Friday, July 29, 2011

Niko Songea

Niko mjini Songea. Niliwasili jana jioni kwa basi kutoka Dar es Salaam. Mchana huu nimekuwa nikikata mitaa ya jiji letu hili la mkoa wa Ruvuma.
Nimepiga picha sehemu mbali mbali. Na leo hapa ninaziweka chache. Zingine nitaziweka baadaye, wadau wapate kujionea wenyewe taswira za jiji letu hili.

Wadau ambao mlifika Songea zamani mkija hapa sasa mtaona mabadiliko mengi.Baada ya kuishi siku kadhaa Dar es Salaam, tukiteseka na mgao wa umeme, nimeshangaa kuona umeme uko siku nzima hapa Songea, na wenyeji wanasema hawana mgao wa umeme hapa. Wanashangaa habari hizi za Dar es Salaam.

Tuesday, July 12, 2011

Nimebeba Maboksi ya Kwenda Njombe (NJOUCO)

Jana na leo nimehenya sana na kazi ya kubeba maboksi. Kwanza niliyafungasha ofisini kwangu, halafu nikayapakia katika gari. Kisha nikaendesha gari maili hamsini na kidogo hadi mjini Coon Rapids, ambako nilihenya tena kuyapakua na kuyaingiza katika stoo kubwa. Hapa nilipo nimechoka na nasikiliza maumivu mwilini.

Hayo maboksi ni shehena ya majarida ambayo nayapeleka chuo kikuu kipya cha Njombe, NJOUCO. Ni majarida ya "New England Journal of Medicine" (NEJM), na "Journal of the American Medical Association" (JAMA), kwa kipindi cha kuanzia miaka nane iliyopita hadi miezi michache iliyopita.

Hata mimi ambaye siko katika taaluma ya udaktari nafahamu kuwa NEJM na JAMA ni majarida maarufu. Majarida hayo nimepewa na mzee moja daktari mstaafu ambaye alipata habari kuwa huwa napeleka vitabu Tanzania. Ninamshukuru sana mzee huyu.

Niliwahi kuongelea habari ya hiki Chuo cha Njombe katika blogu hii. Nilipomweleza Mchungaji Dr. Kimilike ambaye ni mratibu wa NJOUCO kuwa ninayo majarida hayo, aliniunganisha na Global Health Ministries, ambao wanashughulikia miradi ya aina hii sehemu mbali mbali za dunia, hasa upande wa afya. Shukrani tele kwa msaada wao wa kusafirisha majarida hayo. Jumla nimefungasha na kupeleka maboksi 12.

Kinachofurahisha ni kuwa baada ya miezi kadhaa, shehena hii ya majarida itatua NJOUCO. Ni hazina kubwa kwa wanafunzi, walimu, madaktari, na watafiti katika masuala ya afya na matibabu.

Napenda kumalizia kwa kusisitiza kuwa hiki ni chuo kipya, ambacho mahitaji yake ni mengi. Hali hii inakuwa ni changamoto kwetu kushiriki katika kuleta mafanikio yanayotarajiwa.

Sunday, July 10, 2011

Nimeingia Tena Duka la Half Price Books

Jana, nikitokea mkutanoni Minneapolis, nilipita mjini Apple Valley, nikaingia duka la Half Price Books, kama kawaida. Ilikuwa siku nzuri, jua linawaka na hali ya hewa ya joto la kupendeza. Kama kawaida, niliwaona watu wengi dukani, watoto hadi wazee, wake kwa waume, wakiwa katika kuangalia vitabu, kusoma, na kununua.


Wakati wote, watu wanaingia na kutoka. Kwa utaratibu wa maduka ya Half Price Books, ukiwa na vitabu unavyotaka kuviuza, unavileta, na Half Price Books wananunua. Ndio maana daima utawaona watu wanaingia na mizigo ya vitabu, wakati wengine wanatoka na vitabu walivyonunua.

Kama kawaida, ninapokuwa katika duka la vitabu namna hii, ninajiwa na mawazo mengi. Jana, wakati nawaangalia watoto waliokuwemo katika duka hili, nilikumbuka habari niliyoisoma wiki hii kuhusu fiesta mjini Iringa.

Taarifa ilisema kuwa katika fiesta hiyo, kulikuwa na watoto hadi usiku wa manane. Nilihuzunika. Wakati wenzetu wanawalea watoto wao katika usomaji wa vitabu, sisi watoto wetu tunawalea katika fiesta hadi usiku wa manane. Huku Marekani watoto wanaenda kulala kwa wakati unaofaa; hawaonekani kwenye shughuli za usiku namna hiyo.

Wednesday, July 6, 2011

Binti m-Kenya Ang'ang'ania Kitabu

Tarehe 11 Juni, nilishiriki maonesho yaliyoandaliwa na African Health Action, kama nilivyoezea katika makala hii. Shughuli za aina hii huwa zina mambo mengi sana, na haiwezekani kuyaelezea yote katika makala ya blogu. Kuna mambo mengine ambayo yanabaki kichwani kama kumbukumbu isiyosahaulika.

Basi, kumbukumbu mojawapo ni jinsi familia moja ilivyokuja kwenye meza yangu, ambapo nilikuwa nimeweka vitabu na maandishi mengine. Katika kutambulishana, walijieleza kuwa wao ni wa-Kenya.

Wakati wakiangalia vitabu, binti yao mkubwa alisema kuwa amesoma kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differenes. Nilipomwuliza alikisoma wapi, alisema amekisoma Duluth. Nilihisi kuwa atakuwa amekipata kupitia kwa wamiliki wa kampuni ya Kili Culture Tours and Safaris, naye alikiri hivyo. Mama Neema, ambaye ni m-Tanzania, na mume wake, ni mashabiki na wapiga debe wakubwa wa vitabu vyangu.

Huyu binti m-Kenya alipokiona kitabu cha CHANGAMOTO, alisema kuwa anakitaka. Wakati huo baba mtu alikuwa analipia vitabu viwili alivyovichagua. Binti alisisitiza kuwa anakitaka hicho pia, na baba alilipia. Jumla ilikuwa yapata dola 35. Kumbuka kuwa hao si matajiri, bali ni wabeba boksi wenzetu.

Kutokana na uzoefu wangu, naweza kusema kuwa kwa ujumla, wa-Kenya wanavithamini vitabu. Nilianza kuona tabia yao hiyo nilipotembelea Kenya kwa mara ya kwanza, mwaka 1989. Wana maduka mengi ya vitabu, na ukiingia humo utawakuta. Siku za kufungua shule, wazazi na watoto wanafurika katika maduka ya vitabu. Ukisoma magazeti ya Kenya, utaona mara kwa mara wana safu ambamo wanaongelea vitabu. Huku Marekani, nawaona wa-Kenya kwenye matamasha ya vitabu.

Mimi mwenyewe kama mwandishi wa vitabu nimeguswa na wa-Kenya kwa namna mbali mbali. Kwa mfano, muda mfupi baada ya kitabu cha Africans and Americans kuchapishwa, gazeti la Mshale, la wa-Kenya, liliandaa shughuli mjini Minneapolis ya kukitambulisha kitabu changu kwa umma. Soma hapa. Soma pia taarifa hii, na hii.

Nikirudi kwenye habari ya binti aliyeng'ang'ania kitabu, naweza kusema kuwa wa-Kenya ndivyo walivyo. Ningeweza kuleta taarifa zingine. Kwa mfano, niliwahi kwenda chuo cha Principia kutoa mhadhara. Binti mmoja wa Kenya aliposikia kuwa nimechapisha kitabu cha ki-Swahili, alitaka kukipata. Baada ya mimi kumpelekea, alikisoma hima, akaniandikia ujumbe kuelezea hisia na mtazamo wake kuhusu kitabu kile. Naona nina sababu ya kusema kuwa wa-Kenya ndivyo walivyo.

Tuesday, July 5, 2011

Ugali wa Yanga

Ukitamka ugali wa Yanga, utawachokoza wa-Tanzania waliokulia enzi za Mwalimu Nyerere. Utawakumbusha wakati ambapo walilazimika kula ugali wa njano. Kilikuja kipindi ambapo nchi ilikuwa na upungufu wa chakula, na Nyerere alipokea unga wa njano kutoka Marekani. Kwa shingo upande na masononeko, wa-Swahili walitumia unga huo, maarufu kama Yanga, na mpaka leo hawajamsamehe Nyerere kwa kuwalisha Yanga.

Wa-Tanzania walipolalamikia unga huo, Mwalimu Nyerere alijibu kwa ukali kuwa wasiotaka Yanga ni watu wasio na shida. Naomba wadau wenzangu wa wakati ule wanisahihishe kama nimepotosha.

Sio kwamba tulikula Yanga miaka yote ya utawala wa Mwalimu Nyerere, na sio kwamba Mwalimu Nyerere alitaka Yanga ndio iwe chakula cha wa-Tanzania, au kwamba aliifurahia hali hiyo. Nawaomba wadau wanikumbushe ni mwaka upi au miaka ipi ambayo tulipata dhiki hiyo ya kula Yanga.

Je, tunalitafsiri vipi suala la unga wa Yanga? Kwa mtazamo wangu, kuna kipengele muhimu cha tofauti za tamaduni. Tofauti hizi zinajitokeza katika mambo mengi, na kwa namna nyingi, likiwamo hili suala la vyakula.

Tofauti za tamaduni zinaweza kuathiri kukubalika au kutokukubalika kwa bidhaa. Kwa mfano, namna bidhaa inavyotangazwa katika jamii au utamaduni fulani na kuwavutia watu inaweza ikawachefua watu wa jamii na utamaduni tofauti.

Hata rangi zinaweza kuibua hisia tofauti katika tamaduni mbali mbali. Rangi ya bidhaa inayowavutia watu wa utamaduni fulani inaweza kuwachefua watu wa utamaduni tofauti. Mfanyabiashara anaweza kuhujumu biashara yake kwa vile tu ameitangaza kwa kutumia rangi fulani au bidhaa yenyewe ina rangi isiyokubalika katika jamii fulani.

Katika utamaduni wetu wa-Swahili, ambao tunakula ugali, unga wa manjano haukubaliki. Kama ni unga wa mahindi, tunataka uwe mweupe. Hii ndio jadi tuliyozoea. Ni sehemu ya utamaduni wetu. Wengine wanatumia unga wa muhogo au ulezi. Lakini Yanga haikubaliki.

Lakini Marekani, Yanga iko kila mahali, sambamba na unga mweupe. Mwanzoni, katika kuishi kwangu Marekani, nikienda dukani, nilikuwa naikwepa kabisa Yanga. Lakini kidogo kidogo nilianza kuitumia, hadi nikafikia hatua ya kuupenda kabisa ugali ya Yanga.

Uamuzi wa kuleta Yanga Tanzania haukuzingatia suala la tofauti za tamaduni. Sijui ni nani aliyefanya uamuzi ule, lakini naamini haukuwa kwa nia mbaya. Kilichokosekana ni elimu sahihi. Nahisi wangejua wangeweza kubadilisha na kuleta unga mweupe. Hapangetokea manung'uniko, wala jazba za Mwalimu Nyerere.

Suala la ugali wa Yanga ni kielelezo kidogo cha masuala yanayoikabili dunia katika utandawazi wa leo, na masuala haya yatazidi kuongezeka kwa kadri dunia inavyozidi kuwa kijiji. Katika maandishi, warsha na mihadhara, najaribu kuelezea masuala hayo. Ni muhimu sana, kama ninavyosisitiza katika kitabu cha Africans and Americans. Elimu hii kama ingefanyika ipasavyo, ingetuepushia matatizo yaliyojitokeza wakati wa Mwalimu Nyerere, na pia ingepunguza jazba ambazo bado zipo kuhusiana na suala la kulishwa Yanga.

Friday, July 1, 2011

Majungu Kuhusu Nyerere: Jishindie Dola 100

Mengi wanayosema na kuyaamini wa-Tanzania kumhusu Mwalimu Nyerere ni majungu. Hayo nimeyafahamu kwa muda mrefu. Ni wajibu wetu kuandika habari sahihi kuhusu Mwalimu Nyerere kama ilivyo kwa masuala mengine yoyote. Nami, kwa kuanzia, nimechapisha kitabu kiitwacho CHANGAMOTO, ambamo, pamoja na mengine yote, kuna makala na dondoo mbali mbali kuhusu Mwalimu Nyerere.

Kati ya majungu ambayo yanavuma sana ni kwamba Mwalimu Nyerere hatimaye alikiri kuwa Ujamaa umeshindwa. Madai haya yanasikika vijiweni, na nimewahi kuyaona kwenye maandishi pia, kama vile blogu, na gazeti la An Nuur, ambamo kauli alizozitoa Mwalimu Nyerere katika mahojiano na CNN zimenukuliwa, lakini sio kwa usahihi.

Ninavyojua, Mwalimu Nyerere hakuwahi kusema kuwa Ujamaa umeshindwa. Ninajiamini kabisa kwa hilo. Napenda kutangaza kuwa yeyote atakayeleta ushahidi kuthibitisha kuwa Mwalimu Nyerere alikiri kuwa Ujamaa umeshindwa aulete ushahidi huu hapa kwenye blogu yangu. Ikidhihirika kuwa ushahidi umetolewa, nitampelekea mhusika dola 100 kama kifuta jasho na shukrani yangu, kwani atakuwa amenielimisha kwa jambo ambalo sikulijua. Ninathamini sana elimu.

Tangu nilipoanzisha blogu hii, nilitamka kuwa shughuli yake mojawapo itakuwa ni kumwenzi Mwalimu Nyerere. Kuyaanika hadharani majungu dhidi ya Mwalimu Nyerere ni sehemu ya kazi hiyo. Naanza na majungu niliyoyataja hapa juu. Kazi kwenu.