Wasomaji wa blogu zangu, hii na ile ya ki-Ingereza, wanafahamu ninavyopenda kujishughulisha na masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa leo.
Nafanya shughuli hizi si kwa ajili ya kutafuta umaarufu, bali naamini ni wajibu kwa wanadamu kusaidiana katika maisha na kuifanya dunia iwe bora kuliko ilivyo.
Miezi ya karibuni nimejishughulisha sana na matatizo yanayowapata wahamiaji wa ki-Somali katika jimbo la Minnesota, ambalo linaongoza kwa idadi ya wahamiaji wa ki-Somali. Wasomaji wa blogu zangu watakumbuka taarifa za shughuli zangu katika mji wa Faribault.
Matatizo kama haya ya Faribault yako pia katika miji mingine, kama vile St. Cloud. Kutokana uzoefu nilioupata Faribault, nimeanzisha mawasiliano na ndugu Mohamoud Mohamed, mkurugenzi wa SASSO, jumuia inayoshughulikia masuala ya wa-Somali mjini St. Cloud.
Nilimpelekea nakala ya kitabu cha Africans and Americans, kama mchango wangu na changamoto. Jana ameniambia kuwa kitabu amekipata, anaendelea kukisoma, na anakipenda. Atawaonyesha wadau wa St. Cloud: halmashauri ya mji, shule na vyuo, idara ya polisi, mahospitali, na kadhalika. Nami nilimhakikishia kuwa ni jambo bora. Badala ya watu kununiana tu au kugombana, ni vema wakaanza utaratibu wa kuzungumzia matatizo kama ilivyofanyika Faribault, na ikapokelewa vizuri.
Kama ninavyosema katika mihadhara, blogu na maandishi mengine, matatizo ya aina hii yanayoikumba miji ya Faribault na St. Cloud yanajitokeza katika miji na jamii nyingine duniani: Afrika, Asia, Australia, Marekani, Ulaya, na kwingineko, na yataongezeka, kutokana na mwenendo wa utandawazi wa leo. Ninapokuwa Dar es Salaam, kwa mfano, nasikiliza na kutafakari minong'ono na majungu kuhusu wa-China, ambao wanaendelea kuja katika mji ule. Niliwahi pia kuongelea tafrani iliyotokea Zanzibar. Kinachobaki ni sisi kujizatiti kwa kuelimishana kuhusu tofauti zetu na kutafuta namna ya kuishi bila matatizo.
Najiandaa kushiriki katika masuala ya St. Cloud. Mbali ya umuhimu wake kwa jinsi hali ilivyo, ni fursa ya mimi kujiongezea ujuzi na uzoefu nitakaoutumia katika kuwasaidia wengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
4 comments:
Pole sana na majukumu hayo Mkuu Mbele, na juhudi zako tunaziona, kama ningelikuwa mkuu wa nchi ningekuwa kazi moja katika wizara ya mambo ya nchi za nje, kama sio uwaziri kabisa!
Shukrani emu-three, kwa ujumbe wako. Moyo wangu umo katika shughuli hizi, ambazo zimeyapa maisha yangu malengo, mwelekeo, faraja na mafanikio.
Ninaposema mafanikio, namaanisha ule uwezo wa kuwasaidia wanadamu kuelewa mambo na kutatua matatizo yanayowakabili. Hii ndio dhana yangu ya mafanikio, na ninaona mafanikio haya katika shughuli zangu.
Muda wote nawakaribisha watu kuhudhuria warsha zangu, kusoma vitabu vyangu, na kadhalika. Kama ninavyoelezea kwenye blogu zangu, naona mwamko mkubwa huku Marekani, ila Tanzania bado sana, ingawa nimeenda kule kwa miaka mitatu mfululizo, kwa gharama kubwa, na kujaribu kufanya yale ninayofanya huku Marekani.
Profesa Mbele, nadhani kwa Tanzania kazi ya uandishi wa vitabu inakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile ukosefu wa hamasa na pengine soko la vitabu. Kazi ya uandishi si kazi rahisi ukizingatia uhitaji wake muda na gharama za uandikaji na hata uchapishaji.
Ni matumaini yangu kuwa ziara zako katika sehemu mbali mbali za nchi zitakuwa ni chachu katika kutoa hamasa kwa wadau hasa wale waliopo kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu.
Ndugu Matiya, shukrani kwa masuali yako. Nimetumia muda mrefu kuyatafakari, maana si masuali rahisi kuyajadili, achilia mbali kuyajibu.
Tunakubaliana kuwa kazi ya uandishi wa vitabu ni ngumu. Hata hivi, inaweza kutusaidia sana tukikumbuka kwamba, pamoja na ugumu wote tunaokabiliana nao katika nchi kama Tanzania, tuwakumbuke waandishi wa nchi mbali mbali ambao walikuwa gerezani na bado walitafuta mbinu na kuandika.
Mifano ni kama Wole Soyinka wa Nigeria, na kutoka Kenya kuna mifano kama Gakaara wa Wanjau, Abdilatif Abdalla, Ngugi wa Thiong'o, na Alamin Mazrui.
Tukizingatia hilo, tutaona kuwa iwapo hao waliandika wakiwa gerezani, wa-Tanzania hatuna sababu ya kushindwa kuandika. Dhiki tulizo nazo ni kama starehe tupu, tukifananisha na dhiki walizopitia hao wenzetu.
Suala la soko la vitabu nalo tulitafakari. Kama ninavyoandika mara kwa mara katika blogu mbali mbali, wa-Tanzania wana hili tatizo la kutokuwa na mwamko wa kununua na kusoma vitabu.
Lakini, tukumbuke kuwa taaluma haifungwi ndani ya mipaka ya nchi. Ukiandika kitabu kizuri, una soko duniani, iwe umeandika kwa ki-Swahili, au ki-Ingereza. NInaongea hivi kwa kuzingatia uzoefu wangu, yaani vitabu ambavyo nimechapisha. Ninajiandaa kuandika kitabu kuhusu Tanzania. Nitatumia uwezo wangu wote kuhakikisha kimekuwa kitabu bora, na ninajua kitasomwa sehemu mbali mbali za dunia, hata kama wa-Tanzania hawatakigusa. Ni shauri lao.
Kuhusu uchapishaji, ninawahamasisha watu wafuatilie tekinolojia za uchapishaji kama ninavyofanya, maana nimefikia hatua ya kutumia tekinolojia hizi na kujichapishia vitabu kiurahisi, bila gharama. Ninawahamasisha na kuwaelekeza wengine katika maandishi yangu, ili nao watumie fursa hizi.
Kuhusu ziara zangu Tanzania, kuendesha warsha, kwa ujumla msisimko wa watu ni hafifu. Hii ni tofauti kabisa na huku Marekani, ambako watu wananitafuta wenyewe, kuanzia vyuo, jumuia, na taasisi, hadi makampuni kama RBC Wealth Management.
Post a Comment