Sunday, May 25, 2014

Nyumbani mwa Mzee Patrick Hemingway Mjini Craig, Montana.

Hapa ni katika nyumba ya Mzee Patrick Hemingway katika mji mdogo wa Craig, Montana.

Picha hii nilipiga Tarehe 28 mwezi Aprili. Hapo mbele ya Mzee Hemingway kuna vitabu vyangu vilivyoandikwa na Ernest Hemingway, au vilivyoandika juu yake. Nilimpa Mzee Patrick Hemingway avisaini, naye alifanya hivyo bila kusita.

Nina vitabu vingi vya Hemingway au vile vilivyoandikwa juu yake. Siku tulipomtembelea Mzee Patrick Hemingway nilichukua hivi vichache tu, ambavyo vimechapishwa miaka ya karibuni.

Pembani mwa vitabu vyangu hivi vikubwa, kuna pia nakala nne za kitabu cha True at First Light. Mzee Patrick Hemingway alihariri mswada mkubwa wa Ernest Hemingway kuhusu safari na kukaa kwake Kenya, tangu 1953-54. Mzee Hemingway alituzawadia nakala za kitabu hiki. Siku nyingine, panapo majaliwa, nitaandika zaidi kuhusu zawadi hiyo.

Vile vile, hapo hapo mezani, kinaonekana kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilimchukulia nakala Mzee Hemingway, kutokana na ombi lake. Mzee Hemingway anakipenda kitabu hiki, na ameshaniambia, kwa nyakati tofauti, kuwa ni kitabu kilichoandikwa vizuri.

Kauli yake hii, tangu aliponiambia mara ya kwanza, ilinipa furaha kubwa. Siku hiyo nilipopiga picha hii, Mzee Hemingway alifungua kitabu hiki, akatusomea sehemu mojawapo, ukurasa 89, ambapo nimemnukuu Ronald Ngala akiongelea desturi za Wagiriama. Nilijisikia vizuri sana Mzee Hemingway alipendezwa na tafsiri yangu ya maneno hayo ya Ronald Ngala.

Huyu mama anayeonekana pichani ni Mama Carol, mke wa Mzee Hemingway. Aliwahi kuwa profesa, na pia ni mwandishi wa tamthilia.

Hizo ni baadhi ya kumbukumbu zangu za safari yetu ya Montana, kuonana na Mzee Patrick Hemingway. Naziandika kumbukumbu hizi kwa ajili yangu mwenyewe. Sina deni na mtu, wala siwajibiki kwa yeyote.

No comments: