Wednesday, November 30, 2011

Makafiri

Ingawa watu wengi wanaamini kuwa masuala ya dini ni hatari kujadiliwa, blogu yangu haina kipingamizi kwenye kujadili masuala hayo, kama ilivyo kwa masuala mengine. Kama kuna tatizo, tatizo haliko kwenye mada, bali tatizo ni wahusika, kama nilivyoandika hapa.

Leo napenda kuongelea suala ambalo limenikera kwa muda mrefu. Ni suala la watu kuwaita wengine makafiri. Nimeshasoma taarifa kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania ambazo zimenifanya niandike ujumbe huu.

Leo katika mtandao wa Facebook, nimeona taarifa kutoka Mbeya ambamo mtu analalamika kuwa kuna makafiri sana kule. Miezi kadhaa iliyopita, nilisoma taarifa kutoka Zanzibar, kwamba watu wa kijiji fulani walikuwa hawataki makafiri kwenye eneo lao. Ukipita mtandaoni, utaona kuwa jadi hii ya kuwaita wengine makafiri inajitokeza mara kwa mara miongoni mwa watu wa Visiwani.

Sijui hao wanaowaita wengine makafiri walipata wapi uwezo wa kufahamu undani wa watu wengine kiasi hicho. Nilidhani kuwa sote tunaosema tunamwamini Mungu tunafahamu kuwa mwenye uwezo wa kumhukumu binadamu, uwezo wa kujua yupi ni kafiri na yupi si kafiri, ni Mungu tu.

Hatujui ya Mungu, na bora tuwe wanyenyekevu. Hao wanaowaita wenzao makafiri huenda Mungu anawajua kuwa ndio makafiri wenyewe. Binafsi siwezi kumtambua kafiri, kwa sababu sina njia ya kuona yaliyomo moyoni au akilini mwa yeyote. Sithubutu kumwita yeyote kafiri, kwani nitaona kuwa kufanya hivyo ni kufuru, yaani kujifanya mimi ni Mungu.

Sunday, November 27, 2011

Taarifa ya Ikulu Kuhusu Mkutano wa JK na CHADEMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wa Serikali yake leo, Jumapili, Novemba 27, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, yamefanyika katika mazingira ya urafiki na ujumbe wa CHADEMA umewasilisha mapendekezo yake kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania. Serikali imepokea mapendekezo hayo.

Hata hivyo, pande zote mbili zimekubaliana kukutana tena asubuhi ya kesho, Jumatatu, Novemba 28, 2011, ili kuipa nafasi Serikali iweze kutafakari mapendekezo hayo.

Lakini pande hizo mbili zimekubaliana kuwa Katiba ya sasa ni Katiba nzuri iliyolilea Taifa kwa miaka 50 iliyopita kwa sababu ni Katiba ya sasa iliyoliwezesha Taifa la Tanzania kuwa na amani, utulivu na kupata maendeleo makubwa ambayo nchi yetu imepata mpaka sasa.

Pia pande zote mbili zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kutunga Katibu Mpya kama Mheshimiwa Rais Kikwete alivyoliahidi taifa wakati wa salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, mwaka jana, 2010, Katiba ambayo italiongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine 50 ijayo.

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais aliwahakikishia wajumbe hao wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mheshimiwa Freeman Mbowe kuwa ni dhamira yake na ya Serikali yake kuhakikisha kuwa Tanzania inapata Katiba mpya.

Katika mkutano huo, pande zote mbili zimekubaliana kuwa ni jambo muhimu sana kwa mchakato mzima wa kutungwa kwa Katiba Mpya kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Aidha, pande zote mbili zimekubaliana kuwa mchakato huo uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya mambo mengine muhimu kwa taifa la Tanzania kama vile kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, kuligawa Taifa kwa misingi ya udini na ukabila ama kutugawa kwa misingi ya maeneo.

IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

NOVEMBA 27, 2011

Friday, November 25, 2011

Mahojiano na Profesa Joseph Mbele

Nimefanya mahojiano mara nyingi na watu mbali mbali, wakiwemo wa-Tanzania, kuhusu shughuli zangu katika jamii, kama vile maandishi na mihadhara. Hapa naleta mahojiano yaliyofanyika Septemba 2006, ili wale ambao hawajawahi kusikia sauti yangu au namna yangu ya kujieleza katika mazungumzo ya papo kwa papo, wapate fursa hiyo.

(Chanzo: Butiama.podomatic)Tuesday, November 22, 2011

Nimekutana na Wadau wa New Hampshire

Leo nimebahatika kukutana na wadau wawili, mtu na mkewe, kutoka New Hampshire, ambako ni waumini wa Kanisa la Holy Trinity. Wamekuja hapa Minnesota kwa masuala ya shirika la Bega kwa Bega, ambalo linashughulikia ushirikiano na maendeleo katika mkoa wa Iringa.

Wadau hao, Mama Dot na Mzee Kurt, wanajiandaa kwenda Iringa, ambako wameshaenda mara kadhaa. Katika ujumbe wao wa mwanzo kwangu, walisema kuwa Profesa Joe Lugalla, ambaye wako wote New Hampshire, aliwahamasisha tukutane. Profesa Lugalla, kama mimi, anawasaidia wa-Marekani wanaokwenda Tanzania kwa kuwapa ushauri unaohitajika. Kwa msingi huo, amekuwa mdau mkubwa wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences" na amekipigia debe kwa watu hao tangu kilipokuwa mswada tu, mkusanyiko wa dondoo mbali mbali, usio na sura ya kitabu.

Wadau hao wawili nami tumeongea kwa karibu saa mbili. Maongezi yetu yalihusu shughuli wanazofanya Iringa katika mpango wa Bega kwa Bega, na hasa maandalizi wanayofanya ya kupeleka kikundi cha wa-Marekani Iringa katikati ya mwaka ujao. Mama Dot amewahi kufundisha Chuo Kikuu Cha Tumaini, na tuliongelea pia habari za chuo kile, ambacho nami nimekifahamu tangu mwanzo na ninafahamiana na baadhi ya viongozi na walimu wake. Tuliongelea sana tofauti za tamaduni baina ya wa-Marekani na wa-Afrika, kama nilivyozieleza katika kitabu changu, ambacho wamekisoma vizuri. Walikuja na nakala yao, na wakaniomba niisaini. Nami nilifanya hivyo.

Tumefurahi kukutana, na tumekumbushana kuhusu watu kadhaa wa Tanzania na Marekani ambao sote tunawafahamu, kuanzia walioko Chuo Kikuu cha Tumaini hadi walioko New Hampshire. Ni kweli, milima haikutani bali wanadamu hukutana.

Monday, November 21, 2011

Wizard of the Crow: Riwaya ya Ngugi wa Thiong'o

Siku hizi, katika darasa langu mojawapo, tunasoma Wizard of the Crow, riwaya ya Ngugi wa Thiong'o. Kama kawaida yake miaka hii, Ngugi huandika riwaya zake kwanza katika lugha ya Kikuyu. Ndivyo alivyofanya kwa riwaya hii, kisha akaitafsiri kama Wizard of the Crow.

Hatujamaliza kuisoma, bali tunakaribia katikati. Ni moja kati ya riwaya ndefu kabisa zilizowahi kuandikwa na wa-Afrika. Kwa kigezo hiki, riwaya hii inanikumbusha ile riwaya maarufu ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali iliyoandikwa na Aniceti Kitereza.

Katika riwaya hii, Ngugi si yule Ngugi ambaye tumezoea kumsoma kwa miaka yapata thelathini sasa, ambaye vitabu vyake katika kipindi hiki, tofauti kiasi fulani na miaka ya mwanzo, vimebeba hisia za kupambana na uonevu, unyonyaji, na ukoloni mamboleo bila mzaha. Kwa miaka mingi, Ngugi ameonekana kama mwandishi mwenye hasira, na wasomaji na wahakiki wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hasira hizi zimedhoofisha sanaa katika uandishi wake.

Lakini Wizard of the Crow inavutia kwa kigezo cha sanaa. Ngugi amejidhihirisha kuwa msimuliaji wa hadithi mwenye uwezo wa kutumia kejeli na mizaha. Kwa upande wa dhamira, anaelezea hali halisi ya utawala na siasa inayoonekana sehemu nyingi za Afrika ya leo, ambamo wale tunaowaita viongozi ni mafisadi waliobobea katika majungu na ushirikina na uvunjaji wa haki za binadamu. Ingawa hali anayoelezea si ya kufurahisha, Ngugi anafanikiwa kuwaanika hao watu kwa mbinu mbali mbali za kisanii, kama nilivyogusia. Mtu unaposoma Wizard of the Crow, huwezi kujizuia kuwakumbuka madikteta kama vile Mobutu, Bokasa na Banda.

Ngugi wa Thiong'o amejipambanua kama mwandishi bora tangu zamani. Baadhi yetu tunaamini kuwa riwaya yake ya A Grain of Wheat ndio ilitia fora katika kazi zake zote, na wengine wanaihusisha pia Petals of Blood. Lakini naamini wasomaji na wahakiki sasa watakubali kuwa Wizard of the Crow ni bora kuliko zote ambazo Ngugi amewahi kuandika.

Saturday, November 19, 2011

Wabunge wa CCM Wanakera

Leo unatimia mwaka mmoja tangu nichapishe makala hii hapa chini. Kitu kimoja kilichonifanya niitafute na kuileta tena ni mjadala wa siku chache zilizopita katika Bunge la Tanzania kuhusu suala la Katiba. Niliwaona wabunge wakimjadili mtoa hoja, Mheshimiwa Tundu Lisu, au wakiongelea masuala ya kifamilia ya viongozi wa CHADEMA, badala ya kujadili hoja. Inakera. Na mimi ninayesema hivi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa.
-------------------------------------------------------

Chanzo: Hapakwetu

Wabunge wa CCM wanakera.

Tukianzia na wabunge hao walioapishwa safari hii, sitasahau kuwa hao ndio waheshimiwa waliotoroka midahalo wakati wa kampeni. Wote walitoroka midahalo, kitendo ambacho kimenikera. Mimi kama mwalimu, ninayetambua umuhimu wa midahalo, ninawashutumu hao waheshimiwa. Soma hapa.

Kila nitakapokuwa naona sura za hao waheshimiwa wa CCM, nitakuwa nakumbuka kitendo chao hiki cha kutoroka midahalo. Nitakuwa naangalia kama watajirekebisha au kama kitendo kile ni ishara ya tabia na mwenendo watakaofuata kwa miaka mitano ijayo.

Tukirudi nyuma, kwenye awamu iliyopita, wabunge wa CCM walikera. Ni nani atakayesahau yaliyotokea wakati Dr. Slaa alipoanza kutamka kuwa kuna ufisadi katika nchi yetu? Wabunge wote wa CCM walimpinga vikali na kumtupia shutuma nzito kwamba alikuwa mzushi.

Dr. Slaa hakuyumba, bali aliendelea kutoa madai yake. Hatimaye, ilianza kuthibitika kuwa aliyokuwa anayasema ni kweli, kwamba tuna mafisadi. Baada ya wananchi kuanza kuona ukweli huo, ukawa haupingiki tena, tuliwaona baadhi ya wabunge wa CCM wakijitokeza na kuanza kujinadi kuwa nao ni wapiganaji dhidi ya ufisadi. Sijui kama walikuwa wanaongea kwa dhati au kwa lengo jingine.

Tukirudi nyuma zaidi, tunakumbuka suala la machafuko yaliyotokea Visiwani mwaka 2001. Machafuko yale, yaliyotokana na CCM, chama tawala, kushindwa kutumia haki na busara, yaliiletea Tanzania aibu kubwa duniani. Kwa uthibitisho, soma hapa.

Lakini, pamoja na maovu yote yaliyofanyika Visiwani, pamoja na fedheha yote iliyoiangukia Tanzania, wabunge wa CCM hawakukubali kuwa serikali ya CCM ilikuwa na makosa, wala hawakukubali kuwa Tanzania ilikuwa inafedheheka. Wao waliitetea serikali ya CCM. Maadam palikuwa na suala lililohusu chama cha upinzani, yaani CUF, wabunge wa CCM waliamua kuikingia kifua serikali ya CCM, badala ya kusimamia haki za binadamu na heshima ya Tanzania.

Je, kuna kero kubwa zaidi ya hii ya kutojali maslahi ya Taifa na badala yake kuangalia maslahi ya kikundi fulani?

Mjengwablog Iliibua Kashfa ya Pan African Energy Mapema

Chanzo: Mjengwablog

Ndugu zangu,
Nafurahi kuwajulisha, kuwa Mjengwablog. com ndio iliyoibua kwa mara ya kwanza kashfa ya mradi wa gesi unaouhusisha kampuni ya Kisweden ya Pan African Energy , Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini.

Habari kuhusu kashfa hiyo ziliripotiwa kwa mara ya kwanza hapa nchini na blogu hii Ijumaa ya Julai 15, 2011. Ni siku tatu kabla ya Waziri Ngeleja kuwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati Na Madini. Bila shaka yeyote, habari hiyo ilichangia kwenye kuongeza nguvu ya mjadala bungeni. Hapa chini ni habari husika niliyoiposti hapa globuni na kwenye mitandao mingine kama vile Global Publishers, Jamii Forums na Wanabidii. Pichani juu Waziri Ngeleja akipongezwa na wabunge wenzake wa CCM baada ya bajeti ya wizara yake kupitishwa. Ilikwamishwa ilipowasilishwa kwa mara ya kwanza.


Mheshimiwa Ngeleja, Sweden Kuna Kashfa Ya Nishati Yetu
Ndugu zangu,

Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa William Ngeleja leo anawasilisha bajeti ya wizara yake huku kashfa ya nishati yetu ikiwa ni moja ya ajenda ya shirika la Misaada la Kimataifa la Action Aid lenye tawi lake nchini Sweden.

Shirika hili linaishinikiza Serikali ya Sweden kuacha kufadhili kwa kuyapa mitaji ya kuwekeza makampuni yenye kukwepa kodi kama ilivyo kwa kampuni ya Pan African Energy.

Kampuni hii Pan African Energy iliyosajiliwa kwenye visiwa viwili; Mauritius na Jersey inavuna gesi ya Songosongo huku ikiwa imeingia mkataba wa miaka 25 na TANESCO kupitia Shirika la Nishati ina Madini la Taifa TPDC. Ni mkataba wenye kuifanya kampuni hiyo kutokulipa kodi ya faida ya mapato wanayopata kutokana na mauzo ya umeme unaotokana na gesi asilia wanayovuna Songo Songo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid iliyotolewa mwezi Mei mwaka huu, tangu Pan African Energy waanze kuvuna gesi asilia kule Songo Songo mwaka 2004, kampuni hiyo imevuna faida ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 60. Nusu ya faida hiyo ilipatikana mwaka 2009 na kampuni hiyo ilitarajiwa kuongeza uzalishaji. Hivyo, kuvuna zaidi gesi yetu asilia ya Songosongo.

Mpaka kufikia sasa, Pan African Energy imefanikiwa kukwepa kodi inayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 40. Hiki ni kiasi cha fedha kinachotosha kusomesha watoto wa Kitanzania 175,000 ( Laki moja na sabin ina tano elfu) kwa mwaka kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid.

Kwa kifupi tu, ripoti hii inadhihirisha namna ufisadi unavyochangia kutuacha Watanzania tukiwa katika hali ya giza linalotokana na mgawo wa umeme. Tukiwa katika hali ya uzalishaji duni kutokana na uhaba wa nishati ya umeme. Ufisadi umetuletea giza na umasikini.

Kampuni hii ya Pan African Energy inanufaika na ’mkataba wa kifisadi’ usiotanguliza maslahi ya taifa.
Ni wakati sasa wa Waheshimimiwa wabunge wetu ’ kumweka kikaangoni’ Waziri wa Nishati na Madini Mh. William Ngeleja ili atoe maelezo ya kina juu ya kashfa hii ya Pan African Energy. Na atwambie, ni hatua gani zitachukuliwa na lini kwa wote waliochangia kutufikisha kwenye kashfa hii. Hivyo basi, waliochangia kutufikisha katika giza hili tunalolishuhudia sasa kwa kukosa nishati hii muhimu kwa maana ya umeme.

Kama Mheshimiwa Waziri atashindwa kutoa majibu ya kuridhisha, basi, aombwe akae pembeni kupisha Watanzania wengine wenye uwezo wa kushika Wizara hiyo nyeti kwa taifa.

Nawasilisha.

Maggid
Knivsta, Sweden
Ijumaa, Julai 15, 2011
http://mjengwa.blogspot.com
( Unaweza kusoma ripoti ya Action Aid kwenye; http://www.actionaid.se)

Thursday, November 17, 2011

Nimekutana na Mdau Mjini Apple Valley

Leo nimekutana na mdau Dr. Mary Sheedy Kurcinka, mhadhiri na mwandishi maarufu wa masuala ya malezi ya watoto wachanga. Nilishamtaja siku chache zilizopita hapa. Tuliongea kwa saa moja na nusu mjini Apple Valley.

Mama huyu alishatembelea Nigeria na Ghana wakati wa ujana wake, akaandika kuhusu malezi ya watoto wachanga katika jamii ya wa-Yoruba. Sasa anapangia kwenda Tanzania, mwanzoni mwa mwaka ujao.

Mazungumzo yetu ya leo yalihusu suala hilo analofanyia utafiti. Aliponiandikia ujumbe wa kwanza, wiki kadhaa zilizopita, alisema alisikia habari zangu kutoka kwa muumini wa Shepherd of the Valley Lutheran Church.

Leo kaja na nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho alikinunua hivi karibuni. Amesema amekisoma na amekipenda sana. Kimemkumbusha aliyoyaona alipoishi Nigeria na Ghana. Kama ilivyo kawaida kwa wa-Marekani, aliniomba nisaini nakala yake, nami nikafanya hivyo.

Katika kuongea naye, nimepata motisha ya kufuatilia suala la malezi ya watoto wachanga, kwa kuzingatia saikolojia ya hao watoto wachanga, na changamoto zinazowakabili wazazi wao katika tamaduni mbali mbali. Leo tumejaribu kuongelea suala hilo tukizingatia tamaduni za wa-Marekani na wa-Afrika. Leo ulikuwa mwanzo, na tunategemea kuendelea kubadilishana mawazo.

Kwa vile sote wawili ni waandishi, tumepata fursa ya kuongelea masuala ya uandishi pia, kubadilishana uzoefu. Katika maongezi hayo, nilipata fursa ya kumweleza changamoto zilizonifanya nikaandika kitabu changu hiki, na pia nilivyojifunza kutokana na jinsi mwandishi Ernest Hemingway anavyofafanua dhana ya ukweli katika uandishi.

Wednesday, November 16, 2011

Mhadhara wa Jana Ulivyofanikiwa

Mhadhara wangu wa jana kwenye shule ya Mazingira, Apple Valley, ulifanikiwa sana. Ni umbali wa dakika 45 kutoka hapa ninapoishi. Niliongea kuanzia saa tatu hadi saa sita.


Leo Mwalimu Carlson ameniandikia ujumbe huu:

I have described the day to many of our faculty.... That was one of the best classroom sessions I have ever been a part of...the kids were buzzing for the rest of the day. Thank you so much
.

Nitafsiri kwa ki-Swahili:

Nimewaeleza walimu wetu wengi shughuli za leo.... Ni kati ya madarasa bora kabisa ambayo nimewahi kushiriki....vijana wamesisimka wakiongelea siku nzima. Asante sana.


Nahitimisha kwa kusema kuwa nilishagundua tangu zamani kuwa kuwaneemesha wengine kwa kuwafundisha ninayoyafahamu ni kitu kinachonipa raha mimi mwenyewe. Nafurahi kuwatajirisha vijana kitaaluma na kimtazamo. Mara kwa mara nafanya shughuli hizi kwa kujitolea, lakini sipungukiwi. Ninaamini ule usemi kuwa kadiri unavyotoa ndivyo unavyopewa.

Eti Tuupigie Mlima Kilimanjaro Kura, Kwa Lipi?

(Makala hii imechapishwa katika blogu ya kamalaluta)

eti tuupigie mlima kilimanjaro kura, kwa lipi?

sikuupigia kura mlima kilimanjaro na wala sikuwa na mpango wa kuupigia kura na nisingeweza kuupigia kura. ni kweli ungekuwa maajabu ya dunia tungepata pesa nyingi. lakini kwa nini kushiriki kuupigia kura mlima kilimanjaro??

Tanzania hupata pesa nyingi kutokana na utalii, ufadhili na vyanzo vingine.lakini pesa hizo huishia wapi?? tunazidi kukamuliwa kodi na kumasikinishwa. wakulima kama mimi tumekosa mitaji, huku rais wetu akionekana kila siku anawakaribisa matajiri kutoka nje ili wajekuchukua vijishamba vyetu kuwekeza eti.

mapato yoote hayo pamoja na utalii huishia wapi? hamna huduma za msingi za jamii, shule alizozijenga nyerere ndo bado zipo zinakaribia kuwaangukia wanafunzi.

pesa za kufisidi huwa hazikosi na mafisadi wako huru kuiba watakacho, anasa za watawala nazo hazikosagi pesa. wananunua magariya kitajiri, pinda eti anakataa gari la kitajiri kwa kuwa anaendesha gari la kitajiri then gari alilolikataa linapelekwa kwenye idara nyingine, kwa nini kuupigia kura mlima huu?

Tuesday, November 15, 2011

Mhadhara Katika Chuo cha Mazingira, Minnesota

Leo nilikwenda Apple Valley, kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Msomo ya Mazingira. Nilialikwa na mwalimu Todd Carlson, na wanafunzi wake hao wamekuwa wakishughulika na mada ya falsafa za jadi.

Kwa miaka mingi, mwalimu Carlson amekuwa akinialika kuongea na wanafunzi hao.

Katika kuwaandaa, Mwalimu Carlson anawapa sehemu kadhaa za kitabu cha Matengo Folktales wasome. Kutokana na maandalizi hayo, wanafunzi hao wanakuwa na duku duku na masuali mengi ya kuniuliza. Ni wanafunzi makini sana. Wanaulizia kuhusu utafiti wa fasihi simulizi na changamoto za uandishi masimulizi hayo, tafsiri, maana, falsafa na kadhalika, wakizingatia yale niliyoandika katika Matengo Folktales.

Kila ninapotembelea Chuo hiki, nawasimulia hadithi angalau moja kutoka katika Matengo Folktales. Leo niliwasimulia hadithi ya "Jitu Katika Shamba la Mpunga," ambayo ni chemsha bongo ya aina yake, tukatumia muda kuiongelea.

Saturday, November 12, 2011

Vitabu Nilivyonunua Leo Apple Valley

Jioni ya leo nilipita kwenye duka la Half Price Books, mjini Apple Valley. Nilikuwa natoka Minneapolis.

Nilipoingia ndani, niliwakuta watu wengi humo, wanazunguka huko na huko wakiangalia vitabu. Kwenye sehemu ya kulipia, kulikuwa na foleni. Hii ni jioni ya Jumamosi, wikiendi, na wa-Marekani wamejazana katika duka la vitabu. Je, jambo hili linawezekana nchini mwetu?

Baada ya kuangalia vitabu vingi, nilichagua viwili. Kimoja ni The Hottentot Venus kilichotungwa na Rachel Holmes, na kingine ni The Time and the Place and Other Stories kilichotungwa na Naguib Mahfouz.

Hottentot Venus, ni habari ambayo nimeifahamu kwa miaka mingi. Ni jina alilopewa Saartje Baartman, mama mw-Afrika kutoka Afrika Kusini ambaye alipelekwa Ulaya kama kivutio, hasa kwa vile alikuwa na makalio makubwa sana, kutokana na desturi za kwao za kukuza makalio. Huko Ulaya alinyanyasika sana, kwani walimweka kwenye uzio kama mnyama, akitembezwa kwenye miji mbali mbali kwa maonyesho, na kukutana na adha za kila aina. Alifariki mwaka 1815.

Ni habari ya kusikitisha sana. Maiti yake iliwekwa katika jumba la makumbusho kwa miaka mingi, na hata ubongo na sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa na kuwekwa kama kivutio cha aina yake. Hatimaye, serikali ya Mzee Mandela iliweka shinikizo kuwa masalia ya Saartje Baartman yarudishwe Afrika Kusini kwa mazishi sahihi. Mazishi hayo yalifanyika mwaka 2002.

Huo ni ufupi wa habari nilizozifahamu kwa miaka kadhaa. Lakini sasa nimenunua hiki kitabu, nitazifuatilia kwa undani zaidi.

Naguib Mahfouz ni kati ya waandishi maarufu waliopata kuishi. Alikuwa mtu wa Misri. Aliandika riwaya nyingi na hadithi fupi. Mwaka 1988 alipata tuzo ya Nobel kwa uandishi wake. Nimesoma na kufundisha baadhi ya vitabu vyake, kama vile Midaq Alley. Hiki kitabu nilichonunua leo ni kati ya vile ambavyo sikuwa navyo.

Mbeya Nchi, Raisi Sugu

Kabla ya yote, sherti niseme kuwa nasikitishwa na mambo yaliyotokea Mbeya siku mbili tatu hizi zilizopita na kusababisha uvunjifu wa amani. Natoa pole kwa waathirika. Kwa kuangalia habari zilizopatikana, tatizo limesababishwa na ukosefu wa busara za kiuongozi.

Kati ya taswira zilizotolewa kutokana na matukio haya ya Mbeya ni hili bango lisemalo Mbeya Nchi Raisi Sugu. Picha nimeipata kutoka blogu ya Francis Godwin. Bango hili naona lina ujumbe wa kufikirisha. Kwa upande mmoja, mtu anaweza kusema kuiita Mbeya nchi ni makosa na dharau kwa nchi ya Tanzania.

Lakini kwa upande mwingine, inakuwa vigumu kuthibitisha kosa liko wapi. Neno nchi limekuwa likitumika kwa namna nyingi katika maisha yetu. Miaka ya zamani na hadi leo, tunaposema u-Gogoni, au u-Sukumani, tunamaanisha nchi ya wa-Gogo na nchi ya wa-Sukuma. Hakuna ubaya wowote hapa. Katika hali hii, inakuwa vigumu kuwakosoa wenye hili bango lisemalo Mbeya Nchi.

Kuna wakati tulikuwa na nchi ya Tanganyika. Nchi hiyo ilipata Uhuru mwaka 1961 na mwaka 1964 ikatoweka. Pamoja na kuwa nchi ya Tanganyika haipo, mwaka huu kuna shughuli za kukumbuka uhuru wa nchi hiyo ambayo imetoweka.

Leo kuna nchi iitwayo Tanzania. Kesho na keshokutwa, watu wanaweza kuamua kuififisha nchi hiyo pia, kama walivyoififisha Tanganyika. Kwa mfano, wanaweza kuiunganisha hii Tanzania na nchi jirani, wakatunga nchi tofauti kabisa, na Tanzania ikafa kama ilivyokufa Tanganyika. Labda wenzetu wa Mbeya wanakazana kuhakikisha kuwa nchi yao haipotei kienyeji namna hiyo.

Kuhusu Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya, maarufu kama Sugu, jambo moja lililojitokeza ni jinsi anavyokubalika na wananchi, hususan walalahoi. Nimeguswa na jinsi alivyokuja Mbeya wakati wa vurugu, na wakati viongozi wa serikali na polisi wakiwa wameshindwa kuzidhibiti, akaweza kuwahutubia wananchi na kuwatuliza. Napata picha kuwa ana akili na busara ya kiuongozi. Niliwahi kushiriki mjadala kuhusu Sugu hapa. Picha nimeitoa kwenye blogu ya mbeyayetu.

Taarifa tulizozipata ni kuwa wananchi wa Mbeya walikuwa hawataki kumsikiliza kiongozi yeyote isipokuwa Sugu. Hapo ikabidi Sugu aondoke kwenye vikao vya Bunge Dodoma na kuwahi Mbeya. Umati aliohutubia unaonekana kwenye hizi picha, ambazo nimeziona kwenye blogu ya mbeyayetu.

Friday, November 11, 2011

Nitakutana na Mteja Maarufu

Mara kwa mara napata fursa ya kukutana na wateja. Hao ni watu waliosoma vitabu vyangu au wanapangia kufanya hivyo au wamehudhuria mihadhara yangu. Wengine, ambao hatupati fursa ya kukutana uso kwa uso, wanawasiliana nami kwa barua pepe. Kwangu ni jambo la kushukuru, kwamba Mungu kanijalia uwezo na fursa hizo.

Siku chache zilizopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja akisema kuwa alipata taarifa zangu kutoka kwa mama mwingine wa Shepherd of the Valley Lutheran Church. Nilivyoangalia mtandaoni, nimegundua kuwa huyu aliyeniandikia ni mtu maarufu.

Wakati anaulizia kama tungeweza kukutana, alisema kuwa amenunua kitabu changu cha Africans and Americans na atakisoma hima. Anapangia kuandika kitabu kingine, na anapenda kusikia mawaidha yangu kuhusu masuala ya utamaduni katika malezi ya watoto.

Huyu namhesabu kama mteja maarufu, kwa vile anafahamika sana kutokana na shughuli zake za kuandika na kuelimisha umma. Nangojea siku tuliyopanga kukutana, wiki ijayo, nikizingatia kuwa mteja ni mfalme.

Nimalizie tu kwa kusema kuwa niliwahi kwenda Shepherd of the Valley kuongelea suala la tofauti za tamadununi. Kanisa hili lina ushirikiano na waumini wa Tungamalenga, Iringa. Nilifanya hiyo shughuli, na sikutegemea kuwa ingezua hayo niliyoeleza hapa juu. Ndivyo mambo yanavyokwenda hapa duniani. Unaweza kufanya jambo, usijue litazua nini, litaishia wapi au vipi.

Thursday, November 10, 2011

Maktaba Kuu ya Taifa, Dar es Salaam

Sijui ni wangapi kati ya mamilioni ya watu wanaoishi Dar es Salaam ambao wameingia katika Maktaba Kuu ya Taifa, au wana mazoea ya kuingia humo. Hapa siongelei wanafunzi, kwani hao wanaingia humo. Naongelea watu wasio wanafunzi.

Yawezekana wako ambao wana vijiwe vyao hapa nje ya maktaba, ambavyo wanahudhuria kila siku au kila wiki, lakini hawajawahi kukanyaga ndani ya maktaba hii.

Lakini, Mwalimu Nyerere alipofungua maktaba hii, tarehe 9 Desemba, 1967, alitoa ushauri wa maana, na baadhi ya maneno yake ni haya:

I am also forced to say that we shall probably not be able to go ahead as quickly as we would like, because even when a library service is run with the utmost economy, it still costs quite a lot of money. For a public library should not just be a place where books can be borrowed. It must also be a center for much wider adult education work of all kinds – ranging from the promotion of the desire for literacy by story telling and discussion, to the erudite lectures of visiting professors in our country. The libraries also have an important role to play in overcoming one of their own limitations; for a good librarian backed by a good library, can encourage people to write books as well as read them. Our traditional stories and histories can be written in Swahili so that the whole nation can read them; personal experiences, which are of wider interest, can be written as a story or a book; knowledge gained through practical development work can be written down so that it is shared. (…) (W)e can make our libraries into real cultural and community centers. It is up to us to provide them, to help them develop, and to use them to the full.

(Source: The Mwalimu Nyerere Foundation)

Hebu nijaribu kuyatafsiri kwa ki-Swahili:

Vile vile nalazimika kusema kuwa huenda hatutafanikiwa kusonga mbele kwa kasi ambayo tungependa, kwa sababu hata pale maktaba inapoendeshwa kwa umakini kabisa kimatumizi, bado inagharimu hela nyingi sana. Kwani maktaba ya umma isiwe tu mahali pa kuazimia vitabu. Sherti pawe pia mahali pa kutekelezea suala zima la elimu ya watu wazima kwa mapana yake--kuanzia kuhimiza kusoma na kuandika kupitia usimuliaji wa hadithi na uchambuzi wake, hadi mihadhara ya kisomi ya wahadhiri na maprofesa nchini mwetu. Maktaba pia zina wajibu muhimu wa kuchangia katika kurekebisha mapungufu yanayozikabili; kwani mkutubi bora awapo na maktaba bora, anaweza kuwahimiza watu kuandika vitabu sambamba na kuvisoma. Hadithi zetu za jadi na historia zinaweza kuandikwa kwa ki-Swahili ili Taifa zima liweze kuzisoma; taarifa za uzoefu wa watu binafsi, ambazo ni muhimu kwa jamii, zinaweza kuandikwa kama simulizi au kitabu; ujuzi upatikanao katika shughuli za maendeleo unaweza kuandikwa ili na wengine waupate. (...) (Tu)naweza kuzifanya maktaba zetu sehemu halisi za kuendeshea shughuli za kitamaduni na kijamii. Ni juu yetu kuzifanya ziwepo, kuchangia ustawi wake, na kuzitumia kikamilifu kabisa.

Wednesday, November 9, 2011

Hotuba ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Novemba 9

Leo asubuhi, katika kufuatilia habari za mambo yanayotokea Arusha wiki hii, nimesoma kwamba wakati polisi wamewakamata CHADEMA eti kwa kufanya mkutano bila kibali, polisi hao hao hawajawakamata CCM ambao walifanya mkutano bila kibali cha polisi. Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa nimeona kwa miaka na miaka jinsi vyombo vya dola Tanzania vinavyofanya umachinga kwa CCM, chama ambacho hatimaye, Mwalimu Nyerere alikiogopa, kama nilivyoelezea hapa.

Saturday, November 5, 2011

Maktaba ya Mkoa, Tanga

Maktaba ya mkoa, mjini Tanga, ilifunguliwa mwaka 1958. Wa-Ingereza, ambao walikuwa wanatawala Tanganyika, ndio waliojenga maktaba hii. Ni jengo zuri sana, kama inavyoonekana hapa kushoto.
Nimetembelea maktaba hii mara kadhaa. Ni mazoea yangu kutembelea maktaba, kama nilivyoeleza hapa na hapa. Tangu nilipofika hapo maktaba ya Tanga mara ya kwanza, miaka kadhaa iliyopita, nilipata fursa ya kufahamiana na mkurugenzi, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Nimepata fursa ya kuingia ndani na kuangalia vitabu na machapisho mengine, nikachangia nakala za vitabu vyangu.Maktaba hii ilikuwa nzuri sana tangu ilipofunguliwa. Lakini leo, hali si nzuri, kama ilivyoelezwa hapa. Maktaba inahitaji ukarabati, vitabu vipya, majarida na kadhalika. Kwa nchi tajiri kama Tanzania, ambayo ina rasilimali kuliko nchi nyingi, haieleweki kwa nini isiwezekane kukarabati maktaba kama hii. Jawabu linaeleweka: ni ujinga, ufisadi na ukosefu wa uongozi kitaifa.

Uongozi wa maktaba unajitahidi sana kufanya kazi vizuri, ingawa mazingira ni magumu. Wanajitahidi kukidha mahitaji kufuatana na mabadiliko ya wakati. Kwa mfano, mara ya mwisho nilipoingia katika maktaba hii, nilionyeshwa sehemu ambayo imewekwa maalum kwa mahitaji ya wanafunzi wa chuo kikuu huria. Wanastahili pongezi.

Friday, November 4, 2011

Nakunywa Chai na Kahawa ya Tanzania

Ujumbe wangu wa leo ni kuwa wa-Tanzania tunapaswa kutumia bidhaa zinazotengezwa nchini mwetu kila inapowezekana. Iwe tuko Tanzania au nje, tufanye hivyo, kwani manufaa yake ni makubwa.

Nimepata wazo la kuandika ujumbe huu kutokana na ukweli kwamba hapa ughaibuni ninakunywa chai na kahawa ya Tanzania. Sibadili.

Kila ninapokuwa Tanzania, wakati wa kuondoka nahakikisha kuwa nimenunua chai na kahawa ya kunitosha hadi nitakapokuja tena. Mwaka huu, kwa mfano, wakati naenda kupanda ndege uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam, nilimwambia dreva wa teksi anipeleke kwanza sehemu wanapouza chai na kahawa ya Tanzania. Ndivyo alivyofanya
Faida za kutumia bidhaa za nchini mwetu ni nyingi. Kwanza, tunachangia ajira katika nchi yetu. Kama wa-Tanzania wote, walioko nchini na nje, tungekuwa tunanunua vitu vinavyotengenezwa nchini, kama vile nguo, sabuni, sukari, soda, na viberiti, ajira zingeongezeka mara dufu. Waziri wa mambo ya nchi za nje hivi karibuni aliripotiwa akisema kuwa kuna waTanzania zaidi ya milioni mbili katika nchi za nje. Ni wazi kuwa hili ni soko kubwa sana kwa bidhaa za Tanzania, lakini tumekosa upeo wa kujitambua.


Wa-Tanzania wengi, ndani na nje ya nchi, tuna tatizo la kasumba na elimu duni. Tunashabikia vitu vya nje, hata bila sababu ya maana. Ukiwa Dar es Salaam, nenda mahali kama Mlimani City, kwa mfano. Hapo utawaona wa-Tanzania wakihangaika kununua juisi ya vikopo kutoka nje ya nchi, wakati maeneo ya jirani, kama vile Mwenge, yanauzwa mananasi, machungwa, mapapai na maembe.
Wa-Tanzania wanashabikia vitu vinavyoitwa vya mamtoni, bila kutambua kuwa kwa kufanya hivyo, wanawapa ajira watu wa nchi za nje. Tukiorodhesha vitu hivi vinavyotoka nje, wakati sio lazima tuviagize, tutaona jinsi tunavyochangia ukosefu wa ajira katika nchi yetu. Sina nafasi ya kuelezea kirefu suala hili hapa. Nimelielezea katika kitabu cha CHANGAMOTO.
Nina hakika kuwa kwa kununua vikopo na vikasha vya chai na kahawa vinavyoonekana kwenye hizi picha, nimechangia uchumi wa Tanzania, na ajira kwa wa-Tanzania kadhaa.

Thursday, November 3, 2011

Mwanafunzi Albino Aacha Shule Akihofia Kuuawa

Kila kukicha, zinajitokeza habari za kutia aibu, kusikitisha, na kutisha zinazothibitisha kuwa Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu. Hapa ni habari mojawapo kutoka blogu ya Francis Godwin kuhusu mtoto albino. Taarifa hizi za uhayawani zinapojitokeza huwa najiuliza kama Tanzania ni nchi kweli, au imeshakuwa jehenam.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&


Mtoto Albino aliyeacha masomo akifanya mahojiano na waandishi wa habari

MWANAFUNZI wa darasa la pili shule ya msingi Bulongwa wilaya ya makete mkoani Iringa Emeliana Chaula (9)mwenye ulemavu wa ngozi (albino) ambeye pia ni yatima anayelelewa katika kituo cha watoto yatima cha ELCT Bulonga Wilayani Makete ameacha masomo yake kwa kuogopa kuuwawa.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Makete Cony Mpila anaripoti kuwa mkuu wa kituo hicho Dr. Mcheshi alisema mtoto huyo amesimama kwenda shuleni kutokana na vitendo vya kutishiwa usalama wake na baadhi ya watu kutokana na umbali wa kutoka kituo hicho na shuleni anakosoma Emeliana.
Dr. Mcheshi alisema kituo chao kimeshindwa kumlinda mtoto huyo kutokana na changamoto ya ukosefu wa mafuta ya kumpeleka shuleni mtoto huyo. Ili kumnusuru mtoto huyo kimaisha na kumuwezesha aendelee na masomo kituo kimeiandika barua katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Makete ingawa hakuna jitihada zozote zinazoendelea katika kumnusuru mtoto huyo kimaisha na kimasomo.
Dr huyo alieleza pia kituo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwalea watoto yatima wenye umri mdogo na kukosa msaada kutoka katika jamii na serikali pia.