Tuesday, April 30, 2013

Safari ya Montana Kumwona Mzee Patrick Hemingway

Juzi nilileta ujumbe kuwa nimepata fursa ya kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye bado hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Kwangu kama mtafiti na mwalimu, tukio hili ni la kukumbukwa daima. Hapa napenda tu kuongelea mipango ya safari ilivyokuwa.

Nilipokuwa Tanzania mwezi Januari na wanafunzi nikiwafundisha kozi kuhusu Ernest Hemingway, niliwaambia wanafunzi kuwa mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway nina mawasiliano naye kwa simu, na kwamba ni mzee wa miaka 85. Niliwaambia pia kuwa ninapangia kwenda kuonana naye. Mwanafunzi mmoja ambaye amekuwa akirekodi kozi yangu na habari zinazohusika alisema atapenda tutanguzane kwenye hiyo safari. Mwanafunzi mwingine alisema kuwa ana hakika kuwa baba yake atatupeleka kwa ndege yake.

Baada ya kurejea Marekani, tuliendelea na mipango yetu. Niliwasiliana kwa karibu na Mzee Hemingway na huyu kijana wa mwenye ndege aliwasiliana na baba yake, tukakubaliana tufanye safari tarehe 27 wikiendi iliyopita.

Mzee mwenye ndege alikuja kutoka kwao Ohio na rubani wake, nasi tukajumuika nao katika uwanja mdogo wa Lakeville, inavyoonekana pichani kushoto. Kulia kabisa ni mzee mwenye ndege. Kijana wake ni huyu aliyevaa kaptula. Kijana huyu na huyu mwenzake mrefu kabisa ndio wale walifika Tanzania kwenye kozi yangu.

Mzee huyu ni msomi na msomaji wa vitabu. Ni msomaji makini wa mwandishi Hemingway. Wakati nilipokuwa nafundisha kozi yangu kule Tanzania, alitafuta silabasi kutoka chuoni kwangu akafuatilia kozi nzima.

Mzee Hemingway alikuwa ametushauri tukatue uwanja wa Great Falls, Montana. Safari ilichukua yapata masaa matatu, baada ya kutua kwenye mji wa Bismarck, Dakota ya Kaskazini, kwa ajili ya kupata mafuta ya ndege. Hali ya hewa ilikuwa nzuri njia nzima.

Baada ya kufika Great Falls, tulichukua gari tukaenda kwenye mji mdogo wa Craig, ambako Mzee Hemingway alisema angekuwepo.
Tulipata msisimko mkubwa tulipomwona anatungoja nje ya nyumba yake. Nilimwomba hapo hapo tupige picha, kabla hatujaingia ndani kwa mazungumzo, ambayo nitaelezea baadaye. Nimeandika ujumbe huu kwa lengo la kujitunzia kumbukumbu. Mengine ya msingi, yale tuliyojifunza kutoka kwa Mzee Hemingway, yatakuja siku za usoni.

Sunday, April 28, 2013

Hatimaye, Nimeonana na Mzee Patrick Hemingway

Nimerejea jioni kutoka Montana, ambako nilikwenda jana, kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtu maarufu sana. Ni yeye pekee ndiye bado hai kati ya watoto wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway.

Mwandishi Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 jirani na Chicago na kufariki 1961, ni maarufu duniani kote. Kwa miaka yapata kumi, nimevutiwa na jinsi alivyoandika kuhusu Afrika, kutokana na kutembelea na kuishi Afrika Mashariki, mwaka 1933-34, na mwaka 1953-54. Ninasoma na kufundisha maandishi ya Hemingway, kama nilivyoandika hapa, na hapa.

Kwa muda mrefu nilitaka niwasiliane na Mzee Patrick Hemingway, ambaye ni mtoto pekee wa Hemingway aliyebaki. Nilifahamu kuwa aliishi Tanzania miaka yapata 25. Moja ya shughuli alizofanya ni kufundisha katika chuo cha Mweka. Nilisoma sana maandishi yake na kusikiliza mazungumzo yake ambayo yako mtandaoni.

Nilijua kuwa huyu ni hazina kubwa kwa yeyote anayefuatilia maandishi na maisha ya Ernest Hemingway. Siku moja, miaka yapata miwili iliyopita, nilijipa moyo nikampigia simu. Nilifurahi jinsi alivyonifanyia ukarimu, tukaongea sana. Kuanzia hapo, nimeongea naye mara kwa mara.

Hatimaye, jana nilisafiri hadi Montana, ambako tumepata fursa ya kuongea kwa masaa mengi, jana na leo. Nimefurahi kwa namna ambayo siwezi hata kuelezea. Nategemea kuandika taarifa mbali mbali za ziara hii siku zijazo.

Tuesday, April 23, 2013

Nimepata Ugeni Leo

Leo nilitembelewa na wageni ambao naonekana nao katika picha hii kushoto. Kuanzia kushoto ni Mzee Teri, Mrs Teri, mimi, Profesa Ann Wagner, Bill Green.

Bill Green, m-Marekani Mweusi kutoka South Central Los Angeles, akuwa afisa mojawapo wa masuala ya wanafunzi hapa Chuoni St. Olaf, hadi mwaka jana. Ananifahamu vizuri kutokana na miaka mingi tuliyofanya kazi pamoja hapa St. Olaf, na anafahamu shughuli zangu za kuwasaidia wa-Marekani wanaoenda Afrika.

Ni Bill Green ndiye aliyeandaa mpango wa mkutano wa leo. Aliniletea ujumbe wiki chache zilizopita kwamba ana watu ambao wanahusika na Tanzania na angependa kuwaleta Chuoni St. Olaf tuweze kuongea.

Tulivyokutana tu leo, Mzee na Mama Teri wamenikumbusha kuwa niliwahi kutembelea na kutoka mhadhara katika kanisa lao la Hossana, mjini Lakeville. Wana nakala ya vitabu vyangu: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales. Nami nimekumbuka kuwa ni kweli niliwahi kwenda kwenye kanisa hilo, kuchangia maandalizi ya waumini waliokuwa njiani kwenda Tanzania. Mada yangu ilikuwa tofauti za tamaduni, na watu walijipatia vitabu vyangu siku hiyo.

Mzee Teri na Mama Teri wameshafika Tanzania mara nyingi. Wanaifahamu sana Karatu.Wanamfahamu na wanamheshimu Dr. Wilbroad Slaa. Profesa Ann Wagner alifundisha hapa St. Olaf hadi alipostaafu miaka karibu ishirini iliyopita

Maongezi yetu ya leo yalihusu Tanzania, hasa masuala ya elimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo. Hao wazee wanajishughulisha na masuala ya kuchangia Tanzania. Leo tuliongelea zaidi elimu. Tulitathmini elimu  ipi ni sahihi kwa vijana wa Tanzania: wasome Tanzania au wasome nje ya nchi, kama vile Marekani? Faida au hasara zake ni zipi?

Monday, April 22, 2013

Bunge Modern Taarab Kuzindua Albamu ya "FUCK YOU!"

CHANZO: Mwandishi Wetu

Mke_wa_Rais_Mama_Salma_Kikwete_akimnadi_mgombea_CCM jimbo_la_Kigoma_Mjini_Peter_Serukamba_5-10-2010             Bungeni,Dadoma

KITENDO cha wabunge wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania kugeuza jengo hilo lenye heshma ndani ya nchi kuwa jukwaa la malumbano na kuporomoshea matusi ya nguoni imewafanya watanzania kutokuwa na heshma tena na wabunge wao.
Bunge hilo ni moja ya mihimiri mikubwa Tanzania  iliyopewa heshma ya kutunga sheria mbalimbali ya za nchi pamoja na kupanga maisha ya watanzania kwa mwaka mzima kutokana na bajeti za serikali.
Matusi ya wabunge hao ndiyo iliyosababisha wakakumbwa na kashfa na dharau kila mahali huku wakitugiwa mashahiri mbalimbali na kupewa majina mbalimbali ya ajabu.
Moja dhihaka na dharau walizojizolea kutoka kwa wapikura wao ni pamoja kutungiwa bendi mahiri ya taarabu inayoitwa BUNGE MODERN TAARAB bendi hii iliyoanza kutoa matangazo ya kufanya uzinduzi wake wa kwanza inawakaribisha mashabiki wote kwenye uzinduzi wa albamu yao mpya kabisa iliyobeba jina la 'FUCK YOU'!.
NYIMBO hizi ambazo zipo katika mtindo wa mipasho, zitazinduliwa hivi karibuni kwenye ukumbi mmoja huko Dodoma! Albamu hiyo ina nyimbo tano na watunzi kwenye mabano!
1 Mkuki Kwa Nguruwe---(Anna Makinda)
2 Mimba zisizotarajiwa (Livingstone Lusinde)
3 Naongea na Mbwa Siongei na mwenye Mbwa (Juma Nkamia)
4 Mkuki kwa Nguruwe remix (Job Ndugai)
5 Come on fuck you (Peter Serukamba)
Wahi uzinduzi na nunua nakala yako halisi!!!!
Mbali na bendi hiyo pia kuna filamu mahiri iliyochezwa na wasanii mahiri waliosafiri kwa pesa za wananchi hadi  jijini Dodoma na kurekodi filamu hiyo katika Ukimbi wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania huku ikiongozwa na msanii mkongwe na mahiri wa sanaa ya muziki nchini Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr II ama Sugu. Filamu hii itajia kesho hapahapa habarimpya.com usikose, habarimpya.com pia inawaruhusu wasomaji wake kuchati huku wakisoma habari ndani website kwani haina ya haja ya kurudi Facebook kwa ajili ya kuchati.

Saturday, April 20, 2013

Binti Zangu Wamewajibika Leo Minneapolis

Leo binti zangu wawili wameshiriki mbio za kuchangia taasisi ya mafunzo iitwayo ThreSixty Journalism. Mbio hizi zimefanyika asuhubi leo mjini Minneapolis.

Mwaka 2009, binti huyu mwenye kitambaa kichwani alichaguliwa kusoma katika taasisi hiyo. Huchaguliwa vijana kadhaa kutoka shule mbali mbali. Wakiwa kwenye taasisi hiyo husomea masuala ya uandishi katika magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla. Ni fursa inayothaminiwa sana. Vijana hupata mafunzo bora kitaaluma, na pia fursa ya kukutana na waandishi na wanahabari maarufu. Kama sehemu ya mazoezi, binti yangu alipelekwa kwenye jamii ya wa-Somali hapa Minneapolis kufanya nao mahojiano, akachapisha makala hii hapa. Makala yake hiyo, na nyingine, zilichapishwa pia katika Twin Cities Daily Planet na Star Tribune, ambayo ni magazeti maarufu hapa Minnesota.

Nimefurahi binti zangu wamechukua uamuzi kulipia ushiriki wa mbio hizo, kuchangia taasisi hiyo. Napenda waendelee katika moyo huo.

Thursday, April 18, 2013

Mlima Longido, Tanzania

 Hakuna mtu ambaye anaweza kuzitembelea au kuziona sehemu zote za nchi yetu au nchi yoyote nyingine. Hii ni sababu moja ya mimi kuweka kwenye blogu hii picha za sehemu mbali mbali. Nataka wengine nao wafaidike angalau kidogo na kupanua ufahamu wao. Yawezekana, pia, wakahamasika kwenda kujionea.

Leo naleta picha za mlima Longido. Mlima huu uko Tanzania ya kaskazini, baina ya mji wa Longido na Namanga. Unaonekana vizuri kabisa kutoka kwenye barabara itokayo Arusha kwenda Namanga. Picha hizi nilizipiga mwishoni mwa Januari, mwaka huu, nikiwa safarini kutoka Namanga kwenda Longido. Baada ya kuondoka Namanga, picha ya kwanza niliyopiga ni hiyo hapa kushoto.
Muda mfupi baadaye, nilipiga picha hii inayoonekana kushoto.
 Baadaye kidogo nilipiga picha hii hapa kushoto.
Tulivyozidi kukaribia Longido, nilipiga picha hii hapa kushoto.

Nimeshauona mlima Longido mara nyingi, katika miaka zaidi ya ishirini iliyopita, wakati nikisafiri baina ya Tanzania na Kenya. Nimewahi kuutaja mlima huu katika ujumbe huu hapa.

Kitu kimoja kinachonivutia ni jinsi mlima huu unavyoonekana wakati unapoukaribia kutokea Namanga. Ile sehemu iliyochomoka inanifanya niwazie pembe ya kifaru. Picha ninayopata ndio hiyo. Lakini mwaka huu, nimetambua vizuri kwamba ile pembe ya kifaru inabadilika kabisa na kuwa mwamba unaoonekana hapa kushoto. Mwaka huu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuangalia kwa makini taswira hii na kujionea jinsi pembe ya kifaru inavyotoweka na kuwa mwamba uliosimama, ukiwa na sura tofauti.

Monday, April 15, 2013

Hawa Ndio Magaidi wa Tanzania


Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi
! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

 -----------------------------------
Makala yangu hii hapa juu nimeshaichapisha mara kadhaa katika blogu hii. Ila nimeona niilete tena. Ikumbukwe tu kwamba wakati Mwalimu alipoandika, upinzani haukuwa makini na wenye nguvu kama ilivyo leo. Nyerere angekuwa hai leo, nina hakika angeungana na CHADEMA katika kupambana na ufisadi.  Yeyote ambaye amefuatilia mawazo ya Mwalimu katika hotuba na vitabu vyake mbali mbali, atakubaliana nami kwa hilo.

Sunday, April 14, 2013

Tamko la CHADEMA Kuhusu Njama za Kukichafua

TAMKO LA CHADEMA KUHUSU NJAMA ZA KUKICHAFUA ZINAZOFANYWA NA GENGE LA VIONGOZI WAKUU WA CCM NA VYOMBO VYA DOLA, LIMETOLEWA JIJINI DAR ES SALAAM LEO, MACHI 14, 2013 NA MJUMBE WA KAMATI KUU NA MWANASHERIA WA CHAMA, MH. MABERE NYAUCHO MARANDO

Ndugu waandishi wa habari;

LEO tumewaita hapa ili kuwaomba mtufikishie ujumbe kwa Watanzania, kwamba nikiwa mwanasheria na mtu ambaye nimepata ujuzi wa kazi za ushushu, nimefanya uchunguzi matukio haya ya utekaji na utesaji na kugundua mambo mengi mno.

Uchunguzi huu nimeufanya kabla na baada ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wetu wa Ulinzi na Usalama, Willifred Muganyizi Lwakatare, ambaye hivi sasa anashitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kupanga ugaidi.

Nimefanya hivyo kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa langu na chama changu. Katika uchunguzi wangu huo, nimegundua mambo mengi ikiwamo kuwapo kwa genge la watu ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaopanga mipango hii ya kishetani na kisha kuwasingizia watu wengine.

Angalieni mfano huu: Unaoitwa na polisi na Mwigulu Nchemba, “mkanda wa Lwakatare” unadaiwa uliwasilishwa jeshi la polisi Desemba mwaka jana. Lakini jeshi hilo halikumkamata yoyote wala kumhoji, hadi pale Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alipovamiwa na kuumizwa.

Aidha, Nchemba amedai kumiliki video ile Desemba mwaka jana, lakini rekodi hiyo iliwekwa kwenye mitandao ya kijamii (YouTube na Jamii Forum) baada ya kutekwa kwa Kibanda. Hapa mtu makini anaweza kujiuliza, hiki kimelenga nini?

Kwamba genge hili la kina Nchemba na wenzake, walipanga kumteka Kibanda, wakatimiza lengo lao hilo, baadaye wakaingia kwenye plani B ya kutaka kuihusisha Chadema. Wakamtumia Ludovick Joseph Rwezahula ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, kufanikisha mkakati wao huu wa kishetani.

Ndugu waandishi wa habari;

Huu ni mchezo mchafu na wahatari mno ambao kwa vyovyote vile, haupaswi kuvumiliwa. Kuanzia sasa nimeamua kwa dhati kabisa, kukomesha mchezo huu ambao unahatarisha uhai wa taifa letu.

Kwa kuanzia, kesho Jumatatu, nitaongoza jopo la mawakili sita wa Chadema kumtetea Bw. Lwakatare. Wenzangu wengine katika kesi hii, ni Profesa Abdallah Safari, Tundu Lissu, Edson Mbogoro, Peter Kibatara na Nyaronyo Kicheere. Huko mbele tutaongeza mawakili wengine, akiwamo mmoja anayewekwa na familia ya Lwakatare.

Ndugu waandishi wa habari;

Mnaweza kujiuliza, kwa nini Chadema kimechukua uamuzi huu wa kuweka kundi kubwa la wanasheria katika kesi hii ya Lwakatare? Jibu ni kwamba tumegundua kuwa kesi hii imefunguliwa kwa lengo maalum la kuidhoofisha Chadema na kuinusuru CCM ambayo inakabiliwa na dhahama ya kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na kushamiri kwa makundi.

Hivyo wameamfungulia kesi Lwakatare, kwa lengo la kutaka kuaminisha umma kuwa Chadema ni chama cha magaidi, kinapanga ugaidi na hivyo kichukiwe. Hilo ndilo lengo lao. Basi!

Ndugu waandishi wa habari;

Pili, nitakwenda mahakamani kuwasilisha ombi maalum la kuomba amri ya mahakama kuagiza makampuni ya simu za mkononi kuwasilisha mahakamani statement za simu za watu kumi (10) ili kusaidia mahakama kutenda haki na jamii kujua ukweli wa mambo haya.

Watu ambao nitaomba mahakama itoe amri ya kuletwa taarifa zao simu

na meseji (sms) ni Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini (TISS), Jack Zoka, anayetumia simu Na. 255756809535, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Lameck Nchemba, anayetumia simu tano zikiwamo 0754 008888, 0757 946223, 0714 008888 na 0787 513446 na Ludovick Joseph Rwezahula, ambaye simu zake ni,0715 927100 na 0753 927 100.

Mwingine ambaye mawasiliano yake yanahitajika, ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, anayetumia simu Na. 0754 003388, Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Mwananchi, Dennis Msaky anayetumia simu mbili, 0655 331010 na 0764 331010 na Bw. Sinbad Mwagha, ambaye ni afisa wa idara ya usalama wa taifa, anayetumia simu 0754 006355.

Wengine, ni Bw. Shaali Ali, afisa mwinge wa usalama wa taifa anayetumia simu Na. 0716990099, Saumu K. Malungu, mwenye kutumia simu 0719 541 434 na 0789 614 629, simu mbili zinazotumiwa na mtuhumiwa mkuu wa utekaji wa Dk. Steven Ulimboka, Bw. Ramadhani Abeid Igondo ikiwamo 0713 760 473, simu za Bw. Ridhiwani Kikwete ambazo ni 0754 566299, 0784 566 299, simu ya Dr. Steven Ulimboka, ambayo ni 0713 0713 731 610, pamoja na simu zote tatu za Willifred Lwakatare, ambazo ni 0786 774697, 0713 237869 na 0758 417169.

Ndugu waandishi wa habari;

Mtu mwingine muhimu nitakayeomba mahakama itoe amri ya kutolewa kwa taarifa zake, ni mwandishi wa habari na mpigapicha wa magazeti ya serikali, Muhidini Issa Michuzi. Mwandani huyu wa Ikulu, ndiye aliyeandika ujumbe kwa njia ya emeili kuipongeza ofisi binafsi ya rais (OBR) na usalama wa taifa kwa kupata video ya Lwakatare.

Pongezi za Michuzi kwa TISS ndizo zinanisukuma kuiomba mahakama kuagiza kupatikana taarifa zake. Michuzi anaipongeza TISS kwa kuibua njama za wahalifu, lakini mimi ninajua TISS ikipata njama za aina hiyo haraka inapeleka ushahidi polisi, lakini huu wa Lwakatare ulipelekwa Youtube, badala ya kwenye vyombo vya sheria.

Maneno ya Michuzi kwamba ni TISS imeibua hiyo video yanathibitisha ushiriki wa TISS kwenye mchezo huo mchafu, na kwamba Chadema kinajua kuwa Michuzi alishirikiana na watu wa usalama wa taifa katika kazi hiyo chafu. Software za video (editing) walizotumia zilitoka kwake. Fedha ya kuandaa hiyo video zilitoka usalama na Ikulu. Tunajua kuwa wale vijana wa Ada Estate na yule jamaa anayempelekea kigogo wa Jamii Forum, walilalamika sana kwa mmoja wa wamiliki wa JF.

Ndugu waandishi wa habari;

Chadema kinajua kuwa mmoja wa watuhumiwa hawa, Mwigulu Nchemba anafanya mipango na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom ili kumsaidia kufuta taarifa zake. Nachukua nafasi hii, kuionya kampuni hiyo kuacha kucheza mchezo huo kwa kuwa ni kinyume cha sheria za mamlaka ya mawasiliano (TCRA).

Tunahitaji mawasiliano haya kwa kuwa Mwigulu – zinaonyesha mtuhumiwa huyo akifanya mawasiliano mfululizo na Ludovick, yakiwamo yale ya tarehe 4 Machi 2013. Hii ilikuwa siku moja kabla ya Kibanda kutekwa.

Ndugu waandishi wa habari;

Hawa niliowataja ni watu muhimu sana katika upangaji wa mkakati wa utengenezaji wa video ya Lwakatare na vitendo vya kihalifu vya utekwaji wa Kibanda na tukio la kutekwa na kisha kutupwa msutuni kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dr. Steven Ulimboka.

Kwa mfano, simu ya Mwigullu Nchemba, namba 0714 008888, 0756 008888 na 0757 946223, zimefanya mawasiliano mara kadhaa na Ludovick Joseph, Saumu K. Malungu, Jack Zoka, Ali Shaali na Ramadhani Ighondo. Mawasiliano hayo yalifanyika katika kipindi ambacho mgomo wa madaktari ulishamiri; baadaye yakarudi tena kati ya 26 Desemba mwaka jana na 15 Machi mwaka huu.

Miongoni mwa mawasiliano ambayo tunaona yanahusika na ujambazi huu, ni yale ya 28 Desemba, siku ambayo mkanda wa Lwakatare umerekodiwa; tarehe 4 hadi 6 Machi 2013, siku moja kabla ya Kibanda kutekwa na yale ya usiku wa manane (saa 8:17) wa 13 Machi 2013, ambako mchana uliofuata Lwakatare alikamatwa.

Huyu Mwagha ndiye aliyekuwa anatumika kuwasiliana na Saumu Malungu, ambaye tulimtaja kuwa ndiye aliyekuwa amepewa kazi na Mwigulu na usalama wa taifa, kurubuni vijana wetu kwa fedha ili kutoa ushahidi wa uongo juu ya video ya Lwakatare.

Vilevile, mawasiliano ya Mwiguluna Mwagha, katika kipindi hicho nayo tunayahitaji. Kwa sababu, huyu Mwagha anayetumia simu 0754006355, mbali na kuwasiliana na Mwigulu, ndiye aliyekuwa anawasiliana na mmoja wa waliomteka Ulimboka; na ndiye aliyewasiliana na Saumu kati ya 20Januari na Machi 6 mwaka huu.

Ndugu waandishi wa habari;

Ludovick alifanya mawasiliano ya mwisho na Joyece Agustine, ambaye anatumia simu Na. 0717 559210, mawasiliano ambayo yalifanyika saa 5:13 usiku. Hiyo ndiyo ilikuwa simu yake ya mwisho usiku huo; katika siku hiyo Ludovick aliwasilisna na Joyce mara tisa kuanzia saa 12: 54 asubuhi.

Kwa mujibu wa taarifa za kwenye mtandao wa Jamii Forum, ambako video ya Lwakatare ilitumwa, Ludovick alikamatwa Machi 15 mwaka huu. Hata hivyo, rekodi katika simu yake Na. 0715 927100 inaoyesha 17 Machi Ludovick alifanya mawasiliano na Joyce Augustino. Mawasiliano hayo yalifanyika saa 8: 9 usiku, wakati inadaiwa na polisi alishakamatwa.

Naye mhariri wa Mwananchi, Bw. Msaky ambaye anatajwa kutaka kutekwa na Ludovick na Lwakatare, amekuwa na mawasiliano kadhaa na Ludovick – mtu anayepanga kumteka. Ludovick na Msaky walifanya mawasiliano mfululizo kati 27 Desema 2012, siku moja kabla ya video ya Lwakatare haijarekodiwa na 7 Machi siku moja baada ya Kibanda kutekwa.

Msacky alitumia simu zake hizo mbili (0764 331010 na 0655 331010) kuwasiliana na Ludovick, huku Ludovick akitumia 0753927100. Mawasiliano ya 31 Desemba yalifanyika Ludovick akiwa Tegeta, jijini Dar es Salaam. Mawakala hawa wawili wa usalama wa taifa (Ludovick na Msaky), walikutana 31 Desemba 2012, katika hoteli ya Tamal, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ndugu waandishi wa habari;

Baada ya kupitia taarifa hizi za mawasiliano ya simu za Mwigulu Nchemba, Ludovick Joseph, Ramadhani Ighondo na Saumu Malungu tumegundua yafuatayo: Kwamba, Ramadhani Ighondo, amefanya mawasiliano mara nyingi na Mwigulu, Mwagha na Zoka; naye Mwagha amefanya mawasiliano na Mwigulu na Saumu; naye Saumu amefanya mawasiliano na Mwagha, Mwiguluna Shaali Ali, ambaye ni afisa usalama wa taifa.

Tumegundua vilevile, kuwapo mawasiliano kadhaa kati ya Ludovick na Msaky; Ludovick na Mwigulu; Msaky na Nchimbi; Msaki na Mwagha, Samu na Mwagha na Ramadhani Ighondo Abeid, anayetuhumiwa kumteka Dk. Ulimboka na Mwanga na Mwigullu.

Tumegundua pia kuwapo mawasiliano kati ya Ulimboka na Ramadhani; Zoka na Ighondo na Ridhiwani na Ighondo. Mawasiliano haya yalifanywa mfululizo usiku wa Juni 2012 siku ambayo Dk. Ulimboka alitekwa.

Tumepata kufahamu pia kwamba baadhi ya watu waliotajwa na gazeti la MwanaHALISI kuwa waliwasiliana na Ighondo usiku wa Juni 26, mwaka 2012, wamefanya mawasiliano pia na Mwigulu, Mwagha na Shaali Ali.

Ndugu waandishi wa habari;

Mwagha ni afisa usalama wa taifa anayefanyakazi makao makuu ya idara hiyo. Ndiye yule anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga wanasiasa wa CCM na upinzani.Ni Mwagha anayepanga wabunge na kuwapanga waongee nini kwa maslahi ya CCM. Ushenzi wote anaoongea Mwighulu bungeni, hupewa na Mwagha kwa maelekezo ya Jack Zoka.

Naye Shaali ndiye aliyekutana na afisa wetu wa usalama, Ahmed Sabula na mwenzake, Machi 29 mwaka huu katika hoteli ya See Cliff jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo kati ya Sabula, kijana wetu wa usalama na afisa usalama wa serikali Bw. Shaali alitaka Sabula akubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya chama, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya Lwakatare.

Kwenye mpango huu, afisa huyo wa usalama wa taifa ambaye ninamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha Sh. milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa wiki iliyopita. Aliahidiwa pia kwamba kila nyaraka atakayopeleka atalipwa ujira.

Aidha, Sabula aliahidiwa kulipwa shilingi 500,000 (laki tano) kila mwezi; afisa wetu huyu ameripoti tukio hilo kwa viongozi wake wa chama. Yule mwenzake aliandaliwa kuwa shahidi wa kesi ya Lwakatare; aliambiwa akikubali dili hiyo atalipwa kila mwezi Sh. 500, lakini akaombwa kuwa mvumilivu kwa kuwa atalazimika kupotea kwa miezi kama mitano hadi sita.

Ndugu waandishi wa habari;

Kitendo cha Mwigulu kuwasiliana Ramadhani Ighondo, Mwigulu kuwasiliana na Ludovick, Saumu kuwasiliana na Mwigulu, Ighondo kuwasiliana na Ulimboka, Zoka kuwasiliana na Ighondo, tena katika muda uleule ambao Ighondo amewasiliana na Ulimboka na Saumu kuwasiliana na Mwagha, ni uthibitisho tosha kwamba usalama wa taifa wako nyuma ya mipango hii ya michafu ya kupanga utekaji na kisha kutaka kukichafua Chadema.

Aidha, kitendo cha Ludovick kuwasiliana Msaky; Ighondo kuwasiliana na Mwagha, Ridhiwani Kikwete kuwasiliana na Ighondo, tena kila baada ya Ighondo kuwasiliana na Ulimboka na Jack Zoka, ni uthibitisho mwingine kuwa genge hili la wahalifu linashirkiana na baadhi ya watu kutaka kuangamiza taifa.

Ni uthibitisho tosha kwamba hawa ndiyo wanaowahonga wanachama wa Chadema na watu wengine ili watoe ushahidi feki dhidi ya Lwakatare, na kwamba ni usalama wa taifa walioandaa ile video uchwara inayopigiwa chapuo na Mwigulu.

Ndugu waandishi wa habari;

Chama Cha Mapinduzi kinajua kwa hali ya sasa hakiwezi kushinda uchaguzi wa mwaka 2015 huku Chadema ikiwa katika hali nzuri ya kisiasa tunayoiona sasa. Wanajua kabisa CCM imegawanyika, kundi lolote litakalopita ndani ya CCM, litahujumu kundi jingine. Ni kama ilivyotokea uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.

Ndiyo maana wanapanga kila mbinu kutaka kuiangamiza Chadema. Nasi tunasema katu hatutakubali kuona Chadema kinakufa. Tutapambana usiku na mchana. Juna na mvua. Hadi tushinde hila hizi.Tunawaambia wanachama wetu na wale wanaotuunga mkono, Chadema ni chama kikubwa. Kina mtandao kila mahali, kuanzia Ikulu hadi polisi; na hivyo hakitakufa au kuzorota kwa mambo ya kupikwa.

Ni imani yangu kwamba amri ya mahakama itawafichua wote hawa ni kuirudisha Tanzania katika amani yake. Ni lazima tufikike mahala watu hawa wafahamike mbele ya umma, tunataka wafahamu kuwa maisha ya mwanadamu yana thamani kuliko siasa chafu na ufisadi wanaouendeleza.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.

Mabere Marando,

Dar es Salaam

Saturday, April 13, 2013

Maonesho ya Elimu na Huduma za Jamii, Brooklyn Park

Leo nimeshiriki maonesho ya elimu na huduma za jamii yaliyoandaliwa na African Career, Education & Resource, Inc (ACER). Maonesho haya yalifanyika katika shule ya Park Center, Brooklyn Park, Minnesota. Wadau wa huduma kama afya, ajira, elimu, na malezi ya vijana, walikuwepo, kutoa elimu na ushauri, na hasa kuifahamisha jamii kuhusu huduma wanazotoa.
Nilipata fursa ya kukutana na watu ambao tunafahamiana, na wengine ambao hatukuwa tunafahamiana.








Huyu dada anayeonekana kwenye picha ya juu kabisa na hapa kushoto alikuwa mwanafunzi wangu hapa Chuoni St. Olaf, miaka 13 iliyopita. Asili yake ni Ethiopia. Ni shabiki mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences




Kati ya hao tunaofahamiana, ambao tumekutana leo, ni Dr. Alvine Siaka kutoka Cameroon, ambaye ni mratibu wa African Health Action. Mwingine ni Rita Apaloo, kutoka Liberia, ambaye ni mratibu wa jumuia iitwayo African Women Connect. Rita naye ni shabiki wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences

Kati ya watu ambao tumefahamiana leo ni dada Iqbal Duale, m-Somali, ambaye ni mtaalam wa elimu ya jamii.  Tulielezana shughuli zetu kwa jamii, tukaona zinahusiana. Taasisi anayofanyia kazi inaitwa Planned Parenthood.  Tutawasiliana zaidi, Insh' Allah.

 Kama kawaida, kwenye mikusanyiko kama hii, tulipata fursa ya kubadilishana mawazo. Tuliongelea shughuli tunazofanya, changamoto zake na malengo yake, na umuhimu wake kwa jamii. Kitu kimoja cha kuvutia na kutia moyo ni kuwa pamoja na changamoto zote na magumu, kila moja wetu ana msimamo thabiti kuwa hakuna kulegea, kurudi nyuma, wala kukata tamaa. Changamoto hizi ni kama chachu kwetu.

Taasisi iliyoandaa maonesho ya leo, yaani ACER, niliitaja siku chache zilizopita, katika ujumbe wangu kuhusu mkutano wa bodi ya taasisi ya Afrifest. ACER na Afrifest tumeamua kushirikiana, nami niliamua kuhudhuria maonesho ya leo kama njia ya kujenga uhusiano huo.

Mimi ni mwenyekiti wa bodi ya taasisi ya Afrifest. Papo hapo, nilienda nikiwa nimejisajili kwa jina la kampuni ya Africonexion. Nilikuwa na meza, kama inavyoonekana hapa kushoto, ambapo niliweka vitabu na machapisho yangu mengine, nikapata fursa ya kuongea na wadau waliofika hapo. Wengine wana wadhifa katika taasisi zinazoshughulikia masuala ninayoshughulikia, yaani ya elimu kuhusu tofauti za tamaduni. Uzuri wa kukutana namna hiyo ni kuwa tunajenga msingi wa kushirikiana siku zijazo.

Thursday, April 4, 2013

Mhadhara Katika Darasa la Wazee

Leo nilitoa mhadhara katika darasa la wazee, hapa Northfield. Somo wanalosomea ni "Folk and Fairy Tales."

 Hapa Northfield kuna masomo ambayo wazee husoma, yanayoendeshwa na taasisi iitwayo Cannon Valley Elder Collegium. Nimewahi kufundisha mara tatu darasa la wazee katika mfumo huo, na somo langu lilikuwa "The African Experience." Tulisoma na kujadili kitabu cha Things Fall Apart cha Chinua Achebe kama msingi wa kuongelea hali ya Afrika kabla na baada ya ukoloni, na hali ya leo ya ukoloni mamboleo.

 Nilivyoingia tu darasani leo, nilifurahi kuwaona wazee ambao walishasoma somo langu. Walikuwa yapata nusu ya darasa la leo.

 Nilichangia mawazo kuhusu somo hili la hadithi za fasihi simulizi, nikasimulia hadithi mbili za ki-Matengo ili kuthibitisha na kufafanua yale niliyosema kinadharia. Hadithi nilizosimulia ni "The Monster in the Rice Field" na "Nokamboka and the Baby Monster," ambazo zimo katika kitabu changu cha Matengo Folktales.

Tulikuwa na mazungumzo marefu, kuanzia saa saba na nusu mchana hadi saa tisa. Ilipendeza sana kuwaona wazee hao wakiimba nami wimbo wa ki-Matengo uliomo katika hadithi ya "The Monster in the Rice Field," wimbo unaorudiwa tena na tena. Ilivutia sana, na sote tulifurahi, tukazama katika kuichambua hadithi hii na ile ya "Nokamboka," ambazo zote zimejaa falsafa na masuali kuhusu maisha.

Wednesday, April 3, 2013

Nitafundisha "Midnight's Children," Kitabu cha Salman Rushdie

Nimefundisha fasihi ya India mara nyingi sana, hapa Chuoni St. Olaf, kuanzia mwaka 1991. Nimefundisha maandishi ya watu kama Rabindranath Tagore, Mulk Raj Anand, Raja Rao, R.K. Narayan, Ruth Prawer Jhabvala, Nayantara Sahgal, Anita Desai, na Kamala Markandaya.

Sijawahi kufundisha maandishi ya Salman Rushdie, ambaye ni mwandishi maarufu sana, sambamba na hao niliowataja. Suali moja ambalo nimejiuliza miaka ya karibuni ni je, utafundishaje fasihi ya India bila kumjumlisha Salman Rushdie? Utaachaje kufundisha kitabu cha Rushdie kiitwacho Midnight's Children, ambacho kilipata tuzo maarufu ya Booker?

Mwezi Juni hadi Julai nitafundisha kozi ya wiki sita, katika somo liitwalo "Post-colonial Literature." Nimeamua kufundisha kitabu hiki cha Rushdie. Ni kitabu muhimu kwa namna nyingi, sio tu kwa upande wa sanaa, bali pia kwa jinsi kinavyojumlisha masuala na dhamira mbali mbali ambazo ni muhimu katika fasihi ya India. Ni kitabu chenye upekee kihistoria na kisiasa kwa jinsi kilivyofungamana na tukio moja muhimu sana katika karne ya ishirini, yaani kupatikana kwa uhuru kwa nchi iitwayo India.

Tukio hili la uhuru wa India lilitokea mwaka 1947. Ila kwa bahati mbaya sana, ni tukio lililoandamana na mgawanyiko uliosababisha kuwepo kwa nchi mbili, yaani India na Pakistan. Ni tukio lililoandamana na uhasama, mauaji na ukimbizi wa idadi kubwa sana ya watu, mtafaruku ambao ulikuwa baina ya wa-Hindu na wa-Islam. Tukio hili linakumbukwa kwa majonzi, na limeelezwa sana na waandishi kutoka India na Pakistan.

Kwa vile kitabu cha Midnight's Children kina kurasa nyingi sana, nimeona kuwa nisiweke vitabu vingi katika kozi hii ya wiki sita.  Nawazia kutumia vitabu vingine viwili au vitatu, ambavyo navyo vina kurasa nyingi. Nimeamua tu kutumia haya mavitabu makubwa nione itakuwaje. Kimoja ninachowazia sana ni Half of a Yellow Sun, cha Chimamanda Ngozi Adichie, wa Nigeria. Kingine ni Abyssinian Chronicles cha Moses Isegawa wa Uganda. Bado nina muda wa kufikia uamuzi wa mwisho. Huenda nikatumia The Famished Road, cha Ben Okri, au Wizard of the  Crow, cha Ngugi wa Thiong'o. Uamuzi kamili nitafikia katika siku kadhaa zijazo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...