Wednesday, December 31, 2014

Vitabu vya Kukumbukwa Nilivyosoma Mwaka 2014

Leo, siku ya mwisho ya mwaka 2014, napenda kujikumbusha vitabu nilivyosoma mwaka huu ambavyo nitavikumbuka kwa namna ya pekee. Sitavitaja vitabu tulivyovisoma darasani.

Kwanza, napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushuhudia mwaka 2014 ukiisha, huku zikiwa zimebaki saa nne tu hadi kuanza kwa mwaka 2015. Ingawa huu umekuwa mwaka mgumu kwangu kuliko miaka yote ya maisha yangu kwa sababu ya kuugua, nashukuru nimefikia hapa nilipo, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, huduma za madaktari, wauguzi na familia yangu, na maombi ya ndugu na marafiki.

Kutokana na hali yangu hiyo, sikuweza kusoma kama ilivyo mazoea yangu. Hata hivi, kila nilipojisikia nafuu, nilishika kitabu na kusoma, hata nilipokuwa nimelazwa hospitalini. Vitabu ni moja ya vitulizo vyangu, na madaktari na wauguzi walitambua jambo hilo.

Nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Abbott Northwestern, mjini Minneapolis, nilikwenda na kitabu cha mashairi ya Robert Frost kiitwacho Robert Frost: Selected Poems, ambacho binti yangu Zawadi alikuwa amenipa, kama nilivyoelezea hapa. Nilijitahidi kusoma mashairi mengi yaliyomo. Kabla ya kitabu hiki, nilikuwa nimesoma mashairi machache ya Frost wakati wa ujana wangu, na kati ya mashairi hayo, moja ambalo nimelikumbuka daima ni "The Road Not Taken."

Ninafurahi kuwa nimepata fursa ya kusoma mashairi mengi ya Frost mwaka huu 2014, ingawaje, kwa ujumla, yanahitaji tafakari sana, na kama mtu ni mvivu, hatafika mbali katika kuyasoma. Hata hilo shairi la "The Road Not Taken" linatuacha njia panda.

Kwa sababu kama hizi nilizotoa hapa juu, nitamkumbuka Robert Frost kwa namna ya pekee kama mmojawapo wa waandishi niliowasoma mwaka 2014. Nimeweza kupanua upeo wangu wa kumfahamu mshairi huyu maarufu.

Kitabu kilichonigusa kwa namna ya pekee ni The Pearl, riwaya ya John Steinbeck, ambayo niliielezea hapa. Ni riwaya inayosomeka kirahisi na inavutia kama sumaku kwa mtiririko wa matukio yake na jinsi inavyoelezea  tabia za binadamu, kama vile upendo na wivu, wema na ubaya. Ni riwaya ambayo sitaweza kuisahau.

Nimepata fursa ya kujiongezea ufahamu wa Shakespeare kwa kusoma Macbeth, tamthilia yake mojawapo ambayo sikuwa nimeisoma. Niliiongelea tamthilia hii katika blogu hii. Sina matumaini ya kusoma tamthilia zote 37 za Shakespeare. Ni nani amezisoma zote? Hii ndio hali halisi katika ulimwengu wa fasihi. Hata usome saa nyingi kila siku na kwa miaka yote ya maisha yako, utakachokuwa umefanya ni kama kuchota maji ndoo moja katika bahari inayoendelea kujaa maji. Kuna waandishi wengi maarufu, wa zamani, wa siku hizi, na wanaochipuka muda wote.

Lakini, hii isiwe sababu ya kukata tamaa, bali changamoto ya kukufanya ujitahidi kuvuna kila uwezacho katika hazina hii isiyo na mwisho. Nami, tunapoingia katika mwaka mpya, nina viporo vya vitabu ambavyo nilianza kuvisoma na napangia kuendelea navyo katika huu mwaka mpya, na papo hapo, nina shauku kubwa ya kusoma vitabu vingi zaidi, kwa kuwa afya yangu inaendelea kuimarika.

Tuesday, December 30, 2014

Benki ya Mkombozi na Mabilioni Kubebwa Katika Viroba, Magunia, na Mifuko ya Rambo

CHANZO: MKOMBOZI COMMERCIAL BANK

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Akaunti Ya VIP Engineering And Marketing Iliyopo Katika Benki Ya Biashara Ya Mkombozi

Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  • Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP)
Kampuni ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa akaunti husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo. Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho la kampuni kumruhusu moja kati ya wanahisa wake kuendesha akaunti pamoja na picha na hati ya kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo.
2.0     Mauzo ya hisa za VIP
Kampuni ya VIP ilileta mkataba kwenye benki ya Mkombozi wa mauziano ya hisa za asilimia 30 baina ya VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo inamiliki katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Ogasti, 2013. Bei ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani milioni 75. Katika kifungu namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi. Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina ya kampuni hizi mbili ulitambuliwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa na Jaji J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.


  • Mchakato wa kulipa kodi ya serikali
Benki ilitambua kwamba katika mauziano hayo ya hisa ni lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba husika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya kodi husika. Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia barua kampuni ya VIP na nakala ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi. Katika barua hiyo TRA iliitaarifu kampuni ya VIP kuwa makadirio ya kodi yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi 38,186,584,322.00 ikiwa ni kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP kwenda kwa PAP.(Capital gains and stamp duty). TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi kuhakikisha kuwa inalipa kodi hiyo kwa niaba ya VIP mara tu fedha zitakapoingia kwenye akaunti yake.

Malipo ya kodi ya shilingi 38,186,584,322.00 yalilipwa TRA kwenye akaunti 11120100 iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania na TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa barua yake yenye kumbukumbu namba 3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24 Januari, 2014.

  • Ufafanuzi wa mambo mbalimbali
4.1      Benki ya mkombozi kuhusika katika kusafisha fedha chafu
Fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na kuingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi. Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu mawili. Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi 73,573,500,000.00 zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu namba 000000050720 ya tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola za Kimarekani 22,000,000.00 zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba 000000050812 ya tarehe 23 Januari, 2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania. Kutokana na mchakato huo benki ya Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo ni malipo halali na siyo fedha chafu. Benki ya Mkombozi haijihusishi na utakasishaji wa fedha chafu na haramu katika uchumi wa Tanzania.



4.2      Malipo yatokanayo na akaunti ya VIP
Malipo toka kwenye akaunti ya mteja hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja. Benki ikishajiridhisha kuwa fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio lolote toka katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye akaunti ya mteja kutokana na maelekezo yake. Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti ya VIP ni halali kwa kuwa chanzo cha pesa hizo ilikuwa ni halali kutokana na mauzo ya hisa na ulipwaji wa kodi ya Serikali kama ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.

4.3      Malipo taslimu kwa wateja na kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia
Benki inatoa tamko kuwa malipo yote yaliyofanywa katika akaunti ya VIP yalilipwa kupitia akaunti za walipwaji. Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa wateja na kubebwa kwenye viroba au magunia kama ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa iliyotoka kwenye akaunti ya VIP tarehe 6 Februari, 2014 kiasi cha shilingi 3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti nane za wateja tofauti na siyo kubebwa kwenye viroba au magunia. Na zile zilizotoka toka benki ya Stanbic zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo kubeba kwenye magunia au viroba.
4.4      Malipo kwa mfanyakazi wa benki ya Mkombozi
Gazeti la Mawio la tarehe 20-26, Novemba, 2014 tolea namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo toka akaunti ya VIP ya shilingi milioni 40.2. Benki inatoa tamko kuwa haina mfanyakazi anayetambuliwa kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye akaunti ya VIP.
  • Wito kwa umma
Benki ya Mkombozi inachukua fursa hii kuwatarifu wateja wake na umma kutopotoshwa na taarifa au tuhumma zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka wateja wake wote kutokuwa na hofu yeyote kwani benki ipo imara na inafanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhumma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu. Pamoja tunajenga nchi na uchumi wa nchi yetu.

  • Hitimisho
Benki ya biashara ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na utakasishaji wa fedha chafu.


Imetolewa na:

MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA BIASHARA YA MKOMBOZI

Sunday, December 28, 2014

"As You Like It:" Kitabu cha Kumalizia Mwaka

Nimeanza kusoma As You Like It, moja ya tamthilia za Shakespeare. Ni wazi kuwa, nikizingatia kwamba leo ni tarehe 28 Desemba, hiki kitakuwa kitabu cha kumalizia mwaka.

Kama zilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, As You Like It ni hazina kubwa ya mafundisho kuhusu mahusiano baina ya wanadamu na kuhusu maisha kwa ujumla. Tamthilia yoyote ya gwiji huyu, sawa na mashairi yake, ni hazina ya lugha ya ki-Ingereza.

Ningefurahi kama ningekuwa nimesoma angalau kitabu kimoja kwa kila wiki. Padre Lambert Doerr, OSB, mwalimu wetu wa ki-ingereza tulipokuwa tunasoma seminari ya Likonde, ambaye sasa ni abate askofu mstaafu, alitushinikiza kusoma angalau kitabu kimoja kwa wiki. Kila mmoja wetu alipewa daftari ambamo alitakiwa kuorodhesha vitabu alivyosoma, na alitegemewa kuweza kutoa maelezo mafupi kuhusu kila kitabu. Ningefurahi kama ningeweza kuendeleza jadi hii miaka yote.

Nirudi tena kwenye As You Like It. Simulizi inapoanza, tunamsikia Orlando akilalamika kuwa amedhulumiwa na kaka yake mkubwa, Oliver, kuhusu urithi. Anasema kuwa baba yao aliacha wosia kwamba Oliver amgawie yeye Orlando fungu fulani la mali yake na pia amsomeshe, lakini Oliver hakufanya hvyo. Dhuluma hii inamsononesha Orlando.

Mtindo huu wa kuanzia simulizi na mhusika akielezea masononeko tunauona pia katika tamthilia ya Shakespeare iitwayo The Merchant of Venice. Halafu katika sehemu hii ya mwanzo ya As You Like It kuna pia dhamira ya kiongozi kuporwa madaraka na ndugu yake, dhamira ambayo inajitokeza pia katika The Tempest, tamthilia nyingine ya Shakespeare. Hili suala la Shakespeare kurejea tena na tena kwenye dhamira au kipengele fulani cha sanaa yake nimeligusia kabla katika blogu hii.

Tangu mwanzoni mwa As You Like It, Shakespeare anatuweka katika hamaki ya kujua nini kitakachofuata katika mtiririko wa matukio. Vile vile, kama ilivyo kawaida yake, anatupeleka mbali katika ulimwengu wa fasihi na masimulizi na imani za zamani, kuanzia enzi za wa-Griki hadi wa-Ingereza wenyewe. Mifano ya wahusika wa masimulizi hayo ni Fortune na Robin Hood.

Sijui kama nitaweza kumaliza kusoma tamthilia hii kabla ya mwaka mpya kuanza, lakini nitajitahidi. Jambo moja linalonifanya nisome pole pole ni kuvutiwa na umahiri wa Shakespeare katika kutumia lugha kwa namna ambayo aghalabu haionekani katika ki-Ingereza cha leo. Ni aina ya chemsha bongo.

Friday, December 26, 2014

Kitabu Changu Katika Jalada Gumu

Leo nimepata nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kikiwa katika jalada gumu ("hard cover"). Wiki iliyopita, kwa kutumia tekinolojia ya uchapishaji vitabu mtandaoni, niliuchapisha upya mswada wa kitabu changu, ili kitabu kipatikane pia katika jalada gumu. Nilipomaliza tu kuchapisha, niliagiza nakala, ambayo nimepata leo. Ni nakala ya kwanza kabisa, nami nimeridhika nayo.

Ni jambo la kawaida, huku ughaibuni, kwa kitabu kupatikana katika jalada jepesi ("paperback") na pia katika jalada gumu. Kuna vitabu vingine ambavyo hupatikana katika jalada jepesi tu, au katika jalada gumu tu.

Ninaamini, tangu zamani, ingawa sijafanya utafiti, kwamba maktaba ndizo zinazohitaji sana vitabu hivi vyenye jalada gumu, kwani vinaweza kuhimili vizuri zaidi misukosuko ya kuazimwa azimwa na wasomaji. Lakini kuna pia watu binafsi wanaopenda vitabu vya aina hiyo, hata kama nakala zenye jalada jepesi ziko pia.

Mimi mwenyewe nina vitabu vingi vyenye jalada gumu. Kila mtu ana sababu zake za kuvinunua vitabu vya aina hiyo. Kwa upande wangu, kisaikolojia, ninaviona vina hadhi ya pekee, mbali na kwamba vina nafasi ya kudumu zaidi katika hali nzuri.

Nimefurahi kuipata nakala hii ya kitabu changu wakati hali ya Krismasi bado iko hewani. Naona kama nimejipatia zawadi nyingine ya sikukuu. Kuanzia sasa, nitakuwa nachukua nakala hii popote nitakapokwenda kutoa mihadhara inayohusu au inayotokana na yale niliyoandika humo. Ni uamuzi wangu, hata kama hauna mantiki maalum. Ni binadamu gani anatafakari kwa makini kila kitu ambacho moyo wake unapenda?

Yeyote atakayehitaji nakala ya kitabu hiki anaweza kukipata kwenye stoo yangu ya mtandaoni. Nakala ya "kindle" inapatikana Amazon.com. Anayesita au asiyeweza kununua vitu mtandaoni awasiliane nami kwa barua pepe, africonexion@gmail.com au kwa simu, namba (507) 403-9756.

Wednesday, December 24, 2014

Maana ya Krismasi Inavyopotoshwa

Kimsingi, Krismasi ni siku ambayo sisi wa-Kristu tunakumbuka kwa namna ya pekee kuzaliwa kwa Yesu. Au labda niseme, ni siku ambayo wa-Kristu tunategemewa kukumbuka kwa namna ya pekee kuzaliwa kwa Yesu. Ni siku muhimu katika dini yetu, nasi tunategemewa kuwa tumejiandaa kiroho kwa kumpokea Yesu. Ni siku ambapo tunakumbushwa kuhusu utukufu wa Mungu, uokovu wetu, na amani duniani.

Wanataaluma tuna mazoea ya kutafiti mambo, na tunajua kuwa Krismasi ina historia ndefu, na sio vipengele vyake vyote vinatokana au kuhusiana na dini ya u-Kristu. Lakini ninachozingatia hapa ni kuwa, pamoja na hiyo historia ndefu, Krismasi kama tunavyoijua leo, ni siku takatifu, ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu, siku ambayo wa-Kristu tunapaswa kuizingatia kwa misingi hiyo.

Lakini, kwa hali ilivyo, mtazamo huu wa kuiona Krismasi kama siku takatifu unazidi kupungua, na wengi wameshasau jambo hilo. Badala yake, maana ya Krismasi inapotoshwa. Badala ya kuzingatia kuwa maandalizi ya Krismasi ni ya kiroho, watu tunajiandaa kwa mambo ya kidunia.

Tunawazia kununua vitu kama vile nguo, viatu, na zawadi mbali mbali. Wafanyabiashara wanangojea kwa hamu kuuza bidhaa zao. Tunaingojea Krismasi kwa hamu ili tukasherehekee, na tunasherehekea hata kwa namna ambazo zinakiuka mafundisho ya dini.

Kila Krismasi, nalikumbuka shairi la Lawrence Ferlinghetti, liitwalo "Christ Climbed Down," ambalo nimelifahamu tangu mwaka 1991. Ni shairi ambalo linatufanya tuutafakari upotoshaji wa Krismasi:


Christ Climbed Down

Christ climbed down
from His bare Tree
this year
and ran away to where
there were no rootless
Christmas trees
hung with candycanes and
breakable stars

Christ climbed down
from His bare Tree
this year
and ran away to where
there were no gilded Christmas
trees
and no tinsel Christmas trees
and no tinfoil Christmas trees
and no pink plastic Christmas
trees
and no gold Christmas trees
and no black Christmas trees
and no powderblue Christmas trees
hung with electric candles
and encircled by tin electric
trains
and clever cornball relatives

Christ climbed down
from His bare Tree
this year
and ran away to where
no intrepid Bible salesmen
covered the territory
in two-tone cadillacs
and where no Sears Roebuck
creches
complete with plastic babe in
manger arrived by parcel post
the babe by special delivery
and where no televised Wise
Men
praised the Lord Calvert
Whiskey

Christ climbed down
from His bare Tree
this year and ran away to where
no fat handshaking stranger
in a red flannel suit
and a fake white beard
went around passing himself
off as some sort of North Pole
saint
crossing the desert to
Bethlehem
Pennsylvania
in a Volkswagen sled
drawn by rollicking Adirondack
reindeer
and German names
and bearing sacks of Humble
Gifts from Saks Fifth Avenue
for everybody’s imagined Christ
child

Christ climbed down
from His bare Tree
this year
and ran away to where
no Bing Crosby carollers
groaned of a tight Christmas
and where no Radio City
angels
iceskated wingless
thru a winter wonderland
into a jinglebell heaven
daily at 8:30
with Midnight Mass matinees

Christ climbed down
from His bare Tree
this year
and softly stole away into
some anonymous Mary’s womb
again
where in the darkest night
of everybody’s anonymous soul
He awaits again
an unimaginable
and impossibly
Immaculate Reconception
the very craziest of
Second Comings

Copyright 1958 by Lawrence Ferlinghetti

Monday, December 22, 2014

Mkutano na Wanachuo wa Gustavus Adolphus Unakaribia

Siku zinakwenda haraka. Tarehe 5 Januari, ambayo imekaribia, ndio siku nitakayokutana na wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus, kama nilivyoandika hapa. Hao ni wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya Tanzania, kujiongezea elimu kuhusu masuala ya afya na matibabu katika mazingira tofauti na ya Marekani, hasa kwa upande wa utamaduni.

Profesa wao aliniomba nikaongee nao kuhusu masuala ya aina hiyo kwa mapana kufuatia yale niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho watakuwa wamekisoma kabla ya mimi kukutana nao.

Kutokana na kusoma hiki kitabu, wanachuo hao watakuwa wameandaa masuali. Kama ilivyotokea siku zilizopita, masuali mengine yatazuka hapo hapo.

Jukumu hili linanifanya nikipitie tena kitabu changu, angalau kijuujuu, kwani sina mazoea ya kusoma sana yale ambayo nimeshayaandika na kuyachapisha. Napendelea kutumia muda wangu na akili yangu katika kutafiti, kutafakari na kuandika mambo mapya. Ingawa yale yaliyomo kitabuni sijayabadili, na sijaona sababu ya kuyabadili, ninafahamu mengi zaidi na naendelea kujifunza, kwani elimu haina mwisho.

Kutokana na ukweli huu, mazungumzo yangu na hao wanachuo wa safari hii hayawezi kuwa sawa na yale ya miaka iliyopita. Hata kama kutakuwa na masuali yanayofanana na yale ambayo nimeshaulizwa kabla, majibu yangu yatajengeka katika upeo mpana zaidi. Fursa za aina hii zinachangia kupanua upeo huo.

Tutakutana, kama siku zilizopita, Mount Olivet Conference & Retreat Center, pembeni mwa mji wa Lakeville, Minnesota. Nangojea kwa hamu kuonana tena na Profesa Zust, na kuonana na hao wanachuo wapya. Panapo majaliwa, nitaweka ripoti katika blogu hii, kama nilivyozoea.

Sunday, December 21, 2014

Kitabu Kingine: "A Goal is a Dream With a Deadline"

Usiku wa kuamkia leo, nimemaliza kusoma kitabu kiitwacho A Goal is a Dream With a Deadline, ambacho nilikinunua siku za karibuni. Mwandishi wake, Leo B. Helzel, amekusanya kauli za watu mbali mbali wenye ujuzi na uzoefu, ili kuwaelimisha wajasiriamali, mameneja, na watu werevu kwa ujumla, wenye mitazamo ya kimaendeleo.

Kitabu hiki ni tofauti na vingine kwani ni mkusanyo wa misemo ya busara kuhusu mambo kama kujiwekea malengo, kustahimili matatizo, kutafuta masoko au wateja, kujiwekea maamuzi na kuyatekeleza kwa dhati na bila kuchelewa, kuwasikiliza wateja kwa makini na kuwahudumia vizuri, kuzingatia ubunifu, kupunguza urasimu, na kujiamini. Hayo ni baadhi ya yaliyomo katika kitabu hiki.

Sura zote za kitabu hiki zina mambo muhimu. Kwa vile mimi ninashughulika na kutoa ushauri kwa jumuia, taasisi, makampuni, na watu binafsi kuhusu tofauti za tamaduni na athari zake, nimevutiwa sana na sura ya kitabu hiki iitwayo "Going Global." Baadhi ya mawaidha yaliyomo katika sura hii ni haya: "Never assume that business is conducted in a foreign country just as it is at home" (uk. 146), "Learn about your host's people by reading about their history and culture" (uk. 147), " "Always assume that time will be handled differently in a foreign country" (uk. 147), "Latin Americans may refuse to do business with you if you are too serious. So lighten up and slow down" (uk. 151), "In Asia, learn when "maybe" really means "no" (uk. 151).

Mawaidha haya yanafanana na yale ninayotoa na kuyafafanua katika mihadhara na warsha zangu. Yamo katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na pia mara moja moja katika blogu hii.

Nimejifunza mambo kadhaa muhimu katika kusoma A Goal is a Dream With a Deadline, na nakipendekeza kwa yeyote anayetaka mabadiliko yenye manufaa katika fikra, shughuli, maisha yake na ya jamii.

Thursday, December 18, 2014

Kitabu Sasa Kinapatikana Katika "Kindle"

Baada ya kujaribu jaribu, jana nimefanikiwa kukichapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differeces katika "Kindle." Yeyote, sehemu mbali mbali za dunia, mwenye kifaa cha kuingizia na kusomea vitabu pepe anaweza kukipata mtandaoni, kwenye duka la Amazon Kindle.

Kwa miezi mingi nilikuwa nawazia kukiweka kitabu hicho katika Kindle, lakini sikujituma vya kutosha na kufanya kazi hiyo. Wiki hii, nilipania kuitekeleza, na nimefanikiwa. Katika kuhangaika kwangu, nimejifunza mambo ya ziada kuhusu tekinolojia hii, ambayo nilianza kujifunza kwa vitendo wakati nilipochapisha kitabu hiki hiki katika lulu.com.

Kuna sababu zilizonifanya niingie huko Kindle. Kwanza, ninafahamu kuwa kadiri tekinolojia inavyosonga mbele na kuenea, shughuli nyingi zinahamia mtandaoni, kuanzia elimu, biashara na mawasiliano ya aina mbali mbali. Nami najaribu kwenda na wakati.

Vile vile, ninalikumbuka tukio lililonitokea siku moja katika tamasha la vitabu la Twin Cities, mjini St. Paul, Minnesota. Kati ya watu waliofika kwenye meza yangu, alikuwepo bwana mmoja ambaye aliniuliza kama hiki kitabu cha Africans and Americans; Embracing Cultural Differences kinapatikana katika "Kindle." Nilipomwambia hakipatikani, alijibu kuwa yeye ni mtu anayesafiri mara kwa mara kwa ndege, na hataki udhia wa kubeba mzigo wa vitabu safarini. Anatumia vitabu pepe.

Kauli yake hii ilinigusa na kunifanya nijisikie vibaya. Tangu siku ile, kauli ile imekuwa changamoto kwangu, ikinikumbusha umuhimu wa kuwatimizia mahitaji wateja wa aina yake. Sasa, kwa kukichapisha kitabu katika Kindle, ninajisikia kama nimetua mzigo uliokuwa unanielemea moyoni.

Hata hivyo, Kindle sio mahali pekee mtandaoni ambapo huchapishwa vitabu pepe. Kwa mfano, kama nilivyogusia hapa juu, kitabu hiki hiki cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences nilikichapisha kwanza kule lulu.com. Kuna sehemu zingine pia, ambako mwandishi anaweza kuchapisha kitabu chake na wateja wakakipata huko. Kadiri siku zinavyopita, fursa zinaendelea kuongezeka.

Kwa kumalizia, napenda kusema kuwa mara kadhaa nimewahi kuelezea suala hili la kuchapisha vitabu mtandaoni. Mfano ni makala hii hapa na hii hapa. Vile vile, katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, nimeelezea suala hilo (kurasa 27-29), ili kuwagawia wengine yale ninayoyajua na ninayoendelea kujifunza. Ni jambo la kutia moyo kuwa kuna wa-Tanzania wenzangu ambao wanayasikiliza mawazo yangu, kama inavyodhihirika katika makala ya Ibrahim Yamola hii hapa.

Wednesday, December 17, 2014

Mwaliko Mwingine

Leo nimepata mwaliko mwingine wa kwenda kuzungumza na wanachuo wa chuo cha South Central ambao wanajiandaa kwa safari ya masomo Afrika Kusini. Mwaliko umetoka kwa mwalimu wao, Becky Djelland Davis. Hii ni mara pili yeye kunialika. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka jana, naye baadaye aliandika kuhusu mazungumzo yale katika blogu yake.

Nami nimeguswa kwa namna alivyoniandikia leo:

I will be taking students to South Africa again in May. This coming semester, we will again be reading your book Africans and Americans. I hope that perhaps you can talk with my students again? They loved you last time!

Huu ni mwaliko wa tatu kwa siku za hivi karibuni, na yote inangojea utekelezaji katika miezi michache ijayo. Wa kwanza niliuelezea hapa, na wa pili hapa. Mialiko hii ninayopata sio jambo jepesi au la mteremko. Inahitaji tafakari katika kujiandaa ili nitoe mawazo na mitazamo ya kiwango kinachokidhi mahitaji ya hao wanaonialika, na bora zaidi ni kufanya vizuri kuliko wanavyotegemea.

Hiyo inawezekana kutokana na juhudi ya kutafiti na kutafakari mambo kwa kina na upeo mpana zaidi ya yale yaliyomo katika kitabu changu, ambacho ndicho kinachochea hii mialiko. Sijioni kama ni mtaalam, bali mtafutaji wa elimu.

Kwa kuhitimisha, sherti nikiri kuwa ninafurahi kuona kuwa watu walionialika kabla wanaendelea kufanya hivyo, nami siwezi kuwaangusha. Hii ndio habari moja muhimu ya leo, ambayo nimeona niiwekee kumbukumbu katika blogu yangu hii.

Saturday, December 13, 2014

Zawadi ya Vitabu

Nimeona picha hii hapa kushoto katika Mjengwablog. Maggid Mjengwa (kulia) anaonekana akikabidhi vitabu kwa mzee wa kijiji cha Mahango, Madibira, kwa ajili ya maktaba ya kijiji.

Nimeguswa na taarifa hii, kwani vitabu ni sehemu muhimu ya maisha yangu. Hii sio tu kwa kuwa mimi ni mwandishi na mwalimu, bali pia kwa kuwa nathamini sana kitendo cha kupeleka vitabu popote vinapohitajika.

Kwa mtazamo wangu, kitabu cha maana kina thamani isiyopimika. Nikipata fursa ya kuchagua kati ya kitabu cha aina hiyo na kreti ya bia, nitachagua kitabu, kwa furaha kabisa.

Mimi mwenyewe hupeleka vitabu Tanzania. Nimeshapeleka kwenye maktaba mbali mbali, zikiwemo za Mbinga, vyuo vikuu vya Dar es Salaam, Makumira, na Tumaini,  na pia kwa watu binafsi. Kuna wakati niliwahamasisha wanadiaspora wanachama wa jumuia ya mtandaoni ya Tanzanet wakachangia dola 500 kuendeleza jukumu hilo. Mbali na hilo, kila ninapokwenda Tanzania, kwa kadiri ya uwezo wangu, nabeba vitabu kwa madhumuni hayo.

Siandiki makala hii kwa kuwa tu nimeona hii taarifa katika Mjengwablog. Wazo la vitabu kama zawadi nimekuwa nalo kwa muda mrefu. Niliwahi kuongelea jambo hili katika blogu hii. Mimi mwenyewe hufurahi nikipewa kitabu, kama nilivyoandika hapa, na hapa.

Kama ambavyo ninasema mara kwa mara katika blogu hii, ninapenda kununua vitabu. Sio kwamba nina pesa sana, bali ni kutokana na kuviona vitabu kuwa ni muhimu zaidi ya mambo mengi ambayo wengine wanayathamini zaidi. Kwa mfano, kama wewe ni mnywaji wa bia, ukiachana na bia, utagundua kuwa kumbe hela unazo. Ninasema hivyo kutokana na uzoefu wangu.

Nikirudi tena kwenye hii taarifa ya Mjengwablog, napenda kusema kuwa ni jambo jema sana kuanzisha na kuboresha maktaba vijijini. Ingetakiwa katika nchi yetu tuwe na mwamko wa namna hiyo. Kuna wageni ambao wanajitahidi kupeleka huduma ya vitabu vijijini. Mifano ni shirika la TETEA na Friends of African Village Libraries. Ingetakiwa sisi wenye nchi yetu tuwe mstari wa mbele katika kutimiza majukumu hayo, badala ya kuwaachia au kuwaangalia tu wageni wakifanya hivyo.

Kwa miaka mingi kidogo, nimewazia kuanzisha maktaba kijijini kwangu, lakini bado sijafanya hivyo. Kitu kimoja kinachonisukuma ni kuona jinsi wanakijiji wanavyotumia muda wao mwingi kwenye kilabu cha pombe. Papo hapo, kuna shule kadhaa jirani na kijiji, zikiwemo shule za sekondari, ambazo zingefaidika na kuwepo kwa maktaba kijijini. Wazo hili sio lazima alitekeleze mtu mmoja. Ni wajibu kwetu wote tunaotambua umuhimu wa vitabu.

Thursday, December 11, 2014

Sitafundisha Mwezi Januari, 2015

Awali, kwa ratiba iliyopangwa, nilitarajiwa kufundisha mwezi Januari, kozi iitwayo "The Hero and the Trickster." Hiyo ni kozi ambayo nimefundisha karibu kila mwaka, mwezi Januari. Tuna utaratibu, katika chuo hiki cha St. Olaf kuwa na kozi za mwezi Januari ambazo zinaitwa "interim." Kozi yangu ya "Hemingway in East Africa" ambayo nilifundishia Tanzania, ilikuwa ya aina hiyo.

Pamoja na kwamba ilipangwa kwamba Januari ijayo nifundishe, hivi karibuni, viongozi wa chuo wameonelea nisifundishe bali nipumzike, ili niendelee kupona vizuri. Kwa hali yangu ilivyo, nina hakika ningeweza kufundisha, lakini uongozi wa chuo umeamua kunipa hii likizo ambayo sikuitegemea.

Ninashukuru sana. Ninaona ni mipango ya Mungu, kwani kwa miezi niliyokuwa na hali mbaya kiafya, hadi nikashidwa kufanya kazi nilizozizoea, nilikuwa katika majaribu makubwa. Kutoweza kufundisha, kufanya utafiti, kuandika au kurekebisha makala za kitaaluma ulikuwa ni mtihani mkubwa kisaikolojia.

Kwa bahati nzuri, imani ya dini, kwamba yote anayajua Mungu, na kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wote, ilinifanya nisikate tamaa. Hata muuguzi mmoja katika hospitali ya Abbott Northwestern, kule Minneapolis, aliponiuliza inakuwaje kwamba ingawa nilikuwa nimelazwa siku nyingi, sikuonyesha dalili ya kulalamika, kusononeka au kukata tamaa, kama wagonjwa wengine wafanyavyo. Nilimjibu kwamba ninamtegemea Mungu, na sina sababu ya kulalamika, kusononeka wala kukata tamaa. Alivyokuwa ananiangalia usoni, aliona kuwa naongea kwa dhati.

Sasa, huu uamuzi wa viongozi wa chuo kwamba nisifundishe mwezi mzima ninauona kama ni neema ambayo Mungu ananishushia, baada ya kipindi kirefu cha majaribu. Nataka kumia muda ule kwa kujisomea vitabu na kuandika, mambo ambayo, sambamba na ufundishaji, yananiletea raha maishani.

Nimeona niandike ujumbe huu sio tu kwa lengo la kujiwekea kumbukumbu ya yale yanayojiri maishani mwangu, bali kujaribu kuwatia moyo wengine wanaopitia katika kipindi kigumu na majaribu maishani mwao.

Tuesday, December 9, 2014

Uhuru wa Tanganyika na Ukoloni Mamboleo

Siku hii ya leo, ambayo ni ya kumbukumbu ya siku ambapo Tanganyika ilijipatia Uhuru, nilitaka kuandika makala, "Uhuru wa Tanganyika na Ukoloni Mamboleo." Nilianzza kuandika, lakini nilijikuta naandika insha ndefu, sio makala fupi ambayo nadhani inatakiwa katika blogu. Kutokana na jambo hilo, nimeifuta ile makala na badala yake nimeandika kwa ufupi mambo yafuatavyo.

Uhuru tulipata tarehe 9 Desemba, 1961. Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, na ninakumbuka msisimko, hata kule kijijini kwangu. Waalimu wetu, Charles Kinunda, John Pantaleon Mbonde, na Alois Turuka, walikuwa chanzo kikubwa cha ufahamu wetu wa mambo yaliyokuwa yanatokea.

Kati ya kumbukumbu ambazo haziwezi kutoweka akilini mwangu ni picha ya askari Alexander Nyirenda akiweka mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro. Sambamba na tukio hili la kihistoria ni hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, ambamo alisema:

Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau.

Mwalimu Nyerere, alifanya kila juhudi kuliongoza na kulielimisha hili Taifa huru, akisema kuwa tunaingia katika mapambano na maadui watatu: ujinga, umaskini na maradhi. Miaka ilivyopita, alifafanua vizuri malengo mengine ya Taifa hili: kujenga jamii ya usawa kwa wote, isiyo na matabaka; jamii yenye kutoa fursa sawa kwa wote, katika nyanja mbali mbali, kama vile uchumi, elimu, na afya; kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wa kufanya kazi, chini ya kauli mbiu ya "Uhuru na Kazi," kujenga Taifa linalojitambua, kujiheshimu, na kujitegemea, Taifa huru lisilofungamana na upande wowote katika mazingira yale ya "Cold War," Taifa lenye kukaribisha urafiki na nchi yoyote kwa msingi wa kuheshimiana, Taifa ambalo halitamruhusu rafiki kutuchanguia marafiki au maadui, na tuwe mstari wa mbele kuunga mkono harakati za ukombozi Afrika na sehemu zingine duniani.

Hayo ndio yalikuwa malengo muhimu, ambayo Mwalimu Nyerere aliyaelezea katika hotuba zake, makala na vitabu mbali mbali. Alikuwa akienda na wakati, akizingatia mahitaji ya Taifa yalivyokuwa yanajitokeza. Kwa msingi huu, baada ya "Azimio la Arusha," aliendelea kuandika maandishi mengine, kama vile "Mwongozo," "Siasa ni Kilimo," "Elimu ya Kujitegemea," na "Binadamu na Maendeleo."

Hayo yote, tangu enzi za harakati za Uhuru hadi miaka ya mwisho mwisho ya sabini na kitu, yalifanyika chini ya uongozi wa chama cha TANU. Mtazamo na mwelekeo wa TANU ulikuwa wa kuongoza mapinduzi, kufuatana na mazingira ya kihistoria: kwanza ilikuwa kuwaunganisha wa-Tanganyika na kuwaongoza katika kupigania Uhuru, halafu, kuongoza harakati za kujenga ujamaa na kujitegemea.

Mwalimu Nyerere alifahamu fika kwamba Uhuru haukuwa mwisho wa safari. Kulikuwa na haja ya kupambana na urithi wa ukoloni, yaani ukoloni mamboleo na kuleta uhuru wa kweli, unaodhihirishwa na hali ya kujitegemea chini ya uongozi bora.

Miaka ilivyopita, baada ya chama kipya cha CCM kushika hatamu, hali ilikuwa hiyo kwa kipindi cha mwanzo. Lakini, pole pole, mwelekeo huu wa kuwa daima katika harakati za mapinduzi, ulianza kubadilika. Chini ya sera za CCM, kama vile "Azimio la Zanzibar," nchi imeendelea kuzama zaidi na zaidi katika mfumo wa matabaka na ukoloni mamboleo. Kwa lugha rahisi, CCM ni mhujumu wa Mapinduzi.

Ndoto na mategemeo ya Uhuru yametekwa nyara. Pamoja na kwamba tunasherehekea Uhuru tuliojipatia mwaka 1961, tutambue, kama TANU ilivyotambua, kuwa ule haukuwa mwisho wa safari. Enzi za TANU, tulitegemea kuwa tutajenga nchi ambayo iko chini ya mamlaka ya wakulima na wafanyakazi. Lakini, kama nilivyosema hapa juu, tunazidi kuzama katika ukoloni mamboleo. Wakulima na wafanyakazi, pamoja na washiriki wao, bado wana jukumu la kuendeleza harakati za kutafuta Uhuru wa kweli.

Monday, December 8, 2014

Vitabu Nilivyonunua Juzi

Juzi, Jumamosi,  nilienda Minneapolis, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation, ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la Half Price Books, ambalo nimeliongelea mara kadhaa katika blogu hii.

Ingawa ilikuwa jioni sana,  watu walikuwa wengi humo dukani: watu wazima, vijana, na watoto. Nami nilijichanganya nao, nikaangalia angalia sehemu zenye vitabu vya fasihi. Nilinunua vitabu vinne, ambavyo nitavielezea leo.

Lakini kabla ya kuelezea vitabu hivi, napenda kujikumbusha kitu kimoja kilichonigusa, wakati nimesimama katika foleni ya kulipia vitabu. Mbele yangu walikuwepo baba na mama na watoto wadogo wawili wasichana. Walikuwa wameshaweka vitabu vyao kwenye kaunta ya kulipia, huku wakiwaelezea wale watoto jinsi watakavyowasomea vitabu. Kati ya vile vitabu kwenye kaunta, niliviona viwili vikubwa vikubwa vya Harry Potter. Muda wote wale watoto walikuwa na furaha na msisimko. Kwa mara nyingine tena, nilishuhudia jinsi wenzetu wanavyowalea watoto wao katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.

Kitabu kimojawapo nilichonunua ni Much Ado About Nothing, ambayo ni tamthilia ya Shakespeare iliyohaririwa na Barbara A. Mowat na Paul Werstine. Wasomaaji wa Shakespeare wanajua kuwa tamthilia zake zimehaririwa na wahariri mbali mbali katika hii miaka 500 tangu kufariki kwake.

Tamthilia za Shakespeare, ambazo ni 37, hupatikana pia zikiwa zimekusanywa katika kitabu kimoja kikubwa sana. Ingawa ninazo nakala za kitabu hiki--nakala mbili hapa Marekani na nyingine Tanzania--huwa napenda, mara moja moja kununua hivi vitabu vya tamthilia moja moja, kwa vile ni rahisi kubeba katika mkoba na kwenda navyo popote.

Kitabu kingine nilichonunua ni The Pickwick Papers, kilichotungwa na Charles Dickens. Wengi wetu tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu tunamkumbuka Dickens na riwaya zake, kama vile Oliver Twist na A Tale of Two Cities. Binafsi, nilimpenda sana Dickens, na nilisoma vitabu vyake kadhaa. Nimewahi kumwongelea Dickens katika blogu hii.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Hemingway on Hunting. Nimenunua toleo lililochapishwa na The Lyons Press, mwaka 2001. Kitabu hiki ni mkusanyo wa maandishi ya Ernest Hemingway yanayohusu uwindaji. Mhariri wake ni Sean Hemingway, mjukuu wa mwandishi mwenyewe. Pia kuna utangulizi mfupi ulioandikwa na Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Sean amekusanya maandishi kutoka katika vitabu  kama vile Green Hills of Africa, For Whom the Bell Tolls, Across the River and into the Trees, na pia makala na barua mbali mbali alizochapisha Ernest Hemingway katika magazeti.

Ingawa mengi ya maandishi hayo ninayo, niliona ni vema kuwa na kitabu hiki ambacho kinahusu hili suala la uwindaji. Ningependa kusema pia kuna kitabu cha aina hiyo hiyo, ambacho ni mkusanyo wa maandishi ya Hemingway kuhusu uvuvi, na kingine kuhusu uandishi. Hemingway, katika falsafa na nadharia zake, aliongelea uhusiano baina ya  uandishi na uwindaji.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Minaret, riwaya iliyotungwa na Leila Aboulela, ambaye alikulia Khartoum na anaishi Dubai na Aberdeen. Ni mwandishi maarufu, ambaye ameshajitwalia tuzo kadhaa kwa uandishi wake. Ingawa nimesikia habari zake kwa miaka kadhaa, sikuwahi kusoma kitabu chake hata kimoja. Leila Aboulela anajulikana kwa umahiri wake kisanaa, pia kwa jinsi anayowaelezea suala la wanawake katika u-Islam kwa mtazamo tofauti na ilivyozoeleka. Nina dukuduku ya kusoma Minaret, kwa kuanzia, na nitapenda pia kusoma riwaya zake zingine.

Saturday, December 6, 2014

Mapitio ya Kitabu

Kama mwandishi, huwa nina hamu ya kujua maoni ya wasomaji kuhusu vitabu vyangu. Nawashukuru kwa lolote wanalosema baada ya kusoma na kutafakari yaliyomo kitabuni. Kama kitabu kimewaridhisha au kuwafurahisha, nami nafurahi. Wakiona dosari wakazibainisha, nitawashukuru kwa kunielimisha.

Leo nimeona mtandaoni kuwa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimefanyiwa mapitio katika "The Zumbro Current," jarida la kanisa la ki-Luteri la Zumbro, lililopo kusini mashariki mwa Minnesota, Marekani:

Book Review Africans and Americans: Embracing Cultural Differences

The Abner Haugen Library at Zumbro Lutheran Church has a copy of this extremely helpful book on cultural differences between Americans and Africans. It is written by Joseph L. Mbele, a Tanzanian scholar who currently is a professor of English at St. Olaf College. Anyone traveling to another country or continent would find this short book well worth reading. A few of the topics covered are: eye contact, personal space, gender issues, gifts, how “time flies, but not in Africa.” Both my wife Ann and I recommend this 98-page book.

-Duane Charles Hoven. "The Zumbro Current," Oktoba 2014, uk. 7.

Friday, December 5, 2014

Kitabu cha "Siasa Hapo Kale"

Ninasoma Siasa Hapo Kale, kitabu ambacho nilikifahamu na kukipenda tangu nilipokuwa nasoma shule ya msingi kule nyumbani kwangu Litembo, katika mkoa wa Ruvuma. Mtunzi wa kitabu hiki ni Lucius Mabasha Thonya. Kama sikosei, nilikuwa na nakala ya kitabu hiki miaka ile kijijini kwangu. Ingawa sijui kilienda wapi, mara moja moja nimekikumbuka, hasa kwa vile mimi ni mtafiti katika fasihi simulizi. Hilo ni jambo moja katika utangulizi wa makala ya leo.

Jambo jingine ni kuwa kwa miaka kadhaa, nimevutiwa na juhudi za Dada Yasinta katika kudumisha lugha ya ki-Ngoni kwa kuanzisha na kuendesha blogu ya Vangoni. Ingawa ki-Ngoni sio lugha yangu, ninaielewa kiasi fulani nikiisikia au kuisoma, kwa vile inakaribiana na lugha yangu ya ki-Matengo.

Katika kusoma blogu ya Vangoni, nilipata wazo la kumwambia Dada Yasinta kuhusu kitabu hiki cha Siasa Hapo Kale. Hatimaye, nilimpelekea ujumbe, nikijua kuwa atapenda kusikia habari zake, na ndivyo ilivyokuwa. Kupitia maktaba ya hapa chuoni ninapofundisha, nilikipata kwa kutumia utaratibu unaotumiwa na maktaba wa kuazimishana vitabu na machapisho mengine, utaratibu uitwao "interlibrary loan."

Nilifurahi kukipata. Nilitengeneza nakala nikampelekea Dada Yasinta, naye aliandika habari hiyo katika blogu yake.

Siasa Hapo Kale ni mkusanyiko wa methali za ki-Ngoni, ambazo mtunzi amezitungia hadithi za kuzielezea. Katika maelezo yake, amefanikiwa vizuri kutupa maana na matumizi ya methali hizi, kwa kutumia maisha na mahusiano ya wahusika katika hadithi hizo. Anahitimisha kila hadithi kwa kusisitiza ujumbe muhimu uliomo katika methali. Kwa maneno yake mtunzi mwenyewe:

Hadithi zilizomo kitabuni humu zimesimuliwa kwa njia ya kubuniwa tu kupatana na mambo yalivyoweza kutokea katika maisha ya watu wa zamani zile. Hadithi hizo zimebuniwa ili kuwaangalisha wasomaji katika matukio ya namna mbalimbali yalivyopata kutokea katika kabila la Wangoni wa wilaya ya Songea iliyopo kusini mwa Tanganyika iliyo karibu na ziwa Nyasa.

Methali hizi zinathibitisha busara za wahenga, yenye falsafa, maadili, na mafundisho muhimu ya maisha. Napenda kunukuu baadhi ya methali, na tafsiri zilizomo kitabuni: "Njala likoko, yikoma na mhavi" (Njaa ni adui, hata mchawi inaua). "Mbanga kufwata manji kwegihamba" (Fuata maji yanakokwenda). "Katumbi ka ngolyongo ikwela mwe ngolyongo" (Utando wa buibui akwea yeye mwenyewe tu). "Mheka pangende kumwoyo lwitimba lungi" (Yu mcheshi machoni moyoni kuna mengine). "Imekela kandumba ka ngemelelu" (Ajivunia dawa ya bahati).

Mwandishi alifanya kazi kubwa ya kufikiri katika kuzitunga hadithi zilizomo kitabuni. Vile vile, ameandika kwa ki-Swahili sanifu, kinachovutia. Kitabu hiki kilichapishwa mwaka 1960, nami nakumbuka kuwa waandishi maarufu kama Shaaban Robert walikuwa bado hai. Miaka ile ya zamani, shirika la uchapishaji la East African Literature Bureau lilikuwa makini katika kuangalia matumizi ya lugha, kabla ya kuchapisha kitabu.

Wednesday, December 3, 2014

Wazo la Kutafsiri Kitabu

Kwa wiki kadhaa, nimekuwa nikiwazia kutafsiri kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Siku chache zilizopita, niliandika kuhusu kitabu hiki katika blogu hii.

Nawazia kuzirekebisha insha zilizomo, na kuchapisha kitabu cha ki-Ingereza. Kufanya hivyo kutakipa kitabu hadhira kubwa zaidi kuliko ile ya wajuao ki-Swahili. Nina hakika, kwa mfano, kuwa wa-Marekani watakitafuta na kukisoma. Kwa ujumla wasomaji wa vitabu vyangu ni wa-Marekani.

Ninaposhiriki matamasha hapa Marekani, watu kadha wa kadha huja kwenye meza yangu na kuangalia vitabu, kuvinunua, au tu kuongea nami. Wako wanaoniuliza kama nimechapisha kitabu kingine, kwani vile vilivyopo mezani, vya ki-Ingereza, wanavyo au wamevisoma. Kauli hizi hata binti zangu, ambao hushirikiana nami, wamezisikia tena na tena.

Kwa miaka kadhaa, sijachapisha kitabu kipya. Sababu kubwa ni kuwa kuandika kitabu huchukua muda. Yaweza kuwa miezi au miaka. Kwa mfano, ilichukua miaka 23 hivi kuandaa kitabu cha Matengo Folktales. Vile vile, muda mwingi natumia katika kufanya utafiti na kuandika makala. Kutafsiri kitabu cha CHANGAMOTO, ni njia moja ya wazi ya kupatikana hicho kitabu kingine.

Kutafsiri CHANGAMOTO sio jambo la haraka. Kuna kitabu kingine katika lugha ya ki-Ingereza ambacho nataka kumaliza kukiandika kabla ya kuanza kutafsiri CHANGAMOTO. Hata hivi, siwezi kusema kuwa ni lazima ningoje. Muda wote ninakuwa na kazi kadhaa ninazoandika, na huwa sio rahisi kujua ni ipi itamalizika kabla ya ipi. Wanadamu tumejaliwa uwezo wa kufanya shughuli nyingi kwa pamoja, "multitasking" kwa ki-Ingereza. Ninachoombea ni uzima na akili timamu.

Sunday, November 30, 2014

Kuhusu "Macbeth"

Makala hii nilianza kuiandika mara tu baada ya kuanza kusoma Macbeth, tamthilia ya Shakespeare, ambayo niliitaja hapa na hapa. Jana usiku nimefika mwisho wake. Inafurahisha kujisomea namna hii, bila msukumo kutoka popote.

Hapa na pale katika Macbeth nimejikuta nikiyakumbuka maandishi mengine ya Shakespeare ambayo niliyasoma zamani, kama vile The Merchant of Venice, Othello, The Tempest, na Twelfth Night. Hii ni kwa sababu kuna mawazo ambayo yanajitokeza tena na tena katika maandishi ya Shakespeare. Wazo mojawapo ni kwamba dunia ni jukwaa ambapo sisi wanadamu ni waigizaji. Kuna misemo pia ambayo inajitokeza tena na tena.

Kwa mfano, nilivyosoma katika Macbeth kauli ya mchawi kuhusu meli kukumbwa na dhoruba (I, III, 25-26) nimekumbuka The Tempest. Nilivyokutana na usemi huu wa mfalme kwa kapteni shujaa: "So well thy words become thee as thy wounds; They smack of honor both," (I, II, 47-48) nimekumbuka hotuba ya Portia katika The Merchant of Venice, ambamo anaelezea thamani ya huruma.

Kati ya mambo anayosema kuhusu thamani ya huruma ni kwamba "It becomes the throned monarch better than his crown." Kwa tahadhari, niseme kuwa neno "becomes" anavyolitumia Shakespeare, lina maana tofauti kabisa na ile tunayoijua. Jambo hilo nilishaligundua katika kusoma tamthilia za Shakespeare.

Unaposoma Macbeth, sawa na kazi nyingi maarufu za fasihi, mahusiano ya namna hii hujitokeza, sio tu baina ya maandishi ya mwandishi mmoja, bali pia baina ya maandishi ya waandishi mbali mbali. Katika nadharia ya fasihi, mahusiano hayo huitwa "intertextuality" kwa ki-Ingereza.

Kufafanua zaidi wazo hili, napenda kusema kuwa jambo moja lililonistua katika Macbeth ni pale Fleance anaposema, "The moon is down; I have not heard the clock" (II, I, 2). Hapo nilikumbuka riwaya ya John Steinbeck, The Moon is Down, nikapata shauku ya kufuatilia kama kuna uhusiano. Lo, nimegundua kuwa Steinbeck alipata jina la riwaya yake hapo kwenye tamthilia ya Macbeth.

Ni wazi kuwa kusoma vitabu kunasisimua akili. Unaposoma masimulizi ya aina hii, ubongo unafanya kazi muda wote, kukumbuka hiki au kile, kuelewa kile unachosoma, na pia kubashiri kinachofuata katika mtiririko wa matukio.Kuelewa huko na kukumbuka vimefungamana. Akili hailali; inapata mazoezi, sawa na mazoezi ya viungo vyovyote vya mwili. Manufaa yake ni makubwa.

Ninavyosoma Macbeth, nakumbuka vizuri taarifa niliyosoma miaka kadhaa iliyopita kuhusu onesho la Macbeth lililofanywa Uingereza na kikundi cha waigizaji cha wa-Zulu. Niliisosoma makala hiyo, "The Zulu Macbeth," katika jarida la The New African, kama sikosei. Kuna ripoti kadhaa mtandaoni kuhusu onesho hilo la tamthilia ya Macbeth ya ki-Zulu, ambayo ilitungwa na Welcome Msomi na kupewa jina la "Umabatha." Kwa mfano, soma makala hii.

Ningeweza kuandika makala ndefu kuhusu Macbeth, nikijadili masuala kama dhamira, wahusika, mawaidha, falsafa, na umahiri wa Shakespeare katika kutumia lugha. Pamoja na mengine yote, Shakespeare ni mwanafalsafa anayefikirisha. Kwa mfano, tafakari kauli hii maarufu ya Macbeth mwenyewe, mhusika mkuu wa tamthilia hii, anapoambiwa kuwa mke wake amefariki:

She should have died hereafter;
There would have been a time for such a word.
Tomorrow, and tomorrow, and tomorrow
Creeps in this petty pace from day to day
To the last syllable of recorded time;
And all our yesterdays have lighted fools
The way to dusty death. Out, out, brief candle!
Life's but a walking shadow, a poor player,
That struts and frets his hour upon the stage
And then is heard no more. It is a tale
Told by an idiot, full of sound and fury,
Signifying nothing (V, V, 19-30).

Kwa kuhitimisha, napenda kusema kuwa nimefurahi sana kuisoma Macbeth hadi mwisho. Najisikia raha kuwa nimeongeza kitu cha thamani katika akili yangu. Ndivyo inavyokuwa katika kusoma vitabu vyenye thamani.

Thursday, November 27, 2014

Kitabu Changu cha Ki-Swahili

Kitu kimoja ninachojivunia kama mwandishi ni juhudi niliyofanya kwa miaka mingi katika kuandika kwa ki-Swahili. Aliyenihamasisha na kunisukumia katika uandishi wa ki-Swahili ni rafiki yangu Mugyabuso Mulokozi, ambaye sasa ni profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tangu tulipokuwa tunasoma wote "Mkwawa High School," aliona jinsi nilivyokuwa nimezama katika ki-Ingereza bila kujibidisha upande wa ki-Swahili.

Hatimaye, hasa tulipokuwa chuo kikuu, ambapo yeye nami tulikuwa tunafundisha, nilijitosa katika ulimwengu wa ki-Swahili. Kwanza nilisoma maandishi ya ki-Swahili, kisha nikaanza kufanya utafiti na kuandika makala magazetini. Kati ya maandishi niliyochapisha ni mapitio ya tamthilia ya Kijiji Chetu, iliyotungwa na Ngalimecha Ngahyoma.

Baadaye, nilianza utafiti kuhusu tungo za zamani za ki-Swahili, kama vile Utenzi wa Fumo Liongo, Al-Inkishafi na Utenzi wa Ras il Ghuli. Utafiti huu niliuendeleza nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, huku Marekani, miaka ya 1980-86.

Hatimaye, kwa kuombwa na Ndugu Maggid Mjengwa, mmiliki na mwendeshaji wa Mjengwablog, niliandika makala katika gazeti aliloanzisha, Kwanza Jamii. Baadaye, makala hizi nilizikusanya na kuzichapisha kama kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Nilipochapisha kitabu hiki, niliandika taarifa katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Kuandika kwa ki-Swahili ni namna ya kuienzi lugha hii. Lugha ni utambulisho wa utaifa na ni kielelezo cha jinsi mtu unavyoheshimu utaifa wako na unavyojitambua na kujiheshimu wewe mwenyewe, kama alivyobainisha Frantz Fanon hasa katika vitabu vyake viwili: The Wretched of the Earth na Black Skin, White Masks.

Ninajivunia kitabu hiki kwa vile kimenipa fursa ya kupima uwezo wangu wa kuandika ki-Swahili sanifu. Ingawa bado naandika zaidi kwa ki-Ingereza, sijarudi nyuma katika uandishi wa ki-Swahili. Mbali na hili suala la kujitambua na kujitambulisha kwa kuienzi lugha yetu kwa vitendo, kitabu hiki kilitokana pia na msukumo wa watu waliokuwa wananiuliza kwa nini naandika kwa ki-Ingereza tu. Watu hao waliniambia kuwa ingekuwa bora niandike pia kwa ki-Swahili, ili wa-Tanzania walio wengi waweze kuyaelewa mawazo yangu. Nami niliona hii ni hoja nzuri.

Hata hivi, kitabu hiki hakijapata wasomaji wengi. Labda hii ni kwa sababu nilikichapisha huku Marekani, mtandaoni. Kama hili ndilo tatizo, napenda kusema kuwa kitabu hiki, sawa na vitabu vyangu vingine, kinapatikana kutoka kwangu, kwa anwani hii: africonexion@gmail.com au simu namba (507) 403 9756.

Lakini pia kuna suala la kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu miongoni mwa wa-Tanzania, jambo ambalo limekuwa likisemwa na wahusika mbali mbali katika sekta ya vitabu. Tungekuwa na utamaduni huu, tungeona tahakiki na mijadala kuhusu vitabu, sio tu miongoni mwa wanafunzi na wasomi, bali katika jamii, kupitia vyombo vya habari, magazeti, na mitandao ya mawasiliano.

Tuesday, November 25, 2014

Tuna Likizo Fupi ya "Thanksgiving"

Leo hapa chuoni tunaanza likizo fupi itakayokwisha mwisho wa wiki. Ni wakati wa sikukuu maarufu hapa Marekani iitwayyo "Thanksgiving." Kwa mwaka huu, "Thanksgiving" ni keshokutwa, tarehe 27.

Kwa upande wangu, nilianza hayo mapumziko jana mchana, baada ya kufanyisha mtihani katika somo langu la "South Asian Literature." Kwa hivi, kipindi hiki ambacho ni cha mapumziko sitapumzika, bali nitakuwa nasahihisha huo mtihani.

Vile vile, wakati huu ambapo hatufundishi, ninaendelea kujisomea maandishi mbali mbali, hasa tamthilia ya Macbeth. Ninangojea kwa hamu kuandika ripoti yake wiki hii hii katika blogu hii. Pamoja na jukumu la kusahihisha mtihani, naona akili yangu imetulia vizuri, kiasi cha kuniwezesha kuitafakari tamthilia ya Macbeth na kuifaidi vilivyo.

Nikirudi kwenye hii sikukuu ya "Thanksgiving," ningeweza kusema mengi kuhusu historia yake, pia malumbano na migogoro ya kiitikadi ambayo imeigubika sikukuu hii hasa miaka ya hivi karibuni.

Kifupi ni kuwa hii ni sikukuu ambayo ni kumbukumbu ya ujio wa wazungu katika nchi hii ya Marekani. Historia wanayoisimulia ni kuwa wale wazungu wa mwanzo waliwakuta wenyeji, tunaowaita Wahindi Wekundu, na hao wenyeji waliwakaribisha wageni hao, na ndio waliowawezesha hao wahamiaji kustawi katika mazingira ya nchi hii.

Kwa mujibu wa masimulizi hayo, hiyo "Thanksgiving" ni kumbukumbu na fursa ya kutoa shukrani. Batamzinga ndio chakula rasmi kwa siku hiyo, kiasi kwamba wa-Marekani wanapowazia sikukuu hii, wanaiunganisha moja kwa moja na mlo huo. Historia yake nayo ni ndefu.

Lakini, hasa miaka ya karibuni, wanaharakati wa hilo taifa la Wahindi Wekundu na wengine, wanaikosoa historia inayosimuliwa kuanzia katika vitabu vya watoto hadi katika media zingine, kwa msingi kuwa inapotosha ukweli kwamba wale wazungu waliingia nchi hii kwa mabavu, wakafanya maovu mengi dhidi ya wenyeji, yakiwemo mauaji na kupora ardhi. Wanaharakati wanaona hii sikukuu ya "Thanksgiving" kama ni tusi kwao. Wanaiona kama siku ya maombolezo.

Ni vema kwetu ambao hatukukulia nchi hii kujielimisha ili angalau tuelewe huu mgogoro wa kiitikadi. Tuelewe hisia za wenyeji wa asili wa nchi hii. Tusiwe watu wa kusherehekea tu, na kula batamzinga, kama wanavyosherehekea wengine hapa Marekani, bali angalau tufahamu utata wa suala zima la hii sikukuu.

Kwa upande mwingine, kila kabila au taifa hapa duniani lina wakati ambapo wanasherehekea na kutoa shukrani, hasa wakati wa mavuno. Dhana ya kutoa shukrani sio dhana ya Marekani pekee. Ingawa mimi si m-Marekani na hii si nchi yangu, ninaamini kuwa kinachotakiwa ni wao kutafuta njia za kutatua huu mgogoro wa kiitikadi niliouelezea.

Monday, November 24, 2014

Mwaliko wa Profesa Barbara Zust

Asubuhi hii, nimefika ofisini na kukuta ujumbe kutoka kwa Profesa Barbara Zust wa Chuo cha Gustavus Adolphus, Minnesota. Ananiulizia iwapo naweza kwenda kuongea na wanafunzi wake tarehe 4 au 5 Januari, katika matayarisho yao ya kwenda Tanzania kimasomo. Nimempigia simu, tukakubaliana niende tarehe 5.

Profesa Zust amenialika mara kwa mara anapoandaa wanafunzi wake kwa safari ya Tanzania. Nimewahi kuandika taarifa hizo, kwa mfano hapa, hapa, na hapa. Wanafunzi hao huwa wamesoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mihadhara yangu huhusu masuala ninayoongelea kitabuni, nami hupenda sana kujibu au kujadili masuali wanayokuwa nayo.

Nimefurahi kwa jinsi Profesa Zust alivyonieleza umuhimu wa mikutano yangu na wanafunzi hao. Nimefurahi pia kuwa yeye na wanafunzi wanaona ninachofanya kina faida kubwa kwao. Ni wazi kuwa, ingekuwa hawafaidiki, hawangekuwa wananialika tena na tena.

Kwa hivi, siku yangu ya leo imeanza vizuri, nami nimeona niweke kumbukumbu hii hapa.

Nimekumbuka pia jinsi Profesa Zust na mwenzake Profesa Paula Swiggum, walivyoanza kunialika kuongelea kitabu changu kwa wanafunzi ambao wanasomea uuguzi ("nursinng"). Nilijiuliza inakuwaje mimi, ambaye sina utaalam wowote katika uwanja huu, niwe na lolote la kuwagawia wanafunzi wa somo hilo.

Katika kutafakari suala hilo, nilianza kusoma maandishi mbali mbali, nikagundua kuwa kwenye huu uwanja wa uuguzi wameingiza kipengele kiitwacho "transcultural nursing." Maana yake ni kwamba wanawafundisha wanafunzi kuhusu athari za tofauti za tamaduni katika kuwashughulikia wagonjwa.

Watu wa tamaduni tofauti wanauchukulia au wanauelewa ugonjwa, au uponaji, au wadhifa wa muuguzi, kwa misingi tofauti, kufuatana na utamaduni wao. Muuguzi akijua jambo hilo, anakuwa amejiandaa kuepuka kutoelewana na mgonjwa, na ana nafasi nzuri ya kutoa huduma muafaka kwa mgonjwa.

Katika kujisomea kuhusu mambo hayo ya "transcultural nursing," nimejifunza na ninaendelea kujifunza mengi, na papo hapo naelewa kwa nini watu kama Profesa Zust wanapenda niongee na wanafunzi wao. Nimeelewa vizuri kuwa kuna dhana nyingine ambayo inamwangalia mgonjwa katika mkabala mpana kuliko tu kile kinachomsumbua. Kuna uwezekano wa kuwepo masuala ya kisaikolojia na ya mahusiano katika jamii, ambayo ni muhimu katika kumwelewa na kumshughulikia mgonjwa. Kwa ki-Ingereza hii huitwa "holistic approach." Kwa kuzingatia hiyo dhana, nimeelewa zaidi kwa nini mambo kama yale niliyoandika kitabuni yanathaminiwa hata katika fani hii ya uuguzi.

Jana katika blogu hii, mdau Malifa Michael alniuliza kama nina mpango wa kutoa mwendelezo wa kitabu changu, nami katika kumjibu, niliongelea mambo kadhaa, likiwemo hilo la kutoa mihadhara itokanayo na kitabu, kwamba ni sehemu ya mwendelezo.

Namshukuru Mungu kwa kunipa fursa hizi za kuwaandaa vijana wanapoenda nchini kwetu, kutembelea sehemu mbali mbali, kujionea taasisi zinazohusika na masuala ya afya na matibabu, na kujumuika na wa-Tanzania katika utamaduni wetu.

Friday, November 21, 2014

Nilivyohojiwa na Radio Butiama Kuhusu Kitabu Changu

Nimewahi kuandika kuwa kama mwandishi, najikuta nikialikwa kuongelea maandishi yangu, na pengine kuongelea kitabu maalum. Hayo niliandika katika blogu hii

Wakati mwingine, mwandishi unaalikwa kwenye mahojiano katika vyombo vya habari. Nami nimewahi kuhojiwa katika redio, blogu, na magazeti.

Hapa naleta mahojiano niliyofanyiwa mwaka 2006 na m-Tanzania Deus Gunza, ambaye alikuwa anamiliki na kuendesha Radio Butiama, kule Columbus, Ohio. Mahojiano hayo ya papo kwa papo yalihusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Yasikilize mahojiano haya hapa:

http://butiama.podomatic.com/entry/2006-09-02T06_26_37-07_00

Thursday, November 20, 2014

Ninasoma Vitabu Kiholela

Jana, baada ya kufundisha darasa langu la South Asian Literature, nilikuwa ofisini kwa muda, nikawa napekuapekua bila lengo maalum katika makabati ya vitabu vyangu. Niliamua, kiholela tu, kuchukua tamthilia ya Macbeth ya Shakespeare, nikarudi nayo nyumbani na kuanza kuisoma.

Nilikuwa na hamu ya kujikumbusha enzi za ujana wangu, nilipokuwa nasoma sekondari hadi chuo kikuu. Nilipenda kusoma vitabu vya waandishi mbali mbali, kama vile Shakespeare na Charles Dickens.

Leo asubuhi, nilipoamka, niliendelea kusoma Macbeth, lakini nikakumbuka kuwa kuna vitabu kadhaa ambavyo nilianza kuvisoma au nilikuwa navisoma siku kadhaa zilizopita, au wiki kadhaa zilizopita, au miezi kadhaa iliyopita, ambavyo sikuvimaliza. Mifano ni A Moveable Feast na Islands in the Stream, vilivyoandikwa na Ernest Hemingway; Lost For Words, kilichoandikwa na J.W. Patrick Creber, na Nomad, kitabu cha Ayaan Hirsi, yule dada m-Somali anayetishiwa maisha yake kwa vile anaukosoa u-Islam. Hiyo ni mifano tu ya viporo.

Wakati kuna viporo, inatokea mara kwa mara kuwa naanza kusoma kitabu kingine kabisa na kukimaliza. Hivi ndivyo ilivyokuwa niliposoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Nilikiongelea kitabu hiki katika blogu hii, hapa na hapa. Nilikianza nikakimaliza, huku viporo kadhaa ninavyo.

Pamoja na yote hayo, jana nimekurupuka na kuanza kusoma Macbeth. Kwa hakika, nimepania kumaliza kuisoma tamthilia hii, ingawa nimeichagua kiholela tu. Hakuna uhakika kuwa kesho na keshokutwa sitaanza kusoma kitabu kingine tofauti kabisa. Kusema kweli, jana hiyo hiyo nilianza pia kusoma kitabu cha Postcolonial Criticism, kilichohaririwa na Bart Moore-Gilbert na wengine ambacho nilikinunua miaka kadhaa iliyopita, nikawa nimechunguliachungulia tu kurasa zake, bila kukisoma.

Leo nimejikuta nikitafakari tabia yangu hii kama msomaji. Siongelei vitabu ninavyofundisha darasani. Hivyo huwa navisoma kwa nidhamu, tangu ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, kama impasavyo mwalimu, na ninawaongoza wanafunzi katika kuvijadili. Hii tabia ya kusoma vitabu kiholela inahusu vitabu ambavyo ninajisomea mwenyewe, bila msukumo kutoka kokote. Najiuliza kama ni jambo jema kusoma vitabu kiholela.

Lakini, papo hapo, sioni ubaya wake. Wakati huja ambapo napata hamu ya kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikiweka kando siku zilizopita. Ajabu ni kuwa, ninapoamua kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikianza siku zilizopita nikakiweka kando, kumbukumbu hunijia kuhusu yale niliyosoma kabla.

Naamini kila msomaji wa vitabu ana tabia yake katika usomaji. Nimeona nitafakari tabia yangu na kuieleza kama nilivyofanya. Labda hii itawapa wasomaji wengine fursa ya kujitafakari pia.

Tuesday, November 18, 2014

Naulizwa Malipo ya Mihadhara Yangu

Hapa Marekani, mtu unapoalikwa kwenda kutoa mhadhara, nawe ukakubali, huwa unaulizwa malipo yako ni kiasi gani. Hapo unawatajia kiwango cha malipo unayotegemea. Unazingatia umaarufu wako, na wale wanaokualika wanategemea uwatajie kiwango chako bila maneno zaidi. Hata siku chache zilizopita, nilipoletewa mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara mjini Zumbrota, niliulizwa malipo yangu ni kiasi gani.

Miaka yapata mitano iliyopita, kwa nyakati tofauti, nilipata wasaa wa kuongea na wa-Marekani wawili wenye wadhifa katika jamii kuhusu suala hili. Tulikuwa katika mazungumzo kuhusu shughuli zangu za uandishi na utoaji mihadhara katika jumuia na taasisi mbali mbali. Ndipo wakaja na hili wazo la malipo. Ingawa waliongea nami kwa nyakati tofauti, wote walisema kuwa kufuatana na umaarufu niliokuwa nao wakati ule, nilikuwa na haki ya kutegemea kiasi cha dola 2,500 au 3,000 kwa mhadhara.

Kwangu, huu umekuwa ni mtihani miaka yote. Sijaweza kutaja hata siku moja nilipwe kiasi gani. Ukiniuliza sababu zangu, unaweza kushangaa au kunionea huruma. Imekuwa ni kawaida yangu, ninapoulizwa malipo yangu ni kiasi gani, kusema kuwa suala hili nawaachia wanaonialika. Waamue wenyewe wana uwezo gani, nami sitakuwa na tatizo.

Imekuwa hivyo miaka yote. Sibagui wenye pesa na wasio na pesa, au wenye pesa nyingi na wenye pesa kidogo. Nikialikwa kutoa mhadhara, ninakwenda, ili mradi mhadhara hauingiliani na ratiba yangu ya masomo.

Kuna vikundi ambavyo vina hela kidogo tu, au havina. Kwangu hiki si kipingamizi. Ninazingatia kuwa uwezo nilio nao umetoka kwa Mungu, na nina wajibu wa kuutumia kwa faida ya wanadamu. Wako ambao wana uwezo wa kunilipa, tena vizuri kabisa, lakini sijawa tayari kuwaweka kando wale ambao hawana hela za kunilipa. au wale wenye uwezo mdogo. Ninapokea chochote ambacho wameamua kipo katika uwezo wao. Na kama hawana uwezo, nawaambia kabisa kuwa hiki kwangu sio kizuizi.

Wa-Marekani wananishangaa kwa msimamo huo, kwani hauendani na utamaduni waliouzoea. Lakini mimi nafuata  dhamiri yangu. Kama watu wengine wengi, nina mahitaji makubwa ya fedha. Wale wanaoishi Marekani wanajua kuwa hii ni nchi ya madeni kila upande, na hayamaliziki. Hasa wakati huu, ambao nimekuwa katika matibabu kwa miezi mingi, pesa hazishikiki, na pamoja na kuwa na bima nzuri, madeni ni mpaka shingoni.

Lakini hayo yote hayajanifanya nibadili msimamo wangu kuhusu malipo ya mihadhara yangu. Ningekuwa nataja angalau hizo dola 2,500 au 3,000 kwa kila mhadhara, ningekuwa sina madeni, na labda ningeanza kuwa tajiri.

Roho yangu haiko huko.Nawashangaa mafisadi waroho wanaokwapua mabilioni ya hela za nchi yetu, wakati wananchi wana dhiki zisizosemeka, kama vile hospitali zisizo na vifaa na madawa, na madaktari na wahudumu wanateseka kwa kutolipwa wanavyostahili. Nawashangaa mafisadi hao kwa jinsi walivyo waroho wa pesa, na wasivyo na huruma, wakati watoto wengi mashuleni hawana viti wala madawati, wala vitabu, na mazingira ya walimu yanasikitisha.

Hapo juu nimeongelea malipo halali, ambayo naambiwa ningeweza kuyataja kwa wale wanaonialika. Lakini bado roho yangu inasita. Lazima niwashangae mafisadi, ambao hawachukui malipo halali, bali wanaliibia Taifa bila huruma.

Nimewazia kwa miezi mingi kuandika ujumbe huu, lakini sikujua niuandikeje. Leo nimeamua kuandika. Labda kuna wadau wenye ushauri wa kunipa.

Sunday, November 16, 2014

Mwandishi Unapoitwa Kuongelea Kitabu Chako

Siku hizi, mara kwa mara, nawazia jukumu linaloningoja, la kwenda mjini Zumbrota, Minnesota, kutoa mhadhara. Mada ni "Incorporating Immigrants into our Culture and Worship," kama nilivyoeleza katika blogu hii. Mwaliko wa kutoa mhadhara huu umetokana na kitabu nilichoandika, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Sikualikwa nikaongelee kitabu hiki, lakini kwa hali yoyote, baadhi ya yaliyomo kitabuni yatajitokeza katika mhadhara na katika kipindi cha majibu na masuali. Napenda kusema machache kuhusu jukumu la kutoa mhadhara kuhusu kitabu ulichoandika.

Mara nyingi, hutokea kwamba watu utakaozungumza nao wanakuwa wameshakisoma kitabu. Ni lazima utafakari kabla kwamba utaongelea nini, na jambo hilo hutegemea aina ya kitabu.

Kama ni riwaya, watu hutegemea utawaeleza mambo kama vile nini kilikuwa chanzo cha wewe kuandika, yaani nini kilichokufanya uandike, njia uliyopitia katika kuandika, maandishi au waandishi waliokuathiri, matatizo uliyokumbana nayo, na mambo uliyojifunza.

Lakini, watu hutegemea pia, au labda zaidi, kuwa utasoma angalau kurasa kadhaa za riwaya yako, ili wasikie sauti yako na sauti ya wahusika katika hadithi yako kwa mujibu wako wewe kama mtunzi.

Hapa kushoto tunamwona mwandishi Nuruddin Farah wa Somalia, alipokuwa anaongelea riwaya yake mpya ya Crossbones, chuoni Carleton. Anaonekana akisoma kurasa kadhaa.

Wasikilizaji huvutiwa kumsikia mwandishi namna hiyo, kwani usomaji wake ni aina ya tafsiri sio tu ya kile alichoandika, bali kilichokuwa mawazoni mwake wakati anaandika. Watu huamini kuwa usomaji wa mwandishi una ukweli na uhalisi ambao msomaji mwingine hawezi kuufikia.


Hiyo ndiyo halisi inavyokuwa, iwapo kitabu ni riwaya au mashairi. Sauti na usomaji wa mwandishi vina mvuto huo niliouelezea, ingawaje kwa kifupi.

Lakini kuna pia vitabu vya aina tofauti, kama hiki changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Unapokuwa umealikwa kuongelea kitabu cha aina hiyo, ni lazima utafakari vizuri suala zima.

Iwapo watu hao wameshakisoma, nadhani jukumu lako sio kuwasomea kurasa za kitabu, bali ni kuongelea mambo yatokanayo na yale uliyoandika. Jukumu lako ni kufafanua baadhi ya yale uliyoandika, ambayo unaamini yanakidhi mahitaji ya watu watu wale, kufuatana na mwaliko wao.

Pengine, inawezekana uzungumze bila kufungua kitabu, ingawa unacho mbele yako. Kwa mfano, kwenye hii mada ya mhadhara wangu wa Zumbrota, siamini kama nitahitaji kuwasomea kurasa zozote kutoka kitabuni. Badala yake, ikibidi, nitajumlisha mafundisho yatokanayo, yenye kukidhi mategemeo ya mada.

Aina hii ya mhadhara nimeshatoa mara nyingi. Kwa mfano, hapa kushoto ninaonekana nikiongea na wanachuo waliokuwa wanajiandaa kwenda Afrika Kusini kwenye ziara ya kimasomo. Walishasoma kitabu changu, na profesa wao aliniita kuja kuongelea masuala ya aina niliyozungumzia kitabuni, kama sehemu ya maandilizi ya safari ya wanafunzi wale. Kwa vile wanafunzi walikuwa wameshasoma kitabu, mhadhara huu ulitawaliwa zaidi na masuali na majibu. Profesa wao aliandika kuhusu mhadhara wangu katika blogu yake.

Kwa ujumla, fursa hizi hunifurahisha, sio tu kwa sababu nakutana na wasomaji na wadau wengine ana kwa ana, bali pia napata wasaa wa kujipima ni kiasi gani naifahamu mada husika na vipengele vyake.

Friday, November 14, 2014

Kuhusu Kunyanyaswa kwa Jaji Warioba

Kati ya mambo yaliyonishtua sana mwaka huu ni kunyanyaswa kwa Jaji Warioba. Kadhia hii imetokana na kazi murua aliyofanya Jaji Warioba na tume yake ya kukusanya mawazo ya wananchi kuhusu Katiba Mpya.

Kumekuwa na mlolongo wa matukio kadhaa ya unyanyasaji huo, ambao, kwa kadiri ninavyofahamu, mwanzilishi wake ni Ikulu. Tukio la kupigwa Jaji Warioba mkutanoni, ambalo limeripotiwa sana, ni kilele cha utovu huu. Wengi tunaamini kuwa Jaji Warioba ananyanyaswa kwa sababu ya uwazi na uwakilishi wa mawazo ya wananchi, jambo ambalo ni mwiba kwa mafisadi.

Nimeshtushwa vile vile na kauli ya Rais Kikwete kuhusu tukio hili la vurugu na kupigwa Jaji Warioba. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, Rais Kikwete aliishia tu kusema kuwa anaomba yasimkute yaliyomkuta Jaji Warioba. Sikuona popote kama aliongelea suala hili kwa undani na mapana kama linavyostahili.

Yeye kama Rais, nilitegemea kwanza atambue kuwa vurugu zile ni aibu kwa nchi anayoiongoza. Nilitegemea awakemee walioleta vurugu zile zilizohusisha pia kunyanyaswa kwa Jaji Warioba.

Nilitegemea Rais Kikwete atumie fursa ile kuwakumbusha wa-Tanzania, wajibu wao wa kuheshimiana na kulumbana kwa hoja, sio kwa mabavu. Angefanya hivyo, nigesema Rais ameonyesha busara za kiuongozi. Nilitegemea angekemea utovu wa ustaarabu uliojitokeza. Angewakumbusha wa-Tanzania njia ya usataarabu. badala ya yeye kujiwazia yeye binafsi, kwamba anaomba yasimpate. Je, kauli yake hii si sawa na kumezea uovu? Kauli yake haikuonyesha busara za kiuongozi.

Halafu, kuna pia kauli ya Samuel Sitta, ambayo nayo imenikera. Sitta aliripotiwa akisema kuwa Jaji Warioba alijitakia yaliyomkuta. Niliposoma taarifa hii, sikuamini kama mzee Sitta, anayetegemewa ana busara, angeweza kuwa na msimamo kama huo.

Nasikia Sitta ni msomi. Nami najiuliza: ni msomi gani ambaye hatambui wala kutetea mijadala au malumbano ya hoja. Kusema kuwa Jaji Warioba alijitakia yaliyompata ni sawa na kumezea suala la mjadala kuingiliwa na vurugu ambazo hazikubaliki katika mijadala. Kauli ya Sitta ni kama inahalalisha ukosefu wa ustaarabu unaotegemewa hasa kwa wasomi.

Sijui Sitta alikulia wapi na katika maadili gani. Sisi wengine tulilelewa katika maadili ya kuwaheshimu wazee. Kitendo cha kumpiga mzee, kwa mujibu wa maadili yale, ni mwiko kabisa. Kama hukubaliani na mzee, unapaswa kutafuta namna ya kujieleza, ambayo ni ya heshima kabisa. Nilitegemea Sitta atambue na kuzingatia hilo. Atoe mfano kwa watoto na vijana.

Tena na tena, katika jamii yetu, tumezoea kukemea tabia tunazoziiita haziendani na maadili au utamaduni wetu. Nimeshangaa kuona kuwa Sitta, ambaye ni mzee, anayetegemewa kuwa mlinzi na mtetezi wa maadili bora, haonekani kutambua kuwa Jaji Warioba kama mzee, hawezi kuletewa vurugu kama alizoletewa. Nimekerwa kabisa na kauli ya Sitta na kauli ya Rais..



Sunday, November 9, 2014

Nimealikwa Kutoa Mhadhara

Siku chache zilizopita, nilipigiwa simu kutoka Faribault, kwenye Kanisa la First English Lutheran Church. Wananiuliza iwapo nitaweza kwenda kutoa mhadhara katika Cannon River Conferenc utakaofanyika mwezi Aprili mjini Zumbrota, Minnesota.

Mada ya mkutano itakuwa "Incorporating Immigrants Into our Culture and Worship," na mhadhara wangu unatarajiwa kuwa dira ya mkutano.

Miaka kama sita hivi iliyopita, nilialikwa First English Lutheran Church, Faribault, kutoa mihadhara kuhusu yale niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Nimefurahi kuwa mihadhara yangu ile inakumbukwa, tena mama aliyenipigia simu alinikumbusha kuwa anaikumbuka baadhi ya michapo yangu na pia kitabu changu. Hata hivi, kwenye mkutano kama huu wa Zumbrota, mada sio niliyoandika katika kitabu changu, ingawaje nitakitumia kama msingi mojawapo wa kuijadili mada niliyopewa. Patakuwepo pia na muda wa masuali na majibu. 

Huu mkutano wa Zumbrota utawaleta pamoja wanajumuia kutoka makanisa ya eneo hili la Minnesota ya Mashariki Kusini. Hapa Marekani, makanisa yako mstari wa mbele katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi kutoka nchi mbali mbali.

Kwenye mji wa Faribault wenyewe, kwa mfano, makanisa ya kiLuteri na Katoliki yamekuwa yakifanya shughuli hiyo tangu pale wakimbizi na wahamiaji walipoanza kuja, kutoka sehemu kama Amerika ya Kati, Somalia, na Sudan. Hawana ubaguzi, iwe ni kwa msingi wa taifa, dini, au jinsia.

Nami, moja ya shughuli zangu katika mfumo huo imekuwa kuwasaidia wenyeji na wakimbizi na wahamiaji kuzitambua na kuzitafakari tofauti za tamaduni zao. Kuna ugumu kwa wageni kuelewa mambo ya Marekani, na kwa wa-Marekani kuna ugumu kuelewa mambo ya hao wageni. Msimamo wangu, kwenye mikutano ya aina hii, daima umekuwa kwamba sote tunawajibika kufanya juhudi kujielimisha. Hatuwezi kuuachia upande moja tu uwajibike. Wengi hawajazoea kusikia wazo kama hili.

Ninawaenzi hao waumini wa-Marekani  wanavyojitahidi kutatua tatizo hilo kwa namna yoyote iwezekananyo. Mikutano kama huu wa Aprili ni mfano mojawapo, kutoa changamoto ya kuwawezesha kuzitambua na kuzitafakari tofauti za tamaduni, kwa lengo la kuleta maelewano bali pia kuwezesha masuala kama hili suala la ibada za pamoja.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...