Thursday, May 22, 2014

Ninablogu kwa Faida Yangu Mwenyewe

Ninablogu ili kuhifadhi kumbukumbu, fikra, na hisia zangu. Ninafurahi kufanya hivyo. Hadi sasa, nimehifadhi mengi sana ambayo bila shaka ningekuwa nimeyasahau.

Kila mtu ana mawazo, fikra na hisia. Ni mambo binafsi. Hapa ni tofauti na darasani kwangu au katika  majarida na vitabu vya taaluma. Sina mpango wa kuifanya blogu hii iwe sawa na darasa langu la chuo kikuu, au jarida la kitaaluma.

Ikitokea nimeandika humu ujumbe wenye kugusia taaluma, hiyo ni sawa, lakini, kama ninavyosema blogu hii inanisaidia mimi kuhifadhi mambo yangu, mengine yakiwa ni mambo binafsi.

Mara kwa mara naonglea vitabu. Ninapofanya hivyo najitunzia kumbukumbu kuhusu vitabu hivyo. Sijui kama kuna yeyote anayepata dukuduku na hamasa ya kuvitafuta na kuvisoma. Huo ni uamuzi wa mtu. Wako watu ambao hawana hamu na kitu kinachoitwa kitabu. Lakini mimi sitachoka kuandika kuhusu vitabu, kwani navienzi na kuvipenda sana. Ninafurahi kujitunzia habari za vitabu hivyo, ingawaje kwa ufupi.

2 comments:

Anonymous said...

profesa Mbele Mie naona mashule ya Tanzania ungewaandikia watoto vitabu au makala za ushauri wa vijana wengi wa kitanzania, Vijana na Watoto wengi sasa hivi ni whatsaap,games za michezo bila kusoma vitabu vya game zinatengenezwa vipi au Apps zinatengenezwa vipi? Na Vijana wengi wanatumia muda wao Baa kunywa sana kuliko kula au kunywa maziwa na muda mwingi wa Baa wanajikuta kulala ni muda mchache je Tanzania inakosea wapi? Na wengi wa hivi tukitoa watoto ni vijana waliosoma mpaka degree tunaona Tanzania inaendekeza sana Ngono, na matangazo na sehemu za Bia ni nyingi kuliko vituo vya watoto kujisomea au vijana kukutana elimu au waunde kitu gani wengi hukutana Baa ndio kuongelea File gani Lipite ndio sana je Serikali inaendekeza ujinga sana kufanywa kuliko ya maana? Mie bado nashangaa vipi Miss Tanzania iwe kipaumbele vipi vipindi Kama Bibi Bomba vinaachwa kufanywa kazi vipi waganga wakienyeji wa kichwawi na kitapeli wanaawachiwa Kuwa na vibali bila kuvunjiwa kazi zao? Wapi tunakosea? Na kwanini watu wadini zote wanaonekana sio wamaana wanaosema ukweli kusaidia jamii? Na ma profesa Kama nyie blog zenu zingefaa kukemea Blog za ngono Tanzania zimezidi vijana nao wanajianika ovyo kwenye miaka 20 ijayo tutakuwa na viongozi gani? profesa Mbele anza kumtumia muda kuongea na vijana rusha kwa kina michuzi blog na Blog zenye Nguvu kazi yako nzuri, kijana wa Kizaramo.

Mbele said...

Shukrani sana kwa mawazo yako mengi. Tunakubaliana kuhusu haya matatizo unayoelezea. Hili tunaloliita Taifa la kesho ni janga, kwa sababu kwa ujumla, vijana wenyewe hawajitambui, wala hawajizatiti katika kukabiliana na dunia ya kesho. Ingeleta matumaini iwapo wangekuwa wanajibidisha katika kujielimisha.

Kuhusu mchango wangu, ninaamini ninajitahidi kadiri niwezavyo kuwamegea wengine kile ninachojua au kuwazia, katika Nyanja ambazo naamini nina kiasi Fulani cha ufahamu, kama vile fasihi, utamaqduni, siasa, na hata uchumi. Ninaandika makala, hata kwa ki-Swahili, na pia

Mfano moja ni kijitabu kiitwacho CHANGAMOto, ambacho kinaonekana kwenye matangazo hapo kulia. Nilikuwaq nimeulizwa na watu kwa nini siandiki kwa ki-Swahili. Hapo nilijizatiti, nikaandika makala nyingi kwa ki-Swahili, ambazo hatimaye nilizikusanya zikawa kitabu cha CHANGAMOTO.

Ingawa nilisema tena na tena katika blogu hii kuwa kitabu hiki kinapatikana Dar es Salaam, zaidi ya mtandaoni, sijaona dalili kama kuna yeyote anayekitafuta au kukisoma, ukiachilia mbali vijana Fulani wa kijiji cha Msoga, Bagamoyo, ambao mojawao aliniambia kuwa wanakipenda kwa vile kinawapa changamoto ya fikra na mitazamo ya masuala mbali mbali.

Tuna tatizo kuwa utamaduni wa kujisomea vitabu hauonekani Tanzania, isipokuwa kwa wale wanaowania kufanya mitihani, yaani wanafunzi. Hili ni janga la Taifa.

Kuhusu masuala haya unayoongelea, hatuna uongozi Tanzania. Ni ubabaishaji tu, kuanzia kwa hao tunaowaita viongozi, hadi hao vijana. Sidhani kama tuna "kiongozi" anayeonyesha mfano wa kusoma na anahimiza usomaji wa vitabu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...