Friday, May 29, 2015

Toleo Jipya la "Green Hills of Africa" Linaandaliwa

Nilimpigia simu Mzee Patrick Hemingway tarehe 22 mwezi huu, tukaongea kwa saa moja na robo. Tuliongelea mambo mengi, kama nilivyogusia katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Mzee Patrick Hemingway ni mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway.

Mwandishi huyu ni wa pekee, sio tu kwa kuwa alishinda tuzo ya Nobel, bali pia kwa kuwa mtindo wake wa kuandika ulichangia kubadilisha uandishi wa ki-Ingereza wa karne iliyopita. Katika mfumo wa elimu wa Tanzania wa miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu, wanafunzi tulikuwa tunasoma angalau kitabu kimoja cha Ernest Hemingway, For Whom the Bell Tolls, sambamba na vitabu vingine maarufu vya waandishi mbali mbali.

Katika mazungumzo yetu, Mzee Patrick Hemingway aliniarifu kuwa toleo jipya la kitabu cha Green Hills of Africa litachapishwa miezi ya karibuni. Nilifurahi kusikia habari hii. Green Hills of Africa ni masimulizi ya Ernest Hemingway juu ya safari aliyofanya nchini Tanganyika, mwaka 1933-34. Nilisisimka Mzee Hemingway aliposema kuwa katika toleo hili kutakuwemo "diary" ya mama yake, Pauline, aliyoandika wakati wa safari hiyo.

Nilifahamu kuhusu kuwepo kwa hiyo "diary," na nilifahamu kuwa imehifadhiwa katika chuo kikuu cha Stanford. Kwa miaka kadhaa nilikuwa nikiwazia kwenda kuisoma. Kwa hivi, hii habari kwamba itachapishwa imenifurahisha kwa namna ambayo siwezi kuieleza.

Habari ya kuchapishwa toleo jipya la Green Hills of Africa ni muhimu sana. Tanzania ingeweza kuitumia hii kama fursa adimu ya kujitangaza kwa ajili ya utalii.  Lakini kutokana na kukosekana kwa utamadini wa kusoma vitabu, sitegemei jambo hilo litafanyika. Tofauti na zamani, Tanzania ya leo haimjui Hemingway.

Wenzetu katika nchi zingine wamechangamkia fursa za namna hii na wanafaidika. Mfano moja ni mji uitwao Pamplona, nchini Hispania. Mji ule tangu zamani una jadi yake ya mchezo wa "bull fighting" ambao unamshindanisha shujaa na fahali uwanjani. Ernest Hemingway alitembelea Pamplona mwaka 1923 akavutiwa na mchezo huo. Aliandika kitabu The Sun Also Rises, ambacho kilielezea "bull fighting" na kuufanya mji ule uwe maarufu sana, unaovutia maelfu ya watalii, ingawa haukuwa na umaarufu huo kabla. Sehemu zingine ambamo Hemingway aliishi au alipita na kuandika habari zake, kama vile Oak Park (Illinois), Michigan Kaskazini, Paris, Key West (Florida), Bimini, na Cuba, zinavuna faida kutokana na utalii. Nimewahi kuelezea hayo katika blogu hii.

Nina hakika kuwa mimi ni m-Tanzania wa kwanza kuifahamu habari ya toleo jipya la Green Hills of Africa, na nimeona niiweke hapa katika blogu yangu, nikijua kuwa kuna wa-Tanzania watakaoisoma. Laiti nchi yetu ingekuwa imeamka, ingeanza kujiandaa kuchuma faida za toleo jipya la kitabu hiki kwa kuitangaza Tanzania na sehemu zote alizopitia Hemingway nchini mwetu. Ingekuwa jamii yetu inathamini vitabu, ingeandaa matangazo na makaribisho ya toleo hili jipya. Hii ingekuwa pia fursa ya kuhamasisha utalii wa ndani. Lakini, sina imani yoyote kuwa haya yatafanyika. Ninaifahamu nchi yangu: ni kwenye miti ambako hakuna wajenzi.

No comments: