Saturday, August 28, 2010

Maonesho Faribault, Minnesota

Nimerejea muda mfupi uliopita kutoka Faribault, kwenye maonesho ya utamaduni ambayo hufanyika mara moja kila mwaka, chini ya kamati ya Faribault Diversity Coalition. Mimi ni mwanakamati.

Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu.

Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania.
Baada ya meza yangu kukamilika, niliketi nikingojea wateja na watu wa kuongea nao kuhusu shughuli zangu za uandishi na ushauri juu ya masuala ya elimu na tamaduni. Picha hii, na jinsi nilivyokaa imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu uuzaji wa vitabu. Kijuu juu naonekana nimekaa kama muuza dagaaa. Ukweli ni kuwa hapa huwa ni darasa zito siku nzima.

Walikuwepo wacheza ngoma za kabila la Aztec. Hao wamekuwa wakishiriki maonesho haya mwaka hadi mwaka, na huwa ni kivutio kikubwa.
Watu walileta vitu mbali mbali vya kuuza, kama vile vyakula, vinywaji, na kazi za sanaa. Katika maonesho haya, huwa napata fursa ya kukutana na watu wengi wapya.


Leo, kwa mfano, nimekutana na huyu mama, ambaye aliniambia kuwa alisoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hii ilikuwa ni ajabu, kwani nami nilisoma katika Chuo hicho hicho, miaka ya kabla yake. Halafu, aliniambia kuwa alishachukua kozi moja ya Profesa Harold Scheub iliyohusu fasihi hadithi za Afrika. Profesa huyu ndiye aliyesimamia tasnifu yangu ya shahada ya udaktari. Kweli milima haikutani, binadamu hukutana.
Huyu kijana hapa kushoto, baada ya kununua kitabu hiki alichoshika, aliomba tupige picha. Akanipa kitabu changu kingine nishike, na rafiki aliyekuja naye akatupiga picha.

Tabia hii si ngeni kwa wa-Marekani. Huwa wanapenda kumbukumbu za aina hii. Wengi wanapenda mwandishi atie sahihi kwenye kitabu wanachonunua. Nami leo nimefanya hivyo kwa wateja wangu.
Katika mji wa Faribault kuna wa-Somali wengi, ambao wamefika miaka ya karibuni. Leo hapo kwenye maonesho nilikutana na hao wa-Somali wawili. Huyu aliyeko kushoto anaishi kwenye mji mwingine. Lakini huyu wa kulia ni rafiki yangu, ambaye anafuatilia maandishi na shughuli zangu kuhusu masuala ya tamaduni. Ni kijana makini, na tunapangia kushirikiana katika shughuli hizo.

Thursday, August 26, 2010

Ujumbe wa Msomaji wa Kitabu

Naichukulia blogu hii kama mahali ambapo naweka mambo yangu binafsi: kumbukumbu, fikra, dukuduku, hisia na kadhalika. Ingawa najua watu wanasoma ninayoandika, siwezi kusema kuwa wao ndio walengwa. Ninajiandikia mwenyewe, kwa uhuru na namna ninayotaka, mambo yangu binafsi.

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mshiriki mmojawapo wa warsha niliyoendesha Dar es Salaam mwaka jana. Bofya hapa. Ameniulizia naenda lini kutoa warsha zingine akahudhurie.

Pia amesema kuwa kitabu cha Africans and Americans ambacho alikinunua wakati wa warsha kinamsaidia katika kutoa mihadhara na kushughulikia masuala mengine ya mahusiano sehemu za kazi.

Ni wazi nimefurahi kusikia hayo. Nani asingefurahi? Nimemwambia nafarijika kuwa kitabu kimezaa matunda mema kwake, hasa nikikumbuka gharama ya warsha na kitabu. Lengo moja la kuandika kitabu hiki lilikuwa kuwasaidia wanaohitajika kutoa mihadhara kuhusu tofauti za tamaduni na matatizo na changamoto zitokanazo na tofauti hizi. Wengine wanakuwa na majukumu ya kusuluhisha migogoro. Mimi mwenyewe nakitumia kitabu hiki, mahali pa kuanzia.

Maoni ya wasomaji ni msaada mkubwa kwa mwandishi. Nami nina bahati ya kuyapata mara kwa mara. Wengine, kama ilivyo katika ulimwengu wa vitabu, wanayaweka maoni yao hadharani, kama haya hapa. Nawajibika kutoa shukrani.

Sunday, August 22, 2010

Kukutana kwa Wanablogu

Katika ziara yangu Tanzania mwaka huu, pamoja na mengi mengine, nilipata fursa ya kukutana na wanablogu. Tarehe 7 Agosti nilikutana na Kamala na Chacha pale Sinza kama inavyoonekana katika picha hii.
Tuliongea na kubadilishana mawazo ya aina aina, kama alivyoeleza Kamala katika blogu yake. Chacha naye aliandika ujumbe kuhusu mkutano wetu. Bofya hapa.

Tarehe 17 Agosti, hapo hapo Sinza, nilikutana na mwanablogu Maggid Mjengwa. Bofya hapa.Tuliongea kuhusu mambo mengi, kuanzia gazeti la Kwanza Jamii, masuala ya blogu, yakiwemo masuala ya faida na kero zake.

Tuliongelea, kwa mfano, namna ya kuyachukulia maudhi ya baadhi ya watoa maoni kwenye hizi blogu. Tangu tulipokuwa tunaandika katika Kwanza Jamii, sisi wawili tumekuwa na msimamo kwamba ni bora kuwaacha watu waseme hata kama wanachosema kinaudhi, kwa msingi kuwa labda wanahitaji kufanya hivyo kwa manufaa yao kisaikolojia, mbali na kwamba tunazingatia suala la uhuru wa kutoa maoni na fikra. Ni msimamo mgumu unaohitaji uvumilivu, lakini labda ni bora kuwa na msimamo huu kuliko msimamo wa kuwazuia watu uhuru. Msimamo huu nimeuelezea kinaganaga katika kitabu changu cha CHANGAMOTO.

Naona kuwa suala la kukutana na wanablogu wenzangu Tanzania linazidi kuwa jadi. Nilianza kufanya hivyo mwaka jana, nilipokutana na mwanablogu maarufu Issa Michuzi. Waliofanya juhudi kuniunganisha na Issa Michuzi ni Maggid Mjengwa na Frederick Mboma. Hatimaye, Ndugu Mboma ndiye aliyenifikisha ofisini kwa Michuzi, tukaongea kuhusu masuala ya aina aina, hasa blogu. Bofya hapa.

Mikutano hii ya wanablogu ina manufaa mengi, kama walivyosema wanablogu wengine. Ni fursa ya kufahamiana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya blogu na mengine. Katika mkutano wangu na Chacha na Kamala, jambo moja lililosisitizwa ni suala la kujitambua. Hao wawili wanajibidisha katika kufuatilia mada hii wakijumuika na wengine. Nami niliona ni vema nasi wanablogu tuwe tunatakafakari suala hili la kujitammbua. Kwa hivi, niliuliza suali: kwa nini tunablogu? Bofya hapa.

Mwaka jana, wazo la kuwakutanisha wanablogu wa Tanzania lilipendekezwa na kujadiliwa. Ingawa mkutano huu haukufanyika, wazo linastahili kufanyiwa kazi na kutekelezwa.

Thursday, August 19, 2010

Mkutano na Mwenyekiti Mjengwa


Juzi, tarehe 17 Agosti, nilipata fursa ya kukutana tena na mwanablogu maarufu, Maggid Mjengwa. Tulikutana Sinza, tukaongea kwa muda, kuhusu masuala mbali mbali.

Nilikutana na Mwenyekiti Mjengwa mara ya kwanza mwaka jana, kama ilivyoelezwa hapa. Juzi tuliongelea gazeti la Kwanza Jamii, ambalo yeye alilianzisha mwaka jana, nami nikawa mchangiaji wa makala. Tulibadilishana mawazo na kumbukumbu kuhusu yaliyotokea miongoni mwa wasomaji kuhusu gazeti hili, tukatathmini yale tuliyokuwa tunayakumbuka.

Nilikuwa na nakala ya kitabu changu cha CHANGAMOTO, ambacho ni mkusanyiko wa makala nilizoandika Kwanza Jamii. Mwenyekiti alifurahi sana kukiona, akanunua nakala kadhaa kwa ajili ya marafiki zake.

Alinieleza jinsi taasisi fulani kule Njombe ilivyopendezwa na gazeti la Kwanza Jamii, kiasi cha kufanya mkakati wa kuendeleza juhudi za lile gazeti. Hayo ni mambo ya baadaye, ambayo ni changamoto.

Saturday, August 14, 2010

Nimefika Lutheran Junior Seminary, Morogoro

Juzi nilienda Lutheran Junior Seminary, Morogoro, kuangalia kitengo cha ufundishaji wa ki-Swahili na Utamaduni.

Kwa miaka mingi nilifahamu habari za kitengo hiki, kupitia mtandao wao, ila sikuwahi kuwatembelea. Nilifurahi kuonana na walimu na kutembezwa katika mazingira ya shule.


Kwa vile ninashughulika na program za kuleta wanafunzi wa Marekani hapa Tanzania na kwingineko Afrika, niliona ni muhimu nipate ufahamu mzuri wa kitengo hiki cha Morogoro, endapo tutahitaji kuwaleta wanafunzi wetu.

Nilitambulishwa kwa mwalimu ambaye alikuwa darasani akiwafundisha wageni somo la utamaduni. Kumbe anakifahamu kitabu changu cha Africans and Americans na anakitumia. Nilifurahi kuona kuwa niliyoandika yanawanufaisha wengi, hadi huku Morogoro.

Friday, August 13, 2010

Niko Morogoro: Mji Kasoro Bahari

Nimekuwa Morogoro tangu juzi, nikipunga upepo na kutembelea sehemu kadhaa.

Morogoro ni mji maarufu katika Tanzania. Uko katika njia kuu za usafiri baina ya Tanzania na nchi za Afrika ya kati na kusini.
Ni mji uliosifiwa sana na mwanamuziki maarufu Mbaraka Mwinshehe, kwa uzuri wake, na uzuri wa mandhari yake. Katika sifa hizi, aliongelea jinsi maji yanavyotiririka milimani Morogoro. Wenyeji wa hapo, wa-Luguru, ni maarufu miongoni mwa sisi watani zao, kwa jinsi nao wanavyojivunia huu mji, wanaouita Mji Kasoro Bahari.

Kila ninapopita Morogoro, nakumbuka umaarufu wake. Hapo kuna shule na vyuo maarufu tangu zamani, kama vile Kilakala, Kigurunyembe, Mzumbe, na Sokoine. Miaka ya karibuni kimeanzishwa pia chuo kikuu cha Ki-Islam. Ni mji muhimu kwa upande huu, wa elimu.

Thursday, August 12, 2010

Kitabu: "Ualimu Katika Shule za Msingi"


Nimemaliza kusoma kitabu kiitwacho “Ualimu Katika Shule za Msingi” kilichoandikwa na Anael Malewo na kuchapishwa na Dar es Salaam University Press. Nilikiona katika duka la vitabu la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2010, nikakinunua, kwa shilingi 1,500 tu.
Nilivutiwa na kitabu hiki kwa sababu mimi ni mwalimu ambaye napenda kuelewa hali halisi ya shule zetu na mfumo wa elimu, kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu. Sababu nyingine ni kuwa niliwahi kuandika makala juu ya mwalimu wa shule ya msingi katika gazeti la “Kwanza Jamii,” ambayo inapendwa na wasomaji na imo pia katika kitabu cha CHANGAMOTO.
“Ualimu Katika Shule za Msingi” ni kitabu chenye manufaa sana. Kinatoa mwanga kuhusu wadhifa, wajibu, na maadili ya ualimu, falsafa na mbinu za ufundishaji, wajibu wa serikali, wazazi, na jamii kwa ujumla katika elimu ya shule za msingi. Kitabu hiki kinaelezea pia matatizo ya shule za msingi na kupendekeza ufumbuzi.
Mwandishi anathibitisha anavyothamini elimu na maslahi ya Taifa. Anarejea kwenye miongozo ya Taifa letu, kama vile “Azimio la Arusha.” Kitabu hiki kinasisitiza mambo ambayo mwalimu anapaswa kuyazingatia wakati anawafundisha watoto, kama vile tabia zao na mazingira watokako. Nimekisoma kitabu hiki kwa furaha na ari kubwa, kwa jinsi kinavyoelimisha.
Ni wazi kuwa mwandishi wa kitabu hiki ni mtaalam. Katika jalada la nyuma la kitabu tunasoma kuwa mwandishi wa kitabu hiki “ni mwalimu mwenye uzoefu mkubwa katika ufundishaji na uongozi wa elimu hapa nchini.” Ana uzoefu kama mwalimu mkuu wa shule, afisa elimu wa wilaya, mkuu wa chuo cha ualimu, mwalimu katika shule za kati, na katika chuo cha ualimu cha Marangu.
Kitabu hiki ni hazina kwa kila mtu anayethamini elimu, iwe ni ya shule ya msingi au vyuo vikuu. Ni muhimu kisomwe na kila mtu, kwani kina mambo yanayotuhusu sote.

Sunday, August 1, 2010

Ninasoma "Diwani ya Mnyampala"

Kwa siku hizi mbili tatu nimekuwa nikisoma Diwani ya Mnyampala, kitabu nilichonunua katika duka la vitabu la Chuo Kikuu Dar es Salaam tarehe 27 Julai. Nilizikuta nakala kadhaa, kuukuu, nami nikanunua moja, kwa bei ya shilingi 5,000. Kampuni iliyochapisha kitabu hiki, East African Publications, haiko tena, na kwa vile sina hakika kama kitabu hiki kinachapishwa mahali popote pengine, nilijiona nina bahati kukipata.

Ninaona fahari kuwa na kitabu hiki. Kitachangia juhudi zangu za kujiongezea ufahamu wa matumizi ya ki-Swahili, lugha ambayo nataka niweze kuitumia vizuri katika maandishi yangu. Azma hiyo nimeshaitaja kabla.

Mathias Mnyampala ni mwandishi maarufu. Sifa zake nilizifahamu tangu nilipokuwa kijana. Pamoja na tungo zake nyingi, alikuwa akihusishwa na chimbuko la ngonjera. Nilifahamu kuhusu kitabu chake cha Kisa cha Mrina Asali. Hatimaye, nilipokuwa nafundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, nilikijumlisha kitabu hiki katika orodha ya vitabu nilivyovitumia katika somo la fasihi simulizi, kama njia ya kuonyesha kuwa waandishi aghalabu wanakuwa wamejikita katika fasihi simulizi. Kisa cha Mrina Asali ni muendelezo wa hadithi za jadi za ushujaa, ambazo kwa ki-Ingereza zinaitwa epics. Tunaweza kuitafsiri dhana hii kijuujuu kama tendi.

Ninaifurahia Diwani ya Mnyampala. Ni kazi ya mshairi aliyekuwa na nidhamu ya hali ya juu katika utungaji wake. Mashairi yake yanafuata mtindo wa vina na mizani. Anathibitisha jinsi alivyokuwa sambamba na washairi wengine, kwa malumbano na majibizano mengine. Nimeguswa na jinsi anavyomwombea Mwalimu Nyerere, ambaye kwa wakati ule alikuwa anaanza kuiongoza Tanganyika.

Nimeguswa na namna anavyoomboleza kifo cha Shaaban Robert. Katika utungo moja anasema kuwa kufariki na kwa Shaaban Robert ni pigo kubwa, kama kuzimika kwa taa katikati ya usiku. Kama Shaaban Robert, Mnyampala alikuwa anaiheshimu sana lugha ya ki-Swahili, hata akaitungia shairi liitwalo “Lugha Yetu Kiswahili.” Diwani ya Mnyampala ni kioo murua ya masuala mbali mbali ya jamii yaliyokuwepo wakati wa maisha yake na Tanganyika ya wakati wake.