Wote

Mimi ni m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Natoa angalizo kwa wa-Tanzania wenye vyama, hasa CCM, wazingatie kuwa Tanzania ni yetu wote. Naitaja CCM namna hii kwa sababu ni chama tawala, chenye wajibu wa kuongoza njia na kuwa mfano kwa wengine.

Wa-Tanzania wenye vyama wakumbuke kuwa wao ni wachache kwa kufananisha na idadi ya wa-Tanzania kwa ujumla. Wafanye siasa zao, ila wasisahau jambo hilo. Nasema hivyo kwa sababu wana tabia ya kujiona kuwa wao ndio Tanzania, na Tanzania ni wao.

Kinachonikera zaidi ni fujo. Wa-Tanzania wenye vyama wana tabia ya kuleta fujo na kuhujumu amani, hasa kinapokaribia kipindi cha uchaguzi. Ni aibu sana kwamba, kutokana na fujo za wa-Tanzania wenye vyama, tumefikia mahali sasa ambapo watu wanasali na kufanya ibada kuombea amani. Hii ni fedheha ambayo tumeletewa na wa-Tanzania wenye vyama.

Ni sahihi kumwomba Mungu atupate mvua ya kutosha kwa mazao yetu. Ni sahihi kumwomba atuepushe na majanga kama vile matetemeko ya ardhi. Ni sahihi kumwomba atupe uzima siku hadi siku tuweze kujenga nchi yetu na kutimiza majukumu yetu mengine.

Lakini kuombea amani kwa kuwa inatishiwa na utovu wa nidhamu unaofanywa na wa-Tanzania wenye vyama ni jambo lisilokubalika. Kuombea amani kwa sababu ya utovu wa busara wa watu hao ambao wanadhani nchi hii ni yao peke yao, wanaodhani wana haki ya kujifanyia watakalo katika nchi hii, ni jambo lisilokubalika. Hili si suala la kuombea amani. Ni suala la kupambana na hao wahujumu wa amani.

Inashangaza kwamba hata Ikulu imeshindwa kutambua hilo. Haijawahi kutokea Ikulu ikawaita wa-Tanzania wasio na vyama kwa mazungumzo na mashauriano. Ikulu imekuwa tayari kuwaita wenye vyama na kuongea nao, lakini sio sisi tusio na vyama, ambao ndio wengi zaidi na ni mfano wa kuigwa.

Wa-Tanzania wenye vyama wazingatie kuwa sisi tusio na vyama hatujawahi na hatuna mpango wa kuhujumu amani ya Tanzania kama wanavyofanya wao. Tumetunza heshima ya Tanzania wakati wao wanaihujumu. Wajifunze kutoka kwetu ili wote tudumishe amani na tuipe nchi yetu heshima inayostahili.

Saturday, May 23, 2015

Leo Nimenunua Kitabu: "Jesus: Prophet of Islam"

Leo nilikwenda Minneapolis kwenye mkutano mdogo wa watu wanne ambao tulifanyia katika jengo la maduka na biashara mbali mbali liitwalo Somali Mall. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jingo hili. Nilipata fursa ya kuingia katika duka la vitabu liitwalo Akmal Bookstore, ambalo limejaa vitabu vya ki-Islam katika ki-Arabu na ki-Somali.

Niliuliza iwapo kuna vitabu vya ki-Ingereza, nikaonyeshwa. Niliviona vingi vilivyonivutia, nikanunua kimoja, Jesus: Prophet of Islam, kilichoandikwa na Muhammad 'Ata' ur-Rahim na Ahmad Thomson.

Nimefahamu kwa miaka mingi kuwa katika u-Islam, Yesu anatambulika kama mtume maarufu, ila sio mwana wa Mungu, kama tunavyomwona sisi wa-Kristu. Sioni tatizo, wala sikosi usingizi kwa sababu hiyo. Ninachozingatia ni waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana, kila mtu na imani yake. Tukumbuke kwamba dini zinatofautiana, na kuna dini ambazo hamzimjui Yesu kabisa, iwe ni kama mtume au mwana wa Mungu.

Mara yangu ya kwanza kuelewa namna wa-Islam wanavyomwona Yesu ni wakati nilipokuwa nafundisha somo la "Epic" kwa wanafunzi wa uzamili (M.A.) katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1986-88. Kati ya maandishi ya kitaaluma niliyoyaongelea darasani ni insha maarufu ya Alan Dundes, "The Hero Pattern and the Life of Jesus."

Ulipofika muda wa kuandaa tasnifu, mwanafunzi mojawapo, Hamza Njozi, aliniambia kuwa angepnda kuandika kuhusu masimulizi juu ya Yesu (Issa) katika Qur'an. Niliona ni mada murua. Alifanya utafiti na uchambuzi mzuri akamaliza tasnifu yake. Katika kumwelekeza kwa miezi yote ya utafiti na uandishi wa tasnifu, nami niliweza kufahamu msimamo wa Qur'an juu ya Yesu (Issa).

Hii leo, nilipokiona kitabu cha Jesus: Prophet of Islam, nilikumbuka yote hayo, nikakinunua bila kusita. Nangojea kwa hamu kukisoma.

Friday, May 22, 2015

Msikiti Wachomwa Moto Saudia

Nimeona taarifa leo kuwa msikiti umechomwa moto huko Saudi Arabia. Ni msikiti wa dhehebu la Shia. Kwa wale wasiofahamu, wa-Islam, kama walivyo wa-Kristu, wana madhehebu mengi, kama vile Sunni, Shia, Ismailia, Ahmadiya na Tijanniya.

Habari ya msikiti kuchomwa moto imenikera, kama ninavyokerwa na habari za kuchomwa moto kanisa au nyumba nyingine ya ibada ya dini yoyote. Nimesema tena na tena kuwa ninaziheshimu dini zote, ninaiheshimu misahafu ya dini zote, na ninazihehimu nyumba za ibada za dini zote. Ninaamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya busara ambayo tunapaswa kuifuata.

Sawa na waumini wa dini zingine, nami nililelewa katika imani kwamba dini yangu ndiyo pekee dini ya kweli. Nilifundishwa kwamba nje ya dini yangu, nje ya u-Katoliki, hakuna wokovu. Ninajua kuwa wa-Islamu nao wanafundishwa hivyo hivyo, kuwa nje ya u-Islamu hakuna wokovu. Niliwahi kuwa mwanachama katika mtandao wa Radio Imaan, wa wa-Islam. Waliniambia kuwa mimi ni kafiri na kwamba nisiposilimu sitaingia ahera.

Hii ndio hali halisi. Binafsi nimeamua kujitungia mwelekeo nilioutaja hapa juu, ingawa ninajihesabu kama m-Katoliki. Katika hilo, simtumikii wala kumfuata binadamu. Natumia akili yangu na kufuata dhamiri yangu.

Kwa nini mtu uchome moto msikiti wowote, kanisa lolote, au nyumba ya ibada ya dini yoyote? Kwa nini usikemee kuchomwa moto kwa msikiti wa Shia kwa vile tu wewe ni Sunni, au ni m-Kristu, au ni m-Hindu? Kwa nini usikemee kuchomwa moto kanisa, kwa vile tu wewe si m-Kristu?

Kama hukemei, unaufumbia macho uozo ambao siku moja utakuja kusababisha nyumba ya ibada yako ichomwe moto. Usishangae ikitokea hivyo, wala usikasirike, kwani roho yako haina tofauti na ya yule atakayefanya uhalifu huo. Kilichopo ni kujitambua.

Tumelelewa na tunalelewa katika njia ya giza. Tuamke. Tuanze kujijengea mtazamo mpya wa kuheshimiana wanadamu wote, kila watu na imani yao, wenye dini na wasio na dini, na tuwalee watoto wetu katika njia hiyo.

Hayo ndio mawazo yaliyonijia niliposoma taarifa ya kuchomwa msikiti wa Shia kule Saudia. Ni mawazo yanayoendelea kunisonga na kuisumbua akili yangu. Kama unaona nimepotoka au ninapotosha, nawe ni muumini wa dini, kumbuka kuwa una wajibu wa kujitokeza, kukosoa, na kurekebisha. Ukiacha kufanya hivyo, kumbuka kuna jehenam au motoni, kama tunavyoita wa-Kristu. Na ukichangia, ukajiita "anonymous," unajisumbua na unajidanganya, kwani ingawa mimi sitakutambua, Mungu (Allah) anakuona na atakufichua siku ya kiyama. Kazi kwako.

Thursday, May 21, 2015

Kusonga Mbele na Kutoyumbishwa

Naandika makala hii kuwapa moyo wengine, hasa vijana, wanaojituma kujiendeleza katika fani yoyote na kimaisha kwa ujumla. Kwa ujumla, mawaidha haya yanapatikana vitabuni.

Katika vitabu vinavyoelezea mikakati ya mafanikio, kitu kimoja kinachosisitizwa ni kutambua kwamba unaposonga mbele, kuna watu watakaokuandama kwa mategemeo ya kukukatisha tamaa na kukurudisha nyuma. Watabeza shughuli zako na mafanikio yako.

Kwa mujibu wa vitabu hivyo, hao ni watu wa kuwapuuza. Ni muhimu pia kuwapuuza wale wasio na mtazamo wa maendeleo yao wenyewe. Badala ya kupoteza muda kuwa na watu wa namna hiyo, andamana na watu waliomo katika njia ya mafanikio, au waliofanikiwa. Utajifunza kutoka kwao.

Watu wenye mafanikio, wanajiamini, na hawaoni shida kuwashauri au kuwasaidia wengine nao wafanikiwe. Napenda kunukuu maneno ya Henry Rogers mtu maarufu aliyeanzisha na kuendesha Rogers & Cowan, kampuni ya mahusiano ya jamii:

Not only is it essential to make someone feel important, the art of psychorelations demands that we also make the person feel at ease. As I reflect back on my life, I find that powerful and important people have always made an effort to make me feel comfortable. My experience has been that the more important they are, the more gracious they are. Could it be that their ability to reach out graciously to others has helped make them important? I believe so. (Henry C. Rogers, Rogers' Rules for Success, uk. 44.)

Sijui kama wewe ni mmoja wa hao wanaobeza au wanaohimiza juhudi na mafanikio ya wenzao. Siku chache tu zilizopita, nilisoma kauli za Wema Sepetu, dada m-Tanzania maarufu katika maigizo ya filamu. Alielezea jinsi watu wanavyombeza, kumtukana, na kufanya kila juhudi ya kumkatisha tamaa, hadi amewahi kufikiria kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuishi.

Ni ushuhuda ambao ulinigusa sana. Ni ukweli usiopingika kwamba wako wa-Tanzania wengi wa ovyo kama ilivyoelezwa hapa juu. Hata mimi wananiandama kwa kejeli na mabezo humo mitandaoni, lakini hawajitambulishi. Kwa mfano, nimekumbana na watu wanaokibeza kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambacho kinapendwa na kutumiwa sana, hasa hapa Marekani, na ni msingi mojawapo wa mialiko ya mara kwa mara ya kwenda kutoa mihadhara, kama inavyoonekana pichani hapo juu, katika Chuo cha South Central, Minnesota.

Lakini, utakuta mtu anajitokeza na kutoa kauli ya kubeza bila maelezo wala ushahidi, ili mradi amerusha maneno yanayoweza kukatisha tamaa. Wala hatoi ushauri muafaka, kama anaona mapungufu, ili kuisaidia jamii. Ukitaka mfano, soma ujumbe huu. Kuna wakati hao waropokaji niliamua kuwapa vidonge vyao, kama tunavyosema, kwa kuwaambia waandike vitabu vyao, tuone.

Kwa upande wangu, watu wa namna hiyo wanajisumbua bure. Wanapoteza muda ambao wangeutumia kujiendeleza kwa kusoma. Bora hata wangenitafuta niwape mawazo na uzoefu kama wanavyonitafuta wa-Marekani. Ninawaheshimu wa-Marekani kwa hilo. Ni wasikivu wanapoelezwa mambo wasioyafahamu, kama haya ninayowalezea kuhusu athari za tofauti za tamaduni katika dunia ya utandawazi wa leo. Ni watu wanaotaka mafanikio katika ulimwengu huu.

Hao watu aliowaongelea Wema Sepetu na ambao nami ninawaongelea, nawaonea huruma. Labda siku itafika watakapoanza kuwa na mtazamo mpya. Binafsi nina furaha maishani kwa kuwa ninazingatia malengo niliyojiwekea, na mafanikio ninayaona, hasa katika kuwagusa watu na kuwaneemesha. Nimeshasema kabla kuwa lengo langu kuu ni hilo, sio utajiri wa fedha.

Wednesday, May 20, 2015

Kitabu cha Honwana Kimefika Leo

Leo nina furaha sana. Nimepata kitabu cha Luis Bernardo Honwana, We Killed Mangy Dog and Other Stories, ambacho nilikiagiza siku chache zilizopita.

Hiki ni kitabu ambacho nimekuwa ninakikumbuka kwa namna ya pekee, tangu miaka ya mwanzoni kabisa ya sabini na kitu nilipokisoma kwa mara ya kwanza. Furaha iliyoje kuzikumbuka enzi zile za ujana wangu, nilipokuwa tayari nimetekwa moyo na akili na somo la fasihi ya ki-Ingereza.

Ingawa wakati huu ninapoandika, na kwa siku chache zijazo, niko katika kusahihisha mitihani, nitaanza kukisoma kitabu hiki mara. Siwezi kujizuia. Hatimaye, nitaandika uchambuzi mfupi katika blogu hii.

Kama nilivyosema kabla, kitabu hiki, kutoka Msumbiji, kitakuwa ni kianzio kwa ajili ya kufundisha riwaya ya Mia Couto, The Tuner of Silences, wakati wa kiangazi.

Monday, May 18, 2015

Kitabu cha Dr. John C. Sivalon, M.M.

Leo nimejipatia kitabu cha Dr. John C. Sivalon, M.M. Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985. kilichochapishwa na shirika la Kanisa Katoliki la wa-Benediktini, Ndanda. Kutokana na kutopatikana madukani hapa Marekani, nimekipata kupitia maktaba ya hapa Chuoni St. Olaf, kwa utaratibu wa uazimishanaji wa vitabu baina ya maktaba. Nimejitengenezea nakala kwa matumizi yangu, kama inavyoruhusiwa kisheria.

Hiki ni kitabu kinachojulikana Tanzania kwa kuwa kinatajwatajwa sana na viongozi wa wa-Islam wanaosema kwamba wa-Islam wamekuwa wakihujumiwa na bado wanahujumiwa na serikali ya Tanzania kwa manufaa ya kanisa na wa-Kristu.

Kutokana na madai hayo, kwa miaka yote hii nimekuwa na hamu ya kujisomea kitabu hiki. Sikuwahi kusema lolote juu yake, kwa vile sikuwa nimekisoma. Baada ya kukipata, kama saa mbili tu zilizopita, nimekipitia chote, ila bado sijakisoma kwa makini.

Hata hivi, nimeona kuwa mwandishi ameandika kitabu hiki kwa busara bila ushabiki, nikakumbuka kitabu cha Hamza Njozi, Mauaji ya Mwembechai, ambacho nacho amekiandika kwa busara bila ushabiki. Nimeangalia mtandaoni nikaona kuwa Dr. Sivalon ameandika pia kitabu kingine, God's Mission and Postmodern Culture: The Gift of Uncertainty. Hiki itakuwa rahisi kukinunua hapa Marekani.

Napenda kusema kila mmoja wetu ajisomee mwenyewe kitabu hiki cha Dr. Sivalon cha Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985, ayatafakari yaliyomo. Kwa kuzingatia kuwa bado sijakisoma kwa umakini, napenda kutoa fursa kwa yeyote ambaye amekisoma aweze kutuletea maoni yake. Nami, baada ya kukisoma ipasavyo, nitatoa maoni yangu.

Sunday, May 17, 2015

Tuziheshimu Dini Zote

Yeyote anayefuatilia blogu hii anafahamu kuwa ninahimiza tuziheshimu dini zote, tuiheshimu misahafu yote, tuheshimu haki na uhuru wa kila binadamu kuwemo katika dini yoyote anayoona inamfaa, haki na uhuru wa kubadili dini kufuatana na dhamiri yake, na yeyote asiye na dini anastahili heshima sawa na mwenye dini.

Tuzingatie tangazo la kimataifa la haki za binadamu, ambalo linataja uhuru wa kuabudu kama mmoja ya haki za binadamu. Naamini kuwa msimamo wangu, kama nilivyoueleza hapo juu, ndio njia sahihi inayotupasa kuifuata. Kufanya vingine ni kuendeleza matatizo, migogoro, na dhuluma, na hata umwagaji damu, mambo ambayo tumeyashuhudia kwa karne na karne.

Ninamshukuru Mungu kwa kunipa akili na utashi niweze kutafakari mambo na kuyafanyia maamuzi kwa namna ninayoamini inaendana na mategemeo yake. Simanini kwamba Mungu anataka wanadamu tuwe tunagombana, tunadharauliana, tunakandamizana, au tunapigana.

Mungu huyo huyo amenipa fursa ya kutembea katika nchi nyingi na kuonana na watu wa aina mbali mbali. Mwaka 1991, kwa mfano, nilikwenda India, nikaishi na watu wa dini tofauti na yangu. Nilipata bahati ya kutembezwa katika nyumba za ibada za dini ya Hindu, kama inavyoonekana pichani. Picha moja inanionyesha nikiwa nje ya nyumba ya ibada. Kuna sanamu nyingi, ambazo ni za miungu wa dini ya u-Hindu.

Ninapokuwa katika mazingira kama hayo, ninaonyesha heshima itakiwayo. Wenyeji wangu, wa-Hindu, walinikaribisha katika nyumba zao za ibada, nami nilifanya heshima kama wanavyofanya wao wenyewe. Sioni tatizo kufanya hivyo. Hapakuwa na tatizo kwa upande wao pia, ingawa mimi si muumini wa dini yao.

Miaka ya 1989-90 nilikwenda Lamu, Kenya, kufanya utafiti kuhusu tungo za zamani za ki-Swahili. Lamu ni mji mkongwe wa ki-Islam. Nilikaribishwa vizuri. Wazee kadhaa nami tulianzisha "kijiwe" chetu ambapo tulikuwa tunaongea na kupiga soga.

Siku moja, mzee mmojawapo alinifikisha kwenye nyumba ya Mwana Kupona, mtunzi wa utenzi maarufu wa Mwana Kupona, akanipitisha pia misikitini. Sikuwa nimeingia katika msikiti maisha yangu yote. Nilifuatana na yule mzee huku nikiwa na wasi wasi na uoga. Nilikuwa nimebeba kamera, na aliponikaribisha niingie msikitini, nilimwuliza kama ninaruhusiwa kuingia na kamera. Aliniambia kuwa hakuna tatizo lolote, nikaingia. Nilifanya ziara zangu misikitini kwa heshima zote.

Sioni kwa nini waumini wa dini mbali mbali tusiishi kwa kuheshimiana namna hii, kila mtu na imani yake. Mwenye mawazo tofauti aje hapa tumsikie. Blogu hii ni blogu huru kwa yeyote kutoa mawazo yake. Nami sitachoka kuitumia kuenezea mawazo na mitazamo yangu. Sipendezwi na jinsi watu wanavyoendekeza matatizo na uhasama duniani kwa kisingizio cha dini na misahafu. Nimepinga mambo hayo tangu zamani katika blogu hii.

Saturday, May 16, 2015

Vitabu Nilivyonunua Karibuni

Napenda kujiwekea hapa kumbukumbu za vitabu nilivyonunua katika siku chache zilizopita. Ni faraja kuweza kupita tena katika maduka ya vitabu, baada ya miezi ya kuwa katika hali ngumu kiafya.

Yapata wiki moja iliyopita,  katika duka la vitabu la hapa Chuoni St. Olaf, ambamo daima kunakuwa na vitabu vingi ambavyo sijawahi kuviona, niliguswa kukiona kitabu cha Terry Eagleton, How to Read Literature, ambacho nilikuwa sijawahi hata kukisikia.
Terry Eagleton ni mwananadharia wa fasihi ambaye ni maarufu kabisa. Nilinunua vitabu vyake kadhaa na kuvisoma miaka ya 1980-86 nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu Cha Wisconsin Madison. Nimeanza kusoma na kuvutiwa na How to Read Literature.

Juzi tarehe 14, wakati narudi kutoka Columbia Heights, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la vitabu la Half Price Books ambalo nimelitaja mara nyingi katika blogu hii. Nilinunua vitabu vitatu.

Kimoja ni Without a Name and Under the Tongue. Hizi ni riwaya mbili ambazo zimechapishwa katika hiki kitabu kimoja. Mtunzi ni Yvonne Vera wa Zimbabwe, ambaye ni kati ya waandishi wa kizazi kipya wa Zimbabwe. Nilishafundisha riwaya yake Butterfly Burning, na nilivyokiona kitabu chake hiyo juzi, nilifikiwa na hamu ya kusoma zaidi uandishi wake, nisikie tena sauti ya mwandishi anayeandika kuhusu nchi ya karibu na nyumbani Tanzania.

Kitabu kingine nilichonunua, Bluest Eye/Sula/Song of Solomon nacho kimejumlisha vitabu vitatu vya Toni Morrison. Ninahisi ninavyo vitabu hivi, ila sina hakika, kwani nina vitabu vingi sana. Toni Morrison ni mwandishi mmojawapo maarufu kabisa duniani. Alipata tuzo ya Nobel. Nina kitabu chake Playing in the Dark, ambacho kina fikra pevu kuhusu athari za utamaduni na fasihi ya wa-Marekani Weusi katika historia ya fasihi ya Marekani.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Great Expectations, cha Charles Dickens. Ninacho kitabu hiki, pamoja na vingine vya mwandishi huyu maarufu. Lakini hii haikunizuia kununua nakala nyingine. Labda, huko mbele ya safari, nitaweza kukijumlisha katika vitabu ambavyo nimekuwa nikitoa kwa vyuo, taasisi, na watu binafsi Tanzania.

Thursday, May 14, 2015

Hadithi za Luis Bernardo Honwana wa Msumbiji

Leo nimeagiza mtandaoni kitabu cha hadithi za Luis Bernardo Honwana wa Msumbiji kiitwacho We Killed Mangy Dog and Other Stories. Kwa wiki kadhaa, nimemwazia sana mwandishi huyu, ambaye kitabu chake hiki nilikipenda sana nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973. Nilivutiwa na jinsi alivyoielezea maisha nchini Msumbiji, ambayo ilikuwa daima mawazoni mwetu kutokana na vita vya ukombozi vilivyoongozwa na FRELIMO.

Nimeamua kununua kitabu hiki wakati huu kwa sababu katika wiki hizi nimeandaa orodha ya vitabu vya kufundishia kozi yangu ya "Post-colonial Literature" muhula wa kiangazi, mwezi Julai na Agosti. Kwa mara ya kwanza tangu nianze kufundisha hapa Chuoni St. Olaf, nimeamua kuingiza kazi ya fasihi kutoka Msumbiji.

Sitafundisha We Killed Mangy Dog and Other Stories, ingawa ningeweza kufanya hivyo kwa furaha kabisa. Badala yake, nitafundisha riwaya ya mwandishi mwingine maarufu Mia Couto iitwayo The Tuner of Silences, ambayo sijaisoma. Hata hivyo nimeona nijipatie hiki kitabu cha hadithi za Honwana, nilichokipenda enzi za ujana wangu, nikisoma tena wakati nangojea kufundisha The Tuner of Silences,

Ninangojea kwa hamu kusoma na kufundisha The Tuner of Silences. Ninangojea kwa hamu  kujikumbusha na kuwaeleza wanafunzi kuhusu Msumbiji, historia yake, historia ya utamadini na fasihi yake. Ninapangia kuandika zaidi kuhusu hayo katika blogu hii wakati utakapowadia.

Tuesday, May 12, 2015

Vitabu vya Shaaban Robert

Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanzania wepi ambao wamesoma angalau vitabu vichache vya Shaaban Robert. Ni wangapi wamesoma au wanasoma mashairi yake, tenzi zake, insha zake, barua zake, na riwaya zake?

Ni wangapi wamesoma vitabu vyake vingine, kama vile Wasifu wa Siti Binti Saad, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, na tafsiri yake ya mashairi ya Omar Khayyam? Kama hatuna majibu ya kuridhisha, tuache kujigamba, kujidanganya na kudanganyana kuwa tunamwenzi mwandishi wetu huyu maarufu.

Ingawa kulikuwa na kipindi cha uhaba, leo vitabu vya Shaaban Robert vinapatikana kirahisi Tanzania, baada ya kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota kuanza kuvichapisha upya. Mwaka hadi mwaka, ninapokwenda Tanzania, nimekuwa nikijinunulia vitabu hivyo, kama hivi vinavyoonekana pichani, sambamba na vitabu vya waandishi wengine maarufu katika lugha ya ki-Swahili.

Imekuwa ni faraja kwangu kuvisoma, baada ya kuzinduka kutoka katika mazoea ya kusoma zaidi maandishi ya ki-Ingereza. Ninajiona kama vile nimeanza kujikomboa kimawazo. Lugha yako ni utambulisho wako, na kuifahamu na kuitumia vizuri ni ishara ya kuiheshimu lugha hiyo. Ni ishara ya kujiheshimu.

Pamoja na kununua na kusoma vitabu alivyoandika Shaaban Robert, ninajitahidi kupanua akili yangu kwa namna nyngine pia. Ninayo maandishi yanayochambua maandishi ya Shaaban Robert. Mfano ni vitabu vinavyoonekana hapa pichani, kimoja cha A.G. Gibbe, na kingine cha Clement Ndulute. Maandishi mengine yamo katika majarida na vitabu vingine ambavyo baadhi ninavyo pia.

Ninajitahidi, kwa uwezo wangu, kushiriki katika kuandika kuhusu kazi za Shaaban Robert. Nimechapisha insha juu ya Shaaban Robert katika Encyclopaedia of African Literature iliyohaririwa na Simon Gikandi. Katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kuna pia insha yangu iitwayo "Shaaban Robert: Mwalimu wa Jamii." Kadiri nitakavyokuwa naendelea kusoma maandishi yake, nategemea kuandika zaidi. Nina nafasi nzuri ya kufanya hivyo kwa kuwa ni mwalimu wa fasihi za kimataifa na nadharia ya fasihi.

Saturday, May 9, 2015

Neno Jingine Kuhusu Uandishi na Uchapishaji

Mimi ni mwandishi wa vitabu. Ninaandika vitabu vya tahakiki ya fasihi, juu ya masuala ya jamii, fasihi simulizi, na masuala ya athari za tofauti za tamaduni, hali halisi ya uandishi wa vitabu, mbinu za kujichapishia vitabu. Naandika kuhusu utangazaji na uuzaji wa vitabu, na kuhusu hali halisi ya usomaji wa vitabu Tanzania na ughaibuni.

Ninatoa ushauri kwa wengine kupitia blogu hii na katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Yeyote anayetaka kujifunza kutoka kwangu anaweza kufanya hivyo, bila kipingamizi. Lakini namtegemea aanze kwa kusoma nilichoandika, mawasiano ya ziada yafuate baadaye.

Siwezi kuwasiliana na kila mtu na kuongelea hata yale ambayo tayari nimeshaandika. Nina kazi yangu na majukumu mengine kila siku. Nikisema niwasiliane na kila mtu hata kwa yale ambayo nimeshaandika, nitashindwa kufanya kazi zangu zinazoniwezesha kuishi, kulipia nyumba, matibabu, na mahitaji mengine.

Labda niache kazi niliyoajiriwa kufanya, nijiajiri kama mshauri. Ikiwa hivyo, kila anayetafuta ushauri kwangu atatakiwa alipie. Ndivyo wanavyofanya watoa ushauri. Nami ujuzi na uzoefu ninao, kama inavyodhihirika katika taarifa ninazoandika katika blogu hii ya hapakwetu na blogu ya ki-Ingereza.

Suali ambalo ninaulizwa tena na tena ni kuhusu mikakati ya kuchapisha miswada. Ni wazi kuwa watu bado wana fikra za jadi kuhusu uchapishaji. Nawashauri waondokane na fikra za kuwateemea wachapishaji. Badala yake, waingie katika ulimwengu wa kujichapishia vitabu.

Wafanyeje au waanzie wapi ndio aima ya masuala ninayoongelea katika blogu na katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Kama mtu anataka mafanikio, ni lazima awekeze katika elimu inayohusiana na shughuli anayotaka kufanya. Kununua vitabu na kuvisoma ni uwekezaji, sawa na uwekezaji wa kununua trekta ya kilimo au nyavu za kuvulia samaki.

 Suala la kujichapishia vitabu ni tata, hasa kwa upande wa wanataaluma. Jadi iliyopo katika kuchapisha vitabu vya kitaaluma au makala za kitaaluma imekuwa ya kuzingatia umuhimu wa wanataaluma tofauti na mwandishi kufanya uhakiki na udhibiti wa andiko kabla ya kuchapishwa. Ninapangia kuandika zaidi kuhusu suala hilo.  

Friday, May 8, 2015

Vitabu vya Moyez Vassanji

Siku chache zilizopita niliandika taarifa kuhusu vitabu nilivyonunua hivi karibuni. Kati ya vitabu kilikuwepo kimoja cha Moyez Vassanji, The Gunny Sack. Wakati huo, nilikuwa navingojea vitabu vingine viwili vya Moyez Vassanji, ambavyo nilikuwa nimeshavilipia. Vimefika.

Kimoja ni Uhuru Street, mkusanyo wa hadithi za kubuniwa,ambazo zinatokea katika mtaa wa Uhuru, mjini Dar es Salaam. Nasikitika kuwa kitabu hiki sijakisoma ingawa nimetamani kukisoma kwa miaka mingi. Kutokana na taarifa, nilijua kuwa kwa yeyote anayeijua Dar es Salaam, hiki ni kitabu kinachogusa hisia. Nimeanza kukisoma na ninajionea mwenyewe ukweli huo.

Kitabu cha pili ambacho kimewasili ni The Book of Secrets, ambacho, kama nilivyosema, niliwahi kukifundisha katika semina ya walimu katika Chuo cha Colorado. Mtu akisoma kitabu hiki, naamini atapata hamu ya kusoma vitabu vingine vya Moyez Vassanji.

Kitabu cha tatu ambacho kimewasili ni The In-Between World of Vikram Lall. Sijaanza kukisoma, ila nimekuwa nikisoma habari zake.

Kitabu kingine nilichokitaja siku chache zilizopita ni Amriika, ambacho nilikinunua zamani kidogo, ila sijakisoma. Moyez Vassanji ameshaandika vitabu karibu kumi hadi sasa. Ambavyo sijavitaja ni The Assasin's Song, No New Land, The Magic of Saida, A Place Within, na  And Home Was Kariakoo. Orodha haiishii hapo, na kuvisoma vyote itakuwa kazi kubwa. Kwa vyo vyote, baadhi nitavitumia katika kozi yangu ya Post-colonial Literature.

Moyez Vassanji ni mwandishi maarufu, nasi wa-Tanzania tuna haki ya kusema ni mtu wetu, kwani mnali ya kukulia Tanzania, amekuwa akiipeperusha vizuri sana bendera ya nchi yetu katika ulimwengu wa fasihi. Ninaamini tunawajibika kuwa naye bega kwa bega kwa kusoma vitabu vyake.

Ninakiri kuwa si jambo la kuridhisha kwamba vitabu vingi vilivyovitaja hapo juu ambavyo vilichapishwa miaka iliyopita, sikuvisoma na bado sijavisoma. Hiyo ni dosari. Ninapaswa kumfahamu mwandishi kama Moyez Vassanji kama ninavyowafahamu waandishi ninaowasoma katika ki-Ingereza kama Wole Soyinka, Nadine Gordimer, Derek Walcott, J.M. Coetzee, Anita Desai, Athol Fugard, Ngugi wa Thiong'o, Chinua Achebe, Sembene Ousmane, Salman Rushdie, na kadhalika.

Panapo majaliwa, nitaandika katika blogu hii juu ya Abdulrazak Gurnah na Tololwa Mollel, ambao ni waandishi wengine maarufu wa ki-Tanzania huku ughaibuni wanaoandika kwa ki-Ingereza. Tuwe nao bega kwa bega. Ni aibu kwetu kwamba waandishi hao wanasifika nchi za ng'ambo lakini si nyumbani Tanzania.

Going Visual: Kitabu Kuhusu Mawasiliano Kwa Taswira

Leo napenda kukiongelea kitabu kiitwacho Going Visual: Using Images to Enhance Productivity, Decision-Making and Profits, kilichoandikwa na Alexis Gerard na Bob Goldstein. Nilikinunua kitabu hiki miaka michache iliyopita. Kama ilivyo kawaid yangu ninaponunua kitabu, sikiweki katika maktaba yangu bila kukipitia angalau juu juu, ili nijue kinahusu nini.

Hivi ndivyo nilivyofanya niliponunua Going Visual. Niliona ni kitabu kinachoelezea maendeleo katika utumiaji wa taswira katika mawasiliano, kitabu kinachoelezea matokeo ya utafiti na uzoefu na mikakati ya matumizi ya taswira katika biashara na ujasiriamali. Kitabu kinaelezea jinsi tekinolojia ya kuzalisha, kuhifadhi, kuandaa, na kusambaza taswira, kuanzia za digitali hadi video, zinavyowezesha ufanisi katika biashara na ujasiriamali katika ulimwengu wa leo.

Wakati nilipokinunua kitabu hiki, nilikipitia juu juu, nikaelewa haya niliyoelezea. Lakini leo nimekitoa maktabani ili nikisome ipasavyo. Mada yake inanivutia, na ukweli kwamba sina ufahamu wa masuala yaliyomo umenipa shauku ya kufahamu.

Suala la mawasiliano tunalishughulikia katika usomaji na ufundishaji wa fasihi, kwani fasihi hutumia lugha, ambayo ni chombo mahsusi cha mawasiliano. Nadharia za lugha na fasihi zinatueleza mengi kuhusu mawasiliano. Mvuto wa kitabu cha Going Visual kwangu, na duku duku inayonisukuma kukisoma, ni hiyo mikakati na mbinu za kutumia taswira ambazo waandishi wa kitabu wanasema zinawanufaisha wafanya biashara na wajisiriamali wa leo.

Ninajiuliza: hizi mbinu ni zipi? Na hiyo mikakati ni ipi? Kwa hivi, ninaona ni muhimu nikisome kitabu hiki nielimike, ingawa siwezi kujiita mfanyabiashara au mjasiriamali. Elimu haina mwenyewe, haina mipaka, wala haina mwisho.

Wednesday, May 6, 2015

Leo Nimepata Bendera ya Tanzania

Leo nimepata bendera ya Tanzania. Niliwahi kuandika katika blogu hii kuwa mara kwa mara ninashiriki matamasha hapa Marekani ambapo watu huja na bendera za nchi zao, nami nilijisikia vibaya kwa kutokuwa na bendera kubwa ya nchi yangu. Nilifanya uamuzi muafaka, nikaagiza, na leo nimeipata.

Mwaka jana, nilipoandika ujumbe wangu, nilikuwa napeleleza katika tovuti kadhaa zinazouza bendera. Lakini safari hii, kwa kubahatisha tu, nimeingia katika tovuti ya Amazon nikaona bendera ziko, tena kwa bei rahisi sana.




Nimejionea hapa Marekani jinsi wa-Kenya walivyo hodari kwa suala hilo, na hapa naleta picha niliyopiga katika tamasha la Afrifest, tarehe 2 Agosti, mwaka jana, mjini Brooklyn Park, Minnesota. Inamwonyesha m-Kenya akitamba na bendera ya nchi yake.

Jiulize mwenyewe, ungejisikiaje kuwepo mahali ambapo wenzako wanatamba na bendera za nchi zao, nawe huna. Kwa nini ukae mahali hivyo, kama vile huna nchi? Hisia hizi ni kubwa unapokuwa ughaibuni. Sikutaka kuendelea kudhalilika namna hiyo.



Picha nyingine, inayoonekana hapa kushoto, nilipiga tarehe 11 Aprili, 2015, mjini Rochester, Minnesota, kwenye tamasha la tamaduni za ulimwengu. Inaonyesha meza ya wa-Kenya na bendera yao.

Kuna matamasha yanayokuja ambayo nitashiriki, kama vile tamasha la Afrifest, tarehe 1 Agosti, 2015. Nitakapokuwa naandika taarifa za matamasha hayo na maonesho, wadau mtajionea wenyewe bendera ya Tanzania ikipepea kwenye eneo la meza ya vitabu vyangu.

Monday, May 4, 2015

Kuiheshimu Misahafu ya Dini Zote

Pichani hapa kushoto ninaonekana nimeshika nakala yangu ya Bhagavad Gita, msahafu wa dini ya Hindu. Ingawa mimi ni m-Kristu (m-Katoliki), ninaamini kwa dhati kuwa ni wajibu kuiheshimu misahafu ya dini zote.

Kwa mfano, ninayo Qur'an. Siku moja nilimwuliza kijana mmoja mu-Islam kuhusu heshima itakiwayo kwa Qur'an. Kuna baadhi ya mambo niliyajua, lakini kijana aliniambia jambo la ziada. Alisema kwamba pasiwekwe chchote juu ya Qur'an.

Basi, daima ninakumbuka na ninazingatia hilo. Ingawa ofisi yangu imefurika vitabu, na  mezani pangu panakuwa pamefurika vitabu, na Qur'an yangu iko hapa hapa mezani muda wote, siwezi kuweka kitabu, karatasi, au kitu chochote juu yake. Nafanya hivi kwa kufuata dhamiri yangu, si kwa kuogopa labda atafika mtu ofisini akute hali nyingine.

Ninaamini kuwa kama dini yoyote inajinadi kuwa ni dini ya amani, ni lazima idhihirishe jambo hilo kwa kuziheshimu dini zingine. Ni lazima iwaheshimu waumini wa dini zingine, na misahafu yao. Kufanya kinyume ni kuhatarisha amani. Amani inajumlisha pia amani ya akilini na moyoni.

Amani haijengwi kwa kuwadharau wengine. Haijengwi kwa kudharau imani za wengine. Inasikitisha kuona jinsi baadhi ya watu nchini Tanzania wanavyozibeza dini za wenzao, wanavyoibeza misahafu ya wenzao, katika malumbano ambayo hayajengi amani bali yanaweka misingi ya kuhujumu amani.

Wa-Kristu tunawajibika kufanya kila juhudi kufuata agizo la Yesu la kumpenda Mungu kwa uwezo wetu wote, akili yetu yote, roho yetu yote, na kwa moyo wetu wote. Tunawajibika pia kumpenda jirani kama tunavyojipenda wenyewe. Katika mafundisho yake, inadhihirika pia kuwa Yesu alituasa kuwapenda hata maadui zetu. Wa-Kristu tunakatazwa kulipiza kisasi.

Kwa kuwa fundisho la msingi la u-Kristu ni hilo, ambalo linathibitisha kuwa ni dini ya amani, kwa nini nisifanye juhudi ya kuwaelewa wanadamu, kuzielewa tamaduni zao, na kuzielewa dini zao? Mtu asishangae akinikuta ninasoma Bhagavad Gita, Qur'an, au msahafu mwingine, sambamba na Biblia yangu. 

Sunday, May 3, 2015

Vitabu Nilivyonunua Karibuni

Napenda kuendelea na jadi yangu ya kuvitaja vitabu nilivyoongeza katika maktaba yangu katika siku chache zilizopita.

Kitabu kimoja ni The Poetic Edda: Stories of the Norse Gods and Heroes, kilichotafsiriwa na Jackson Crowford. The Poetic Edda ni kitabu maarufu sana ambacho nimekisikia kwa miaka mingi. Ni mkusanyo wa hadithi na mashairi ya mapokeo juu ya miungu na mashujaa wa Iceland.

Nimeamua kujipatia nakala wakati huu ambapo nimekuwa nafundisha utungo maarufu wa Finland uitwao Kalevala. Kwa pembeni nimekuwa nayapitia pia mashairi ya mapokeo ya Finland yaliyokusanya na Elias Lonnrot katika kitabu kiitwacho Kanteletar. Nina hamu ya kuona kama The Poetic Edda inahusiana na hizo tungo zingine, kwa kuzingatia kuwa zote ni za Ulaya ya kaskazini.

Kitabu kingine nilichonunua ni The Village by the Sea, cha Anita Desai wa India. Nilipangia kukifundisha muhula huu katika kozi yangu ya Post-colonial Literature, lakini tumeishiwa muda. Nimeshafundisha riwaya kadhaa za Anita Desai. Ni mwandishi bora sana. Ndio maana nikaamua kukiweka kitabu chake cha The Village by the Sea katika orodha ya muhula huu.

Kitabu kingine nilichonunua ni Monkfish Moon. Ni mkusanyo wa hadithi fupi za Romesh Gunesekera wa Sri Lanka, ambaye riwaya yake ya Reef nimeifundisha. Gunesekera ni mwandishi hodari sana. Nilikijumlisha kitabu chake cha Monkfish Moon katika orodha yangu ya Post colonial Literature. Lakini, muda umeshindikana.

Kitabu kingine nilichonunua, yapata wiki moja iliyopita, ni See Now Then cha Jamaica Kincaid wa Antigua, Carribean. Niliwahi kuhudhuria mhadhara wake katika Chuo Kikuu cha Minnesota.

Kitabu kingine nilichonunua, ambacho nimekipata leo, ni The Gunny Sack, cha Moyez Vassanji. Moyez Vassanji alizaliwa Kenya lakini alikulia Dar es Salaam. Ni mwandishi maarufu ambaye anaishi Canada. Kati ya vitabu vyake vinavyovuma sana ni Uhuru Street na The Book of Secrets., ambacho niliwahi kukifundisha katika semina ya waalimu Chuo cha Colorado. Kinavutia sana kwa ustadi uliotumika katika kukiandika. Kitabu chake kingine, Amriika, nilikinunua miezi mingi iliyopita ila sijakisoma bado.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...