Wednesday, February 29, 2012

Wadau Walionitembelea "Danish," Arusha

Mwaka 2007, nilikuwa Tanzania na wanafunzi na mwalimu mmoja kutoka Chuo cha Colorado waliokuja kwenye kozi yangu ya Hemingway in East Africa. Ni kozi ya wiki tatu. Tulifika na kuanzia kozi kwenye kituo cha "Danish," Arusha, wiki ya mwisho ya Mei.

Kama ilivyo kawaida ninapokuwa Tanzania, wadau mbali mbali hunitafuta. Basi hapo Danish alikuja Mama Esther Simba, mwenye gauni jekundu pichani, na rafiki yake, ambaye jina lake limenitoka.

Tulikuwa tumewasiliana kwa kitambo, kwa barua pepe. Yeye alikuwa mshauri katika programu ya Cross Cultural Solutions, ambayo inaleta watu wa kujitolea Tanzania. Alikuwa anawapokea na kuwahudumia, pamoja na kuwaelimisha kuhusu maisha na utamaduni wa Tanzania.

Mama Simba ni mdau wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Shughuli zetu zinahusiana vizuri, kwani nami huwaelimisha wa-Marekani kuhusu utamaduni wa wa-Afrika, na pia nawaelimisha wa-Afrika kuhusu utamaduni wa wa-Marekani chini ya kampuni ya Africonexion.

Kukutana na wadau namna hiyo ni fursa nzuri ya kubadilishana mawazo. Unaweza kumsikiliza Mama Simba anavyoelezea kwa ufasaha kabisa shughuli na manufaa ya Cross Cultural Solutions hapa.

Monday, February 27, 2012

Kwa Kuzuia Misa, wa-Kwere Mmechemsha

Nimesoma taarifa kuwa waumini wa Kanisa Katoliki la Lugoba, wamemzuia padri asisome misa, eti kwa vile anawasema vibaya. Napenda kusema machache kuhusu suala hilo.

Wakwere mmechemsha, tena mno. Mimi ni mtani wenu, kwa hivyo lazima niwape vidonge vyenu!

Mimi pia ni m-Katoliki, na ninafahamu fika kuwa waumini hatuna wadhifa wa kuzuia misa isisomwe. Hapo mmekosea kabisa! Mbali ya hilo kosa lenyewe, tambueni kuwa mmewakwaza hata watoto, ambao tunapaswa kuwalea katika njia ya kuheshimu misa na mamlaka ya Kanisa. Tena bora mwende mkaungame.

Kama mlikuwa na malalamiko dhidi ya padri, mngeweza kabisa kukaa naye kikao, au kulalamika kwa askofu, na suluhu ingepatikana. Kuzuia misa ni kitendo kiovu sana. Sijawahi kusikia kitu kama hiki.

Inaonekana padri alikuwa anawatolea uvivu kwa yale aliyoyaamini kuwa yanakwamisha maendeleo yenu. Sasa nyinyi badala ya kutafakari ili kubaini kama alikuwa anasema ukweli au la, na kama ilikuwa ni ukweli, badala ya kukiri mnarukia hoja ya kwamba anawakera. Kumbukeni kuwa wakati mwingine ukweli unauma. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ni kwamba padri ana uchungu na maendeleo yenu.

Mmekosea sana, wa-Kwere.

--------------------------------------------------------------------

Taarifa ya tukio imechapishwa katika gazeti la Habari Leo:

--------------------------------------------------------------------

PADRI wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Lugoba Jimbo la Morogoro, Philipo Mkude amezuiwa na waumini kuongoza misa baada ya kudaiwa kuwakashifu waumini wa kabila la Wakwere.

Padri Mkude alizuiwa kuongoza misa jana asubuhi parokiani hapo, baada ya waumini zaidi ya 200 kuandamana wakiwa na mabango zaidi ya 20 wakidai ahamishwe kwa kuwa amewatukana katika mahubiri yake, kwamba watoto wao ni wachafu na wao wamebaki kucheza ngoma badala ya kufanya maendeleo.

“Tumechoka na mahubiri ya huyu Padri, kila akihubiri kanisani lazima atuseme Wakwere,
tumemkosea nini?

Mara atuseme tu masikini, mara watoto wetu wachafu na hatuwapeleki shule tunashindia ngoma, tumechoka, hatumtaki,” alisema muumini ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

“Leo tumemzuia asisome misa kabisa, hakuna haja maana hakuna amani kanisani, hatujui ana kitu gani na sisi, sijui kwa sababu parokia hii ipo kwa Wakwere?

“Hata Jumatano ya Majivu wiki iliyopita katusema tena, eti watoto wetu ni wachafu sana ukilinganisha na makabila mengine, hii ni kashfa.”

Wakwere ni moja ya makabila katika Mkoa wa Pwani linalopatikana wilayani Bagamoyo,
lakini katika mfumo wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Lugoba ipo chini ya Jimbo la Morogoro.

Muumini huyo aliyezungumza kwa simu na gazeti hili jana, alidai mahubiri ya Padri huyo ya kuwasema Wakwere hayakuanza siku za karibuni, bali ni ya muda mrefu na yamekuwa kama ya kusutwa badala ya kulishwa Neno la Mungu.

“Hali hiyo imesababisha watu kutokwenda kanisani wakijua leo Padri huyo anaongoza misa, lakini akiongoza Katekista, misa inajaa utadhani Askofu amekuja, tunachotaka hapa ni Padri mwingine, kama Askofu anatujali atuletee mwingine,” alisema muumini huyo.

Kwa mujibu wa muumini huyo, walifanya maandamano ya amani kuanzia saa moja asubuhi kabla ya misa iliyopaswa kuanza saa 2.30 asubuhi huku wakiimba nyimbo za dini na mabango yenye ujumbe mbalimbali ukionesha kauli tofauti za padri huyo na namna walivyomchoka.

Alidai pia hali hiyo ilisababisha misa isifanyike baada ya Polisi pamoja na Diwani wa Msoga,
Mohamed Mzimba kufika kanisani hapo na kumshauri Padri huyo aondoke eneo hilo na kwenda Parokia ya jirani ya Chalinze umbali wa kilometa 22 ili kurejesha amani eneo hilo.

Diwani Mzimba alipoulizwa alikiri na kusema; “nilifika hapo nilipopewa taarifa kwamba hali si
shwari, mimi si wa Kata ya Lugoba, lakini mwenzangu anaumwa…kweli wameandamana,
lakini kwa amani na wana madai yao.”

“Ujumbe wameutoa kwa mabango, mengine yaliandikwa hatumtaki kapoteza kikombe chetu
cha dhahabu cha divai na mengine anatukana Wakwere, mimi si Mkristo sasa sijui zaidi, ila kuondoa jazba waliyokuwa nayo, Polisi walimshauri Padri aende kanisa la Chalinze huku viongozi wa kanisa wakimaliza mzozo,” alisema Mzimba.

Katekista (Mwalimu wa Mafundisho wa Dini) wa Parokia hiyo, Prosper Semindu alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, alikiri kutokea na kueleza kuwa haelewi sababu ni nini ila waumini hao walikuwa na mabango huku wakiimba nje ya kanisa na kusababisha misa isifanyike.

Padri Mkude alonga
Padri Mkude alipoulizwa jana alikana kuwatukana na badala yake alidai kuwa katika mahubiri yake amekuwa akiwasisitiza kusoma kama ambavyo viongozi kadhaa, akiwemo Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwaeleza.

“Watu kuwasema Wakwere kuhusu elimu ipo tangu zamani, nilikuwa nawasisitiza hata
wachimbe vyoo, hawataki, wanauza mashamba ambayo ni urithi kwa watoto, niliwaambia
jamani msiuze mtashindwa kusomesha watoto, hawanisikii, wanabaki kucheza ngoma, sasa
nimewatukana wapi?

“Jumatano ya Majivu niliwaambia wabadilike hasa kuhusu elimu, kwamba tufanye bidii katika shule yetu hapa Lugoba kidato cha nne wapo wanafunzi 250 kutoka Pwani, angalau 70 waende kidato cha tano na tukipata watoto angalau 10 vyuo vikuu miaka 10 ijayo tutakuwa na
wasomi wengi, leo wanasema unatunyanyasa na kututukana,” alisema Padri Mkude.

Alisema alipoona maandamano aliwaeleza kuwa kama amefanya makosa ya jinai watoe taarifa kwa vyombo vya usalama na kama ni makosa ya kikanisa, wafikishe mahali husika, lakini si kuvamia ibada na kufanya maandamano bila ruhusa.

Walivyoanzisha vurugu
Akielezea hali ilivyokuwa, Padri Mkude alisema wakati akijiandaa kuanza ibada baada ya kengele ya kwanza na ya pili kulia, muumini mmoja alimfuata kumsalimu na kisha alimwambia hawataki aongoze Misa na kama akifanya, hakutakuwa na usalama kwenye Misa.

“Wakati huo tofauti na siku nyingine, hakukuwa na mtu kanisani, niliwauliza kwa nini,
wakasisitiza niondoke, huko nje walikuwa wengi wanaimba, nikawaambia kama mmekataa misa, basi.

Viongozi wa Baraza la Walei walitoa taarifa Polisi, wakaja na mimi nikaondoka,” alisema Padri Mkude.

Alisema hivi sasa yupo Parokia ya Chalinze na anasubiri uamuzi wa kikao kati ya Ujumbe wa Askofu wa Morogoro na kundi la waumini hao ili kumaliza suala hilo. Mpaka jana jioni, kikao hicho kilikuwa kikiendelea.

Saturday, February 25, 2012

Picha za Wadau Wakiwa na Vitabu

Hapa naleta picha niizopiga na wadau mbali mbali wa vitabu vyangu. Kila picha inanikumbusha tukio la kukutana na wadau hao. Kila picha inabeba historia fulani, na ningeweza kuisimulia. Kitu kimoja kinachonifikirisha ni jinsi watu wanavyoshika vitabu wakat wa kupigwa picha. Karibu wote wanaweka kitabu sehemu ya kifuani, karibu na moyoni, na wengine karibu na tumboni. Mtu unaweza kuandika insha kuhusu suala hilo, kuelezea saikolojia inayoandamana na upigaji picha kwa upande wa mpiga picha na mpigwa picha, kama watafiti wengine walivyofanya, halafu ukajikita katika kuwaelezea hao wadau wanaopigwa picha wakiwa wameshika vitabu vyao.

Hapa ni mjini Faribault, Minnesota, wakati wa tamasha la tamaduni mbali mbali.
Hapa ni Sinza, Dar es Salaam. Huyu mdau ni Gilbert Mahenge, mwanakijiji wa Msoga, Bagamoyo. Huyu ni kati ya wa-Tanzania wachache ambao nawaona wameelimika kiukweli, kwa maana kwamba anatafuta elimu bila kuchoka. Mara ya kwanza kukutana naye, tulikuwa kwenye basi tukitokea Dar es Salaam. Katika begi lake alikuwa na vitabu. Hapo Sinza pia, tulipokutana tena, alikuwa na vitabu, hata akaniulizia kuhusu kitabu fulani ambacho sikuwa nimekisikia. Yeye alishakisoma. Hasomi kwa sababu ya mitihani, bali kwa kujielimisha.

Hiyo ni familia ya ki-Jerumani. Tulipiga picha hii kituo cha mabasi Ubungo, Dar es Salaam, wakati wao walipokuwa wanasafiri kwenda Ruvuma, ambako alizaliwa huyu mama wa familia, aliye pembeni yangu.

Hapa ni Brooklyn Park, Minnesota, kwenye tamasha la nchi za ki-Afrika. Huyu wa katikati ni mdau Richard Fillie kuoka Sierra Leone. Alimleta huyu mwingine, ambaye anatoka Sudan. Staili yao ya kushika vitabu ni tofauti na ya wengine.
Hapa ni viwanja vya makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam, Septemba, 2004, wakati wa tamasha la vitabu. Niko na dada yangu na mdau Eiko Kimura kutoka Japani.

Hapa ni ndani ya maktaba ya Chuo cha St. Olaf. Huyu kijana ni mwanafunzi.

Hapa ni Minneapolis, Minnesota, kwenye mkutano wa watu wenye asili ya Afrika. Huyu mdau naye ni mwandishi M. Ann Pritchard.

Hapa ni Madison, Wisconsin, nyumbani kwa mwalimu Wade Dallagrana, huyu aliyeshika kitabu.
Hapa ni viwanja vya makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam, Septemba, 2004, wakati wa tamasha la vitabu. Niko na mdau kutoka Japani. Yeye amevisogeza vitabu karibu na kifua changu.Hapa ni viwanja vya makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam, Septemba 2004, wakati wa tamasha la vitabu. Niko na dada yangu na wadau wa Canada.

Friday, February 24, 2012

Ualimu Kazi Ngumu

Mimi ni mmoja wa walimu ambao tunapenda ualimu. Moyo wangu daima umekuwa kwenye ualimu, na sijawahi kuwazia kubadili mwelekeo.

Walimu wanakumbana na vipingamizi kadhaa, kuanzia sera katika sekta ya elimu, hadi tabia za baadhi ya watoto na wazazi. Namsikitikia mwalimu anayeonekana katika hii katuni. Huenda wizara imeamua kuwa watoto wafundishwe dhana kama istilahi, kutohoa au kifyonzeo kabla ya wakati ufaao. Kila somo lazima liende hatua kwa hatua, kufuatana na umri wa mtoto. Utaratibu huu ukifuatwa, itadhihirika kwamba hakuna somo gumu.
(Namshukuru mchoraji wa katuni hii, ingawa nimeshindwa kumtambua na kumtaja ipasavyo).

Thursday, February 23, 2012

Dini Inayoenea kwa Kasi Kuliko Zote Tanzania

Mara kwa mara ninawasikia watu wakiongelea suala la dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania, Afrika au duniani kwa ujumla. Kila mtu ana mtazamo wake. Wengine wanatoa pia takwimu, ambazo sijui kama ni za kweli au ndoto. Ni mchezo wa kuringiana nani zaidi kwa kutumia takwimu, wakati dini ni suala la mtu binafsi. Wala hutaingia ahera kwa msingi kuwa dini yako hapa duniani ilikuwa na wafuasi wengi kuliko dini nyingine.

Kwa mtazamo wangu, dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania ni ufisadi na ushirikina. Ufisadi na ushirikina huo unaendelea kushamiri kiasi kwamba unajitokeza hata kwenye nyumba za ibada za dini mbali mbali. Hebu tutafakari hilo.

Wabunge Wakipanda Basi Kwenda Dodoma, 1984

Picha hii murua nimeiona kwenye blogu ya wavuti. Namshukuru Da Subi.

Picha hii ni kumbukumbu ya mambo yalivyokuwa enzi za Mwalimu Nyerere. Viongozi hawakuwa mbali na wananchi. Wote walikuwa wanafahamika kwa jina moja la "ndugu," ambayo ni kielelezo muhimu cha itikadi iliyokuwa inatawala. Hapakuwa na usultani kama ilivyo leo.

Tunapiga ngonjera kuwa sultani aliondolewa Visiwani, wakati usultani unaendelea kushamiri nchini.

Wednesday, February 22, 2012

Nilivyoanza Kupeleka Wanafunzi Tanzania

Nimetoka mbali, katika suala la kuwapeleka Tanzania wanafunzi wa vyuo vya Marekani. Mara baada ya kuja kufundisha katika Chuo Cha St. Olaf, nilianza kujishughulisha na masuala ya programu zinazowapeleka wanafunzi Afrika. Kama mmoja wa washauri wa programu hizo nilijifunza mengi. Baada ya miaka michache, nilianza kuwapeleka wanafunzi Tanzania.

Hapa kushoto niko na wanafunzi kwenye chuo kilichokuwa kinaitwa Danish, eneo la Usa River. Hii ilikuwa ni programu ya vyuo vilivyomo katika mtandao wa LCCT. Nadhani hiyo ilikuwa ni mwaka 1997. Hapo Danish, tulikuwa tunawapa wanafunzi mafunzo kuhusu masuala mbali mbali ya Tanzania, kwa wiki moja na kidogo. Baada ya hapo, kwa mujibu wa programu hii, niliwapeleka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kusoma kwa muhula mmoja.Hapa kushoto niko na wanafunzi wale wale katika nyumba niiyokuwa naishi pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu iitwayo "Research Flats."

Kadiri miaka ilivyopita, nimejijengea uzoefu na ufahamu mkubwa wa programu hizi. Nafahamu mikakati, mahitaji, changamoto, na faida za programu hizo kwa wahusika wa pande zote. Uzoefu wa kuwaandaa wanafunzi wa ki-Marekani kuishi katika utamaduni wa kigeni uliniwezesha kuandika kitabu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilikiandika mahsusi kuchangia programu hizo, na walimu wengine wanaopeleka wanafunzi Afrika wanakitumia, bila kuwataja watu wanaoenda Afrika kwa utalii, shughuli za kujitolea, na kadhalika.

Tuesday, February 21, 2012

Mtoto atoweka nyumbani na anatafutwa

Mtoto huyu pichani afahamikaye kwa jina la Fatuma katoroka nyumbani kwao maeneo ya Mbweni Masauti jana mchana na hajulikani alipo mpaka sasa. Alikuwa amevaa nguo ya kichwani na ameshika begi dogo jeusi. Kwa yeyote atakayemuona tunaomba awasiliane nasi kwa namba 0713 716 656 au ampeleke kituo chochote cha polisi kilicho karibu yake.

Chanzo: Michuzi blog

Monday, February 20, 2012

Kabumbu Mto wa Mbu

Miaka michache iliyopita, nilikuwa Mto wa Mbu na wanafunzi katika kozi kuhusu mwandishi Hemingway. Katika kupitapita mitaani, tulitokezea kwenye kiwanja cha mpira. Kabumbu ikuwa inaendelea kama kawaida. Lakini nilivutiwa kumwona mbuzi mweupe akivinjari hadi ndani ya uwanja.Kabumbu iliendelea bila wasi wasi. Najua kuwa ingekuwa mechi kubwa mjini kama Dar es Salaam, halafu mbuzi atinge uwanjani namna hii, watu wangesema mengi.

Sunday, February 19, 2012

Mitaani Arusha

Nimefika Arusha mara kadhaa, na nina picha nyingi za mji huo. Kama nilivyofanya kwa miji mingine, kwa mfano Namanga na Mbinga, naleta picha chache. Hapana shaka kuwa baadhi ya wasomaji wa blogu hii hawajafika Arusha. Nataka wapate fununu fulani.
Hapa kushoto ni mtaa wa kati kati ya mji, ambapo pana posta na ofisi za usafiri wa ndege, na hoteli na migahawa. Pana maduka ambamo mtu unaweza kununua vitabu na nguo na kazi za sanaa.

Hapa kushoto ni mnara wa kumbukumbu ya Azimio la Arusha. Azimio la Arusha lilitangazwa hapa Arusha, mwaka 1967.

Mji huu una historia ya kusisimua. Kati ya waasisi wake ni Kenyon Painter, mwekezaji m-Marekani kutoka Ohio. Alijenga posta, kanisa, hospitali, na majengo mengine muhimu, zaidi ya kufungua mashamba ya kahawa na kituo cha utafiti cha Tengeru.
Kwa zaidi ya karne moja, watu wengi maarufu kutoka duniani kote wamefika au kupita Arusha, kuanzia viongozi wa nchi hadi watengeneza filamu na waandishi maarufu kama Ernest Hemingway.

Umaarufu wa Arusha siku hizi uko zaidi kwenye utalii, mahakama ya Rwanda, vyuo na taasisi kama vile ESAMI na Tropical Pesticides Research Institute.Picha ninazoleta leo zimepigwa katika eneo la katikati ya mji.

Kwa vile nimefika Arusha mara kadhaa, na wanafunzi kutoka Marekani, baadhi ya watu mitaani wananifahamu, kama hao jamaa ninaoonekana katika picha hapa kushoto. Tunafurahi tunapokutana, na michapo inakuwa mingi.


Saturday, February 18, 2012

Sera ya Madini Tanzania: Wizi Mtupu

Nimeguswa na katuni hii ya Kijasti, ambayo nimeiona wavuti. Naamini kuwa sera ya madini Tanzania ni wizi mtupu. Hebu fikiria, kwa mfano: serikali ya CCM inatuambia kuwa inaipitia mikataba mibovu ya madini, ili kuziba mianya inayoliletea Taifa hasara, na ili kuhakikisha kuwa Taifa linafaidika na madini hayo.

Hapo nina suali: Je, waliosaini mikataba hii mibovu walikuwa wajinga wasioweza kuelewa kilichoandikwa, au walikuwa wamelewa gongo waliposaini, au walikuwa ni mafisadi? Na je, kwa nini hawawajibishwi?

Halafu, kwa kuzingatia kuwa serikali ya CCM bado inawaambia hao wanaoitwa wawekezaji waje nchini, je, imeshaandaa mikataba mipya ambayo inatoa kipaumbele kwa nchi? Kukosekana kwa uwazi katika suala hili la madini kunanipa hisia kuwa serikali ya CCM kwa makusudi inaihujumu nchi.

Ni fedheha kwa Tanzania kuonekana kuwa ni nchi maskini, na hata hao tunaowaita viongozi wanasema Tanzania ni nchi maskini, wakati ni nchi tajiri kwa rasilimali mbali mbali. Dhahabu yetu, kwa mfano, inayaneemesha makampuni kama Barrick Gold. Ni aibu kwa Tanzania.

Friday, February 17, 2012

Wadau Wangu wa Canada

Mara moja moja, katika blogu zangu, nimekuwa nikiandika kuhusu wadau wangu kama mwandishi wa vitabu. Kwa mfano, nimewahi kuandika kuhusu wadau wa Arusha, na Nebraska. Leo napenda kuwakumbuka wadau wangu wa Canada.

Hapa kushoto ni picha iliyopigwa Dar es Salaam mwaka 2004, wakati wa maonesho ya vitabu kwenye viwanja vya kumbukumbu za Taifa. Niko na dada yangu na wadau wa Canada, waliokuwa wanaishi Tanzania. Wakati ule nilikuwa nimechapisha vitabu viwili tu: Matengo Folktales na Notes on Achebe's Things Fall Apart.

Hao akina mama walipita kwenye meza yangu, wakaviangalia vitabu, halafu wakasema watapita tena baadaye kununua kitabu cha Matengo Folktales. Baada ya kusema hivyo, waliendelea na mizunguko yao katika vibanda vingine. Kwa kawaida, watu wakipita namna hii, huwa si rahisi kukumbuka kurudi tena. Lakini hao, baada ya muda mrefu, walirudi, wakanunua kitabu na tukapiga hiyo picha.

Hapa kushoto ni Jeff Msangi, mmiliki na mwendeshaji wa blogu maarufu ya Bongocelebrity. Alihusika katika kuinukia kwangu kwenye ulimwengu wa kublogu, kama nilivyoelezea hapa. Yeye ni mdau na mpiga debe mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kama inavyodhihirika hapa, na hapa. Sijawahi kuonana naye, ila namwona mtu wa karibu kwangu, kutokana na mawasiliano yetu.

Mdau mwingine ni Rene Kakou. Huyu ni bosi wa kampuni ya Groupe Macrobell, Inc. Anatoka Ivory Coast, lakini anaifahamu Tanzania vizuri, na anaipenda kama vile nchi yake. Tulionana mara moja tu, katika ndege kutoka Tanzania kwenda Ulaya, tukafahamiana na kubadilishana anwani na namba za simu.

Hatimaye alikisoma kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Ana michapo mikali kuhusu jinsi mambo yalivyokuwa wakati anakisoma kitabu hicho. Mara kwa mara ananikumbuka, kwa simu au katika ukumbi wa Facebook.

Ndoto ya mwandishi ni kuona maandishi yake yanasomwa. Nami nawashukuru wadau hao, na wengine wote ambao siwajui.

Thursday, February 16, 2012

Watu Tuliosoma Darasa Moja

Kitu kimoja kinacholburudisha moyo wangu ninapokuwa Tanzania ni kukutana na watu tuliosoma pamoja. Mwaka jana, wakati napita Songea, nilionana na Bwana Alto Kapinga, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Anatoka Lundumato, katika wilaya ya Mbinga. Tulisoma darasa moja, kuanzia la tano hadi la nane, katika Seminari ya Hanga, 1963 hadi 1966. Hiyo ilikuwa ni shule bora kabisa mkoani Ruvuma. Ingawa tulisoma zamani vile, tumebahatika kukutana ghafla mitaani Songea mara kadhaa katika miaka iliyofuata.

Baada ya kupita Songea, nilienda hadi kwetu milimani u-Matengo. Wakati wa kutembelea Maguu, nilikutana na Padri Simon Ndunguru, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Picha tulipiga kijijini Chicago. Padri Ndunguru, mwenyeji wa Mbinga, tulisoma darasa moja, kuanzia la tisa hadi la kumi na mbili, katika Seminari ya Likonde, 1967-70. Hiyo ilikuwa ni moja ya shule bora kabisa Tanzania kwa kufaulisha wanafunzi.

Tunapokutana namna hii, tunamshukuru Mungu kwa kutuweka hai hadi leo, kwani ni mapenzi yake tu, wala hatustahili. Tunawakumbuka pia wenzetu ambao wameondoka duniani.

Tamasha la Vitabu, Houston

Kila mwaka kunafanyika tamasha la vitabu mjini Houston, liitwalo National Black Book Festival. Ni tamasha linalowajumuisha waandishi, wachapishaji na wauzaji wa vitabu, klabu za wasoma vitabu, wahudumu wa maktaba, na wadau wengine wengi. Wanapata fursa ya kukutana na kufahamiana, kuongelea masuala mbali mbali yanayohusu vitabu.

Nimeshiriki tamasha la vitabu Minneapolis kwa miaka kadhaa, kama nilivyoandika hapa na hapa. Mimi hushiriki kama mwandishi wa vitabu hivi hapa. Hili tamasha la Houston nimelifahamu kwa miaka kadhaa, kwa kusoma taarifa zake. Kwa miaka yapata miwili iliyopita, nimekuwa nikiwazia kushiriki tamasha hilo.

Sio lazima niende mwenyewe Houston au kila mahali kwenye shughuli kama hizi. Ingekuwa nina washirika, kama nilivyodokeza katika blogu hii, wangeweza kuniwakilisha, kama nilivyowakilishwa na wadau wa utalii Mto wa Mbu katika maonesho ya utalii Arusha. Yote hiyo ni mipango ya kuitafakari na changamoto za kuzifanyia kazi. Penye nia pana njia, wala hakuna wasi wasi.

Wednesday, February 15, 2012

Maskat: Mbunifu wa Mitindo

Katika pita pita zangu mtandaoni, nilikumbana na taarifa kwenye blogu ya Swahili na Waswahili kuhusu mwanamitindo Maskat, m-Tanzania ambaye jina lake jingine ni Hayakuhusu. Nilivutiwa na taarifa hiyo, nikaifuatiliza zaidi, nikaona jinsi dada huyu alivyo mjasiriamali makini.

Sio tu anajibidisha katika fani hii ya mitindo, bali anazitumia vilivyo tekinolojia za mawasiliano ya kisasa. Utamkuta sehemu kama Youtube, Facebook na blogu yake. Anwani yake ni maskatdehaan@hotmail.com. Napenda kusoma habari za watu wa aina hii na pia kuzitangaza katika blogu yangu, kwani ni changamoto kwa wengine, hasa watoto na vjiana wetu. Wanasema kuwa picha inajeleza sawa na maneno elfu. Kwa kuangalia picha za Dada Maskat, napata hisia kuwa ni dada anayejipenda na kujiamini, anayejua anachofanya na anakoelekea. Hili ni fundisho muhimu kwa watoto wetu, na sisi wenye mabinti tuna sababu ya ziada ya kuuenzi mfano wa dada Maskat.

Monday, February 13, 2012

Mitaani Mbinga, 2011

Mwaka jana, tarehe 2 Agosti, nilipita Mbinga, mji mkuu wa wilaya yangu, nikapiga picha kadhaa. Hapa kushoto ni kituo cha mabasi. Hapo ndipo unapandia mabasi ya kwenda Mbamba Bay na Songea. Hapo pia unapanda mabasi au magari mengine yanayoenda vijijini katika wilaya hiyo.


Hapa kushoto ni mtaa mojawapo wa pembeni, karibu na kituo cha mabasi, upande wa barabara iendayo Songea.
Hapo ni mtaa mwingine, sehemu ya bondeni kutoka kituo cha mabasi.
Huo nao ni mtaa wa pembeni. Udongo wa Mbinga ni kama inavyoonekana pichani, sawa na ilivyo katika eneo lote kuanzia Songea hadi karibu na Mbamba Bay. Kahawa inastawi katika udongo huo, na hapa Mbinga kuna kiwanda cha kusindikia kahawa.

Siku zijazo ninapangia kuleta picha za mashamba ya kahawa, ngano, na kadhalika, ambayo yanazipendezesha sehemu za vijijini katika wilaya ya Mbinga.


Huo ni mtaa mwingine upande wa chini kutoka kituo cha mabasi. Mbinga ya leo sio kama ya miaka kumi au ishirini iliyopita. Ingawa nafika hapo karibu kila mwaka, daima naona mambo mapya. Kwa mfano, hoteli nzuri zinaongezeka. Mwaka jana nilifikia kwenye hoteli ambayo iko hapa kwenye dishi la satalaiti.


Mbinga ni mji ulio karibu na nyumbani kwangu Litembo. Kama unatoka Songea, ukitaka kufika Litembo, unapita hapa Mbinga na kuelekea mbele, juu milimani. Wilaya ya Mbinga kwa ujumla ina hali ya vuguvugu na pia baridi, na kadiri unavyoelekea milimani zaidi, baridi inaongezeka. Katika hiyo picha tumevaa kwa kufuata hali hiyo, nami nimejihami na jaketi la Shidolya Safaris ya Arusha.

Baadhi ya ndugu zangu wanaishi hapa Mbinga. Hapo kushoto niko na binamu yangu Remigius Komba ambaye anaishi hapo. Tulikutana hapo kituoni bila kutegemea. Hapa nyuma yetu unayaona magari yamepakia, tayari kwa safari. Hayo ndio magari ninayopanda kwa safari ya kutoka hapa Mbinga kwenda Litembo. Ingawa niko ughaibuni, ninapofika hapo Mbinga nagundua kuwa madereva na utingo wananifahamu vizuri.

Sunday, February 12, 2012

Iringa: Ofisini kwa Mwenyekiti Mjengwa

Katika mizunguko yangu mwaka jana nchini Tanzania, pamoja na wanafunzi wangu wawili, nilikaa siku kadhaa mjini Iringa. Hapo nilimtafuta Mwenyekiti Mjengwa, mmiliki na mwendeshaji wa Mjengwablog. Tulienda ofisini kwake katika Akiba House. Tulikaribishwa vizuri, tukaelezwa shughuli za ofisi hii.Hatukukaa sana hapa ofisini. Tuliulizia mahali pa kupata chakula cha mchana na Mwenyekiti akatupeleka Neema Craft. Tulipata fursa ya kuongea naye kuhusu mambo kadhaa, yakiwemo ya utaratibu wa vyuo vingi vya Marekani wa kupeleka wanafunzi kwenye masomo nchi za nje na pia kuhusu mawasiliano ya kijamii kama vile blogu. Baada ya hapo tulipanda dala dala tukaenda Kalenga. Natumia dala dala kwa sababu ni njia nzuri ya wanafunzi wangu kufahamiana na wa-Tanzania.

Saturday, February 11, 2012

Matangazo ya Biashara

Wengi tumeshaliona tangazo hilo hapa kushoto, kwani limetokea sana mitandaoni. Linachekesha na kuvutia. Linatosha kumfanya mtu atafute mgahawa huu ili akashuhudie mwenyewe huduma za huyu Hassan.

Mtangazaji ametumia ubunifu wa kuwateka watu kisaikolojia. Anatafuta biashara, lakini anafanya ucheshi pia. Hiyo ni mbinu ya aina yake.

Kuna biashara za namna mbali mbali. Ziko zinazouza bidhaa na nyingine zinauza huduma. Kwa vyovyote vile, ubora wa kinachouzwa ni msingi wa mafanikio kwa mfanyabiashara.

Lakini, pamoja na ubora wa kinachouzwa, ni muhimu kwa mfanyabiashara kuielewa saikolojia ya wateja. Mteja ajisikie amekaribishwa vizuri, sio tu auziwe alichokitafuta. Ajisikie amethaminiwa. Kumvumilia na kumjibu vizuri mteja mkorofi ni muhimu. Kumshukuru mteja ni muhimu.

Mfanya biashara daima ajiulize mteja wake anajisikiaje wakati wa kuhudumiwa na baada ya kuhudumiwa. Mteja asiyeridhika, au aliyeudhika ni balaa. Atakwenda kuwaambia wengine maudhi yaliyomfika, nao hawataenda mahali hapo, labda iwe hakuna mahali pengine. Ni silika ya binadamu kuwa tukiwa na machungu moyoni, tunahitaji kumpata mtu au kuwapata watu wa kuwaelezea, watusikilize. Ndivyo mteja aliyeumia anavyofanya. Biashara ikididimia, mfanyabiashara ajitafakari mwenyewe kwanza, kabla ya kutafuta wachawi

Kwa upande mwingine, mteja aliyeridhika na kufurahi ni mpiga debe mkubwa. Hatakosa kuwaeleza wengine. Ni ukweli usiopingika kuwa maamuzi yetu ya nini cha kununua, au wapi, mara nyingi tunafuata ushauri wa watu wengine. Mwulize mtu mahali kama Dar es Salaam akuambie teksi ipi uchukue au ukalale gesti ipi, au uende mgahawa upi, au baa ipi, hutakosa kuelezwa. Atakuelekeza kule ambako alipata au anapata huduma bora. Kila mmoja wetu ni mpiga debe, kwa maana kwamba tunawaambia wenzetu wapi kwa kupata huduma au bidhaa bora. Tunafanya hicho kibarua kwa furaha, bila malipo, na mfanyabiashara mwenyewe tunayempelekea wateja huenda hajui. Mambo yanakwenda kwa mtindo wa watu kuambiana. MMambo

Masuala haya yananivutia na yana umuhimu kwangu kwa vile nami naendesha kikampuni ambacho nilielezea habari zake hapa. Ninapata changamoto kadha wa kadha, lakini kwa kusoma vitabu na kuhudhuria warsha, najifunza namna ya kuzikabili na kuiboresha kampuni yangu. Suala la kumridhisha kila mteja, kwa mfano, iwe ameagiza kitabu au ameomba ushauri, ninalizingatia sana.
(Mchora katuni inayoonekana hapa juu ni Nathan Mpangala)

Thursday, February 9, 2012

Mfanya Usafi Anajivunia Kitabu Hiki

Jioni hiii, hapa chuoni St. Olaf, nikiwa katika jengo kubwa ambamo kuna mgahawa, posta, na vyumba vya mikutano, amenizukia mzee moja ambaye ni mfanya usafi. Nimefahamiana naye miaka kadhaa.

Alivyoniona tu, kwa mbali kidogo, alinipungia mkono akiniita, "Come, come, come!," kama vile kuna dharura. Sikujua kuna nini, bali nikamfuata.

Alitangulia kuelekea kwenye sehemu alipokuwa anafanya usafi. Wakati ametangulia, akienda kwa kasi, aliniambia kuwa anataka nisaini kitabu. Alitokomea ndani kisha akaibuka na nakala ya Matengo Folktales. Niliguswa sana, nikasaini, naye akafurahi sana, kama vile amepata tuzo fulani.

Mzee huyu, ambaye jina lake ni Maurice, alishaniambia miezi mingi ilyopita kuwa anasoma kitabu changu. Sikushangaa kwa jinsi ninavyowafahamu wa-Marekani. Mtu aliyelelewa katika utamaduni usiothamini vitabu atashangaa inakuwaje mzee achape kibarua cha kusafisha majengo, halafu atumie dola nyingi kununulia kitabu. Kwa jinsi ninavyowafahamu hao wa-Marekani, kwenye suala la vitabu wako makini. Hudhuria tamasha la vitabu, au nenda kwenye maduka ya vitabu, utajionea mwenyewe.

Wednesday, February 8, 2012

Buriani: Mwandishi Faraji Katalambula

Jana tumepata habari kuwa mwandishi Faraji Katalambula, amefariki Dar es Salaam. Nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School, 1971-72, Faraji Katalambula alikuwa anavuma kuliko waandishi wote wa ki-Swahili waliokuwa hai wakati ule. Picha ya Faraji Katalambula hapa kushoto nimeipata Hiluka Filmz.


Nakumbuka jinsi riwaya yake ya Simu ya Kifo ilivyoleta msisimko kwa wafuatiliaji wa riwaya za upelelezi. Laiti ningesoma maandishi yake tangu miaka ile. Leo ningeweza kuelezea hili au lile kwa kujiamini.

Lakini miaka ile mimi nilikuwa sijishughulishi sana na ki-Swahili. Nilizama katika maandishi ya ki-Ingereza. Vijana wenzangu waliopenda riwaya za ki-Ingereza walikuwa wanapenda sana riwaya kama za Ian Fleming na James Hadley Chase. Mimi sikuwahi kuzisoma hizo.

Nikirudi kwenye uandishi wa ki-Swahili, napenda kusema kuwa nashukuru kuwa miaka iliyofuata, nilijirudi, kama ninavyoelezea katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Nami sasa nimejiunga na wasomaji wanaowaenzi waandishi wetu wanaotumia ki-Swahili.

Faraji Katalambula aliandika pia riwaya zingine, akaingia pia katika tasnia ya filamu. Ametoa mchango mkubwa kwa jamii, na ingawa ameondoka, kama walivyoondoka akina Mgeni bin Faqihi, Shaaban Robert, Amri Abedi, na Mathias Mnyampala, mchango wake utadumu duniani. Apumzike kwa amani.

Tuesday, February 7, 2012

Kumbukumbu ya Kuzaliwa Charles Dickens

Leo ni kumbukumbu ya kuzaliwa Charles Dickens yule mwandishi maarufu sana wa riwaya katika lugha ya ki-Ingereza. Alizaliwa February 2, 1812, Landport, maeneo ya Portsea, Uingereza.

Sisi tuliosoma shule zamani, tulibahatika kusoma maandishi ya Dickens. Mimi nilianza darasa la kwanza mwaka 1959. Tulianza kujifunza ki-Ingereza darasa la tatu, na miaka michache tu baadaye tulikuwa tunaweza kusoma maandish ya ki-Ingereza na kuongea ki-Ingereza. Dickens ni mmoja wa waandishi waliotupa motisha kubwa ya kusoma maandishi ya ki-Ingereza

Tulipokuwa sekondari, tulikuwa tunasoma maandishi ya waandishi mashuhuri kama Shakespeare, Jules Verne, Robert Louis Stevenson, Chinua Achebe, Daniel Defoe na Charles Dickens.

Nani atasahau tulivyovutiwa na riwaya ya Dickens ya Oliver Twist? Ni nani anayeweza kuwasahau wahusika wake wakuu, kama vile Oliver Twist, The Artful Dodger, na m-Yahudi Fagin? Katika riwaya hii, Dickens alielezea, kwa namna isiyosahaulika, matatizo ya watoto wa shule miaka yake, ikiwa ni pamoja na uongozi mbaya, na mazingira duni ya kuishi, ikiwamo shida chakula. Ni matatizo yanayowakumba watoto katika shule zetu leo.

Vitabu vya Dickens ni pamoja na Hard Times, The Old Curiosity Shop, A Tale of Two Cities, Dombey and Son, David Copperfield, Martin Chuzzlewit, A Christmas Carol, Nicholas Nickleby, na Pickwick Papers. Wiki chache zilizopita, nilielezea jinsi nilivyoshiriki katika kuwakilisha kitamthilia hadithi ya A Christmas Carol.

Dickens alikuwa na kipaji cha hali ya juu cha kuelezea matatizo ya jamii na tabia za wanadamu, akitia chumvi na kutumia lugha ya kuvutia sana. Alikuwa mtetezi wa walalahoi nchini mwake na duniani kwa ujumla. Alitembelea Marekani, ambako aliunga mkono harakati za kuleta uhuru wa watumwa. Ni mwandishi aliyeiteka dunia ya wakati wake na hadi leo aneendelea kuwika.

Sunday, February 5, 2012

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

(Makala hii nilishaichapisha katika blogu yangu. Ninaichapisha tena, wakati huu CCM inapoazimisha miaka 35 ya kuwepo kwake)

--------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

Saturday, February 4, 2012

Wanafunzi Walioenda Tanzania Wameongea Leo

Mwaka jana, niliandika katika blogu zangu kuhusu mizunguko yangu Tanzania na wanafunzi katika programu ya LCCT. Baadhi ya taarifa ni hii hapa na hii hapa.

Baada ya kuwa nao Tanzania kwa wiki tatu, niliwaacha Chuo Kikuu Dar es Salaam, ambapo walisoma kwa muhula moja, kwa mujibu wa programu. Wakisharejea Marekani, wanapata fursa ya kuongelea safari yao, masomo waliyosoma, na maisha yao Tanzania kwa ujumla.

Shughuli hiyo imefanyika leo, Chuoni St. Olaf. Kwa vile wanafunzi hao wanasoma kwenye vyuo hapa Marekani, wanakuwa na upeo wa kufananisha mambo ya Chuo Kikuu Dar na vyuo vyao, kuanzia maisha ya wanafunzi, viwango vya ufundishaji, na kadhalika.Wanapokuwa Chuo Kikuu Dar, wanafunzi hao wa LCCT wanapata fursa ya kujitolea kama waalimu wasaidizi katika shule ya msingi ya Mlimani. Mwezi Agosti mwaka jana, nilipoenda hapo shule ya msingi kutoa taarifa kuhusu ujio wa wanafunzi hao, walimu walisema mpango huu wa wanafunzi wa ki-Marekani kujitolea pale una manufaa. Kwa mfano, watoto wanapata fursa ya kuboresha ufahamu wao wa ki-Ingereza.Kila mwaka sisi washauri na waendeshaji wa programu tunapata fursa ya kuwasikia wanafunzi wetu wakielezea mengi wanayojifunza wakiwa Tanzania, na jambo moja la msingi ni kule kuifahamu nchi na jamii ya Tanzania. Wanafunzi hao huwa tumewaandaa vilivyo, kwani wanapaswa kusoma vitabu mbali mbali vinavyohusu historia, siasa, uchumi, na utamaduni wa Tanzania, yakiwemo maandishi ya Mwalimu Nyerere.


Napenda kumalizia kwa kusema kuwa shughuli za kuendesha programu hizi ni za kujitolea. Hivi vikao vyetu, ambavyo vinadumu siku moja nzima na vinaendelea kwa nusu siku ifuatayo, ni vya kujitolea. Hapa Marekani sijaona utamaduni wa posho za vikao kama ilivyo Tanzania. Mnaletewa chakula, saa ifikapo, lakini sijawahi kuona wala kusikia kuhusu vibahasha kama Tanzania. Nimeona niseme hivyo, ili kuonyesha tofauti ilivyo, na papo hapo, hapa Marekani kazi inafanywa kwa roho moja.