Showing posts with label warsha. Show all posts
Showing posts with label warsha. Show all posts
Tuesday, January 14, 2020
Saturday, April 8, 2017
Mwaliko Chuo Kikuu cha Winona
Tangu mwaka uanze, nimetoa mihadhara au kufanyiwa mahojiano nje ya chuo ninapofundisha, mara nyingi kuliko kawaida. Nilitegemea kuwa kuanzia mwezi huu wa Aprili, hali ingebadilika. Lakini dalili hazionyeshi mabadiliko.Tarehe 6, nilipata mwaliko kutoka kwa Alex Hines, mkuu wa idara ya Inclusion and Diversity katika Chuo Kikuu cha Winona, wa kwenda kutoa mhadhara:
We would like to extend an invitation for you to attend HOPE Academic & Leadership Academy during the week of June 26th through June 29th and conduct a two hour presentation from 7-9 p.m. on Embracing African and African American Culture.
Hii itakuwa ni mara ya tatu mimi kwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Winona. Mara ya kwanza, niliongelea masuala ya utamaduni kama nilivyoyaeleza katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mara ya pili, niliongelea mahusiano ya binadamu na uongozi, kwa kutumia kitabu cha Matengo Folktales, kama nilivyoandika katika blogu hii
Mwaliko huu wa sasa, kama ilivyoelezwa katika barua niliyonukuu hapa juu, msingi wake ni kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alex Hines, tangu tulipofahamiana, miaka mingi iliyopita, amekuwa ni mmoja wa wale wanaonitegemea katika programu zao. Ninafurahi kwa imani ya wadau juu yangu, nami ninahamasika kufanya makubwa zaidi kwa ajili yao.
Blogu hii ni mahali ninapohifadhi kumbukumbu zangu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Labda kuna siku nitapata wazo la kuandika kitabu kuhusu shughuli zangu. Ikitokea hivyo, kumbukumbu hizi zitanifaa.
Friday, February 17, 2017
Umuhimu wa Kuzifahamu Tamaduni za Wengine
Umuhimu wa kuzifahamu tofauti za tamaduni unaonekana wazi wazi wakati tunapokumbana na matatizo katika mahusiano yetu na watu wa tamaduni ambazo si zetu. Tusijidanganye kwamba jambo hilo ni la kinadharia tu na kwamba halituhusu. Miaka michache iliyopita, wafanya biashara wa Tanzania walikwenda Oman kushiriki maonesho ya biashara. Walipata shida kutokana na kutojua utamaduni wa watu wa Oman. Taarifa hiyo iliandikwa katika blogu ya Michuzi.
Suala hili haliwahusu wafanya bashara tu, bali wengine pia, kama vile wanafunzi wanaokwenda nchi za nje, wanadiplomasia, watu wanaokwenda mikutanoni, na kadhalika. Kwa kuzingatia hayo, na kwa kuwa nimekuwa nikifanya utafiti katika masuala hayo, nimekuwa nikipata mialiko ya kutoa ushauri kwa jumuia na taasisi mbali mbali hapa Marekani. Vyuo vya Marekani, kwa mfano, vinapopeleka wanafunzi nchi za nje, kama vile nchi za Afrika, vinazingatia suala la kuwaandaa wanafunzi kwa kuwaelimisha kuhusu utamaduni wa huko waendako. Mwaka hadi mwaka nimealikwa kutoa elimu hiyo.
Nimewahi pia kuendesha semina Tanzania, kwenye miji ya Arusha, Tanga, na Dar es Salaam. Vile vile, kwa kuombwa na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, niliwahi kutoa mihadhara Zanzibar na Pemba, juu ya utamaduni wa Marekani, kama nilivyoelezea katika blogu hii.
Kwa jinsi ninayofahamu umuhimu wa suala hili, nimekuwa nikikumbushia mara kwa mara kila ninapoweza. Kwa mfano, uhusiano ulipoanza kuimarika baina ya Tanzania na u-Turuki, nilikumbushia suala hilo katika blogu hii. Ningependa kuona suala hili la athari za tofauti za tamaduni linapewa kipaumbele katika maisha yetu kwani kulipuuzia ni kujitakia matatizo yasiyo ya lazima. Hii ndio sababu iliyonifanya nianzishe kampuni ya kutoa elimu na ushauri iitwayo Africonexion: Cultural Consultants.
Saturday, October 8, 2016
People Before Profit: Kitabu Kuhusu Utandawazi
Leo nimejipatia kitabu kiitwacho People Before Profit kilichoandikwa na Charles Derber. Nimeanza kukisoma leo hii hii.Kwanza, niseme kuwa kitabu hiki kina utangulizi ulioandikwa na Noam Chomsky. Hilo pekee ni ishara ya thamani ya kitabu hiki, kwani Chomsky ni mchambuzi maarufu wa masuala ya ulimwengu kwa mtazamo wa kimaendeleo. Ninamheshimu sana, kama ninavyowaheshimu wachambuzi kama Seymour Hersh na Amy Goodman.
People Before Profit ni hazina ya elimu. Kinafafanua dhana ya utandawazi. Kwanza kinaelezea ukale wa utandawazi, na kwamba utandawazi una historia ndefu. Haukuanza zama zetu hizi, bali umekuwepo kwa miaka maelfu na maelfu, ukibadilika katika kila zama.
Pili kitabu kinaelezea uhusiano wa utandawazi na tekinolojia, kama vile mapinduzi ya miundombinu na viwanda. Tatu, kitabu kinaelezea mahusiano ya utandawazi na utamaduni, na hasa katika mazingira ya leo, kuna suala la mahusiano ya utandawazi na itikadi, kama vile demokrasia.
Kuna dhana kadhaa juu ya utandawazi ambazo tunapaswa kuzihoji, kwa mfando dhana ya kwamba utandawazi unaondoa tofauti miongoni mwa nchi na jamii mbali mbali, na kuifanya dunia iwe na sura moja. Dhana hii imekuwa ikijadiliwa sana.
Inahojiwa, kwa mfano na watu wanaosema kwamba pamoja na juhudi za utandawazi kuufunika ulimwengu, kuna pia nguvu za jamii na tamaduni mbali mbali zinazopambana ili kujilinda, kujihami, na kuendelea kuwepo kwa misingi tofauti na ile ya utandawazi. Nami, katika warsha zangu, kama zile nilizowahi kuendesha Arusha na Dar es Salaam, nilijaribu kuibua masuala haya.
Kifupi ni kwamba kitabu hiki kinaibua masuala muhimu ya kuelimisha kuhusu hiki kinachoitwa utandawazi. Ninakipendekeza kwa yeyote anayethamini elimu.
Thursday, August 20, 2015
Tumemaliza Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma
Leo, hapa chuoni St. Olaf, tumemaliza warsha yetu kuhusu jamii na taaluma. Nimeshaandika kuhusu warsha hii katika blogu hii. Tumehitimisha warsha kwa kujadili kitabu cha George Yancey, Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education. Lakini, kabla ya kuongelea mjadala wa leo, napenda kwanza kugusia mjadala wa jana.Jana tulijadili sura za 1, 5, na 8 za Professors and Their Politics, kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons. Insha zilizomo katika kitabu hiki zinabainisha vizuri aina mbali mbali za mitzamo ya kisiasa inayoongoza fikra, utafiti, uongozi, na mambo mengine katika vyuo vikuu vya Marekani. Kitabu hiki kinajadili soshiolojia ya wanataaluma, kwa kuchambua mahusiano miongoni mwao na siasa zinazoendesha vyuo. Kinatoa mwanga juu ya mahusiano baina ya wanataaluma na jamii kwa ujumla, ikiwemo ushiriki wa waalimu na wahitimu katika masuala ya siasa za Marekani.
Tulisoma pia maandishi mengine ambayo hayamo katika kitabu hiki, tukayajumlisha katika mjadala. Andiko mojawapo ni "The Coddling of the American Mind." Mjadala ulikuwa wa kufikirisha na kuelimisha, sawa na mijadala ya siku mbili zilizotangulia.
Leo, tulijadili sura ya 2, 5, na 8 za Compromising Scholarship. Kwa kiasi fulani, mambo yaliyojitokeza leo ni mwendelezo wa yale tuliyoyajadili jana, ingawa kitabu hiki kinakwenda mbali katika kutufanya tujitambue kwamba tunapoangalia suala lolote, tunaliangalia kwa kutumia misingi, mitazamo, au kasumba tulizo nazo vichwani. Kwa mtu ambaye anafahamu angalau kiasi falsafa ya watu akina Immanuel Kant, au nadharia za kisasa za fasihi, msisitizo kwamba sisi sote tuna misingi hiyo vichwani mwetu, kitabu hiki si kigumu kukielewa.
Mjadala wa leo ulionekana kuamsha hisia za ndani na hamasa miongoni mwa wengi wetu. Labda ni kwa sababu ya aina ya masuala tuliyokuwa tunazungumzia, au labda ni kwa sababu tumezoeana baada ya siku tatu za kukaa pamoja na kujadili masuala, mjadala wa leo haukuwa wa kawaida. Ingekuwa warsha inaendelea kesho na keshokutwa, kwa mfano, joto la mjadala lingezidi kupanda.
Nimejifunza mengi katika warsha hii. Kama nilivyosema awali katika blogu hii, nafurahi kujipatia vitabu muhimu bila gharama, ambavyo nitavisoma kwa wakati wangu. Elimu ya bure namna hii, na vitabu muhimu, ni marupurupu adhimu ya ualimu.
Thursday, July 30, 2015
Nimepata Vitabu vya Warsha: Jamii na Taaluma
Washiriki wa warsha tunapata vitabu vya bure, ambavyo tutavijadili katika warsha. Tutaanza na viwili. Kimoja ni Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities, kilichotungwa na Martha C. Nussbaum. Cha pili ni Versions of Academic Freedom, kilichoandikwa na Stanley Fish. Kwetu tuliomo katika masomo ya nadharia ya fasihi, maandishi ya Stanley Fish katika uwanja huo ni maarufu sana.
Baada ya vitabu hivyo, tutajadili Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education, kitabu cha George Yancey, na Professors and Their Politics, ambacho kimehaririwa na Neil Gross na Solon Simmon. Hiki cha pili ni mkusanyo wa insha za wataalam mbali mbali.
Warsha itakuwa nzito, sawa na masomo ya kiwango cha juu kabisa. Tutakuwa tunasoma kurasa nyingi kila siku kwa maandalizi ya mjadala wa masaa mawili kila siku. Ni fursa ya kujinoa katika fikra na mitazamo juu ya masuala muhimu ya taaluma, ufundishaji, na nafasi na mchango wetu katika jamii. Ni fursa pia ya sisi wenyewe kubadilishana mawazo na kufahamiana. Cha zaidi ni kuwa ninapenda vitabu vya kufikirisha na kuelimisha, na kuvipata vya bure si jambo dogo.
Tuesday, January 20, 2015
Mihadhara Nisiyolipwa
Nimewahi kuongelea suala la kulipwa ninapotoa mihadhara. Nilisema kuwa wa-Marekani wanapokualika kutoa mhadhara huuliza malipo yako ni kiasi gani. Nilitamka kuwa huwa sitaji kiasi ninachotaka kulipwa, bali nawaachia wanaonialika waamue kufuatana na uwezo wao. Hata kama hawana uwezo, niko tayari kuwatimizia ombi lao.Napenda kufafanua kidogo kuhusu utoaji wa mihadhara bila kulipwa. Labda wako watu ambao watashangaa kwa nini ninaridhika kutoa mihadhara ya aina hiyo. Labda wako watakaosema ninapoteza muda wangu. Huenda wengine wataniona nimechanganyikiwa. Ni jambo la kawaida kwetu wanadamu kuwa na fikra na mitazamo inayotofautiana.
Nina sababu zangu kwa kuwa na huu msimamo wangu. Kwanza ninatanguliza ubinadamu na utu, sio hela. Kuwasaidia wengine ni jambo jema sana, ambalo lina maana kuliko hela. Unaweza kuwa na hela nyingi ukazifuja, zisikuletee faida yoyote maishani, lakini, kama walivyosema wahenga, wema hauozi.
Kuna usemi mwingine, "Tenda wema nenda zako; usingoje shukrani." Ni usemi unaoniongoza na kunipa faraja maishani. Nazingatia kuwa kuna Mungu, ambae ndiye anayenipa uzima siku hadi siku, na akili timamu ya kuweza kuelewa mambo na kuwafundisha wengine. Siwezi kujivunia au kuringia vipaji alivyonipa Mungu, kwani ni dhamana kwa manufaa ya walimwengu. Falsafa hii inanitosha kikamilifu.
Ninapotoa mhadhara popote, kwa watu wenye kunilipa, wasio na uwezo wa kunilipa, au wenye uwezo kidogo sana, ninajua kuwa ni fursa ya mimi kujiongezea uzoefu na elimu, hasa wakati ninapojiandaa na wakati wa masuali na majibu. Uzoefu na elimu ni bora kuliko hela. Ni mtaji unaoweza kutumiwa kuzalisha hela nyingi. Huenda ni mtaji imara kuliko yote.
Nilipwe nisilipwe, ninapotoa mhadhara ninalichukulia jukumu langu kwa dhati na umakini wa hali ya juu. Ninajua kuwa ni fursa ya kujinadi, bila mimi kulipia, kama tunavyolipia matangazo. Kwa ufafanuzi zaidi, napenda niseme kuwa mihadhara ninayoongelea hapa aghalabu huhusu masuala ya elimu na tofauti za tamaduni na athari zake katika dunia ya utandawazi wa leo. Wanaonialika hufanya hivyo kutokana na kusoma maandishi yangu, kama vile kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kwenye mhadhara, nakala zinakuwepo na zinauzwa.
Kutoa mihadhara bila kulipwa si kupoteza muda wala si hasara. Ni aina ya uwekezaji. Huwezi kujua hao wanaokusikiliza ni watu wa aina gani. Huenda wako ambao wana uwezo wa kukuunganisha na jumuia, taasisi au kampuni zitakazopenda kukualika na zenye uwezo wa kukulipa. Mungu husawazisha yote, tena kwa namna tusiyotegemea. Narudi kwenye usemi kuwa wema hauozi. Kukataa kuwahudumia watu kwa vile tu hawana uwezo wa kukulipa ni kukosa upeo wa kuona mbali.
Nimeona niseme hayo machache, kujiwekea kumbukumbu za mtazamo wangu kwa wakati huu. Akili yangu haijasimama, bado natafakari masuala ya aina hii, na hakuna ubaya iwapo nitarejea tena siku za usoni na kufafanua zaidi mtazamo wangu, kuongeza na kuboresha, au kurekebisha baadhi ya vipengele vyake. Ni matumaini yangu kuwa wako ambao watajifunza kitu kutokana na mawazo yangu.
Sunday, December 21, 2014
Kitabu Kingine: "A Goal is a Dream With a Deadline"
Usiku wa kuamkia leo, nimemaliza kusoma kitabu kiitwacho A Goal is a Dream With a Deadline, ambacho nilikinunua siku za karibuni. Mwandishi wake, Leo B. Helzel, amekusanya kauli za watu mbali mbali wenye ujuzi na uzoefu, ili kuwaelimisha wajasiriamali, mameneja, na watu werevu kwa ujumla, wenye mitazamo ya kimaendeleo.Kitabu hiki ni tofauti na vingine kwani ni mkusanyo wa misemo ya busara kuhusu mambo kama kujiwekea malengo, kustahimili matatizo, kutafuta masoko au wateja, kujiwekea maamuzi na kuyatekeleza kwa dhati na bila kuchelewa, kuwasikiliza wateja kwa makini na kuwahudumia vizuri, kuzingatia ubunifu, kupunguza urasimu, na kujiamini. Hayo ni baadhi ya yaliyomo katika kitabu hiki.
Sura zote za kitabu hiki zina mambo muhimu. Kwa vile mimi ninashughulika na kutoa ushauri kwa jumuia, taasisi, makampuni, na watu binafsi kuhusu tofauti za tamaduni na athari zake, nimevutiwa sana na sura ya kitabu hiki iitwayo "Going Global." Baadhi ya mawaidha yaliyomo katika sura hii ni haya: "Never assume that business is conducted in a foreign country just as it is at home" (uk. 146), "Learn about your host's people by reading about their history and culture" (uk. 147), " "Always assume that time will be handled differently in a foreign country" (uk. 147), "Latin Americans may refuse to do business with you if you are too serious. So lighten up and slow down" (uk. 151), "In Asia, learn when "maybe" really means "no" (uk. 151).
Mawaidha haya yanafanana na yale ninayotoa na kuyafafanua katika mihadhara na warsha zangu. Yamo katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na pia mara moja moja katika blogu hii.
Nimejifunza mambo kadhaa muhimu katika kusoma A Goal is a Dream With a Deadline, na nakipendekeza kwa yeyote anayetaka mabadiliko yenye manufaa katika fikra, shughuli, maisha yake na ya jamii.
Wednesday, March 9, 2011
Mteja ni Mfalme
Kwa kawaida nadharia ni rahisi, ila utekelezaji unaweza kuwa mtihani mgumu. Hayo ninayaona wakati huu ninapoandika makala hii. Kuna mtu ameanza mawasiliano nami, kunialika nikazungumze kwenye kampuni anapofanyia kazi, kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans.
Ingawa nimethibitisha kuwa shughuli hii itafanyika, nimeona kuwa huyu mhusika hana uzoefu mzuri katika kupanga mipango ya aina hii. Nimeanza kupata usumbufu fulni, kwani wakati fulani anasema kitu nami nikadhani nimemwelewa, kumbe baadaye inaonekana hatukuelewana. Hata tarehe aliyopangia tufanya hiyo shughuli ameniambia kuwa imebidi waibadili.
Ninajua kabisa kuwa hatimaye nitaenda kutoa huo mhadhara, lakini usumbufu unanikera. Sasa hapo ndipo suala la mteja ni mfalme linapoingia. Mimi ninatoa huduma ya ushauri katika masuala kama haya niliyoongelea katika kitabu changu. Nimesajili kijikampuni kiitwacho Africonexion hapa Minnesota na huduma nazitoa chini ya kivuli cha kampuni hiyo. Huduma hizo ni pamoja na ushauri, warsha, na vitabu.
Sasa basi, kwa mujibu wa dhana ya kwamba mteja ni mfalme, ni wazi kuwa nawajibika kuwa sambamba na huyu jamaa anayenisumbua, nimsikilize vizuri muda wote na kuongea naye kwa uchangamfu, kama vile hakuna kinachonikera. Kero zake nizione kuwa ni fursa ya mimi kujiongezea uzoefu katika kuwashughulikia wateja na kuimarisha sifa ya kikampuni changu.
Najua kuwa pamoja na yote, kikampuni changu kitafaidika. Kwanza, malipo tumeshapatana, na maandalizi yake yameanza. Siku itakapofika, nitaenda kutoa mhadhara wa kusisimua na kuelimisha. Wao watafaidika, nami nitajipatia wapiga debe wengi.
(Katuni ni ya Nathan Mpangala)
Thursday, August 26, 2010
Ujumbe wa Msomaji wa Kitabu
Naichukulia blogu hii kama mahali ambapo naweka mambo yangu binafsi: kumbukumbu, fikra, dukuduku, hisia na kadhalika. Ingawa najua watu wanasoma ninayoandika, siwezi kusema kuwa wao ndio walengwa. Ninajiandikia mwenyewe, kwa uhuru na namna ninayotaka, mambo yangu binafsi.
Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mshiriki mmojawapo wa warsha niliyoendesha Dar es Salaam mwaka jana. Bofya hapa. Ameniulizia naenda lini kutoa warsha zingine akahudhurie.
Pia amesema kuwa kitabu cha Africans and Americans ambacho alikinunua wakati wa warsha kinamsaidia katika kutoa mihadhara na kushughulikia masuala mengine ya mahusiano sehemu za kazi.
Ni wazi nimefurahi kusikia hayo. Nani asingefurahi? Nimemwambia nafarijika kuwa kitabu kimezaa matunda mema kwake, hasa nikikumbuka gharama ya warsha na kitabu. Lengo moja la kuandika kitabu hiki lilikuwa kuwasaidia wanaohitajika kutoa mihadhara kuhusu tofauti za tamaduni na matatizo na changamoto zitokanazo na tofauti hizi. Wengine wanakuwa na majukumu ya kusuluhisha migogoro. Mimi mwenyewe nakitumia kitabu hiki, mahali pa kuanzia.
Maoni ya wasomaji ni msaada mkubwa kwa mwandishi. Nami nina bahati ya kuyapata mara kwa mara. Wengine, kama ilivyo katika ulimwengu wa vitabu, wanayaweka maoni yao hadharani, kama haya hapa. Nawajibika kutoa shukrani.

Saturday, June 5, 2010
Warsha Zangu Hazina Posho
Tangu mwaka juzi, nimeendesha warsha Tanzania, kuhusu masuala ya utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nina malengo kadhaa katika kufanya hivyo.
Lengo moja ni kuwapa wa-Tanzania ujuzi ambao ninaendelea kuupata huku ughaibuni, kutokana na kusoma vitabu, kuongea na watu, na kuendesha warsha kuhusu masuala niliyotaja hapo juu. Natambua umuhimu wa kutoa fursa kwa wa-Tanzania kuyaelewa masuala hayo, waweze kujizatiti kwa ushindani wa dunia ya leo. Hakuna msingi bora na imara kuliko elimu.
Lengo la pili la kuendesha warsha hizi Tanzania ni kuleta mwamko mpya katika mfumo na uendeshaji wa warsha. Kwanza, kuna mtindo wa kutegemea wafadhili. Watu wamezoea kuona warsha zikifanyika kwa kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili au taasisi fulani. Wahudhuriaji wa warsha wanategemea kulipiwa gharama za ushiriki, pamoja na posho. Vibahasha vya posho ni sehemu ya utamaduni wa warsha katika Tanzania.
Ninapinga utamaduni huu. Sitafuti wafadhili wa kulipia warsha zangu, na warsha zangu hazina posho. Badala yake, wanaohudhuria wanalipia.
Kwa mtazamo wangu, warsha ni fursa ya kujielimisha. Elimu ni mtaji mkubwa, pengine muhimu kuliko mitaji yote. Kama mtu analipia trekta limzalishie mazao shambani, kwa nini asilipie mtaji huu mkubwa kuliko yote, yaani elimu?
Huku Marekani, ninaona utaratibu huu wa kulipia warsha. Mimi mwenyewe nimeshalipia hela nyingi kuhudhuria warsha hizi. Ninajua umuhimu wake. Niligusia kidogo jambo hili katika blogu hii, nilipoongelea suala la kununua vitabu.
Ninanunua pia vitabu na kuvisoma. Kati ya vitabu nilivyonunua hivi karibuni ni Global Literacies. Kwa kusoma vitabu na kuhudhuria warsha, ninajiongezea mtaji wa elimu. Ufanisi wangu kama mtoa mada na mwendesha warsha unaendelea kuongezeka.
Katika kuendesha warsha zangu Tanzania, nataka kujenga utamaduni wa kuthamini elimu. Msimamo huu unanipa wajibu mkubwa. Nawajibika kujielimisha kwa uwezo wangu wote, ili niweze kuwa mwelimishaji bora. Ndio maana ninafanya bidii kuhudhuria warsha, kununua vitabu na kuvisoma, na pia kuendesha warsha. Ninaelimika hata ninapoendesha warsha.
Nawakaribisheni kwenye warsha zangu za mwaka huu:
Juni 12, "Culture, Globalization and Development," Meeting Point Tanga.
Julai 3, "Culture and Globalization," Arusha Community Church.
Julai 10, "Cultural Tourism," Arusha Community Church.
Natarajia kupanga warsha nyingine moja au mbili. Wasiliana nami: info@africonexion.com

Thursday, June 3, 2010
Umuhimu wa Warsha Zangu
Sijui kama kuna jambo ninaloongelea mara nyingi zaidi katika blogu hii kuliko suala la tofauti za tamaduni duniani, athari zake, na umuhimu wa kuzielewa. Ni suala muhimu sana, hasa katika dunia hii ya utandawazi.
Nimekuwa nikiendesha warsha kuhusu masuala haya huku Marekani, na miaka ya karibuni nimeanza kufanya hivyo Tanzania. Masuala haya yanaendelea kufahamika vizuri katika makampuni, mashirika,taasisi, vyuo na jumuia mbali mbali huku Marekani na sehemu zingine za ughaibuni.
Lakini haya si mambo ya ughaibuni tu, na wala pasiwe na mtu akadhani ni mambo ya ughaibuni tu. Ndio maana naendesha warsha Tanzania. Kama kuna asiyeamini hayo, napenda kuleta tangazo la ajira lilitolewa na World Food Program la Umoja wa Mataifa hapa Tanzania, kama lilivyoripotiwa katika blogu ya Michuzi. Bofya hapa.
Kigezo cha ufahamu wa tamaduni tofauti, ufahamu wa namna ya kushughulika na watu wa tamaduni mbali mbali, kimesisitizwa kama sifa mojawapo ambayo mwomba ajira anatakiwa awe nayo. Watu waliohudhuria warsha zangu wanafahamu kuwa hapo ndipo kwenye msisitizo wa warsha zangu. Warsha zangu hazina mbwembwe wala madoido. Ni darasa, kama inavyoonekana hapa, hapa, na hapa.
Nimefurahi kuona tangazo hili la World Food Program, hasa kwa kuwa zimebaki siku chache tu kabla sijasafiri kuelekea Tanzania, ambako nitaendesha tena warsha. Kitu kimoja kinachotajirisha warsha hizi na kuzipa umuhimu wa pekee ni kuwa washiriki wanachangia uzoefu wao katika kuhusiana na watu wa tamaduni mbali mbali, sehemu zao za kazi au katika shughuli zingine. Hapo najifunza mengi, na natambua umuhimu wake. Warsha yangu ya kwanza ni tarehe 12 Juni, mjini Tanga, kama nilivyoeleza hapa.
Kwa taarifa zaidi, wasiliana nami: info@africonexion.com

Saturday, May 8, 2010
Tamaduni Zinapogongana
Yeyote anayefuatilia blogu zangu na maandishi mengine ataona kuwa ninashughulika sana na masuala ya tofauti za tamaduni hapa duniani. Ninatoa ushauri kwa taasisi, vyuo, makampuni, na watu binafsi kuhusu masuala hayo. Ninaendesha warsha hapa Marekani na Tanzania, na ninapangia kufanya hivyo katika nchi zingine za Afrika na duniani kwa ujumla.
Haya ninayoongelea si mambo ya kinadharia tu wala ya kuyafanyia mchezo. Yasipoeleweka na kushughulikiwa ipasavyo, yanaweza kuwa na athari kubwa katika jamii na katika dunia yetu. Mifano ni mingi, nami naitaja katika warsha zangu.
Napenda kuongelea kisa kimoja kilichosababisha niitwe kwenye mji wa Faribault, Minnesota, katikati ya mwezi Aprili mwaka huu, kutatua mgogoro uliokuwa unafukuta baina ya wa-Marekani ambao ni wafanyabiashara katika mji ule na wa-Somali ambao wamehamia katika mji ule, wengi wao wakiwa ni wakimbizi.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro kati ya jamii hizi mbili. Wa-Somali, kama ilivyo kwetu Afrika wana jadi ya kuwa wanapokutana na wenzao njiani, mitaani, au popote pale wanasimama na kuongea, aghalabu kwa muda mrefu, hata kama ni kwenye sehemu wanayopita watu. Vikundi hivi vya wa-Somali vimesababisha wafanyabiashara kupata hasara, kwani wateja wao wanaogopa. Hii ni hali halisi ya Marekani, kufuatana na historia ya mahusiano baina ya Wamarekani wazungu na Wamarekani weusi, pia taratibu zao za kutoziba njia.
Wasomali wa Faribault hawakuwa na fununu kuwa mila na desturi zao haziendani na mila na desturi za hapa Marekani. Kuziba njia, kama tunavyofanya Afrika wakati tunapokutana na kuongea na wenzetu, hairuhusiwi hapa Marekani.
Kutokana na hali hiyo, rais wa wafanyabiashara wa Faribault, Mama Kymn Anderson, akishirikiana na taasisi ya Welcome Center, walifanya mpango wa kunialika nikaongee na hao wa-Marekani na wa-Somali, tarehe 15 Aprili. Kwa wiki kadhaa waandaaji walinipa fununu kuhusu suala lililokuwa linaukabili mji wao nami nilijiwa na mawazo mengi, kwani halikuwa suala rahisi. Katika kulitafakari na kujiandaa nilipatwa na mawazo mengi, na hata niliandika ujumbe kwenye blogu yangu ya ki-Ingereza. Bofya hapa.
Siku iliwadia, nami nilienda Faribault. Tulikutana katika ukumbi wa maktaba ya Faribault. Walikuwepo watu zaidi ya ishirini, wawakilishi wa pande zote mbili. Sikuona nyuso za furaha, kutokana na hali ya mgogoro. Niliona niko katika mtihani. Nilijitahidi nilivyoweza katika hotuba yangu, na mambo yalienda vizuri. Bofya hapa.
Kwa kutambua kuwa hili lilikuwa suala linalohusu wa-Marekani na wa-Afrika, Mama Anderson alikuwa ameniagiza nichukue nakala za kitabu changu cha Africans and Americans, ambacho alishakisoma. Nilichukua nakala kadhaa ambazo, baada ya mazungumzo yangu, zilinunuliwa upesi na wengine wakakosa. Uamuzi uliofikiwa ni kuwa tutaendeleza utaratibu huu wa mazungumzo siku za usoni.
Kwa wale walioko Tanzania, nitaendesha tena warsha kadhaa mwaka huu, kuhusu utamaduni na utandawazi. Warsha ya kwanza itafanyika Tanga, tarehe 12 Juni. Kwa taarifa zaidi, bofya hapa.

Thursday, April 1, 2010
Warsha Zangu Tanzania, 2010
Niko katika maandalizi ya kuendesha warsha Tanzania, kama nilivyofanya mwaka jana na mwaka juzi. Kwa taarifa fupi, bofya hapa na hapa. Maandalizi yanakwenda vizuri, na hadi leo, kwa kutumia mawasiliano ya barua pepe, nimeshapanga ratiba hii:
Juni 12, 2010, warsha kuhusu, "Culture and Globalization," Meeting Point Tanga.
Julai 3, 2010, warsha kuhusu, "Culture and Globalization," Arusha Community Church.
Julai 10, 2010, warsha kuhusu, "Cultural Tourism," Arusha Community Church.
Niko katika mawasiliano na wadau wa Zanzibar, ili kuandaa warsha Visiwani. Taarifa nitaleta baadaye. Nafanya mpango wa warsha Dar es Salaam pia.
Warsha hizi zitaendeshwa kwa ki=Ingereza, kama siku zilizopita, kwa sababu wahudhuriaji huwa wa mataifa mbali mbali. Yeyote anakaribishwa.
Nina mengi yanayonisukuma kuja kuendesha warsha hizi Tanzania. Kadiri ninavyotoa mihadhara huku ughaibuni, katika vyuo, taasisi, makampuni, na mashirika kuhusu athari za tofauti za tamaduni duniani, nazidi kutambua kuwa waTanzania tutapata shida katika dunia hii ya utandawazi kama hatufanyi juhudi ya kujielimisha na kujiandaa.
Haijalishi kama wewe ni mwanadiplomasia, mfanyabiashara, mwanafunzi, mmiliki wa shule, mfanya kazi katika kampuni, au mtafiti. Katika dunia ya leo, hatuwezi kukwepa kukumbana na watu wa tamaduni tofauti, na bila kuelewana, tutaishia katika migogoro na kuyumba au kuharibika kwa yale tunayotegemea kuyafanikisha. Mifano ni mingi duniani kote, na nchi mwetu pia.
Warsha hizi ni fursa si tu ya kunisikiliza mimi na kuniuliza masuali, bali pia fursa ya washiriki kufahamiana. Kwa hivi, nawahimiza wahudhuriaji kuja na taarifa za shughuli zao, iwe ni biashara, au shughuli nyingine yoyote. Ni njia nzuri ya kujitangaza na kujijengea mtandao. Nami nitaleta taarifa zangu, pamoja na vitabu vyangu.
Ninafanyia warsha hizi Tanzania, kama kianzio tu, lakini mkakati wangu ni kuzipeleka katika nchi zingine za jirani, nikianzia na Kenya. Hatimaye nataka kufanya warsha hizi katika nchi mbali mbali za Afrika na kwingineko, kwani elimu haijui mipaka ya nchi.
Kwa taarifa zaidi, na pia kujisajili kwa warsha, andika ujumbe: info@africonexion.com. Kama unataka kununua vitabu vyangu Tanzania, piga simu 0717 413 073 au 0754 888 647.

Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanza...