Tuesday, February 23, 2010

Nimejiunga "twitter"

Napenda kuwafahamisha wasomaji wa blogu hii na maandishi yangu mbali mbali kuwa nimejiunga "twitter," mtandao wa mawasiliano ya haraka haraka. Bofya hapa.

Shukrani kwa kuwa pamoja nami katika blogu hii. Nawakaribisha kujumuika nami "twitter" vile vile na kufuatilia shughuli zangu kwa karibu zaidi.

Saturday, February 20, 2010

Maandalizi ya "Afrifest 2010"

Leo nilienda Minneapolis kwenye mkutano wa maandalizi ya Afrifest, tamasha la utamaduni linalofanyika hapa Minnesota kila mwaka, kama kielelezo cha historia na mchango wa wa-Afrika katika ulimwengu.
Tulikutana katika mgahawa uitwao 1st Cup Cafe. Ni sehemu ambapo wa-Afrika hupenda kukutana na shughuli nyingi hufanyika hapo, kama vile mihadhara, uzinduzi wa vitabu, na burudani.

Mwanzilishi wa Afrifest ni Nathan White, ambaye anaonekana katika picha hapa juu, wa pili kutoka kulia. Mimi ninayeonekana kulia kabisa nimekuwa mwanachama wa kamati hii tangu mwanzo. Mchango wangu umekuwa zaidi katika kuelezea historia ya watu wenye asili ya Afrika, tangu chimbuko la binadamu katika Afrika hadi kuenea kwa wa-Afrika hao sehemu mbali mbali za dunia. Hilo ndilo somo ninalotoa siku ya tamasha, nikiwa na vielelezo kadha wa kadha vya kimaandishi.
Shughuli zote tunazofanya kama wanakamati ni za kujitolea, lakini tunazifanya kwa moyo mmoja kwa vile tunaamini umuhimu wa kuwakutanisha watu wenye asili ya Afrika kwa kufuata nyayo za wale waliotutangulia, kama vile Marcus Garvey, Kwame Nkrumah, W.B. Dubois, Gamal Abdel Nasser, Jomo Kenyatta, Julius Nyerere, Malcolm X, Bob Marley na Walter Rodney. Ni fursa ya kujielimisha sisi wenyewe, kujikumbusha tulikotoka katika historia yetu na harakati tulizopitia, mafanikio na matatizo, na pia ni fursa ya kuwaelimisha wa-Marekani na wengine.
Kwenye mkutano wetu huu tulishughulikia zaidi masuala ya kuandaa katiba ya "Afrifest Foundation." Tulianza shughuli za Afrifest tukiwa na mfumo tofauti, ila sasa tunataka kujiimarisha zaidi kwa muundo wa "Foundation."

Kwa mwaka huu, tumepangia kufanya tamasha la Afrifest tarehe 7 Agosti. Wanakamati tutakuwa na mikutano mingi hadi kufikia siku ya tamasha. Wajumbe wawili watatu hawaonekani kwenye taarifa hii, kwa vile walikuwa na udhuru siku hiyo.

Wednesday, February 17, 2010

Maongezi Mjini Faribault, Minnesota

Asubuhi leo nilikwenda mji wa Faribault, mwendo wa nusu saa. Nilikuwa nimealikwa na Mama Delane James, mkuu wa maktaba ya Faribault, kwenda kuongea na wafanyakazi wa maktaba kuhusu masuala ya utamaduni wa wa-Afrika.

Mji wa Faribault unazidi kuwa na watu kutoka pande mbali mbali za dunia, wengine wakiwa wakimbizi au wahamiaji wa kawaida au watafuta ajira. Miji mingi hapa Marekani inajikuta katika hali hiyo. Matokeo yake ni kuwa wenyeji wa miji hiyo na hao wageni wanakumbana na masuala yatokanayo na tofauti za tamaduni. Wahudumu wa maktaba wanakumbana na masuala hayo pia, kwani wageni hao nao ni wateja wa maktaba, ambapo wanatafuta ujuzi wa aina mbali mbali, kama vile lugha, ili kuweza kuyafahamu mazingira na maisha katika nchi ya Marekani.

Ingawa nilishafika katika maktaba ya Faribault mara kadhaa, sikutambua kuwa ina wafanykazi wengi kama niliowaona kwenye mkutano wa leo. Nilipata fursa ya kutoa mawaidha ya msingi kuhusu umuhimu wa kujifunza suala la tofauti za tamaduni, ili kuepusha matatizo. Nilizingatia uzoefu wangu na juhudi ninazofanya katika kujielimisha kuhusu tofauti hizo na kuwaelimisha wengine, iwe ni hapa Marekani au Tanzania.

Mji wa Faribault umewapokea watu wengi kutoka Afrika, hasa Somalia na Sudan. Kwa hivi, suala muhimu lililomfanya mkuu wa maktaba anialike ni kuelezea utamaduni wa watu hao. Mkuu wa maktaba na baadhi ya waliohudhuria walikuwa wameshasoma kitabu changu cha Africans and Americans, na waliuliza masuali kutokana na yaliyomo kitabuni. Pia waliwahamasisha wengine wote wakisome.

Mkutano ulikuwa wenye manufaa, na wahudhuriaji walisisitiza kuwa mazungumzo ya aina hii yanapaswa yafanyike sehemu zingine pia, kama vile shuleni na katika taasisi mbali mbali. Wanafanya mpango niende tena Faribault kutoa mhadhara kwa jamii na kusaini vitabu. Hayo nitaelezea yatakapotokea, panapo majaliwa.

Sunday, February 14, 2010

Fursa za Kuwatoa Upepo wa-Tanzania

Pamoja na kuwa kazi yangu ya msingi huku Marekani ni kufundisha, ninajishughulisha pia na mipango ya uhusiano baina ya vyuo vya Marekani na Tanzania na nchi zingine za Afrika. Mipango hii ni ile ya kupeleka wanafunzi Afrika. Kwa upande wa Tanzania, napata pia fursa ya kufanya mahojiano (intavyuu) na wasomi wanaotafuta nafasi ya kuja Marekani kwa masomo zaidi au utafiti.

Hizi ni kazi za kujitolea, lakini nazifanya kwa moyo moja, nikizingatia umuhimu wake kwa upande wa Marekani na nchi zetu, kwani, pamoja na kutoa fursa mbali mbali kwa wahusika, zinakuza maelewano duniani.

Mtu unapokuwa na fursa au wadhifa kama wangu, wa-Tanzania wanasema umeula. Wanaamini unalipwa hela nyingi sana, tena dola, si madafu. Pili, wanategemea kuwa unatumia fursa hizi kujitajirisha sana kifedha kwa msingi wa "akili mkichwa." Zaidi ya yote, wa-Tanzania wanataka wakuone unaishi maisha ya hali ya juu, si uwe unakula pilau au chapati kwenye vihoteli vya Ubungo au Kinondoni.

Siku moja, miaka ya tisini na kitu mwishoni, nikiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam kwenye shughuli hizi za intavyuu, nilipanda dala dala pale Mwenge kuelekea Tegeta. Niliposhuka kituoni Tegeta, nilikutana na wa-Tanzania wanaonifahamu. Walishangaa kuniona nimepanda dala dala, wakaanza kunisema kwa nini ninahangaika na dala dala, wakati ningeweza kujipatia gari kutokana na hizi hizi intavyuu ninazowafanyia wasomi.

Mmoja wao aliniambia: "Sisi hapa Bongo, intavyuu ya kufagia ofisi za kampuni tunatoa laki tatu kwa bosi. Sasa je intavyuu za kwenda Marekani? Mbona mtu atakupa milioni, tena kwa hiari yake! Profesa Mbele unajitakia mwenyewe matatizo ya dala dala."

Sikujua namna ya kujitetea, nao waliendelea kunipa vidonge vyangu. Nategemea kwenda tena Tanzania, miezi ya usoni, kwenye shughuli nilizoongelea, na nafahamu kuwa vidonge zaidi vinaningoja.

Thursday, February 11, 2010

Mwaliko wa Mhadhara: Kampuni ya RBC Wealth Management

Nimealikwa na kampuni ya RBC Wealth Management mjini Minneapolis, kwenda kutoa mhadhara tarehe 19 Februari. Kampuni hii ambayo shina lake ni nchini Canada, inafanya shughuli zake sehemu mbali mbali duniani, ikiwa na wafanyakazi wanaozidi 80,000.

Kama ninavyosema mara kwa mara katika blogu zangu na maandishi mengine, dunia ya leo inavyozidi kuwa kijiji, na watu wa mataifa na tamaduni mbali mbali kujikuta wakifanya kazi pamoja maofisini, vyuoni, katika biashara, na kadhalika, ni muhimu kujielimisha na masuala ya tofauti za tamaduni. Kujielimisha huko ni msingi mojawapo wa mafanikio.

Kampuni ya RBC Wealth Management imenialika makusudi ili kuongelea suala la mahusiano baina ya watu wa tamaduni mbali mbali wanaofanya kazi katika kampuni hiyo, kwani wafanyakazi hao wanatoka sehemu mbali mbali za dunia. Kampuni hii ilishanialika miaka michache iliyopita, kuongea na viongozi na maofisa wa kampuni kuhusu masuala haya haya. Walitaka kupata mawaidha kuhusu namna ya kushughulika na wafanyakazi wao kwa jinsi ya kujenga na kuimarisha mahusiano mema. Hii ni njia ya kuboresha ufanisi na kujiimarisha kibiashara.

Katika mwaliko wa awali, na katika mwaliko wa sasa, nimeombwa nikaongelee masuala yaliyomo katika kitabu changu cha Africans and Americans na yatokanayo. Wameagiza nakala za kuwatosha watakaohudhuria. Naafiki wazo hilo, kwani mtu anaweza kusahau yasemwayo katika mhadhara, lakini kitabu ni kitu cha kudumu, nyenzo ya elimu endelezi.

Kuanzia mwaka juzi nimeenda Tanzania na kuendesha warsha kuhusu utamaduni na utandawazi. Niliamua kufanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa suala hili la kujiandaa. Nimeona jinsi taasisi, makampuni na jumuia za huku Marekani zinavyojiandaa. Na kwa vile ninashuhudia mwenyewe, nina uhakika na ninachosema. Ili wa-Tanzania waweze kushindana vizuri na kupata mafanikio katika dunia hii inayozidi kuwa kijiji, ni muhimu wajiandae pia. Huu ndio ujumbe wangu.

Mihadhara ninayotoa huku Marekani, ambayo naiongelea kwenye blogu zangu, inanijengea ujuzi na uzoefu. Si tu kwamba nawafundisha wale ninaoongea nao, bali nami naelimika. Ninapoenda kwenye sehemu kama hii kampuni ya RBC Wealth Management, ninasikiliza masuali kwa makini na kuelewa hali halisi ya sehemu hii. Ni uzoefu ambao naamini utawafaidia wa-Tanzania, wa-Afrika, na wengine hapa duniani. Huwa daima napenda kukutana na watu wenye ari ya kujielimisha, kwani mimi mwenyewe sichoki kutafuta elimu na kuwapa wengine. Ni mzunguko ambao naamini unainufaisha dunia.

Ratiba ya warsha zangu Tanzania mwaka huu inaandaliwa. Warsha ya kwanza, "Culture and Globalization," itafanyika Arusha Community Church, tarehe 3 Julai, kuanzia saa 4 hadi saa 7. Itafanyika kwa lugha ya ki-Ingereza kwani wahudhuriaji huwa ni wa mataifa mbali mbali. Karibuni.

Saturday, February 6, 2010

Wamarekani Safarini Malawi

Leo nilikwenda mjini Chippewa Falls, katika jimbo la Wisconsin, umbali wa maili 123 kutoka Northfield, ambapo naishi. Nilienda kuongea na kikundi cha wa-Marekani wanaojiandaa kwenda Malawi kwa shughuli za kujitolea. Nilialikwa na Mama Diane Kaufmann, ambaye anaonekana kushoto kwangu, katika picha hapa juu. Yeye ameenda Malawi mara kadhaa, katika wadhifa wake kama mratibu wa mpango wa ushirikiano baina ya dayosisi ya Kanisa la kiLuteri Kaskazini Magharibi ya Wisconsin na Malawi. Ana uzoefu wa kupeleka vikundi vya wanadayosisi Malawi katika mpango huo. Vile vile tumeshirikiana kwa miaka kadhaa katika kuendesha mafunzo kwenye kituo cha Luther Point.
Kikundi nilichoenda kukutana nacho leo kinaenda Malawi kuwashughulikia watu wenye matatizo ya macho, na kuwagawia miwani. Wanatarajia kufanya shughuli hizo Karonga na Chitipa.
Baadhi yao wameshaenda Malawi, na kwa wengine hii itakuwa ni mara yao ya kwanza. Mama Kaufmann aliniita niongee nao kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans. Alinieleza kabla kuwa washiriki wote watakuwa wamekisoma kitabu hiki kabla ya ujio wangu. Kama kawaida, mazungumzo na watu waliojiandaa namna hii yanakuwa ya kina, kwani yanalenga katika kufuatilia yale ambayo wamesoma.
Walifurahi kuwa nami, kwani walijisikia kama vile wameshanifahamu, kutokana na ninavyojieleza kitabuni. Nami nilifurahi kuwa nao na kuwasisitizia mambo ya msingi kuhusu kuishi au kushughulika na watu wa utamaduni tofauti na wetu. Kwa vile hao wanaenda kwa shughuli za matibabu, mazungumzo yetu yalilenga zaidi kwenye hali halisi ya kushughulika na watu katika hospitali. Tofauti za tamaduni zinajitokezaje katika mazingira ya hospitali.
Kwa bahati nzuri haya ni mambo ambayo nimeyawazia kwa muda mrefu, na katika kitabu changu nimeyagusia. Vile vile, nimekuwa nikijipatia uzoefu katika mazungumzo na wanafunzi wa masomo ya uuguzi wanapojiandaa kwenda Tanzania kimasomo.

Baadhi ya wasafiri hao walisoma katika chuo cha St. Olaf, na tulipata fursa ya kuongelea na kupiga soga kuhusu maisha chuoni hapa. Baadhi wamesoma maandishi yangu mengine, kama vile Matengo Folktales na Notes on Achebe's Things Apart. Niliona wazi kuwa hao ni watu makini ambao wanajishughulisha kufahamu habari za huko waendako.

Thursday, February 4, 2010

Kioo cha Lugha: Jarida la Kiswahili la Isimu na Fasihi

Leo nilienda posta nikakuta bahasha yenye vitabu ikiwa imetumwa Dar es Salaam. Sikujua ni vitabu gani. Nilipofungua nikakuta ni nakala za jarida la Kioo cha Lugha.
Nimefurahi kupata hazina hii nikiwa huku ughaibuni ambako natumia ki-Ingereza karibu muda wote. Sasa, kwa kusoma makala maridhawa zilizoandikwa na watafiti na walimu mahiri wa Tanzania, Kenya, na kwingineko, nitajiongezea ujuzi wa kutumia ki-Swahili katika taaluma, hasa isimu na fasihi.

Miaka ya karibuni nimepata msisimko wa kuandika kwa ki-Swahili, ili kujitoa katika giza la ujinga linalotukabili wasomi wengi. Ujinga huu ni pamoja na kutoelewa namna ya kutumia ki-Swahili ipasavyo, na pia kudhani kuwa ki-Swahili hakina uwezo sawa na lugha zingine katika kuelezea mambo, hasa taaluma.

Ninajitahidi kujikomboa. Mwaka jana, kwa mfano, niliandika makala nyingi kwa ki-Swahili, hadi nikachapisha kitabu. Wakati wa kuandika nilisoma kazi kadhaa za Shaaban Robert ili kujijengea uwezo na kujiamini katika kutumia lugha ya ki-Swahili. Ni kama muujiza kuwa leo nimeletewa majarida haya, kwani kiu yangu ya kujielimisha bado na itaendelea kuwa kubwa.

Natoa shukrani tele kwa Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kunikumbuka hivyo.