Tuesday, May 25, 2010

Warsha Kuhusu Utamaduni na Utandawazi, Juni 12, 2010

Hebu fikiria: hao wa-Tanzania wanaoondoka nchini kwenda kufanya kazi nchi za mbali au kutafuta biashara, kusoma, na kadhalika, wanakuwa wamejiandaa vipi kukabiliana na tamaduni za huko wanakoenda? Wageni wanaokuja Tanzania kwa shughuli mbali mbali, au kama wahamiaji, nao wanakuwa wamejiandaa vipi kuishi katika utamaduni wetu?

Masuala ya aina hii yameanza kupata umuhimu wa pekee duniani, kutokana na kuimarika kwa utandawazi. Ni aina ya masuala ambayo ninayashughulikia sana, kama mwandishi, mtoa mada na mwendesha warsha, hasa huku Marekani.

Ni muhimu wa-Tanzania nao wajipange na kujiandaa ipasavyo, kwani kama ninavyosema mara kwa mara katika blogu hii, ushindani unaendelea kushamiri duniani, na uwezo wa kukabiliana na ushindani huu unatokana na elimu, ujuzi na maarifa.

Tarehe 12 Juni nitaendesha warsha Tanga, kuhusu utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nimeshaendesha warsha za aina hii kabla hapa Tanzania. Yeyote anakaribishwa.

Kwa taarifa zaidi kuhusu warsha ya tarehe 12 Juni, soma hapa.

Sunday, May 23, 2010

Wa-Tanzania Hawana Hela za Kununulia Vitabu?

Katika malumbano yetu kwenye hizi blogu, wakati mwingine tunajadili tatizo sugu na la kukera la wa-Tanzania kutokuwa na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Baadhi ya watu wanadai kuwa kipato cha m-Tanzania ni duni kiasi kwamba wazo la kununua vitabu haliwezi kuwa kichwani mwake. Anahangaika apate angalau mlo moja kwa siku.

Hii hoja ina ukweli kwa baadhi ya wa-Tanzania. Lakini kuna maelfu ya wa-Tanzania wenye uwezo wa kununua vitabu ila hawana utamaduni huo. Ushahidi kuwa wana uwezo kifedha uko kila mahali, kuanzia baa hadi kwenye michango ya sherehe ambayo haiishi, na makamuzi mengine mengi.

Nimeona picha leo kwenye blogu ya Michuzi ambayo imenikumbusha haya malumbano yetu. Inawaonyesha mashabiki katika ukumbi wa Arcade, Mikocheni, wakishangilia mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha hii haihitaji maelezo zaidi, maana vyupa vya bia vinaonekana wazi vikiwa vimeota kama uyoga, na hapo pembeni kushoto vuvuzela linapigwa kwa nguvu kuboresha haya makamuzi.

Friday, May 21, 2010

Mteja wa Pili wa CHANGAMOTO

Kitabu cha Changamoto kimepata mteja wa pili leo, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Amenunua nakala tano.

Kwanza ninamshukuru mteja huyu kwa imani yake juu ya kitabu hiki, kama nilivyomshukuru mteja wa kwanza. Jambo la pili ni kuwa nafurahi kuona kuwa habari za kitabu hiki zinaenea. Hii ni ndoto na mategemeo ya kila mwandishi. Kwa upande wangu, nangojea kwa hamu mijadala itakayotokana na changamoto niliyotoa katika masuala mbali mbali ya jamii ya Tanzania na dunia ya leo.

Nikizingatia imani ya wateja, namalizia kwa kuahidi kuwa nitaendelea kujibidisha katika kuifahamu zaidi lugha hii ya ki-Swahili, ili niweze kuitumia kwa ufasaha zaidi na kuandika maandishi bora zaidi. Hii ndio shukrani yangu kwao.

Friday, May 14, 2010

Mteja Wangu wa Kwanza

Tarehe 8 Mei, 2010, mteja alinunua kitabu changu cha Changamoto, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Niliguswa na kitu hicho, nikasema itabidi nikiongelee hapa kwenye blogu.

Nimechapisha vitabu kadhaa, na wateja ninao. Siri moja ya uchapishaji vitabu mtandaoni kama ninavyofanya ni kuwa ninaweza kufuatilia mauzo ya vitabu saa yoyote. Ndio maana niliweza kuona kuwa mteja wa kwanza wa Changamoto amepatikana.

Kitabu hiki ni cha pekee kwangu kwa sababu ni kitabu changu cha kwanza cha ki-Swahili. Mimi si mwandishi bora wa ki-Swahili, lakini naona nina haki ya kujipongeza kwa juhudi niliyofanya, hasa nikizingatia kuwa sisi wasomi ni wavivu katika kutumia ki-Swahili, na wengi tunaamini kuwa ki-Swahili hakina utajiri kama ki-Ingereza. Kwa vile nilisomea taaluma ya lugha na isimu ya lugha, ninaelewa kuwa dhana kama hii ni potofu. Hakuna lugha maskini.

Kama mimi, ambaye ni mwalimu wa ki-Ingereza, nimeweza kujibidisha hadi kuandika kitabu kwa ki-Swahili, sioni kwa nini wasomi wengine wasiweze kufanya hivyo hivyo.

Ninapomwazia huyu mteja wangu wa kwanza nijiuliza masuali. Sijui ni nini kilichomfanya akanunua kitabu cha ki-Swahili kilichoandikwa na mtu kama mimi. Au labda kasoma makala zangu katika gazeti la Kwanza Jamii? Au labda ni mteja wa maandishi yangu ya ki-Ingereza? Au labda ana dukuduku ya kujua nimeandika nini na ninaandika vipi? Kwa vyovyote, napenda kumshukuru na kumfahamisha kuwa ameweka historia kwa kuwa mteja wangu wa kwanza.

Saturday, May 8, 2010

Tamaduni Zinapogongana

Yeyote anayefuatilia blogu zangu na maandishi mengine ataona kuwa ninashughulika sana na masuala ya tofauti za tamaduni hapa duniani. Ninatoa ushauri kwa taasisi, vyuo, makampuni, na watu binafsi kuhusu masuala hayo. Ninaendesha warsha hapa Marekani na Tanzania, na ninapangia kufanya hivyo katika nchi zingine za Afrika na duniani kwa ujumla.

Haya ninayoongelea si mambo ya kinadharia tu wala ya kuyafanyia mchezo. Yasipoeleweka na kushughulikiwa ipasavyo, yanaweza kuwa na athari kubwa katika jamii na katika dunia yetu. Mifano ni mingi, nami naitaja katika warsha zangu.

Napenda kuongelea kisa kimoja kilichosababisha niitwe kwenye mji wa Faribault, Minnesota, katikati ya mwezi Aprili mwaka huu, kutatua mgogoro uliokuwa unafukuta baina ya wa-Marekani ambao ni wafanyabiashara katika mji ule na wa-Somali ambao wamehamia katika mji ule, wengi wao wakiwa ni wakimbizi.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro kati ya jamii hizi mbili. Wa-Somali, kama ilivyo kwetu Afrika wana jadi ya kuwa wanapokutana na wenzao njiani, mitaani, au popote pale wanasimama na kuongea, aghalabu kwa muda mrefu, hata kama ni kwenye sehemu wanayopita watu. Vikundi hivi vya wa-Somali vimesababisha wafanyabiashara kupata hasara, kwani wateja wao wanaogopa. Hii ni hali halisi ya Marekani, kufuatana na historia ya mahusiano baina ya Wamarekani wazungu na Wamarekani weusi, pia taratibu zao za kutoziba njia.

Wasomali wa Faribault hawakuwa na fununu kuwa mila na desturi zao haziendani na mila na desturi za hapa Marekani. Kuziba njia, kama tunavyofanya Afrika wakati tunapokutana na kuongea na wenzetu, hairuhusiwi hapa Marekani.

Kutokana na hali hiyo, rais wa wafanyabiashara wa Faribault, Mama Kymn Anderson, akishirikiana na taasisi ya Welcome Center, walifanya mpango wa kunialika nikaongee na hao wa-Marekani na wa-Somali, tarehe 15 Aprili. Kwa wiki kadhaa waandaaji walinipa fununu kuhusu suala lililokuwa linaukabili mji wao nami nilijiwa na mawazo mengi, kwani halikuwa suala rahisi. Katika kulitafakari na kujiandaa nilipatwa na mawazo mengi, na hata niliandika ujumbe kwenye blogu yangu ya ki-Ingereza. Bofya hapa.

Siku iliwadia, nami nilienda Faribault. Tulikutana katika ukumbi wa maktaba ya Faribault. Walikuwepo watu zaidi ya ishirini, wawakilishi wa pande zote mbili. Sikuona nyuso za furaha, kutokana na hali ya mgogoro. Niliona niko katika mtihani. Nilijitahidi nilivyoweza katika hotuba yangu, na mambo yalienda vizuri. Bofya hapa.

Kwa kutambua kuwa hili lilikuwa suala linalohusu wa-Marekani na wa-Afrika, Mama Anderson alikuwa ameniagiza nichukue nakala za kitabu changu cha Africans and Americans, ambacho alishakisoma. Nilichukua nakala kadhaa ambazo, baada ya mazungumzo yangu, zilinunuliwa upesi na wengine wakakosa. Uamuzi uliofikiwa ni kuwa tutaendeleza utaratibu huu wa mazungumzo siku za usoni.

Kwa wale walioko Tanzania, nitaendesha tena warsha kadhaa mwaka huu, kuhusu utamaduni na utandawazi. Warsha ya kwanza itafanyika Tanga, tarehe 12 Juni. Kwa taarifa zaidi, bofya hapa.

Thursday, May 6, 2010

Vitabu Pepe

Kadiri siku zinavyopita na mabadiliko ya aina aina kutokea, yakiwemo mabadiliko ya tekinolojia, lugha nayo inawajibika kukabiliana na mabadiliko haya.

Katika kuyamudu mabadiliko katika uwanja wa uandishi wa barua, kwa mfano, leo hii tuna kitu kiitwacho barua pepe. Zamani tulizoea barua ya karatasi na bahasha. Lakini leo tunaandika barua pepe, bila karatasi.

Kama ninavyoeleza hapa na katika kitabu cha Changamoto, ulimwengu wa vitabu nao unabadilika kufuatana na mabadiliko ya tekinolojia. Leo vitabu vinaandikwa na kusomwa bila karatasi, sawa na barua pepe. Sasa sijui vitabu hivi tutaviita vitabu pepe au vipi.

Tuesday, May 4, 2010

Utalijua Jiji

Tangu kuanza kwa miji katika historia, wanadamu wamekuwa na hisia na fikra kuhusu miji na maisha ya mijini. Wametofautisha maisha ya mjini na maisha ya shamba, kama inavyojulikana. Kwa ujumla miji inachukuliwa kuwa sehemu ya maendeleo na usasa, na shamba ni sehemu iliyo nyuma au iliyolala usingizi.

Mitazamo hii imeelezwa vizuri katika semi mbali mbali, hata katika utamaduni wetu. Kwa mfano, kuna usemi kuwa jogoo la shamba haliwiki mjini. Nakumbuka pia wimbo mmoja wa Mbaraka Mwishehe, mwanamuziki maarufu wa Tanzania, ambao una maneno ya kumbeza mtu wa shamba, kwamba "ulipotoka shamba kuingia mjini, mimi nilikuona...."

Siti binti Saad yule mwimbaji maarufu wa zamani wa taarab alibezwa sana na wwashindani wake alipoingia mjini Unguja akitokea shamba alikokuwa mfinyanzI.

Siku hizi Tanzania, mtu ukipata matatizo mjini, unaambiwa "utalijua jiji." Matapeli na wajanja wengine wa mjini wakikuibia, unaambiwa "umeingizwa mjini."

Kutokana na mitazamo na itikadi hizi, kila mtu anayeishi mjini au kuja mjini, hataki kuonekana mshamba. Matokeo yake ni kuwa watu wa mjini wanaweza kuwa na tabia za ajabu ajabu, ili mradi wasionekane washamba. Wanaweza wasiwe na heshima au unyenyekevu, maana kwa utamaduni wa mjini, kuwa na heshima na unyenyekevu inaweza kuonekana kama ni kuzubaa. Kuitwa mtoto wa mjini ni jambo la kujivunia, hata kama tabia zenyewe ni hizo nilizoelezea. Kuitwa mshamba ni dharau.

Dhamira hizi zimeelezwa vizuri katika fasihi za mataifa mbali mbali pia. Kwa mfano, hadithi ya kale ya shujaa Gilgamesh iliyoandikwa miaka yapata elfu sita iliyopita huko Iraq kutokana na masimulizi ya mdomo, inasimulia jinsi mtu aliyeishi maporini na wanyama alivyorubuniwa na watu wa mjini hadi akaletwa mjini, kwa msingi kuwa haimfai mtu kuishi porini na wanyama.

Naye mtunzi maarufu Carl Sandburg wa Marekani, katika shairi lake liitwalo "Chicago," alielezea jinsi vijana wa wakulima walivyokuwa wanaingia jijini Chicago na kuharibika kimaadili. Wazo la mji kuwa ni mahali panapoharibu utu na maadili limeelezwa na waandishi wengi. Pamoja na yote hayo, miji inaendelea kuwa sumaku inayowatuva watu wa vijijini.