Saturday, October 8, 2011

Mkutano wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi Umefana

Mkutano wa leo wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi umefana mjini Minneapolis. Walihudhuria wa-Afrika kutoka nchi mbali mbali kama vile Kongo, Nigeria, Kameroon, Somalia, Liberia, Ghana na Togo. Wa-Marekani Weusi walikuwa wengi, na nilipata fursa ya kufahamiana pia na dada mmoja kutoka Guyana. Nilifurahi kumweleza jinsi wa-Tanzania tunavyomkumbuka Profesa Walter Rodney. Nilimweleza nilivyomfahamu Profesa Rodney, kuanzia niliposoma Mkwawa High School, 1971-72 hadi Chuo Kikuu Dar.

Hapa kushoto ni kiongozi mmojawapo wa Pan African Council, ambayo ndio iliandaa mkutano huu. Anatoka Togo. Katika hotuba yake, aliawasomea wasikilizaji taarifa niliyoandika kuhusu mkutano wa kwanza wa jumuia hii. Nafurahi kwamba tangu mwanzo, viongozi wa jumuia hii wanaitumia taarifa yangu kama kumbukumbu ya mkutano ule. Isome hapa.





Niliguswa pale dada huyu aliponiambia baadaye kuwa anaziheshimu sana kazi zangu. Nafahamu anavyo vitabu vyangu. Alivinunua siku zilizopita.











Katika picha hii hapa kushoto, aliyesimama kulia kabisa kwenye kamera, ni Josiah Kibira, mmiliki wa Kibira Films. Yuko mzigoni akirekodi mkutano huo. Yeye tumefahamiana miaka mingi. Katika mkutano huu tulikuwa sisi wa-Tanzania wawili tu. Hata mwaka jana ilikuwa hivyo hivyo, na huwa tunakaa na kujiuliza kwa nini wa-Tanzania hawahudhurii shughuli kama hizi zenye kuelimisha.



Hapa kushoto ni mtoa mada Lester R. Collins, mkurugenzi mtendaji wa Council on Black Minnesotans.
Aliongelea mengi, akasisitiza umuhimu wa kufahamiana kikweli kweli sio kijuu juu, ili kila mmoja aelewe mahitaji, mategemeo, na mataizo ya mwingine, ndipo tuweze kujenga mahusiano na mtandao wa kutupeleka mbele. Tuwe na moyo na kusaidiana, na hii ni pamoja na kusaidiana kuelimisha watoto wetu wote.


















Hapa kushoto ni mtoa mada mwingine, Profesa Samuel Zalanga wa Chuo Kikuu cha Bethel. Alifafanua vizuri maana ya utajiri na mafanikio, akizingatia kuwa yote hayo hutegemea mkabala wa jamii. Hakuna dhana moja ya mafanikio ambayo inafaa kila mahali na katika kila mazingira.




































Watu walisikiliza mada kwa makini. Mkutano huu ulikuwa wa kuelimisha sana.











Msichana huyu mdogo alionyesha kipaji chake cha kucheza kwa kufuatilia muziki wa waimbaji fulani. Anatumia miondoko ambayo kwa ujumla inafanana na "ballet" ila niliona yeye anatumia zaidi ubunifu wake mwenyewe. Ni binti mahiri na alishangiliwa sana.







Hapa kushoto niko na mdau ambaye tumekutana mara kadhaa katika shughuli za aina hii. Anaitwa M. Ann Pritchard. NI mwandishi, mchoraji, mtunzi wa nyimbo, na muigizaji. Ni mmiliki wa kampuni ya MAMP Creations. Alitaka tupige picha, na tukafanya hivyo.







Lakini aliona hii picha ya kwanza haitoshi, akataka nyingine, kama inavyoonekana hapa kushoto, akiwa ameshika vitabu vyangu.

6 comments:

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Mbele said...

Ndugu Kitururu, shukrani kwa kupita hapa kijiweni pangu. Sasa nimekumbuka jambo kutokana na hiyo picha ya mama aliyeshika vitabu. Nawe ulivishika vitabu hivyo hivyo kwenye picha inayoonekana hapa.

Nawashukuruni wadau kwa kusoma ninayoandika. Ni faraja kwa mwandishi yeyote.

Simon Kitururu said...

@Prof.J: Ni kweli ! Kumbe unakumbuka!:-)

Mie kijiwechako sikosi kupita ingawa mara nyingi ni kimyakimya!

Ila siku ukinidai nilipie niliyojifunza hapa ,... samahani kukuambia kuwa nafikiri bili imeshapitiliza ,sitaweza tena kuafodi kulipa kwa kuwa ni ghali sana tayari kwa jinsi nilivyodoea hapa shule burebure!:-(

Simon Kitururu said...

Nyongeza:

Wakati nasikia BONGO siku hizi hata semina za watu kufunzwa kitu KIWANUFAISHACHO WAO WENYEWE usipoahidi kuwalipa BONUS fulani au NGAWIRA PESA FULANI kwa kuhudhuria semina hiyo na kuahidi pia kuwa watakula bure halafu kutakuwa na pati fulani ambazo watakuja kunywa KILAJI bure, ....SEMINA hiyo huonekana ni ya kifala na haji MTU,...

...na na hata bila hilo nawasikitikia watu wasiochukua elimu nguli za burebure kama hizi ambazo uhitajicho ni kuingia tu kijiweni nakujichotea shule.

Mbele said...

Kila ambaye ninaongea naye ambaye alihudhuria, anausifia mkutano huu kuwa ulikuwa wa manufaa sana.

Kuhusu semina, napenda kusema kuwa mwaka jana nilijaribu kuandaa semina Tanzania (katika miji ya Tanga na Arusha), nikaenda kule kwa gharama yangu, na hoteli nikajilipia, na sehemu ya mkutano nikalipia, lakini hakuna m-Tanzania aliyehudhuria.


Huku Marekani huwa siandai, bali naalikwa nikazungumze. Nahisi kuwa wa-Tanzania wanaona sina la kuwaeleza. Nami sina ugomvi na hilo. Nitaendelea kushughulika na wale wanaoona nina la kuwaambia.

Hapa Marekani nimewahi kulipia dola mia mbili na kidogo kuhudhuria warsha moja. Ukifahamu kuwa elimu ni mtaji wa thamani kubwa, huwezi kusita kulipia.

Somo hili hadi sasa halieleweki nchini mwetu, ndio maana watu wanatarajia kupewa kibahasha cha ruzuku wanapohudhuria warsha, na bila hicho kibahasha hawaji.

Anonymous said...

Kuhusu semina, napenda kusema kuwa mwaka jana nilijaribu kuandaa semina Tanzania (katika miji ya Tanga na Arusha), nikaenda kule kwa gharama yangu, na hoteli nikajilipia, na sehemu ya mkutano nikalipia, lakini hakuna m-Tanzania aliyehudhuria.

HAPO PROF MBELE PANATAKIWA KUFANYIWA UTAFITI KWA NINI IMETOKEA HAYO....WANASIASA WA WATANZANIA WAO KWA SABABU WANAFAHAMU SISI WATANZANIA TULIO WENGI TUNA-UMASKINI WA UELEWA HIVYO WANASIASA WANACHOFANYA KUWAPIKIA PILAU WAKATI UACHAGUZI ILI WAWAPIGIA KURA.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...