Saturday, December 4, 2010

Nimekutana na Mratibu wa Chuo Kikuu cha Njombe

Tarehe 9 Oktoba nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Bill, akisema kuwa angependa kumleta kwangu mgeni kutoka Tanzania, kwa mazungumzo. Alimtaja mgeni kuwa ni Dr. Peter Kimilike.

Basi, tarehe 11 walifika hapa Chuoni St. Olaf. Tulifurahi kufahamiana. Dr. Kimilike ni mchungaji m-Tanzania ambaye anaratibu shughuli za kuanzisha Chuo Kikuu cha Njombe. Tulifurahi kutambua kuwa kuna watu maarufu ambao yeye na mimi tunafahamiana nao, kama vile Danford Mpumilwa, afisa habari wa Mahakama ya ki-Mataifa inayoshughulikia mauaji ya Rwanda (ICTR), na Rev. Dr. Anneth Munga, mkuu wa Chuo cha Sebastian Kolowa

Maongezi yetu yalilenga zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Njombe. Nilimweleza Dr. Kimilike kuwa ninafuatilia kwa karibu maendeleo ya vyuo Tanzania. Kila ninapoenda kule, ninatembelea vyuo. Nikampa mifano ya vyuo nilivyotembelea: Tumaini (Iringa), Makumira (Arusha), na Sebastian Kolowa (Lushoto). Ninaelimika sana ninapoongea na walimu na wengine kuhusu hali halisi ya vyuo vyetu na mahitaji yaliyopo. Kwa mtu anayekaa ughaibuni, kuna fursa za kuchangia vitu kama vitabu.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ninakitembelea mara kwa mara. Nilisoma na kufundisha hapo, na kila mwaka napita hapo kufanya utafiti, kuongea na walimu na pia wanafunzi. Napenda kutembelea shule za kila aina, kuanzia shule za msingi, kujielimisha kuhusu hali halisi.

Kuhusu Chuo Kikuu cha Njombe, nilimwambia kuwa nimefuatilia habari zake kwa miezi mingi, mtandaoni, kama vile Arusha Times. Alinieleza hatua iliyofikiwa na mipango inayoendelea. Kuna mahitaji mengi, kuanzia ya kukarabati majengo na kujenga mengine, kununua vitabu na majarida, vifaa vya maabara, kompyuta, na kuleta walimu.

Mwanzo ni mgumu, kama kawaida. Unahitajika mtandao wa wadau na washiriki wa aina mbali mbali. Cha kutia moyo ni kuwa msingi umeshajengwa kwa kutumia uwezo na nguvu za wananchi, ambao wamechanga chochote walicho nacho, iwe ni fedha, mazao, hata jogoo.

Chuo kina mikakati ya kujiendesha, kwa kuanzisha miradi kama ya kupanda miti kwa ajili ya mbao za kuuza, na pia kupanda mazao kama vile matunda. Dr. Kimilike anaelezea zaidi suala hili hapa.
Nimewekwa katika mtandao wa wahamasishaji wa Chuo Kikuu Cha Njombe. Nimelipokea jukumu hili kwa mikono miwili. Hizi picha tulipiga ndani ya uwanja wa ndege wa Minneapolis, Minnesota, wakati Mchungaji Kimilike alipokuwa anarudi Tanzania, Oktoba 24, baada ya ziara yake ya Marekani.

5 comments:

Emmanuel said...

Salam Prof,
Ninakupongezeni sana sana ninyi mnaojitolea kuleta mabadiliko ya kweli kwa elimu ya Tanzania. Ni wajibu wa kila raia kuipenda na kuisaidia jamii yake kwa hali na mali. Ninakuombeeni heri na fanaka katika majukumu yenu wewe na Mchungaji mwanzilishi wa chuo cha Njombe

SIMON KITURURU said...

Mmmmh!

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe Ndugu Emmanuel. Kusema kweli, wanaostahili pongezi ni hao walioanzisha wazo hili na kujitosa katika utekelezaji kama wanavyofanya. Hao ndio wa kushukuriwa kwa kweli.

Angalia, kwa mfano, huyu bibi mzee aliyechangia jogoo. Ni mfano wa kuigwa, kwani unatukumbusha kwamba hata kama hatuna pesa, tuna mihogo, mananasi, na kuku ambazo tunaweza kuchangia, tukajenga au kuendesha chuo kikuu.

Watani zangu Wasukuma wana ngombe za kutosha kuendesha chuo kikuu chochote, ila tu sisi wasomi tukipata chuo tuendeshe, hatuwazii hilo. Tunadhani njia pekee ni kwenda serikalini tukapate mgao wa bajeti, au kungojea wafadhili wa ng'ambo. Mchakato huu wa Chuo Kikuu cha Njombe unatufundisha kuwa wakati umefika wa kuwafuata Wasukuma :-)

Lechion said...

HERI YA SIKUKUU YA NOELI NA MWAKA MPYA

Kwa wote wenye mapenzi mema na elimu taehe 27 Desemba 2010 Chuo Kikuu cha Njombe kinawaalika katika jukwaa wazi la kutathmini maendeleo ya kuasisi Chuo Kikuu Bora. Mkutano huo utafanyika Kidugala, Njombe mahali ambapo ndipo vitivo vya kwanza vinatarajiwa kuanza 2011. Karibu kwa hali na mali.
Dr. Peter Kimilike
MRATIBU NJOUCO

Mbele said...

Mpendwa Mchungaji Kimilike

Shukrani kwa ujumbe. Umefanya vema kuuleta hapa, kwani blogu hii inasomwa na wadau kutoka nchi nyingi duniani, sio Tanzania tu. Wataupata vizuri, hata kama hawataweza kusafiri kuja kuhudhuria.