Friday, September 30, 2011

Shule Niliyotembelea Madison

Jana asubuhi nilitoa mhadhara katika shule inayoonekana pichani hapa kushoto, ambayo iko mjini Madison, Wisconsin. Kama nilivyoandika kabla, mhadhara ulihusu yale niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cutural Differences.

Wanafunzi yapata 150 walikuwepo darasani kunisikiliza. Mwalimu wao alikuwa amewapa vifungu vingi kutoka katika kitabu hicho wasome, na pia aliwapa masuali ambayo waliyatafakari na kuyajibu kabla ya ujio wangu. Walikuwa wamejiandaa vizuri. Ni wanafunzi makini, wenye duku duku ya kufahamu mambo, nami nilifurahi kupata fursa ya kuwahamasisha kuhusu kuzifahamu tamaduni mbali mbali, kwa kusoma, kujumuika na watu wa tamaduni hizo, na ikiwezekana, kwenda kwenye nchi mbali mbali, hasa katika programu za masomo kama hizo ninazoshughulika nazo.

Hii ni shule ya Kanisa Katoliki. Ilinikumbusha utoto na ujana wangu, nilivyosoma katika shule ya msingi na seminari za Kanisa Katoliki mkoani Ruvuma. Nakumbuka katika seminari kulikuwa na kauli mbiu iliyokuwa inahimizwa muda wote: "Ora et Labora." Huo ni usemi wa ki-Latini, na maana yake ni "Sala na Kazi." Tulifundishwa kuzingatia yote mawili, na kuwa kazi inahitaji kufanywa kwa dhamiri na uaminifu, ili kazi nayo tuione kama sala. Shule ya Edgewood ilinikumbusha mambo ya aina hiyo.

Wednesday, September 28, 2011

Safari ya Madison, Kuongelea Kitabu

Naandika makala hii nikiwa katika gereji ya Car Time, mjini Northfield, Minnesota. Nimeleta kijigari changu kichekiwe, ili kesho nikiendeshe kwenda Madison, Wisconsin, kuongelea kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Kwa wanaopenda kufahamu zaidi masuala haya, ni kwamba huku Marekani, ukiandika kitabu kinachowagusa watu, utegemee kupata mialiko ya kwenda kuongelea kitabu hicho.

Shughuli ya kukutana na wadau namna hii inategemea aina ya kitabu. Kama ni riwaya au kitabu cha mashairi, unategemewa kusoma visehemu vya riwaya au mashairi hayo. Kama ni kitabu cha elimu jamii kama hicho changu, sio lazima kusoma sehemu yoyote. Watu hupenda kusikia maelezo ya yatokanayo na ulichoandika, na pia uyajibu au kuyajadili masuali yao.

Hapa Marekani, watu wanapenda kuwasikiliza waandishi kwa namna hizo nilizoelezea. Wanamlipia mwandishi usafiri, malazi, na ruzuku, bila kusita, ili waweze kumsikia.

Monday, September 26, 2011

Ziara ya Lyulilo, Ziwa Nyasa

Ukifika Matema Beach, Ziwa Nyasa, hutakosa kusikia kuhusu vijiji vya jirani, kama vile Lyulilo na Ikombe. Nilikuwa maeneo hayo tarehe 20 Agosti mwaka huu katika msafara wa programu ya LCCT, kama nilivyoelezea hapa.

Hapa kushoto ni Matema Beach, ambapo unapata mtumbwi wa kukuvusha hadi Lyulilo. Hapa mwendesha mtumbwi anaandaa safari. Nauli ni makubaliano.


Safari inaendelea. Hatukukumbana na mawimbi wala usumbufu mwingine.
Kadiri dakika zinavyopita, Lyulilo inazidi kuonekana vizuri.

Hapa sasa tumekaribia sehemu ya kutua.
Baada ya kutia nanga, tunaingia mitaani Lyulilo. Ni siku ya soko. Watu wamejaa kila mahali katika mtaa mkuu wa Lyulilo.


Kuna bidhaa tele, kama vile vyungu. Lyulilo ni maarufu kama soko la vyungu, ambavyo hutengenezwa na wafinyanzi katika kijiji cha Ikombe, mbele kidogo ya Lyulilo. Hatukufika
Ikombe; nategemea mwakani, Insh'Allah.


Hapo kushoto wanaonekana wauzaji na wateja wa pombe za kienyeji. Mzee mwenye kiko alisisitiza nimpige picha vizuri ili kiko kionekane.Hiyo ni fursa ya wenyeji kukutana na wageni.

Sunday, September 25, 2011

Hotuba ya Rais Mugabe, Kikao cha 66 cha Umoja wa Mataifa

Hotuba hii imenigusa. Inanikumbusha enzi za Mwalimu Nyerere, ambapo alikuwa anapambana na hao wakoloni mamboleo ambao leo sisi wa-Tanzania, kwa kukosa mwelekeo na fikra thabiti, tunawaenzi kama marafiki na wadau wa maendeleo yetu.


Saturday, September 24, 2011

Kweli Blogu Inaweza Kuwa Shule

Baadhi yetu wanablogu tumewahi kutafakari na kujadili suala la blogu kama shule. Binafsi, nashukuru kuwa mara kwa mara napata ujumbe kutoka kwa wadau wanaosema wanajifunza kutokana na blogu zangu.

Leo kule Facebook kajitokeza mama mmoja mw-Arabu anayeishi Kuwait City. Kaniambia kuwa yeye ni mwalimu wa ki-Ingereza, na anafanya utafiti wa shahada ya juu kuhusu mwandishi J.M. Coetzee, hasa kitabu cha "Waiting for the Barbarians." Amesema kuwa amefurahi kuwa nilikubali kuwa rafiki yake Facebook na anangojea kwa hamu kupata ushauri wangu kuhusu tasnifu anayoandika. Ameendelea kusema kuwa katika kupitapita mtandaoni aliiona makala yangu kuhusu kitabu hiki. Makala yenyewe ni hii hapa.

Haya basi, mambo ya aina hii yanapotokea, kwa nini nisikiri kuwa blogu inaweza kuwa shule? Simaanishi kuwa taaluma yote husika inapatikana hapa kwenye blogu. Hata shule ni hivyo hivyo; haikuwezeshi kumaliza masomo, wala huwezi kuhitimu, ingawa walimwengu wanajidanganya na wanadanganyana kuwa wanahitimu. Shule inatoa dokezo na changamoto, na mwenye akili anafuatilia baada ya pale.

Ninaposema blogu inaweza kuwa shule nina maana hiyo hiyo, kwamba kile kinachowekwa katika blogu kinaweza kuwa dokezo na changamoto ya kuwawezesha walimwengu kutambua mtu unahusika na masuala gani na kisha wakafuatilia. Ndicho kilichotokea kwa huyu mama wa Kuwait City, na Insh'Allah nitafanya lolote niwezalo katika kumpa ushauri.

Thursday, September 22, 2011

Kwa Mnyakyusa, Mbamba Bay

Katika pitapita zangu kwenye mji mdogo wa Mbamba Bay, kule Ziwa Nyasa, Agosti 2 na 3 mwaka huu, niliona tangazo ukutani, "Kwa Mnyakyusa." Tangazo hili lipo pembeni tu mwa kituo kikuu cha mabasi.


Sikupata wasaa wa kufuatilia tangazo hili na kujua asili yake au kumfahamu mhusika. Kwa vile hapo ni madukani, nilihisi kuwa ni jina la duka liliopo hapa.

Kitu kidogo kama hiki ni changamoto kwa yeyote anayetafakari mambo. Suala la majina ya mahali mbali mbali ni suala linaloweza kutafitiwa, na sehemu mbali mbali duniani wataalam wanafanya utafiti wa namna hii.

Hapa kwetu Tanzania napo tunahitaji utafiti huo, tuweze kujua asili ya majina ya sehemu mbali mbali na hivyo kutunza kumbukumbu zake.

Hii sehemu ya Mbamba Bay, "Kwa Mnyakyusa" inatuonyesha jadi iliyopo Tanzania ya kuzipa sehemu majina yanayotaja kabila. Nina hakika majina ya aina hii ni mengi. Kwa mfano, kuna sehemu kule Kibaha iitwayo "Kwa Mfipa."

Majina mengine ya sehemu mbali mbali yanawataja watu maalum. Kwa mfano, kuna sehemu kule Msasani iitwayo "Kwa Mwalimu." Katika hospitali ya Muhimbili kuna wodi iitwayo Sewa Haji. Wangapi wanajua asili ya jina hili? Kuna sehemu pale Sinza iitwayo "Kwa Remmy." Nasikia kuna sehemu kule Manzese iitwayo "Kwa Mfuga Mbwa." Kama nilivyosema, haya ni masuala ya kutafitiwa.

Tuesday, September 20, 2011

Nimekutana na Wapiga Debe Wangu Indianapolis

Nilikuwa Indianapolis kuhudhuria mkutano wa Africa Network, Septemba 16-18. Pamoja na mijadala kuhusu masuala mbali mbali, kuna mengi mengine yanayotokea katika mikutano ya aina hii. Nilikutana na wasomaji kadhaa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambao ni wapiga debe wakubwa.

Hapa kushoto ni Profesa Tom Benson, mwanzilishi wa Africa Network, ambaye kabla ya hapo alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Asia Network. Ni mzee maarufu katika ulimwengu wa taaluma na mashirika na taasisi za kimataifa. Yeye ni shabiki mkubwa wa kitabu hiki. Anakipenda na kukipigia debe.


Aliyesimama hapa kushoto akitoa mada ni Profesa John Tawiah Boateng wa Chuo cha Augustana. Anatoka Ghana. Ni shabiki mwingine mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans. Katika programu yake ya kupeleka wanafunzi Ghana, wanafunzi wanakisoma kitabu hiki. Habari zake niliwahi kuzielezea hapa na hapa.


Aliyeweka mikono kidevuni, hapa kushoto, mbele kabisa, ni Profesa John Watkins anayefundisha hisabati katika Chuo cha Colorado. Ni mhamasishaji mkubwa wa masomo yahusuyo Afrika. Naye ni shabiki wa kitabu cha Africans and Americans. Wanafunzi wengi wanaoenda Afrika wamekisoma kitabu hiki kutokana na yeye kuwahamasisha.

Hapa kushoto anaonekana Profesa Edith Miguda wa Chuo cha St. Mary. Anatoka Kenya. Nilishawahi kumwona mara moja katika mkutano wa Africa Network. Katika mkutano wa Indianapolis aliniambia kitu ambacho sikujua, kwamba anakitumia kitabu cha Africans and Americans katika programu ya kupeleka wanafunzi Afrika. Nilifurahi kusikia hivyo.

Blogu yangu ni sehemu ninapojiwekea mambo yangu, iwe ni mawazo, hisia, kumbukumbu, au kingine chochote. Ni hiari yangu. Nimeona niwaenzi hao niliowataja. Imani yao juu ya kazi yangu inanifanya nijibidishe kufanya makubwa zaidi.

Saturday, September 17, 2011

Mkutano wa "Africa Network" Umefana

Mkutano wa Africa Network hapa Indianapolis umefana sana. Hapa kulia anaonekana Dr. Tom Benson, mwanzilishi wa Africa Network, ambaye alitukusanya watu kadhaa miaka mitano iliyopita tukaunda bodi ya Africa Network. Ni miaka mitano sasa na Africa Network inaendelea kupiga hatua.

Tumetafakari masuala mengi, kuanzia ujasiriamali, ufundishaji, hifadhi za nyaraka na kumbukumbu nyingine, taasisi zinazohusika na masomo yahusuyo Afrika, kuandaa na kutekeleza mipango ya kupeleka wanafunzi Afrika, utafiti, na shughuli za kujitolea.


Kama kawaida, ni fursa ya watafiti na walimu wa vyuo mbali mbali kukutana na kubadilishana mawazo. Kama inavyotokea katika kila mkutano, wengine tulifahamiana kabla na wwngine ni wapya.
Kati ya watu wapya niliowakuta na kufahamiana nao ni Bernard Woma ambaye ni msanii kutoka Ghana. Anaonekana katika picha hapa kushoto, mbele kabisa, amevaa kofia. Anaendesha kituo nchini Ghana ambapo anawafundisha wageni sanaa na utamaduni wa kutumia ala za kiasili za muziki na mambo kadha wa kadha mengine. Hebu jionee mwenyewe anavyoimudu kazi hapa.Hapa kushoto naonekana nikiwa na mtoa mada mmojawapo, wakati tulipokuwa tunatoa mada zatu.Hapa kushoto naonekana nikitoa mada yangu, "Engaging with Somali Immigrants in Minnesota." Niliongelea uzoefu nilioupata katika jimbo la Minnesota, jimbo ambalo lina wakimbizi na wahamiaji wengi kutoka Somalia na nchi zingine za Afrika, hasa Liberia. Kitu kimoja nilichowatajia wasikilizaji ni ripoti inayopatikana hapa, ambayo ni utafiti waliofanya wanafunzi wa Idara ya Siasa, Chuo cha St. Olaf, katika mji wa Faribault kuhusu masuala yanayowahusu wa-Somali ambao wanaishi katika mji ule. Utafiti huu ulikuwa ni njia nzuri ya kuwapa wanafunzi uzoefu wa kufanya utafiti katika jamii na kujifunza kuhusu masuala ya watu wa utamaduni tofauti na wao. Ripoti hii imenigusa kwa namna ya pekee kutokana na jinsi inavyothibitisha namna ufundishaji wetu unavyoweza kuwekwa katika misingi mipya kwa kuwapa wanafunzi kufanya utafiti katika jamii. Pia ripoti hii inaonyesha jinsi viongozi na wadau mbali mbali wa jamii wanavyoutambua mchango wangu katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wanajamii wa miji kama Faribault ambayo ina idadi kubwa ya hao wahamiaji na wakimbizi. Sina sababu ya kuficha faraja ninayoipata kwa kuona viongozi na wadau hao wanakipigia debe kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nashukuru kwamba kina mchango muhimu kwa watu wanaokabiliwa na masuala magumu ya jamii.

Kitu kimoja ambacho ni cha pekee sana ni kuwa tumepata pia fursa ya kuona sanaa za kale za Ife, Nigeria, ambazo kwa sasa ziko katika jumba kuu la makumbusho mjini Indianapolis. Hizo ni sanamu za shaba na "terra cota." Zimeletwa na zinaonyeshwa hapa Indianapolis kwa mpango maalum kutoka hifadhi ya Taifa ya Nigeria.

Friday, September 16, 2011

Nimetua Indianapolis

Nimerejea kutoka Tanzania tarehe 6 mwezi huu, na tayari nimeshaanza mizunguko. Leo alasiri nimetua Indianapolis, Indiana, kuhudhuria mkutano wa Africa Network, mtandao wa vyuo vya hapa Marekani ambao lengo lake ni kuhamasisha na kuendeleza masomo yahusuyo Afrika. Tunajenga mikakati ya ushirikiano katika utafiti, ufundishaji, na kubadilishana uzoefu wa aina mbali mbali. Hatimaye tunataka kuendeleza ushirikiano baina ya vyuo vyetu hivi na vyuo vya Afrika, kwa mfano kwa kupeleka wanafunzi na watafiti Afrika na kupokea wanafunzi na watafiti kutoka Afrika.

Nimekuwa mwanabodi wa bodi ya Africa Network tangu ilipoanza, miaka mitano iliyopita. Ni shughuli ya kujitolea, lakini napenda shughuli za aina hiyo. Kuna mambo mengi yanayonivutia katika mikutano yetu, kwa mfano kukutana na walimu ambao wanaandaa programu za kupeleka wanafunzi Afrika na kuwapa ushauri na mawaidha.

Thursday, September 15, 2011

Kitabu Kipya cha Haji Gora Haji

Kama ilivyo kawaida ninapokuwa Dar es Salaam, mwaka huu nilizungukia mara kadhaa maeneo ya Chuo Kikuu Dar es Salaam. Katika duka la vitabu la Taasisi ya Uchunguzi wa Ki-Swahili, ambako nilienda kuangalia vitabu, nilifurahi kuona kitabu kipya cha Haji Gora Haji kiitwacho "Siri ya Ging'ingi," ambacho kilichapishwa na Taasisi hiyo mwaka 2009. Nimeanza tu kukisoma.

Nilikuwa sijakisikia kitabu hiki na nilikinunua hima. Haji Gora Haji ni mtafiti na mwandishi maarufu katika masuala ya ushairi utamaduni na lugha ya ki-Swahili. Upeo wa fikra zake na kina cha uchambuzi wake ni hazina isiyomithilika.

Haji Gora Haji ni mzaliwa wa kisiwa cha Tumbatu. Hakusoma katika hizi shule tunazosomea sisi wengine. Elimu yake aliipatia katika madrasa, kisha akafanya kazi mbali mbali, kama vile uvuvi na ubaharia.

Nimebahatika kuonana naye mjini Zanzibar na kufanya mahojiano naye. Ni mtaalam aliyebobea, mwenye mengi ya kutufundisha. Nina vitabu vyake kadhaa, na napangia siku zijazo kuandika makala kuhusu mchango wake uliotukuka katika sanaa na taaluma. Kwa mfano, mbali na vitabu vyake vya tenzi na mashairi, amefanya utafiti wa kina na kuandika "Kamusi ya Kitumbatu," ambayo ni hazina kubwa.

Kitu kimoja kilichonivutia sana katika kamusi hii ni jinsi ilivyosheheni majina ya aina mbali mbali za samaki na viumbe vingine vya baharini. Yeyote anayedhani kuwa ki-Swahili hakina msamiati wa taaluma kama hii aangalie kamusi hii. Atatambua alivyopotoka.

Tuesday, September 13, 2011

Mdau Kaleta Wadau Wengine


Kama nilivyowahi kuandika, tarehe 31 Agosti nilitembelewa na mdau Renatus Mgusii, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Ni mtu wa pekee kwangu, kwani ni msomaji makini wa vitabu vyangu. Ametumia hela zake nyingi kuvinunua na anapenda kuongelea yaliyomo. Pia ni mfuatiliaji wa blogu zangu. Ni wazi kuwa alivutiwa na mazungumzo yetu, hadi akaamua kuwaleta marafiki zake tuonane.


Wageni hao, ambao ni Mariana Ilieva na mumewe, aliwaleta tarehe 3 Septemba, pale Lion Hotel, Sinza. Mariana ni mkurugenzi wa Evin School of Management kwa upande wa Tanzania. Anajua lugha za ki-Bulgaria, ki-Rusi, ki-Swahili na ki-Ingereza. Mume wake, anayeonekana pichani, kulia kabisa, ni daktari m-Tanzania. Tuliongea mengi kuhusiana na taaluma na shughuli zetu sote wanne, na uwezekano na umuhimu wa kushirikiana. Ni jambo la kufurahisha kukutana na watu makini kama hao.

Sunday, September 11, 2011

Nyumba za Ibada Mjini Songea

Kama ilivyo katika miji mingine ya Tanzania, na hata katika vijiji vingi, mjini Songea kuna nyumba za ibada za dini mbali mbali, nami huvutiwa ninapoziona. Ni faraja kuona jinsi wa-Tanzania tulivyo na jadi ya kuishi pamoja bila kujali tofauti za dini. Picha hizi zinazoonekana hapa ni za baadhi ya nyumba za ibada zilizopo katikati ya mji wa Songea.

Hapa kushoto ni kanisa ambalo nalikumbuka tangu nilipofika Songea kwa mara ya kwanza, kwenye mwaka 1963 mwanzoni, nilipokuwa nakwenda kuanza darasa la tano katika Seminari ya Hanga. Kila ninapopita karibu na kanisa hili kumbukumbu hizi zinarudi akilini mwangu.


Hapa kushoto ni kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Songea. Nimewahi kuhudhuria misa katika kanisa hili.
Hapa kushoto ni msikiti. Sioni shida kupiga picha makanisa, lakini sina hakika kuhusu misikiti. Niliwahi kupiga picha msikiti mmoja katika mji fulani mkubwa Tanzania na dakika chache baadaye walikuja watu kunihoji kwa nini nimefanya hivyo. Nilifanya kazi kubwa kuwapa maelezo, na bado haikuwa rahisi kuwaridhisha. Lakini mimi natafuta kumbukumbu na taarifa hizi kwa nia njema, kama nilivyoelezea hapa. Sisiti kukiri kuwa navutiwa na taswira za misikiti.

Hapo nje ya msikiti niliwaona watu wakiuza vitu mbali mbali, kama vile vitabu. Nilivutiwa na uwepo wa vitabu, kwani tangu mwanzo wake, dini ya Islam ilikuwa inahimiza elimu. Inavyoonekana, hata dhana ya madrasa ilimaanisha mahali pa kufundishia taaluma mbali mbali, sio dini tu. Kama kumekuwa na upotoshaji, umetokea baadaye.

Friday, September 9, 2011

Hoteli ya Masista, Mbamba Bay

Mwaka huu nilipotembelea Mbamba Bay, tarehe 2 hadi 4 Agosti, nilifikia katika hoteli ya St. Bernadetha ambayo ni ya masista wa Kanisa Katoliki. Ni mradi wao katika kuendeleza huduma kwa jamii. Papo hapo, kuwepo kwa hoteli hii ni kivutio kwa utalii.

Ukiwa mjini Mbamba Bay, hoteli hii inaonekana vizuri, kwani iko kilimani. Ukiwa hapo hotelini, unaliona Ziwa Nyasa vizuri na mji wa Mbamba Bay chini yako.

Hoteli hii ni nzuri kwa kila hali, kuanzia mazingira hadi huduma za malazi na chakula. Ni aina ya hoteli ambayo unategemea kuiona katika miji mikubwa, si mji mdogo kama huu.

Wednesday, September 7, 2011

wa-Marekani Wajifunza u-Islam Kalenga

Mwaka huu, wanafunzi niliowaleta Tanzania kutoka Marekani wamepata fursa ya kujifunza kuhusu u-Islam kutoka kwa wahusika wa dini hiyo. Nilitaka wapate fursa hiyo, ili wapate mwanga angalau kidogo kuhusu dini hiyo, na pia waifahamu Tanzania kama nchi yenye dini mbali mbali, na waweze kujua tunavyoishi pamoja.

Mimi kama m-Kristo, ninaweza kuelezea masuala ya u-Kristo Tanzania kwa kiwango cha kuridhisha. Vile vile, kutokana na juhudi zangu za kujielimisha kuhusu dini mbali mbali, ningeweza kutoa maelezo kuhusu u-Islam, kama ninavyofanya ninapofundisha fasihi.

Lakini niliona ni muhimu kuwapa wanafunzi hao fursa ya kukutana na kujifunza kutoka kwa viongozi wa dini ya ki-Islam. Fursa nzuri ilijitokeza tulipokuwa Kalenga, mkoani Iringa, kwenye Makumbusho ya Mkwawa. Hiyo ilikuwa ni tarehe 11 Agosti. Baada ya ziara ya makumbusho, niliona msikiti, nikamwambia mkurugenzi wa makumbusho, ndugu Nicholaus Kulanga, kuwa ningependa kuonana na imam wa msikiti, ili anisaidie kuwaelimisha wanafunzi wangu kuhusu u-Islam. Mkurugenzi aliahidi kututambulisha.

Siku ya pili, alasiri, tulienda tena Kalenga, tukapata fursa ya kuongea na Imam Zuberi Suleiman. Nilimweleza lengo na madhumuni yangu, yaani kuwapa wanafunzi wangu fursa ya kuelewa kidogo kuhusu u-Islam, kwani fursa za aina hiyo ni nadra Marekani, na wa-Marekani wengi hawaelewi chochote au wana mawazo potofu kuhusu u-Islam.

Imam, anayeonekana pichani amevaa kanzu na kofia, alivutiwa na ombi hilo, akatuongoza hadi kwenye msikiti wa mwanzo wa Kalenga. Wakati anajiandaa kuongea nasi, alimwita pia mwenzake, ambaye ni Ustaadh Maneno, akajumuika nasi.

Imam na Ustaadh walitoa maelezo ya chimbuko la u-Islam na misingi yake kwa ufasaha kabisa. Hata mimi ambaye ninaelewa mambo kadha wa kadha kuhusu u-Islam nilipata mwanga mpya. Imam alinionyesha kitabu kiitwacho "Tafsiri ya Sehemu ya Kumi ya Mwisho ya Qur'an Tukufu." Nilivutiwa na kitabu hiki, na nitakinunua.

Sote tulifurahi kupata fursa hii ya kuongea. Nilijisikia vizuri pale Imam na Ustaadh waliposema wamefurahishwa kuwa nafahamu mengi kuhusu u-Islam. Wakati tunaagana, Ustaadh Maneno aliwapa majina mapya hao wanafunzi: huyu mvulana jina lake ni Abdi Karim na huyu dada jina lake ni Bi Aisha. Jambo hili lilitufurahisha wote, tukacheka kwa furaha. Niliwaeleza hao wanafunzi heshima ya majina hayo katika u-Islam, na kuanzia siku ile nimekuwa nikiwaita kwa majina hayo.

Tumejenga uhusiano mzuri hapo Kalenga. Mwakani, Insh'Allah, natawapeleka wanafunzi wengine hapo.