Friday, October 7, 2011

Mkutano wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi, Minneapolis

Kesho kutakuwa na mkutano mwingine wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi mjini Minneapolis, Minnesota. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Miaka michache iliyopita, baadhi ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi wa Minneapolis na maeneo ya jirani waliona umuhimu wa kuwakutanisha watu wa pande hizi mbili ili kufahamiana na kuelimishana, kama hatua muhimu ya kujenga uhusiano bora. Tumeshafanya mikutano kadhaa.

Kwa yeyote anayefahamu, mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi yamekuwa na utata wa aina mbali mbali. Baadhi wamekuwa na ari ya kufahamiana na kujenga uhusiano bora, na baadhi wamebaki katika ujinga na migongano. Tatizo la ujinga ni kubwa, kwa maana kwamba wako wa-Afrika wengi ambao hawajui historia na maisha ya wa-Marekani Weusi, na wako wa-Marekani Weusi wengi ambao hawajui historia na maisha ya wa-Afrika. Hao wakikutana, huwa ni balaa tupu ya kuogopana, kuchukiana, kudharauliana, na hata kurushiana maneno, kila mmoja akiamini kuwa anajua.

Lakini, tukiangalia historia, tutaona kuwa kulikuwa na viongozi wa zamani wa pande hizi mbili ambao walifanya kila juhudi za kuwakutanisha wa-Afrika na wa-Marekani Weusi ili waweze kufahamiana na kupigania maslahi yao katika dunia iliyokuwa imewafanya watumwa au kuwaweka nchini ya ukoloni.

Viongozi hao waliotukuka ni kama George Padmore, Henry Sylvester Williams, W.E.B. Dubois, Jomo Kenyatta, Kwame Nkrumah, Peter Abrahams, Walter Rodney, na Julius Nyerere.

Kwetu waTanzania, ni muhimu kukumbuka juhudi kubwa aliyofanya Mwalimu Nyerere katika harakati hizo kabla na baada ya uhuru wetu. Baada ya uhuru, kwa mfano, Mwalimu Nyerere alipigania umoja wa Afrika na aliunga mkono kwa hali na mali harakati za wa-Marekani Weusi. Wengi wa hao wa-Marekani Weusi ambao walikuwa ni wanaharakati katika kupigania haki nchini mwao Marekani, walikimbilia Tanzania kutokana na kunyanyaswa na kutishiwa na mfumo dhalimu wa ubaguzi waliokuwa wanaupinga.

Leo hii, ni jambo jema kukumbuka hayo yote na kuendeleza harakati hizi, kwani ukombozi kamili bado haujapatikana, kama walivyoelezea vizuri watu maarufu kama Franz Fanon na Malcolm X.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...