Saturday, May 8, 2010

Tamaduni Zinapogongana

Yeyote anayefuatilia blogu zangu na maandishi mengine ataona kuwa ninashughulika sana na masuala ya tofauti za tamaduni hapa duniani. Ninatoa ushauri kwa taasisi, vyuo, makampuni, na watu binafsi kuhusu masuala hayo. Ninaendesha warsha hapa Marekani na Tanzania, na ninapangia kufanya hivyo katika nchi zingine za Afrika na duniani kwa ujumla.

Haya ninayoongelea si mambo ya kinadharia tu wala ya kuyafanyia mchezo. Yasipoeleweka na kushughulikiwa ipasavyo, yanaweza kuwa na athari kubwa katika jamii na katika dunia yetu. Mifano ni mingi, nami naitaja katika warsha zangu.

Napenda kuongelea kisa kimoja kilichosababisha niitwe kwenye mji wa Faribault, Minnesota, katikati ya mwezi Aprili mwaka huu, kutatua mgogoro uliokuwa unafukuta baina ya wa-Marekani ambao ni wafanyabiashara katika mji ule na wa-Somali ambao wamehamia katika mji ule, wengi wao wakiwa ni wakimbizi.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro kati ya jamii hizi mbili. Wa-Somali, kama ilivyo kwetu Afrika wana jadi ya kuwa wanapokutana na wenzao njiani, mitaani, au popote pale wanasimama na kuongea, aghalabu kwa muda mrefu, hata kama ni kwenye sehemu wanayopita watu. Vikundi hivi vya wa-Somali vimesababisha wafanyabiashara kupata hasara, kwani wateja wao wanaogopa. Hii ni hali halisi ya Marekani, kufuatana na historia ya mahusiano baina ya Wamarekani wazungu na Wamarekani weusi, pia taratibu zao za kutoziba njia.

Wasomali wa Faribault hawakuwa na fununu kuwa mila na desturi zao haziendani na mila na desturi za hapa Marekani. Kuziba njia, kama tunavyofanya Afrika wakati tunapokutana na kuongea na wenzetu, hairuhusiwi hapa Marekani.

Kutokana na hali hiyo, rais wa wafanyabiashara wa Faribault, Mama Kymn Anderson, akishirikiana na taasisi ya Welcome Center, walifanya mpango wa kunialika nikaongee na hao wa-Marekani na wa-Somali, tarehe 15 Aprili. Kwa wiki kadhaa waandaaji walinipa fununu kuhusu suala lililokuwa linaukabili mji wao nami nilijiwa na mawazo mengi, kwani halikuwa suala rahisi. Katika kulitafakari na kujiandaa nilipatwa na mawazo mengi, na hata niliandika ujumbe kwenye blogu yangu ya ki-Ingereza. Bofya hapa.

Siku iliwadia, nami nilienda Faribault. Tulikutana katika ukumbi wa maktaba ya Faribault. Walikuwepo watu zaidi ya ishirini, wawakilishi wa pande zote mbili. Sikuona nyuso za furaha, kutokana na hali ya mgogoro. Niliona niko katika mtihani. Nilijitahidi nilivyoweza katika hotuba yangu, na mambo yalienda vizuri. Bofya hapa.

Kwa kutambua kuwa hili lilikuwa suala linalohusu wa-Marekani na wa-Afrika, Mama Anderson alikuwa ameniagiza nichukue nakala za kitabu changu cha Africans and Americans, ambacho alishakisoma. Nilichukua nakala kadhaa ambazo, baada ya mazungumzo yangu, zilinunuliwa upesi na wengine wakakosa. Uamuzi uliofikiwa ni kuwa tutaendeleza utaratibu huu wa mazungumzo siku za usoni.

Kwa wale walioko Tanzania, nitaendesha tena warsha kadhaa mwaka huu, kuhusu utamaduni na utandawazi. Warsha ya kwanza itafanyika Tanga, tarehe 12 Juni. Kwa taarifa zaidi, bofya hapa.

7 comments:

Fadhy Mtanga said...

Daima navutiwa sana na kazi zako. Ninafurahi kujifunza juu ya ushiriki wako kwa maendeleo ya jamii.

Yasinta Ngonyani said...

Ni mada nzuri ya kufunza imenikumbusha mbali kidogo na nimeipenda.

Mbele said...

Ndugu Mtanga na Dada Yasinta

Shukrani. Mambo haya ni mazito na yataendelea kutusumbua kadiri watu wa tamaduni mbali mbali wanavyozidi kukutana. Matatizo yatazidi, iwapo hatutafanya juhudi endelevu za kujielimisha na kuelimishana, watu wa tamaduni mbali mbali.

Kama nilivyosema, haya masuala si ya kinadharia tu, bali yanatokea, na hapa Tanzania yanatokea. Mfano ni huu hapa.

Bennet said...

hii ya mbwa naikumbuka sana, pole sana na kazi ngumu ya kukutanisha tamaduni tofauti na zikaelewana

Katu said...

Napenda kuongezea namna ya haya mambo ya tamaduni tofauti na miingiliano yake kutokana na dunia kuwa kijiji katika nyanja zote za maisha yetu kila siku...Wadau wengine pia wajitokeze kutoa mchango wao kama hawa wanaotegeneza filamu kuhuusisha hizi tamaduni za kutoka sehemu nyingine za dunia katika tungo zao za hizo filamu...

Na pia wale wote wenye zana zingine za kuwakilisha hii mada kwa watu wengine..

Profesa Mbele tunaomba kama utawea kuongeza namna ya hii habari kutufukia iwapo kama inawezekana hiyo warsha ikawa imerekodiwa kwa njia ya video na kaseti na kutafsiriwa kwa kitekenolojia katika lugha ya kiswahili na kurushwa kutoka vituo vya runinga vya hapa nyumbani badala kutegemea sisi Milioni arobaini tunaongea lugha moja tuu ya kiswahili na hizi lugha zetu za kienyeji kama vile kimbunga, kitamba na kipogoro nk....

Hii mada inanikumbusha nilipokuwa nikiishi nchi za Scandinavia kwa mwongo mmoja hivi ...Nilipata mshtuko wa na mbwa zao...wakitembea nao barabarani maana mazoea yangu kuwa mbwa ni kwa ajili ya security basi barabarani nilikuwa nahangaika kila mara ninaopowaona hao umbwa mpaka nilipoelemishwa na wenyeji kuhusu hii tamaduni ya wanyama domestic....hata famili moja hapo ilala Dar es salaam walipatiwa zawadi na familia ya kitaliano kwa ukarimu wa wageni wakapatiwa umbwa mdogo mweupe yule alikuwa akifungiwa kama hwa mbwa wetu wa ulinzi..

Na miaka kama miwili ile familia ya kitaliano ikarudi kutembelea Tanzania na hiyo familia.

Jinsi walivyomwona huyo umbwa anavyotunzwa huku akiwa amebadilika rangi kutoka nyeupe mpaka kijivu!!!!

Wakaomba wamnunue ingawa hiyo familia ya Kitanzania waliamua kuwarudishia bure na yule umbwa kurudishwa Italy....hii nikusisitiza hiyo Mada kuu Profesa Mbele ni jambo sahihi kwa dunia kutambuana.

Nguvu ya teknolojia ya mwasiliano inaniwezesha kuwakailisha kutoka hapa Kijijini Lungongole-Kikwawila-Ifakara

Mbele said...

Ndugu Bennet, shukrani kwa mchango. Ndugu Katu, nimefurahi sana kusoma mchango wako. Nashukuru kwa pendekezo la kurekodi warsha zangu. Naona itakuwa jambo jema sana iwapo itawezekana kupatikana CD ya angalau yale muhimu zaidi.

Mwaka jana warsha niliyofanya pale Dar es Salaam ilirekodiwa. Niliandika taarifa ya warsha hii hapa. Sina ukanda wenyewe, lakini nilitaka kuwasiliana na wahusika ili tuone namna ya kuutengeneza ukawa kielelezo cha yale yaliyoongelewa.

Visa ulivyoelezea kuhusu mbwa vinasisimua. Ni ushahidi wa hayo ninayosema. Hayo uliyoelezea kuhusu mbwa aliyetunzwa na wa-Swahili yamenichekesha sana. Lakini ndio ukweli wenyewe, na mimi kwenye kitabu changu nimeyaelezea.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nimeoa mke amabye sio mhaya-ni mnyambo, inahitaji kufikiri na kuvumiliana kwa sababu tu ya tofauti ya tamaduni na lugha

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...