Sunday, October 30, 2011

Wa-Islamu Vyuoni Marekani

Leo tulikuwa na mjadala mjini Faribault, Minnesota, kuhusu wa-Islam vyuoni Marekani. Walioandaa mjadala ni Anna na Rachel, wanafunzi wa Chuo Cha Carleton. Walengwa walikuwa ni wazazi na vijana wa ki-Somali, ambao ndio jamii ya ki-Islam inayofahamika hapa Minnesota ya Kusini Mashariki. Hapa kushoto tunaonekana wanajopo tukiwa mzigoni.
Rachel amejishughulisha na wa-Somali kwa kitambo. Aliwahi kufanya mahojiano nami miezi kadhaa iliyopita kuhusu changamoto zinazowakabili wa-Islam Marekani.

Rachel na Anna waliniomba nikawe mwanajopo katika mjadala wa leo, kwa vile wanafahamu ninafahamika na kukubalika katika jamii ile. Mjadala ulilenga kuwapa fursa wazazi na vijana kufahamu hali halisi, faida na changamoto za vyuo kwa wa-Islam ambao pia ni wahamiaji kutoka Afrika.

Wazazi na vijana walipata fursa sawa ya kuelezea mawazo yao, mitazamo, mategemeo, wasi wasi na mapendekezo. Zilijadiliwa changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kiIslam wanapowazia au kujiandaa kupeleka maombi ya kujiunga na vyuo vikuu, hadi masuala ya tofauti za dini na tamaduni wanazokabiliana nazo kwenye vyuo.

Mjadala ulihusu pia namna ya kujizatiti na hali hizo, na misaada iliyopo ya kuwawezesha wanafunzi wa ki-Islam kufanikiwa katika masomo vyuoni hapa Marekani. Msichana anayeonekana kwenye picha ya mwanzo pale juu, mwanajopo, ni mwanachuo. Alisema yeye kama mu-Islam anaona kuwa changamoto zilizopo vyuoni si kikwazo cha kumfanya kijana asiende chuoni.
Wazazi wote walisema na kusisitiza kuwa wanataka watoto wao wafanikiwe shuleni na vyuoni. Tatizo moja, ambalo walilitaja na kulisisitiza ni utaratibu wa shule za Marekani wa kuwaweka watoto katika darasa fulani kufuatana na umri. Kwa watoto wa ki-Somali ambao wamezaliwa au kukulia hapa Marekani, hili halina utata.

Lakini, watoto wa ki-Somali wanaofika kutoka Somalia, wanaweza kuwa na umri mkubwa lakini hawakupata nafasi ya kusoma kule watokako, kwa mfano kwenye makambi ya wakimbizi. Wanapowekwa katika darasa la watoto wa umri wao hapa Marekani, wanakuwa hawana msingi wa kuweza kufanikiwa katika masomo hayo, hata tu kwa upande wa lugha. Matokeo yake ni watoto hao kushindwa na kuishia kuacha kwenye vyuoni.

Wednesday, October 26, 2011

Mwandishi Nuruddin Farah Katutembelea

Jana jioni, mwandishi maarufu Nuruddin Farah, mzaliwa wa Somalia, alikuja chuoni Carleton, hapa Northfield, kuongea na wadau kuhusu riwaya yake mpya, Crossbones, ambayo imechapishwa mwaka huu.

Nilienda kumsikiliza. Kama ilivyo kawaida katika shughuli za aina hii, vitabu vyake vilikuwepo, vinauzwa. Kwa vile ninavyo vitabu vyake vingine, nilinunua hiki kipya. Hapa pichani mwandishi anasaini nakala yangu. Bei yake ni dola 27.95, yapata shilingi 50,000 za Tanzania. Hiki ni kiasi kidogo sana ukifananisha na hela tunazotumia wa-Tanzania kwenye ulabu na makamuzi mengine. Bora kununua kitabu.
Ingawa bado sijaisoma riwaya ya Crossbones, kwa kufuatilia mazungumzo ya jana na kuiangalia kijuu juu, ni riwaya inayohusu Somalia kabla tu na baada ya uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Ethipia miaka michache iliyopita. Ni riwaya inayoelezea athari za matukio hayo katika maisha ya wahusika.

Kwa bahati, nimeshamwona Nuruddin Farah mara kadhaa akihutubia, hapa Marekani. Vile vile, nimepata kufundisha baadhi ya maandishi yake. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1974. Nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwa vile nilikuwa nasomea ualimu, nilienda shule ya wasichana ya Iringa kufanya mazoezi ya kufundisha. Kitabu cha Nuruddin Farah From a Crooked Rib kilikuwa kinatumika katika somo la "Literature."

Miaka ya hivi karibuni, hapa chuoni St. Olaf, nimefundisha pia riwaya zingine za Nuruddin Farah. Ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika, ambaye ameshapata tuzo nyingi kwa uandishi wake.

Tuesday, October 25, 2011

Vitabu Vyangu Vinapatikana Bagamoyo

Ukiwa Bagamoyo, kwenye barabara itokayo kwenye makumbusho ya historia, Caravan Serai, kuelekea kwenye mgahawa wa Top Life, utaona duka upande wa kushoto liitwalo Sanaa Sana Art Shop.

Mmiliki ni Dada Neema, mjasiriamali anayeuza vitu mbali mbali, kuanzia vinyago, vikapu, na nguo za ki-Tanzania, hadi picha na postikadi za ki-Tanzania.

Nilionana naye hapa Bagamoyo mwaka jana, na ndipo alipofahamu habari za vitabu vyangu, akaamua awe anaviuza, kama wanavyofanya wajasiriamali wengine wawili watatu nchini Tanzania. Mimi si mfanyabiashara bali mwalimu na mwandishi. Ila niko tayari muda wote kuwawezesha wajasiriamali kuvipata vitabu vyangu. Namba ya simu ya duka la Dada Neema ni 0754 445 956.

Sunday, October 23, 2011

Taswira za Mjini Songea

Nchi yetu ya Tanzania ni kubwa sana. Ina mikoa, wilaya na vijiji vingi, na siamini kama yuko m-Tanzania atakayeweza kupita kila sehemu. Mimi mwenyewe nimebahatika kutembelea sehemu nyingi katika mikoa mbali mbali. Hata hivyo, kuna sehemu ambazo sijafika, kama vile Bukoba, Mpanda, Sumbawanga, na Singida.

Kutokana na ukweli huo, ninawashukuru wanablogu ambao wamekuwa mstari wa mbele kutuletea habari na taarifa za sehemu mbali mbali za nchi yetu. Blogu ya Mwenyekiti Mjengwa ilinigusa kwa namna ya pekee tangu mwanzo, kwa jinsi alivyokuwa anatembelea vijiji ambavyo wengi wetu hatutavifikia. Kutokana na jinsi nilivyofaidika na jambo hilo, nami najaribu kuleta picha za sehemu mbali mbali, ili wa-Tanzania wengine wapate kuzifahamu sehemu ambako nimefika.

Leo naleta baadhi ya picha nilizopiga mjini Songea mwaka huu. Nimeshaleta taarifa kadhaa za Songea katika blogu hii, kama vile hii hapa. Napangia kuleta taarifa na picha zaidi. Wale ambao hawajafika Songea watapata fununu kidogo kuhusu mahali hapo, ingawa picha zote ni za sehemu ya katikati ya mji.

Saturday, October 22, 2011

Ukiwa na Siri, Iweke Kitabuni

Hapa kuna picha nilizopiga kwenye tamasha la vitabu mjini Minneapolis, Oktoba 15, mwaka huu. Habari za tamasha hilo niliziandika hapa.

Picha zote hizi nilizipiga kwa muda wa dakika mbili hivi, nikiwa nimesimama sehemu moja.
Niliangalia jinsi watu walivyokuwa wanavichangamkia vitabu. Nilikumbuka ule usemi kuwa ukiwa na siri, iweke kitabuni. Hapo watu makini na wasio makini watajipambanua wenyewe.

Kwa uzoefu wangu, kama ninavyosema tena na tena katika blogu na sehemu zingine, wa-Marekani ni kati ya hao watu makini. Ukiweka siri kitabuni, wataiona.


Friday, October 21, 2011

Sehemu za Kupumzikia, Mbamba Bay

Mbamba Bay ni mji mdogo, kando kando ya Ziwa Nyasa, upande wa Tanzania. Ingawa umaarufu wa mji huu tangu zamani ni bandari, hapo ni mahali pazuri kwa mapumziko. Picha ninazoleta hapa nilipiga mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu.

Unaweza kusogea hapo ufukweni, ukawa unapunga upepo na kuangalia shughuli za wavuvi, wauzaji wa samaki, akina mama wakifua nguo, na watoto wakicheza majini. Kama unajua kuogelea, mahali hapo utafafurahia. Ukija siku ambapo meli inakuja, utajionea ujio wa meli na kuondoka kwake.


Kama unapenda kukaa kwenye mwinuko, uangalie mji na Ziwa kwa chini yako, hoteli ya masista panafaa. Habari zake niliandika hapa. Ukipata chumba kinachoangalia upande wa Ziwa, huko nyuma ya hoteli, utafaidi mandhari ya Ziwa na sehemu kadhaa za Mbamba Bay. Ukitoka nje ukaingia bustanini, utapanda mawe na kuliona Ziwa vizuri sana.

Hapo kwenye paa la blue ni baa ya Four Ways, ambayo picha zake niliwahi kuziweka hapa. Mwaka huu, nilipokuwa Mbamba Bay sikupata fursa ya kuingia ndani.


Hapa kushoto niko katika baa ya Bush House na wadau niliokutana nao humo, ambao walitaka tupige picha.

Monday, October 17, 2011

Ziara ya Uyole Kufuatilia Chuo Kikuu Kipya

Mwaka huu, nilipokuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya LCCT, tulipata fursa ya kutembelea Uyole, mkoani Mbeya. Hiyo ilikuwa ni tarehe 19 Agosti. Hapo tulienda kuangalia mipango ya uanzishwaji wa Chuo Kikuu ambao ni mradi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania. Kabla ya yote, napenda kuwashukuru wachungaji Dr. Mwalilino na Dr. Stephen Kimondo kwa kuandaa mawasiliano yaliyotuwezesha kufanya ziara hii.


Mwenyeji wetu alikuwa Mchungaji Dr. Gwamaka Mwankenja, ambaye ndiye mratibu wa mpango huu wa kuanzisha chuo kikuu. Alitukaribisha vizuri na tuliongea kirefu. Alituelezea mpango mzima na changamoto zake, akatutembeza maeneo ya chuo.
Kama mwanataaluma na mwalimu, nafuatilia sana hali na maendeleo ya elimu Tanzania, sio tu kwa kusikia au kusoma taarifa, bali kwa kutembelea shule na vyuo kila ninapokuwa nchini. Napenda kufuatilia vyuo vikuu vipya. Kwa mfano, nilishazuru Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa kilichoko Lushoto. Niliangalia ukarabati wa majengo ya shule ya zamani ya Magamba, ambao ndio msingi wa chuo hiki kipya. Pia nimekuwa nikifuatilia mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Njombe, kama nilivyoelezea hapa.

Chuo Kikuu cha Uyole kinatarajiwa kuanza kwa kutumia majengo ya Chuo cha Ualimu cha Uyole, sambamba na harakati za kujenga majengo mapya na miundombinu itakiwayo.


Naona huu ni uamuzi bora. Kitu cha muhimu, kwa mtazamo wangu, ni kuwa na wahadhiri bora na vifaa vya msingi, kama vile vitabu, na wanafunzi wenye nia ya kweli ya kutafuta elimu. Binafsi, nisingeona shida kufundisha katika madarasa niliyoyaona hapa ya Chuo cha Ualimu. Unaweza ukawa na majengo ya kisasa kabisa, lakini elimu bado ikawa duni. Mwisho wa siku, ingawa majengo bora ni muhimu, elimu haitoki kwenye majengo.Kwa kweli, niliona ni sehemu nzuri na kubwa. Wakati tunapitishwa katika mazingira ya hapo tuliwakuta wanafunzi uwanjani wakifanya mazoezi ya kwaya. Mchungaji Mwankenja alitutambulisha, nami nikapata fursa ya kuwasalimia na kuwahamasisha katika kutafuta elimu kwa dhati. Walituzawadia CD ya nyimbo zao.

Binafsi, naunga mkono mipango ya kujenga vyuo vipya kama hiki cha Uyole. Kwanza, idadi ya waTanzania inaongezeka muda wote, na mahitaji ya vyuo hayatapungua. Ni vema kujenga sasa, kwa kadiri iwezekanavyo, kuliko kungoja hadi baadaye, wakati gharama zinaendelea kupanda.

Hata kama vyuo vitakuwa vingi mno na wanafunzi wasiwe wa kutosha, jambo la kuzingatia ni kuwa vyuo vyetu vikiwa bora sana vitawavutia wanafunzi na watafiti kutoka nchi za nje, kama ilivyokuwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya zamani. Faida zake ni nyingi, kuanzia za kitaaluma, kwa maana ya fursa ya kubalishana mawazo baina ya watu wa mitazamo mbali mbali, hadi kiuchumi. Kwa mfano, Marekani inatambua jambo hilo, na inajivunia malaki ya wanafunzi wanaosoma katika nchi hiyo kutoka duniani kote. Pamoja na faida kubwa za kitaaluma, wageni hao wanaingiza mamilioni ya dola katika uchumi wa Marekani kila mwaka.

Ni muhimu kwa sisi wa-Tanzania kuwa na mawazo mapana kuhusu masuala ya aina hii. Tuwekeze katika vyuo pia, ila tuwe makini katika kuhimiza na kuboresha taaluma, utafiti, na maadili yahusikayo. Lakini kwa hali ilivyo, tuko nyuma sana. Baadhi ya wanaoongoza vyuo vyetu hawana upeo utakiwao, na serikali haina upeo huo. Serikali imekuwa na historia ya kuwapachika watu kwenye nafasi za uongozi wa vyuo bila kuzingatia masuala muhimu ya misingi, maana na wajibu wa vyuo vikuu. Kukosekana kwa upeo huu ni msingi mkubwa wa migomo na vurugu zisizoisha katika vyuo vyetu ambazo hukwamisha uwezo wa kuviweka vyuo vyetu katika viwango vitakiwavyo.

Sunday, October 16, 2011

JK na Pinda Wakiwapagawisha Wadau

Kati ya kali zote nilizoziona mwaka huu, hii ya JK na Pinda ni kiboko. Imenivunja mbavu kabisa. Wako mzigoni kikweli kweli, wala si utani. Halafu nikizingatia kuwa wote wawili ni watani wangu, naishiwa nguvu kabisa. Niliiona hapa.

Saturday, October 15, 2011

Tamasha la Vitabu, Minneapolis

Leo, mjini Minneapolis lilifanyika tamasha la vitabu, ambalo hufanyika kila mwaka, mwezi Oktoba. Tamasha hili huandaliwa na jarida la Rain Taxi.


Ingawa kila mwaka, kwa miaka kadhaa sasa, nimeshiriki tamasha hili, kwa maana ya kupeleka vitabu vyangu, mwaka huu nilighilibika kidogo. Nilidhani nimefanya mpango wa kulipia meza, halafu nikaenda Tanzania. Niliporudi kutoka Tanzania, nikagundua kuwa hapakuwa na meza iliyobaki. Mwakani, Insh'Allah, nitakuwa makini zaidi.


Kutokana na kughafirika huko, vitabu vyangu havikuwepo mwaka huu. Hata hivi, nilifunga safari, maili 45, kwenda kuangalia tamasha hili.


Pamoja hali ya uchumi wa Marekani kuwa mbaya miaka hii, na watu wengi kukosa ajira au kuishi katika wasi wasi mkubwa kuhusu hali yao ya uchumi kwa siku za usoni, inashangaza jinsi tamasha la vitabu linavyowavutia. Wanafahamu umuhimu wa vitabu kiasi kwamba wako tayari kusamehe mengi mengine ili hela walizo nazo waje kuzitumia hapa.

Nilifurahi kumwona huyu mama hapa kushoto, Shatona Kilgore-Groves, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Ni mwandishi na mhamasishaji wa elimu katika jamii, hasa wa-Marekani Weusi. Mwaka huu niliandika mapitio ya kitabu chake cha kwanza. Soma hapa.Niliangalia jinsi watu walivyokuwa wanavichambua na kuvinunua vitabu, na mtu huwezi kudhani kuwa hali ya uchumi wa nchi hii ni mbaya kama ilivyo. Unaona wazi kuwa hii ni jamii iliyoelimika. Kuelimika, kwa mtazamo wangu, ni kuwa na kiu au ari ya kutafuta elimu kwa maisha yako yote.Siku nzima, tangu asubuhi, watu wanafurika kwenye tamasha hili, na wanaonekana wakiwa makini sana katika kuviangalia vitabu, kuongea na waandishi na wachapishaji. Wanakuwepo pia wahariri.

Wazazi wengi huja na watoto wao. Ni wazi kuwa malezi ya aina hii yanawafanya watoto hao wakue katika mkondo huo huo wa kuthamini vitabu maisha yao yote. Hata kwetu Tanzania, watoto wanapenda vitabu. Tunawaangusha sisi watu wazima, kama nilivyoelezea hapa.Nilivutiwa na meza ambapo palikuwa panauzwa vitabu vilivyotumika. Sio kwamba ni vitabu vichakavu. Nilitumia muda kwenye meza hii, nikajionea uwingi wa vitabu vya fani mbali mbali, kwa bei nafuu.

Thursday, October 13, 2011

Ni Msimu Mwingine kwa Wanafiki Kumkumbuka Nyerere Kinafiki!

Tafakuri Jadidi

Chanzo Raia Mwema

Ni msimu mwingine kwa wanafiki kumkumbuka Nyerere kinafiki!
Johnson Mbwambo
12 Oct 2011


KESHOKUTWA, Ijumaa, Oktoba 14, Taifa litatimiza miaka 12 kamili tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kilichotokea kule London, Uingereza katika hospitali ya Mtakatifu Thomas.

Kama ambavyo imekuwa kwa miaka 11 iliyopita, Watanzania wataitumia pia keshokutwa kumkumbuka mpendwa wao huyo; huku wakitafakari, kama Taifa,
zile “t” tatu maarufu : Tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.

Na kama ilivyokuwa kwa miaka 11 iliyopita, Taifa litaiadhimisha siku hiyo ya Ijumaa, Oktoba 14, kwa makongamano, semina na matamasha yenye mahusiano na maisha ya Baba wa Taifa.

Kama ilivyokuwa kwa miaka 11 iliyopita, maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya Nyerere yatapambwa na kauli nzito kuhusu mchango wake katika kujenga Taifa letu, mawazo yake na visheni yake.

Wengi wataonyesha kwa dhati hisia zao za mapenzi waliyokuwanayo kwa mtu huyo ambaye, kwa jinsi alivyoipenda Tanzania, mimi naamini itatuchukua miaka 50 mingine kumpata anayemkaribia japo kwa asilimia 60 tu!

Lakini watakuwepo pia viongozi wachache wanafiki ambao watasimama majukwaani na, kwa unafiki, kuisifu visheni na uongozi wa Nyerere; huku kiutendaji wakiendelea kuibomoa misingi yote ya taifa ambayo mzee wetu huyo alitujengea.

Ndugu zangu, ni kipindi kama hiki ambapo tutawasikia hata wale waliokuwa wafuasi wake wakubwa katika kuitekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea katika Tanzania, lakini baadaye wakaitelekeza siasa hiyo, wakitoa kauli za kumsifu Mwalimu Nyerere kwa yale yote aliyoyasimamia. Ni Oktoba 14 ya kila mwaka wanapodhihirisha unafiki wao huo.

Ngoja tuwakumbushe unafiki wao viongozi hao wanafiki ambao zamani walikuwa wafuasi wa Nyerere, lakini sasa ni wafuasi wa Ubeberu wa Magharibi unaozidi kuwakamua wakulima na wafanyakazi masikini wa nchi hii.

Tuanze na Siasa ya Kujitegemea: Nyerere aliwaambia hivi kuhusu hilo, na wakajitia wako naye: “Tutaijenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe. Akipatikana mtu wa kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine.”

Natujiulize; Baada ya kifo cha Mwalimu, Oktoba 14, 1999, wafuasi wake hao ambao bado wapo madarakani ndivyo wanavyoiendesha nchi? Je; wanaamini na kutekeleza dhana hiyo ya kujitegemea?

Jibu langu ni “hapana”. Angalau bado tunamkumbuka mtawala wa sasa (Rais Kikwete), kwenye kampeni za mwaka jana, alipoomba apewe kura kwa sababu yeye ni hodari wa “kuhemea vibaba Ughaibuni”.

Mtawala mwenye mtazamo huo hawezi kamwe kuwa muumini wa kweli wa Siasa ya Kujitegemea ambayo Mwalimu Nyerere alipigania kuijenga nchini wakati wote wa uhai wake.

Kwa hiyo, si siri kwamba watawala wetu wa sasa si waumini wa kweli wa dhana ya kujitegemea, na ndiyo maana safari zao kwenda Ughaibuni kutembeza bakuli la ombaomba zimekuwa nyingi tangu Mwalimu afariki. Majuzi tu hapa Kikwete karejea kutoka Marekani (kuhemea!?) na aliporejea, Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda naye akapanda ndege kwenda Brazil (kuhemea?!).

Vyovyote vile; kama wafuasi hawa wa zamani wa Mwalimu Nyerere watazungumza lolote la kumkumbuka hiyo Ijumaa, Oktoba 14, na kusema kuwa wanafuata nyayo zake katika suala hilo la kujitegemea, watakuwa wanadhalilisha uwezo wetu wa kufikiri, na kwa hakika, watakuwa wanauanika tu hadharani unafiki wao!

Kuhusu ujenzi wa Ujamaa na kuupiga vita Ubepari; wafuasi hao wa Mwalimu wanaonyesha unafiki huo huo. Si siri kwamba Ujamaa aliouhubiri Nyerere sasa umebaki kwenye Katiba tu; huku wakubwa wakiimba na kucheza ngoma ya Ubepari.

Haikuwachukua hata miaka saba tangu Nyerere aondoke madarakani kwa wafuasi wake hao kuliua Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwa kuweka Azimio la Zanzibar mwaka 1992. Na bado Ijumaa, Oktoba 14, kina Ngombale Mwiru watakuwa na ujasiri wa kupanda jukwaani na kutoa kauli za kulisifu Azimio la Arusha alilolipigania Nyerere; ilhali ndio hao hao walioliua kwa azimio lile la Zanzibar!

Wafuasi hao wameliua Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na wakaamua kuukumbatia Ubepari, lakini sote tunajua jinsi Mwalimu alivyouchukia Ubepari (kiasi cha kuuita ni unyama). Alipata kusema hivi: “Ni majitu (mabepari) yanayokaa na uwezo wao na yanatumia wengine kama vyombo vya uzalishaji. Kwa hiyo, kwao mfanyakazi na randa ni sawa sawa. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ni nchi ya kibepari.”

Katika suala la fursa sawa kwa wote, pia matendo yao hayaendani na ya Mwalimu. Enzi za Mwalimu, kila mwananchi alikuwa na fursa sawa, na haikujalisha utajiri au umasikini wake, kabila lake, elimu yake, dini yake au rangi yake.

Lakini tangu Mwalimu aondoke, mambo yamebadilika kwa kasi. Hivi sasa kuzungumzia fursa sawa kwa mtoto wa kiongozi (tajiri) na mtoto wa masikini, kunahitaji ujasiri wa ‘ki-uendawazimu’.

Hali imebadilika mno. Mfano mzuri ni katika elimu. Wakati watoto wa wakulima masikini wanakalia ndoo shuleni kwa sababu ya ukosefu wa madawati, watoto wa viongozi ama wanasoma nje ya nchi au katika shule za binafsi zenye kila kitu.

Hata katika suala la ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini pia wameitelekeza visheni ya Mwalimu. Mwalimu alisema hivi kuhusu viwanda: “Maana ya maendeleo ya leo ya uchumi wenye nguvu, ni maendeleo ya viwanda. Nchi yenye viwanda tunasema ni nchi iliyoendelea. Nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na viwanda vya kisasa.”

Ili kulitekeleza hilo kwa vitendo, Mwalimu alisimamia ujenzi wa viwanda vingi nchini. Kwa mfano, mpaka wakati anaondoka madarakani, nchi ilikuwa na viwanda vya nguo 12.

Lakini alipong’atuka madarakani, hao waliokuwa wafuasi wake wakaanza mbio za kuuza viwanda hivyo vya umma kwa watu binafsi; tena kwa bei ya kutupa. Ilikuwa ni katika kutekeleza sera yao mpya ya uchumi wa soko huria.

Matokeo yake ni kwamba hivi sasa ni kama vile sekta ya viwanda haipo kabisa katika Tanzania! Kutoka kwenye viwanda 12 vya nguo (kwa mfano) sasa nchi ina viwanda vitatu tu vya nguo! Leo hii, hata leso tu za kujifutia jasho zinatoka Beijing kwenye viwanda vya Wachina!

Pamoja na usaliti huo, bado watawala wetu watakuwa na ujasiri, hiyo Oktoba 14, kupanda jukwaani na kutudanganya kuwa wanaifuata sera ya Mwalimu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda! Unafiki mtupu!

Hata katika suala la kudumisha amani na usalama ambao ndio umekuwa wimbo wao mkubwa siku hizi wa kuwatisha wapinzani, ni hivyo hivyo. Watasimama majukwaani na kutuongopea kwamba wanaijenga misingi iliyowekwa na Mwalimu ya kudumisha amani na usalama nchini!

Uongo mtupu; maana sote tunakumbuka kwamba Mwalimu alisema kuwa “usione vinaelea, vimeundwa”; kwamba amani tuliyonayo inatokana na misingi ya usawa iliyojengwa, na kwamba hatuwezi kubaki nayo kama tutaachia pengo kati walio nacho na wasio nacho liongezeke.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, pengo hilo limekuwa kubwa mno. Wakati wanavijiji wengi nchini wanaishi katika nyumba za mbavu za mbwa, viongozi mijini wanamiliki majumba kadhaa ya kifahari.

Wakati masikini wanakula mlo mmoja kwa siku, matajiri wanakula na kusaza, na wakati Watanzania wengi wanashindwa kumudu kununua hata baiskeli moja tu, viongozi na matajiri wanamiliki misururu ya magari ya kifahari nk.

Mwalimu alipata kututahadharisha kuhusu hali hiyo kwa kusema hivi: “Wachache wanapoonekana waziwazi wakiogelea katika utajiri wa wizi na magendo na unyonyaji, wakati wengi wanakabiliana na dhiki ya kweli kweli, si rahisi kulinda amani na umoja wetu.

Je; watawala wetu wa sasa wanazingatia tahadhari hiyo ya Mwalimu kwamba tusiruhusu pengo kati ya matajiri na masikini liongezeke? Jibu unalo mwenyewe mpenzi msomaji.

Tukija kwenye suala la ardhi na maliasili zetu nyingine ni hivyo hivyo. Mwalimu alitambua na kuthamini haki ya wananchi kumiliki ardhi, lakini baada ya kifo chake sote tumeshuhudia ekari kwa ekari za ardhi za wananchi wakipewa wawekezaji. Hali hii imeibua misuguano mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji hao huko Loliondo, Babati, Manyara na Mbarali.

Katika sekta ya madini, stori ni hizo hizo. Mwalimu hakuwa na pupa kubinafisha migodi yetu kwa wageni. Alitaka Watanzania wajiandae vyema kabla ya kuchimba migodi hiyo ili iweze kuwaletea maendeleo. Lakini alipokufa, sote tuliiona kasi ya kina Mkapa kuibinafsisha migodi hiyo kwa wawekezaji wa kigeni! Na sasa, muda si mrefu watatuachia mashimo matupu!

Ndugu zangu, ninaweza hata kuandika vitabu vitatu kueleza mambo mengi mema ambayo Mwalimu alituwekea misingi na kutuonyesha njia; lakini wale waliokuwa wafuasi wake wakaamua kuyatelekeza na kutuchagulia njia potevu baada ya kifo chake; lakini itoshe tu kusema kwamba laana yake itawashukia.

Nina hakika kama muujiza ungetendeka na Mwaliimu akafufuka leo, na kuyaona hayo yanayofanywa na waliokuwa wafuasi wake, angewakana mara moja kwa kusema: “Hakika, siwajua watu hawa waovu”.

Nihitimishe safu yangu kwa kukumbusha tena kwamba, huu ni msimu mwingine kwa viongozi wanafiki kumkumbuka Mwalimu Nyerere ki-nafiki. Kwa mwaka mwingine tena, watapanda majukwaani, Ijumaa, Oktoba 14 na kumpamba Nyerere na kusifia sera na miongozo yake; huku wakijua mioyoni mwao kwamba si waumini wa kweli wa fikra zake, na kwamba wanachokifanya ni kinyume kabisa na mafundisho yake.

Hata hivyo, unafiki huo wanaoufanya ni kwa madhara ya afya zao wenyewe! Niwakumbushe wanafiki hao maneno ya Yurii katika riwaya ya Doctor Zhivago ya mwandishi mahiri wa kale wa Urusi, Boris Pasternak.

Yurii anasema hivi: Your health is bound to be affected if day after day, you say the opposite of what you feel, if you grovel before what you dislike ”; yaani kwamba utaathirika kiafya iwapo siku hadi siku utazungumza kinyume ya kile unachokiamini.

Kama hivyo ndivyo, basi, nawashauri wanafiki hawa ambao zamani walikuwa wafuasi wa kweli wa Mwalimu Nyerere lakini wakayatosa mafundisho yake baada ya yeye kufariki; kuzijali, basi, afya zao na kuepuka hiyo Ijumaa, Oktoba 14, kuyasifia mafundisho yake na yale yote aliyoyasimamia wakati wa uhai wake; ilhali mioyoni mwao wanajua kwamba hawayaamini!

Ujumbe wangu kwao ni huu: Watakuwa wanazilinda afya zao kama watakuwa wakweli kuhusu waguswavyo na Nyerere. Waache unafiki.

Lakini kwa waumini wa kweli wa Mwalimu Nyerere, niwakumbushe tu kwamba wana kila sababu ya kusimama kijasiri majukwaani na kumtetea Mwalimu kwa nguvu zao zote; maana hata kama alifanya makosa ya hapa na pale, yake yalikuwa ni makosa ya kibinadamu.

Yake hayakuwa ni makosa yaliyochochewa na uchu wa kutajirika zaidi na zaidi katikati ya mamilioni ya watu masikini; kama ilivyo kwa watawala wetu wa sasa.

Nawatakieni nyote maadhimisho mema ya kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha mpendwa wetu, J.K. Nyerere. Tafakari.

Wednesday, October 12, 2011

Maktaba ya Mkoa, Ruvuma

Nilipiga picha hii ya maktaba ya Mkoa, Ruvuma, tarehe 30 Julai mwaka huu. Niliwahi kuingia katika maktaba hii, ambayo iko mjini Songea, miaka kadhaa iliyopita, lakini safari hii sikupata muda. Nilizunguka maeneo mengine, kama vile Makumbusho ya Maji Maji, ambayo habari zake nategemea kuziandika baadaye.

Napenda kuandika habari za maktaba za Tanzania. Nimeshaandika kuhusu maktaba ya Lushoto, Kilimanjaro, na Iringa. Nitaendelea kufanya hivyo.

Monday, October 10, 2011

Kitabu Kinapopigwa Marufuku

Tutafakari suala tata la kupiga marufuku vitabu. Sijui kama wewe mdau unaafiki suala la kitabu kupigwa marufuku. Mimi huwa nakerwa. Kwa kawaida, kitabu kikipigwa marufuku, huwa nakitafuta ili nikisome. Nimeelezea mtazamo wangu kuhusu suala hili kinaganaga katika kitabu cha CHANGAMOTO. Hapa naleta mifano miwili ya vitabu vilivyopigwa marufuku Tanzania.

Hapa kushoto ni kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai. Wako ambao waliona ni muhimu kitabu hiki kupigwa marufuku. Lakini mimi nilikitetea kwa kila namna, hata Njozi mwenyewe amenishukuru katika kitabu chake kilichofuata.
Kitabu kingine ni Satanic Verses, cha Salman Rushdie. Wako ambao waliona ni muhimu kitabu hiki kupigwa marufuku. Ayatollah Khomeini wa Iran alitangaza fatwa juu ya Salman Rushdie, kwamba ni ruksa kumwua popote. Tangu mwanzo, watalaam wa dini ya ki-Islam sehemu mbali mbali za dunia walipishana mawazo kuhusu jambo hilo. Wako ambao waliafiki fatwa na wengine walipinga. Chuo Kikuu maarufu cha ki-Islam cha Al-Azhar kilisema asiuawe bali kwanza apate fursa ya kujitetea na kutubu.

Suali langu ni je, unaafiki suala la kitabu kupigwa marufuku? Halafu, kwa ujumla wa-Tanzania hawana utamaduni wa kusoma vitabu. Kuna maana gani kupiga marufuku vitabu Tanzania, wakati hata vikiwepo, watu hawavisomi, na huenda wasitambue kwamba vipo?

Kupiga marufuku vitabu Tanzania ni kuwapa wa-Tanzania umaarufu ambao hawastahili, kwamba ni wasomaji wa vitabu. Nimeongelea kirefu zaidi masuala hayo katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Saturday, October 8, 2011

Mkutano wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi Umefana

Mkutano wa leo wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi umefana mjini Minneapolis. Walihudhuria wa-Afrika kutoka nchi mbali mbali kama vile Kongo, Nigeria, Kameroon, Somalia, Liberia, Ghana na Togo. Wa-Marekani Weusi walikuwa wengi, na nilipata fursa ya kufahamiana pia na dada mmoja kutoka Guyana. Nilifurahi kumweleza jinsi wa-Tanzania tunavyomkumbuka Profesa Walter Rodney. Nilimweleza nilivyomfahamu Profesa Rodney, kuanzia niliposoma Mkwawa High School, 1971-72 hadi Chuo Kikuu Dar.

Hapa kushoto ni kiongozi mmojawapo wa Pan African Council, ambayo ndio iliandaa mkutano huu. Anatoka Togo. Katika hotuba yake, aliawasomea wasikilizaji taarifa niliyoandika kuhusu mkutano wa kwanza wa jumuia hii. Nafurahi kwamba tangu mwanzo, viongozi wa jumuia hii wanaitumia taarifa yangu kama kumbukumbu ya mkutano ule. Isome hapa.

Niliguswa pale dada huyu aliponiambia baadaye kuwa anaziheshimu sana kazi zangu. Nafahamu anavyo vitabu vyangu. Alivinunua siku zilizopita.Katika picha hii hapa kushoto, aliyesimama kulia kabisa kwenye kamera, ni Josiah Kibira, mmiliki wa Kibira Films. Yuko mzigoni akirekodi mkutano huo. Yeye tumefahamiana miaka mingi. Katika mkutano huu tulikuwa sisi wa-Tanzania wawili tu. Hata mwaka jana ilikuwa hivyo hivyo, na huwa tunakaa na kujiuliza kwa nini wa-Tanzania hawahudhurii shughuli kama hizi zenye kuelimisha.Hapa kushoto ni mtoa mada Lester R. Collins, mkurugenzi mtendaji wa Council on Black Minnesotans.
Aliongelea mengi, akasisitiza umuhimu wa kufahamiana kikweli kweli sio kijuu juu, ili kila mmoja aelewe mahitaji, mategemeo, na mataizo ya mwingine, ndipo tuweze kujenga mahusiano na mtandao wa kutupeleka mbele. Tuwe na moyo na kusaidiana, na hii ni pamoja na kusaidiana kuelimisha watoto wetu wote.


Hapa kushoto ni mtoa mada mwingine, Profesa Samuel Zalanga wa Chuo Kikuu cha Bethel. Alifafanua vizuri maana ya utajiri na mafanikio, akizingatia kuwa yote hayo hutegemea mkabala wa jamii. Hakuna dhana moja ya mafanikio ambayo inafaa kila mahali na katika kila mazingira.
Watu walisikiliza mada kwa makini. Mkutano huu ulikuwa wa kuelimisha sana.Msichana huyu mdogo alionyesha kipaji chake cha kucheza kwa kufuatilia muziki wa waimbaji fulani. Anatumia miondoko ambayo kwa ujumla inafanana na "ballet" ila niliona yeye anatumia zaidi ubunifu wake mwenyewe. Ni binti mahiri na alishangiliwa sana.Hapa kushoto niko na mdau ambaye tumekutana mara kadhaa katika shughuli za aina hii. Anaitwa M. Ann Pritchard. NI mwandishi, mchoraji, mtunzi wa nyimbo, na muigizaji. Ni mmiliki wa kampuni ya MAMP Creations. Alitaka tupige picha, na tukafanya hivyo.Lakini aliona hii picha ya kwanza haitoshi, akataka nyingine, kama inavyoonekana hapa kushoto, akiwa ameshika vitabu vyangu.