Mwaka huu, nilipokuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya LCCT, tulipata fursa ya kutembelea Uyole, mkoani Mbeya. Hiyo ilikuwa ni tarehe 19 Agosti. Hapo tulienda kuangalia mipango ya uanzishwaji wa Chuo Kikuu ambao ni mradi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania. Kabla ya yote, napenda kuwashukuru wachungaji Dr. Mwalilino na Dr. Stephen Kimondo kwa kuandaa mawasiliano yaliyotuwezesha kufanya ziara hii.
Mwenyeji wetu alikuwa Mchungaji Dr. Gwamaka Mwankenja, ambaye ndiye mratibu wa mpango huu wa kuanzisha chuo kikuu. Alitukaribisha vizuri na tuliongea kirefu. Alituelezea mpango mzima na changamoto zake, akatutembeza maeneo ya chuo.
Kama mwanataaluma na mwalimu, nafuatilia sana hali na maendeleo ya elimu Tanzania, sio tu kwa kusikia au kusoma taarifa, bali kwa kutembelea shule na vyuo kila ninapokuwa nchini. Napenda kufuatilia vyuo vikuu vipya. Kwa mfano, nilishazuru Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa kilichoko Lushoto. Niliangalia ukarabati wa majengo ya shule ya zamani ya Magamba, ambao ndio msingi wa chuo hiki kipya. Pia nimekuwa nikifuatilia mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Njombe, kama nilivyoelezea hapa.
Chuo Kikuu cha Uyole kinatarajiwa kuanza kwa kutumia majengo ya Chuo cha Ualimu cha Uyole, sambamba na harakati za kujenga majengo mapya na miundombinu itakiwayo.
Naona huu ni uamuzi bora. Kitu cha muhimu, kwa mtazamo wangu, ni kuwa na wahadhiri bora na vifaa vya msingi, kama vile vitabu, na wanafunzi wenye nia ya kweli ya kutafuta elimu. Binafsi, nisingeona shida kufundisha katika madarasa niliyoyaona hapa ya Chuo cha Ualimu. Unaweza ukawa na majengo ya kisasa kabisa, lakini elimu bado ikawa duni. Mwisho wa siku, ingawa majengo bora ni muhimu, elimu haitoki kwenye majengo.
Kwa kweli, niliona ni sehemu nzuri na kubwa. Wakati tunapitishwa katika mazingira ya hapo tuliwakuta wanafunzi uwanjani wakifanya mazoezi ya kwaya. Mchungaji Mwankenja alitutambulisha, nami nikapata fursa ya kuwasalimia na kuwahamasisha katika kutafuta elimu kwa dhati. Walituzawadia CD ya nyimbo zao.
Binafsi, naunga mkono mipango ya kujenga vyuo vipya kama hiki cha Uyole. Kwanza, idadi ya waTanzania inaongezeka muda wote, na mahitaji ya vyuo hayatapungua. Ni vema kujenga sasa, kwa kadiri iwezekanavyo, kuliko kungoja hadi baadaye, wakati gharama zinaendelea kupanda.
Hata kama vyuo vitakuwa vingi mno na wanafunzi wasiwe wa kutosha, jambo la kuzingatia ni kuwa vyuo vyetu vikiwa bora sana vitawavutia wanafunzi na watafiti kutoka nchi za nje, kama ilivyokuwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya zamani. Faida zake ni nyingi, kuanzia za kitaaluma, kwa maana ya fursa ya kubalishana mawazo baina ya watu wa mitazamo mbali mbali, hadi kiuchumi. Kwa mfano, Marekani inatambua jambo hilo, na inajivunia malaki ya wanafunzi wanaosoma katika nchi hiyo kutoka duniani kote. Pamoja na faida kubwa za kitaaluma, wageni hao wanaingiza mamilioni ya dola katika uchumi wa Marekani kila mwaka.
Ni muhimu kwa sisi wa-Tanzania kuwa na mawazo mapana kuhusu masuala ya aina hii. Tuwekeze katika vyuo pia, ila tuwe makini katika kuhimiza na kuboresha taaluma, utafiti, na maadili yahusikayo. Lakini kwa hali ilivyo, tuko nyuma sana. Baadhi ya wanaoongoza vyuo vyetu hawana upeo utakiwao, na serikali haina upeo huo. Serikali imekuwa na historia ya kuwapachika watu kwenye nafasi za uongozi wa vyuo bila kuzingatia masuala muhimu ya misingi, maana na wajibu wa vyuo vikuu. Kukosekana kwa upeo huu ni msingi mkubwa wa migomo na vurugu zisizoisha katika vyuo vyetu ambazo hukwamisha uwezo wa kuviweka vyuo vyetu katika viwango vitakiwavyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Prof Mbele,
Ubarikiwe sana kwa kuwa na moyo wa uzarendo na wenye tija katika kufuatilia elimu kwa nchi yetu.Pia umekuwa ukitoa makala nyingi nyendelevu na zenye tija ya elimu na ufanisi katika nyanda za kijamii,kielimu, kiuchumi na kisiasa.Wewe kama profesa unaonyesha moyo wa kihalisia sana kwa Watanzania wenzako wenye elimu ya juu, ya kati na wale ambao wanaichuchumilia elimu kwa kiwango chochote.Cheche zako na jitihada zako zitazaa matunda mema sana.Binafsi nakupongeza sana kwa kutembelea vyuo vyetu na kupata nafasi ya kuona mazingira ya miundo mbinu na kuongea na wakuu wa vyuo ili kupeana mawazo ya hapa na pale katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya elimu nchini kwetu.Mungu anendelee kukutia nguvu na kukupa minya mingi zaidi ili kusaidiana na wenzetu hao.Mdau wa Mbeya-USA
Asante sana Mdau wa Mbeya-USA, kwa ujumbe wako. Ninapoenda kwenye hivi vyuo na kuona hali halisi, na kuwasikiliza viongozi, wanavyoelezea juhudi zao, changamoto na vipingamizi, na papo hapo naona moyo wao wa kujituma, na imani yao ya mafanikio, na huwa naguswa sana.
Ni elimu kubwa kwangu, ingawa mimi mwenyewe niko katika mkondo huu huu tangu zamani, wa kujibidisha katika masuala ya elimu, na kuchangia juhudi za wengine.
Sasa, watu wa aina hii mnapokutana, furaha inakuwa kubwa na mnapeana moyo wa kusonga mbele. Halafu, ukizingatia kuwa Mungu ndiye anayeongoza njia na kututaka tufanye mambo mema kama haya, kila siku inakuwa ni siku ya shukrani na furaha kwa wahusika.
Ndio maana, ninapoandaa safari ya kwenda Tanzania, ziara hizi za vyuoni huwa ni kipaumbele kimojawapo. Wakati huu naandaa safari, na lazima nikafike tena Uyole.
Asante sana kwa ujumbe wako wenye kuongeza imani moyoni. Tuko pamoja, na Mungu atatubariki.
Post a Comment